Maajabu ya mapacha walioungana

Donatila

JF-Expert Member
Oct 23, 2014
7,575
21,687
pic+Mapacha.jpg


Miaka 21 iliyopita, familia ya Alfred Mwakikuti na Naomi Mshumbusi ilijaaliwa kupata watoto pacha, Maria na Consolata. Lakini hawakuwa pacha wa kawaida; walikuwa wameungana na hakukuwapo na uwezekano wa kuwatenganisha.

Hawakuweza kujulikana mapema hadi walipofikia umri wa kwenda shule. Hapo ndipo vyombo vya habari vilipotangaza kwa nguvu habari ya watoto wao, baada ya Mwananchi kuiibua.

Mwaka 2010 walimaliza elimu ya msingi na 2014 elimu ya sekondari na mwaka huu wamemaliza elimu ya juu ya sekondari.

Wakati wote huo gazeti hili limekuwa nao pamoja katika kila hatua na sasa linakuletea habari mfululizo za maisha yao kuanzia leo. Mwandishi wetu, Tumaini Msowoya anaongea nao kwa kirefu kuhusu maisha yao, changamoto, mafanikio na matamanio yao. Sasa endelea…

Kilolo. Acheni Mungu aitwe Mungu kwa kuwa maajabu yake ni makubwa na hayaelezeki.

Maajabu hayo ya Mungu yanadhihirika katika muujiza wa watoto pacha, Maria na Consolata Mwakikuti waliozaliwa wakiwa wameungana.

Pacha wengi walioungana huwa wanadumu kwa kipindi kifupi na wengine hupoteza maisha yao wakati madaktari wanapojaribu kuonyesha ubingwa kwa kuwafanyia upasuaji ili watenganishwe.

Maria na Consolata ni miongoni mwa pacha ambao Mungu ameruhusu waishi pamoja mpaka leo.

Si tu kwamba, Mungu ameruhusu pacha hao kuishi, bali amekuwa akionyesha maajabu yake kwa kuwawezesha kufanikiwa katika kila hatua.

Maria na Consolata ni pacha wa kipekee waliogeuka kivutio, si tu kwa sababu wameungana, bali ni kutokana na namna walivyochukulia maisha hayo ya kuishi katika mwili mmoja na kuzishinda changamoto za kimaisha, wakifanya vizuri katika elimu ambayo ndiyo changamoto yao kubwa kwa sasa.

Hivi karibuni walihitimu kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Udzungwa iliyopo kijiji cha Kifabaga, Kilolo mkoani Iringa.

Pacha hao walizaliwa mwaka 1996, katika hospitali ya Misheni ya Ikonda, iliyopo kijiji cha Ikonda, Wilaya ya Makete mkoani Njombe .

Mwaka 2010, walitikisa taifa baada ya kufaulu mitihani yao ya darasa la saba na hivyo kuwa na sifa ya kuendelea na masomo ya sekondari.

Miaka minne baadaye mapacha hao walitikisa tena baada ya kufaulu mitihani mingine ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Maria Consolata ya Kilolo.

Hivi sasa kila mmoja ndani na nje ya nchi, anasubiri matokeo ya kidato cha sita ya kinadada hao yatakapotangazwa.

“Japo sisi ni yatima na wenye ulemavu kutokana na kuungana kwetu, haya yote si sababu ya kufeli darasani na kushindwa katika maisha. Tunajiamini na tuna uhakika kwamba tunaweza. Ni bidii tu,” anasema Consolata.

Siku niliyopata nafasi ya kushinda nao, si tu nilipata habari bali nilijifunza mengi kutoka kwao.

Ni wakarimu, wacheshi, wapole, wenye upendo na si watu wa kukurupuka kujibu, bali hutafakari kwanza.

Haichukui muda mrefu kuwazoea mapacha hawa, kwa kuwa ni wachangamfu.

Japokuwa safari yangu ya kuelekea Kidabaga, Kilolo wanakoishi mapacha hao ilikuwa ya kusuasua kutokana na uhaba wa usafiri, uchovu uliisha mara nilipobisha hodi nyumbani kwao na kupokelewa kwa nyuso zilizojaa tabasamu na bashasha.

“Karibu nyumbani kwetu, jisikie huru,” alisema mmoja wao wakati wakinikaribisha kwa furaha. Mara nyingi wanapozungumza, huwa wanatamka maneno kwa pamoja.

Pacha hawa ni watoto yatima. Baba yao Alfred Mwakikuti na mama yao Naomi Mshumbusi walifariki dunia nyakati tofauti.

Baba alifariki wakati wakiwa na umri wa miaka mitatu na mama yao alifariki wakati wakiwa vichanga.

“Bora baba tuna kumbukumbu kidogo alikuwaje, mama yetu hatukuwahi kumuona kabisa,” anasema Consolata.

