Maalim Seif, Maalim Seif, Maalim Seif

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,920
30,261
"MAALIM SEIF, MAALIM SEIF, MAALIM SEIF"
Naangalia matangazo haya mubashara kutoka Bungeni, Dodoma. Hakika lilikuwa jambo la fedheha kwani kibwagizo kile cha jina la Maalim kilikuwa kinasema mengi na kuashiria mengi. Dunia ilikuwa inashuhudia upeo wa mwisho wa nguvu na ushawishi wa Maalim Seif katika siasa za Tanzania. Lakini ukweli ni kuwa dunia haikuwa inaangalia upeo wa mwisho wa mapenzi ambayo watu na khasa wapiga kura wa Zanzibar waliyokuwanayo kwa Maalim Seif.

Uchaguzi wa Zanzibar wa 2015 ulimalizika kama ilivyokuwa kawaida ya chaguzi zote za Zanzibar kuanzia uchaguzi wa 1995. Katika uchaguzi wa 2015 kulikuwa na usiku wa "La ilaha ilallah," wapiga kura walipokusanyika nje ya ofisi ya ZEC wakidai na kusubiri mshindi halali wa uchaguzi wa Rais Maalim Seif Shariff atangazwe. Wakati wakisubiri Maalim Seif atangazwe mshindi huu ndiyo ulikuwa uradi wao.

Bunge Dodoma lilikuwa limeshuhudia miujiza ya Maalim Seif. Sasa ilikuwa zamu ya waliokuwa mitaani Bara na Visiwani na wao kushuhudia miujiza ya Maalim. Maalim Seif aliitikisa nchi nzima kwa lile ambalo halijapata kutokea popote ulimwenguni katika siasa za vyama vingi.

Hili lilinishughulisha kwa muda nikiwauliza marafiki zangu mabingwa na wanafunzi wa elimu ya siasa kama limepata kutokea popote? Majibu kwangu ni kuwa niwape muda waendelee kutafuta.

Mahakama Kuu ilipomthibitisha Prof. Lipumba kuwa Mwenyekiti wa CUF, Maalim Seif pale pale, siku hiyo hiyo na bila ya kupepesa jicho alitangaza kujitoa CUF na kuhamia ACT Wazalendo.

Huu ulikuwa mwaka wa 2019.

Baina ya Adhuhuri na Maghrib yake wanachama karibu ya wote wa CUF Visiwani na Bara walihama na Maalim kuhamia chama kipya cha ACT Wazalendo wakiwa na kauli mbiu, " Shusha tanga pandisha tanga safari iendelee."

Baina ya L' Asr na Isha yake ofisi zote za CUF zikawa zimepakwa rangi mpya ya zambarau ya ACT Wazalendo. Ghafla CUF ikawa imepotea katika macho ya watu, haipo na haionekani kama vile ardhi imefunguka ikaimeza. Prof. Lipumba alikuwa kweli Mwenyekiti wa CUF lakini chama kikawa kimekimbiwa na wanachama wake wengi sana.

Chama hakiwezi kuwa chama kama hakina wanachama.

"Maalim Seif, Maalim Seif, Maalim Seif."

Hili lilikuwa kubwa na zito kupita lile la Bungeni Dodoma. Huu ulikuwa muujiza. Wafuatliaji wa siasa za Zanzibar wengi wao walisema kuwa Maalim hawezekani. Zanzibar ikaingia katika uchaguzi wake wa sita mwaka wa 2020 Maalim akiwa mgombea wa ACT Wazalendo dhidi ya mgombea wa CCM Dr. Hussein Mwinyi.

Fupa lililomshinda fisi mbwa ataliweza? Nina kumbukumbu nyingi za Maalim Seif toka siku ile tulipokutana kwa mara ya kwanza Starlight Hotel mwaka wa 1992. Nimempiga picha nyingi. Nakumbuka mara ya mwisho kukaa faragha nyumbani kwake Ilala, Shariff Shamba nilimwambia tukae kitako tuandike kitabu cha maisha yake kama kinavyostahili kuandikwa.

Maalim alicheka. Msomaji wangu nakuachia wewe ukhitimishe makala haya kwa kuandika para ya mwisho hapo chini kwenye comments.


View: https://youtu.be/yEGNIM4gWlg
 
Uzuri Lipumba swala tano laiti angekuwa Mgalatia tungeanza kusema mfumo Kristo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom