Wakuu msichoke , haya mambo ya Zanzibar kiukweli hayajaisha , ndio kwanza yanaanza .
Taarifa mpya zilizonakiliwa kwenye gazeti la Mwananchi zinaeleza kwamba Shujaa Maalim Seif atazungumza na dunia kesho tarehe 10 / 4 ambapo atapata nafasi ya kuweka wazi mustakabali wake kisiasa .
Mwamba huyo wa siasa za nchi hii ambaye sasa dunia nzima inamtambua na kumkubali ataelezea mikakati , mipango na mwelekeo wa chama chake cha CUF katika siasa za Zanzibar .
Kila la heri Maalim Mungu akulinde .
====================
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad kesho ataelezea mwelekeo wake kisiasa, ikiwamo kufafanua kiundani uamuzi wa chama hicho kususia uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu.
Mgombea huyo wa urais Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana ataeleza mambo hayo ikiwa imepita takribani wiki moja tangu Baraza Kuu la chama hicho kutoa msimamo wake wa kutomtambua Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein pamoja na wawakilishi na madiwani.
CUF kilisusia kushiriki uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu baada ya Oktoba 28 mwaka jana, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya urais, uwakilishi na udiwani, akisema kulikuwapo na ukiukwaji wa sheria na kanuni za uchaguzi.
Habari kutoka ndani ya chama hicho zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa mkutano wa kiongozi huyo utakuwa wa kwanza kwake, tangu kumalizika kwa uchaguzi wa marudio na ataeleza mambo muhimu yatakayotoa picha halisi ya mwelekeo wake na CUF.
“Katika mkutano uliopita tamko lilikuwa la Baraza Kuu ila keshokutwa (kesho) Maalim Seif atazungumza kama Katibu Mkuu na aliyekuwa mgombea urais. Kuna masuala mengi atayaeleza kwa kina, hasa hili la uamuzi wa CUF kususia uchaguzi,” zilieleza taarifa hizo.
“Atazungumzia kwa kina uchaguzi ulivyokuwa na kujibu maswali ya watu wa kada mbalimbali waliokuwa wakihoji nini hatima ya CUF, baada ya kususia uchaguzi na hivyo kupoteza nafasi za uwakilishi.”
Chanzo: Mwananchi.