Tangu wakati huo, wamekuwa wakilelewa na wamisheni na kwa sasa wapo chini ya Shirika la Masista Wamisionari wa Shirika la Maria Consolata, Nyota ya Asubuhi linalofanya shughuli zake Kijiji cha Kidabaga wilayani Kilolo.

Mkuu wa shirika hilo, Sister Idda Luizer anasema wanafurahi kuwalea watoto hao ambao alisema ni wacha Mungu.

Kwa kweli wamebadilika tofauti kabisa na miaka sita ya nyuma wakati nilipozungumza nao, wakiwa Ikonda wilayani Makete mara baada ya kuhitimu darasa la saba.

“Zamani tulikuwa na hisia tofauti, tulipenda tofauti lakini kwa sasa tumejikuta tukipenda na kuhisi pamoja,” anasema Consolata.

Consolata anaongea zaidi kuliko Maria na wanapotembea, hutumia mikono na miguu.

Wanao uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu, kwa sababu licha ya kuwa mara ya kwanza kukutana nao ilikuwa 2010, bado waliweza kunitambua na hata kuniita kwa jina.

Mwaka huo nilipozungumza nao walitamani kusomea teknolojia ya mawasiliano, ndoto iliyozima kutokana na namna wanavyoendelea na elimu ya juu.

Ndoto yao sasa ni kuwa walimu.

Pia, wanataka kufika chuo kikuu na wakihitimu wafunge ndoa ya mume mmoja.

Miujiza ya Mungu inaonekana katika umbile lao. Maria na Consolata wameungana kuanzia kifuani. Wanachangia tumbo, wana kitovu kimoja, kiuno kimoja, mikono minne yote ikiwa na nguvu za kufanya kazi na miguu mitatu.

Mguu mmoja una miguu miwili ndani yake; ni kama wameunganishwa kwa kufunikwa na ngozi.

Hii inamaanisha kwamba ukiugusa mguu huo upande mmoja wa ngozi ataitika Maria na upande mwingine, ataitika Consolata.

“Mguu huu mmoja ni wa kwetu wote, ukiugusa upande mmoja Maria anasikia na upande mwingine, mimi nasikia,” anasema Consolata.

Maumbile haya ndio sababu kubwa ya pacha hao kutembea kwa mikono na miguu.

Watembeapo mara zote Maria huwa chini kidogo na mara zote huwa anapumua kwa shida, hali inayoonyesha kwamba Consolata huwa anamuelemea mwenzake.

Matembezi yao huwa ni katika eneo la nyumbani kwao na wanapotaka kutoka, huwa wanatumia kiti cha magurudumu.

Pamoja na kwamba wameungana, kila mmoja ana sehemu zake za siri na kila mmoja anajisaidia kwa wakati wake.

Consolata anasema kila mmoja huwa anasikia maumivu kwa wakati wake.

Kitu pekee ambacho huwa wanapata maumivu kwa pamoja ni makalio ambayo huchoka zaidi wanapokaa kutokana na aina ya ulemavu. Ikiwa mmoja atahitaji kulala basi mwingine hulazimika kumvumilia mwenzake hadi anapoamka au naye aamue kulala.

“Mchana mwenzangu akisinzia, huwa tunalala tu kwenye kochi kwa sababu ni kubwa na haina haja ya kuingia chumbani. Mmoja akilala, mwingine hubaki akimsubiri mwenzake au basi wote tulale,” anasema.

==========


Jana tuliishia sehemu inayoeleza jinsi pacha hawa walioungana, Maria na Consolata, wanavyochangia hisia za baadhi ya viungo vyao.

Pengine ni kuchangia huko kwa hisia za viungo, kumefanya wawe pia na hisia moja katika masuala ya kimaisha. Wawili hawa wanahisia moja ya kimapenzi. Sasa endelea…

Si rahisi kufikiria maisha ya ndoa ya Maria na Consolata kwa jinsi walivyo, lakini pacha hawa walioungana wako wazi kuhusu matamanio yao ya maisha ya ndoa.

Katika mazungumzo yao na gazeti hili, Maria na Consolata waliweka bayana mipango yao ya ndoa mara watakapomaliza elimu ya chuo kikuu.

Ingawa ni kitu cha kushangaza, Maria na Consolata hawatakuwa mapacha wa kwanza katika maisha ya ndoa. Chang na Eng Bunker ni pacha wanaume waliozaliwa mwaka 1811 nchini Thailand ambako zamani kuliitwa Siame.

Tofauti na mapenzi ya akina Maria na Consolata, pacha hao kila mmoja alioa mke wake na kufanikiwa kupata watoto.

Kama ilivyokuwa kwa pacha hao, Maria na Consolata wanatamani kuwa wanandoa na ndoto zao ni kuolewa na mwanaume mcha Mungu na atakayewajali.

