Maalim sefu bado ngangari!!!!! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Maalim sefu bado ngangari!!!!!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Kadogoo, Jan 11, 2012.

 1. K

  Kadogoo JF-Expert Member

  #1
  Jan 11, 2012
  Joined: Feb 26, 2007
  Messages: 2,072
  Likes Received: 5
  Trophy Points: 135
  KUMBE HUYU MZEE MAALIM SEFU SHARIFF HAMAD BADO IMARA HIVYO!! SIKUJUA! HABARI ZAIDI SOMA HAPA MAKALA TOKA TANZANIA DAIMA:

  NA Absalom Kibanda

  TAIFA linao viongozi wawili tu maarufu zaidi ambao majina yao halisi yameunganishwa na uasilia wao wa kitaaluma na kikazi waliokuwa nao kabla hawajaingia katika ulimwengu wa siasa.

  Viongozi hao wawili si wengine bali ni Baba wa Taifa ‘Mwalimu' Julius Kambarage Nyerere na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), ‘Maalim' Seif Sharif Hamad.

  Ni jambo la bahati tu kwamba, viongozi hao wawili wa kisiasa walio na ushawishi mkubwa na ambao wamefanikiwa kuishi na sifa yao ya kitaaluma ya ‘Mwalimu' (Maalim) kabla ya kuingia katika siasa walikuwa ni walimu.

  Ingawa kifalsafa, kiuongozi na hata kimaono wanasiasa hawa wawili hawawezi kufananishwa achilia mbali kulinganishwa, bado ukweli unabaki pale pale kwamba, kazi walizofanya zimeweka alama ya kudumu katika maisha ya watu waliopata kuwaongoza.
  Ukimwacha Baba wa Taifa ambaye wasifu wake unafahamika miongoni mwa Watanzania walio wengi, Maalim Seif anabakia kuwa mmoja wa wanasiasa adhimu ambao Zanzibar imepata kuwa nao tangu mapinduzi ya visiwa hivyo, Aprili mwaka 1964.

  Alama alizoweka katika medani ya siasa na uongozi, tangu akiwa Waziri wa Elimu Zanzibar na baadaye Waziri Kiongozi miaka ya 1970 na 1980, kabla hajalazimishwa kuingia katika vuguvugu la siasa za upinzani mwanzoni mwa miaka ya 1990 kwa kiwango kikubwa ndizo ambazo zinamweka katika daraja la juu la kiuongozi katika taifa hili kwa kiwango ambacho hakijapata kufikiwa na mwanasiasa mwingine yeyote ukiwaacha waasisi wawili wa taifa hili, Nyerere na Abeid Amani Karume.

  Viatu vya kisiasa na kuongozi anavyovaa au alivyopata kuvivaa mwanasiasa huyo kwa namna yoyote ile vinawapwaya makumi ya viongozi wa kisiasa waliopata kutokea katika visiwa vya Zanzibar, achilia mbali wale wa Tanzania Bara.

  Kwa miaka mingi, Maalim Seif, amekuwa ndiye rais aliyekuwa ndani ya mioyo ya Wazanzibari walio wengi tangu aliponyimwa fursa hiyo kimizengwe mwanzoni mwa miaka 1980 na nafasi yake ikachukuliwa na marehemu, Abdul Wakil Nombe.

  Ingawa ndani CCM na hata akiwa CUF hajapata kutawazwa kuwa Rais wa Zanzibar kwa sababu za kufitiniwa kisiasa, Maalim Seif ameendelea kuwa mwanasiasa mwenye mvuto mkubwa na wa kipekee kisiasa na kiuongozi ndani na nje ya visiwa hivyo.

  Heshima aliyojijengea kama kiongozi wa watu aliye na ushawishi na nguvu kubwa kwanza katika kisiwa cha Pemba na kisha Unguja ndiyo ambayo kwa upande mwingine imemfanya ajikute akizalisha maadui wengi wa kisiasa.

  Uadilifu wake kifikra na kimaisha, uchapaji kazi wake usiomithilika, utu wake uliotukuka na mapenzi yake ya kweli kwa watu anaowaongoza, mbali ya kumjengea sifa na heshima vimemjengea maadui wa kila namna katika maisha yake ya kisiasa.

  Jina jipya lililoingia katika orodha ya maadui wa kisiasa wa Maalim Seif ambaye sina shaka hata kidogo kusema kwamba naye amenaswa katika mtego ule ule uliowanasa wanasiasa wengine kabla yake ni Hamad Rashid Mohammed mmoja wa wanasiasa wenye majina makubwa hapa nchini.

  Katika mazingira ambayo si rahisi kuyaeleza kwa ufasaha, Hamad Rashid kwa matendo na maneno alijiweka katika mtego wa kutimuliwa ndani ya CUF tangu siku alipopata ujasiri wa kuamua kukabiliana na Maalim Seif ana kwa ana na nje ya vikao rasmi vya chama hicho.

  Ingawa katika fikra za wadadisi wa masuala ya siasa, wakiwamo wanasiasa wa ndani na nje ya CUF, wanazuoni na wanahabari, Hamad Rashid alionekana akifanya jambo sahihi lililomfanya aonekane kuwa shujaa wa kisiasa ndani ya moyo wa chama hicho, kile alichokifanya kilibeba taswira moja kubwa; usaliti.

  Mara moja, mwanasiasa huyo ambaye alijipatia umaarufu mkubwa Tanzania Bara pengine kuliko ilivyokuwa kwa mwanasiasa mwingine yeyote ukimwacha Maalim Seif mwenyewe kwa namna ambayo hakutarajia akashangaa akijikuta akibaki mpweke ndani ya chama chake kadri siku zilivyokuwa zikisonga mbele.