“Ndoa ni sakramenti takatifu, tukishamaliza masomo yetu ya chuo kikuu tunatamani kuja kuwa wanandoa,” anasema Maria.

Kwa namna walivyo, si rahisi kwao kuolewa na wanaume tofauti isipokuwa mume mmoja na wanalijua hilo.

Haya ndio yalikuwa mahojiano baina yangu na wao kufuatia ndoto hiyo.

Mwandishi: Baada ya masomo, nini ndoto zenu?

Maria: Ndoto zetu ni kuwa wanandoa. Zamani tulikuwa tunapenda tofauti, lakini kwa sasa tumempenda mtu mmoja. Tumegundua tuna hisia moja.

Mwandishi: Tayari kuna mtu mmempenda nini?

Maria na Consolata kwa pamoja: Ndio tumempenda mtu mmoja.

Mwandishi: Nani alimwambia mwenzake kwanza kuhusu hisia za kupenda?

Consolata: Sisi ndio tuliomwambia kwamba tunampenda, naye alitusikiliza.

Mwandishi: Aliwajibu nini?

Maria: Yupo kwenye tafakari, hawezi kusema akurupuke na kuingia bila tafakari. Lazima tumpe muda wa kutafakari.

Mwandishi: Ni mwanaume wa aina gani mnayempenda?

Consolata; Tunapenda kuolewa na mwanaume wa kawaida, mwenye tabia njema na mcha Mungu asiwe tajiri. Ikiwa tutamaliza masomo yetu, huyu tuliyempenda anafaa kuwa mume wetu.

Kihalisia tunatamani mwanaume mcha Mungu, mwenye upendo na ambaye atathamini utu wetu.

Mwandishi: Kwa nini hampendi kuolewa na tajiri?

Consolata: Ni kwa sababu matajiri wengi huwa wanathamini pesa zao sio utu. Samahani hapa sio matajiri wote, ila wengi wao kwa hiyo sisi tunataka mtu anayeweza kuthamini utu.

Mwananchi: Ndoa ni mume na mke mmoja kwa Wakristo. Mmewahi kutafakari hilo?

Consolata; Ndio, Biblia inasema kwamba Mungu aliweka agano kati ya mume na mke mmoja. Sasa kwa kuwa sisi tumeungana wawili na tuna hisia moja, hatuwezi kuolewa na wanaume tofauti. Tutaolewa na mume mmoja.

Tunatamani sana kumtumikia Mungu kupitia sakramenti ya ndoa. Mungu akitujalia tumalize masomo yetu basi tunataka kuolewa ili tumtumikie Mungu katika huo wito vizuri.

Pacha hao waliweka bayana jina la kijana waliyempenda, ingawa kwa sababu za kimaadili tunalihifadhi. Hata hivyo, baba mdogo wa kijana huyo alikuwa tayari kuzungumza na gazeti hili.

Baba huyo mdogo alisema ana taarifa za kijana wao kupendwa na pacha hao.

“Unajua nilishangaa kuona watu wananiita baba mkwe wa akina Maria na Consolata. Baadaye ndio nikajua kuwa kuna mahusiano baina yao (kijana na mapacha hao), japo wote wanaendelea na masomo. Kupenda ni moyo na kama ikitokea wakafikia ndoto hizo huko baadaye, basi itakuwa hivyo,” anasema.

Mwalimu mkuu wa Shule ya Maria Consolata, Jefred Kipingi anasema hisia za kuolewa kwa mabinti hao ni jambo la kawaida na kwamba, wanapenda kuishi maisha ya kawaida kama walivyo watu wengine.

“Uzuri wake ndoto yao ni kuwa walimu na wanasema wataolewa wakishamaliza masomo yao. Jambo hilo ni jema na hapo Mungu ndipo atadhihirisha utukufu wake zaidi,” anasisitiza.

Ingetegemewa kwamba katika dunia ya utandawazi, taarifa za kuzaliwa kwa pacha walioungana zingetapakaa kila mahali zikipamba magazeti, redio, luninga na hata mitandao ya kijamii.

Lakini haikuwa hivyo kwa Maria na Consolata. Hakuna chombo chochote kilichopata taarifa ya kuzaliwa kwa pacha hao wa kipekee.

Ulemavu wao ulisababisha wafichwe hadi walipofikisha umri wa kuandikishwa elimu ya msingi katika Shule ya Ikonda na kutafutiwa mlezi wa kuwaangalia, baada ya wazazi wao kufariki dunia wakiwa wadogo.

Habari zao zilianza kufahamika baada ya kuandikishwa darasa la kwanza na kutafutiwa mlezi aliyewalea hadi wakati walipofaulu vizuri mitihani yao ya darasa la saba mwaka 2010.