  Yale yaliyotokea ndani ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la CUF siku ajenda yake ilipokuwa ikijadiliwa, yalitosha kumfanya Hamad Rashid abaini haraka haraka kwamba, wabunge wenzake na baadhi ya watu aliokuwa akiamini kwamba walikuwa upande wake wa pili na si kwake.

  Ni jambo la kutatiza sana kwamba, Hamad Rashid aliingia katika mapambano hayo akisahau kwamba, Maalim Seif ndani na nje ya CUF ana nguvu za kitaasisi zaidi pengine kuliko walizonazo au walizopata kuwa nazo wanasiasa wengi wengine ndani na nje ya chama hicho.

  Matamshi ya Hamad Rashid na yale yaliyokuwa yakitoka vinywani mwa wafuasi wake kabla ya vikao vya kumjadili yalimfanya yeyé na wenzake wengi kuamini kwa dhati kwamba kwa mara ya kwanza walikuwa wamepata mbinu ya kumbwaga kutoka katika kiringe cha siasa jabali la siasa za Zanzibar, Maalim Seif.

  Hamad Rashid alifanya hivyo akisahau kwamba, Maalim Seif aliyekuwa akijaribu kupimana naye nguvu ndiye mwanasiasa pekee aliyepata kukabiliana na Baba wa Taifa na akaendelea kubakia na heshima ya kipekee kwa watu wake.

  Mbunge huyo wa Wawi alionekana dhahiri akisahau ukweli kwamba, Maalim Seif ndiye mwanasiasa pekee anayeishi leo aliyepata kukabiliana na ‘maguvu' ya CCM na dola tangu mwaka 1980 na akaendelea kudumu na kubakia na ushujaa alionao leo pasipo kutetereka.

  Kama hiyo haitoshi, Hamad Rashid na mashabiki zake waliingia katika vita hiyo wakisahau kwamba ajenda ya mabadiliko ya kisiasa Zanzibar yaliyoilainisha CCM haiwezi kufanikiwa pasipo kuunganishwa na jina la Maalim Seif.

  Wapinzani hao wa Maalim Sef walisahau kwamba kile ambacho Hamad Rashid alikiita ‘CCM B' akinaswa na mtego wa hoja za washindani wao, CHADEMA kwa wana CUF wenzake na hususan viongozi wa chama hicho walio ndani ya serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar ni mtaji wa ushindi mkubwa siku zijazo.

  Hamad Rashid aliingia katika vita hivi huku akisahau kwamba alikuwa akipambana huku akisahau historia ya yeye mwenyewe kupata kukaribia kukataliwa katika mchakato wa kusaka mgombea mbunge wa Wawi kwa tiketi ya CUF kabla ya jina lake kurejeshwa na Maalim Seif yule yule aliyedhani angeweza akamkabili na kumshinda pasipo kwanza kupata baraka za wapigakura wake.

  Pengine kikubwa ambacho, Hamad Rashid na wenzake walikisahau wakati wakipambana ni kosa lao la kushindwa kumtambua adui wa kweli wa CUF ambaye, yumkini siyo Maalim Seif ambaye walimlenga na kumshambulia.

  Ni jambo lisiloingia akilini hata kidogo kwa wanasiasa makini wa aina ya Hamad Rashid kumtwisha mzigo wote wa lawama Maalim Seif za kukwama kwa chama hicho kupenya ngome ya kisiasa ya upande wa pili wa muungano.

  Zile lawama walizokuwa wakivurumisha kwa Katibu Mkuu wao kwamba alikuwa ameshindwa kuchukua hatua zozote za maana kukijenga chama chao Tanzania Bara wakati wenyewe wakijua fika kwamba jukumu hilo ni la viongozi wote wa chama hicho akiwamo mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba, japo zilionekana kuungwa mkono na wapambe wengi bado zilikuwa hazitoshi kuwafanya wakabaki salama.

  Katika mazingira ambayo nguvu ya kipekee na ya kihistoria ya jina la Maalim Seif iliyokijengea uhalali chama hicho kwanza Pemba na kisha Zanzibar nzima, yalitosha kabisa kuwaadabisha na kuendelea kuwaumiza mbele ya safari Hamad Rashid na wafuasi wake ambao ama wamesahau walikotoka au hawajui nini wanakitafuta Wazanzibari na wapenda mageuzi huko tuendako.

  Kushindwa kwao kuutambua ukweli huo, ndiko kulikowafanya waonekane haraka haraka kuwa mawakala watu wasioitakia mema Zanzibar na mamluki waliotumwa kuiua CUF badala ya kuijenga kama ambavyo wao walitaka waonekane kuwa.

  Katika mazingira ambayo nguvu na historia ya mtu mmoja anayeungwa mkono na kulindwa na rekodi ya fikra, maamuzi na matendo yake kama alivyo Maalim Seif, kujitokeza na kuamua kumkabili kwa namna walivyofanya kina Hamad Rashid ni kujitakia kifo cha kudumu cha kisiasa. Ingawa ni kweli kama kiongozi na mwanasiasa, Maalim Seif anayo mapungufu mengi, Hamad Rashid na wenzake walipaswa kulijua hili mapema kwamba, si jambo rahisi hata kidogo ukamshinda kwa namna ya kumuumbua mtu ambaye mnajua fika kwamba taswira anayoibeba ina sura ya kitaasisi zaidi kuliko alivyo mtu binafsi
   
Loading...