Mlezi wao, Bestina Mbilinyi alikuwa alifanya hivyo chini ya wamisionari lakini, alikuwa akiishi nao nyumbani kwake Ikonda.

“Niliombwa niishi na watoto hawa kwa sababu kutoka kwangu hadi shuleni sio mbali, nilijengwa choo kinachokidhi maumbile yao na niliishi nao hadi wanamaliza darasa la saba,” alisema wakati akizungumza na Mwananchi wakati walipomaliza darasa la saba.

Baadhi ya wakazi wa mikoa ya Iringa na Njombe wanasema kama watoto hao wasingelelewa chini ya misheni huenda wangepoteza maisha yao au kuuawa kwa imani finyu kuhusu watu walemavu.

Mmoja wa wananchi hao Richard Ndendya mkazi wa Kidabaga anasema mara nyingi walemavu wamekuwa wakichukuliwa kama mkosi kwenye jamii, hivyo huenda kama wasingezaliwa misheni wangepoteza maisha yao aidha kwa kuuawa kutokana na imani finyu au kufariki kawaida, kwa kukosa huduma sahihi.

“Tena tunashukuru Mungu kwa sababu wamisheni waliamua kuwalea watoto vinginevyo huu ushuhuda tunaoupata hivi sasa tusingeupata ushuhuda huu tunaouona,” anasema.

Anasema wanakila sababu ya kulishukuru kanisa la Roman lililojitolea mhanga tangu mwanzo kuwatunza watoto hao ambao leo hii wanaliletea taifa sifa ya kipekee.

Mkazi mwingine wa Kilolo, Eda Kihongozi anasema Tanzania ina kila sababu za kujisifia na kuandaa mazingira mazuri zaidi kwa mapacha hao kufikia ndoto zao kimaisha.

Wanavyolala usiku

Kutokana na namna walivyoungana, ikiwa mmoja atalala kabisa basi mwingine kichwa chake huwa juu juu hivyo hulazimika kuwekwa mto mkubwa ili aweze kuegamea.

“Tunaweza kulala kwa aina nyingi. Anaweza kutangulia Maria mimi nikawa juu au tukabadilishana,”anasema.

Chumbani kwao kuna redio. Kwa kuwa hawapendi kupitwa na jambo lolote linaloendelea nchini na duniani kwa ujumla, huwa wanaiacha redio yao hewani usiku kucha.

Kuungana kwa baadhi ya viungo vyao kumewafanya wapendane zaidi, tofauti na pacha wengine.

Kila mmoja anamuhisi mwenzake, na hilo limewafanya wafurahi na kuhuzunika pamoja.

Chumba wanacholala ni kisafi wakati wote, na wao wenyewe ndio watu wanaosafisha ikiwa ni pamoja na kutandika kitanda kwa ustadi.

Maisha yao

Kiujumla wanaishi maisha ya mazuri kwenye kituo chao cha Nyota ya Asubuhi.

Maria na Consolata wanasema maisha yao ni ya kawaida kama ilivyo kwa watu wengine na kwamba, wanafurahi kulelewa kituo hapo kwa kuwa licha ya kupewa mahitaji yote muhimu, wanapendwa.

Maria anasema hawana wasiwasi kutokana na malezi bora wanayopewa na kikubwa zaidi ni kufundishwa kumcha Mungu.

“Tuna kila sababu za kumshukuru Mungu na masista wanaotulea kwenye kituo hiki kwa kuwa wao ni sababu ya sisi kuishi na kufikia hatua hii kubwa kielimu,” anasema Consolata.

Kwenye nyumba yao waliyojengewa, yupo dada anayewalea, Fransisca Mlangwa, ambaye anasema hajawahi kujuta kuwa mlezi wao.

“Inapotokea wapo mbali nami huwa nawakumbuka, nawaona kama wadogo zangu wa kuzaliwa. Hawa ni mabinti wa kipekee kwa kweli, sijawahi kununa nikiwa nao, mara nyingi huwa wananichekesha na ninaona fahari kuwa mlezi wao,” anasema.

Francisca ni mwanafunzi anayesomea masuala ya mifugo kwenye kituo hicho.

Maria anasema nyumba hiyo imewekwa miundombinu yote muhimu inayowafanya wajisikie vizuri wakati wote wanapokuwa nyumbani.

“Tuna TV na simu ya mkononi ya kisasa hivyo tunasikia na kupata habari mbalimbali zinazoendelea nchini,” anasema Consolata.


Chanzo: Mwananchi



 
dah jamani ninawaza sana juu ya uumbaji wa Mungu, niliwahi kusoma sehemu wakisema wangependa kuolewa na mwanaume mmoja tuu mwenye upendo wa kweli mmh nikaona aisee itakuwa tabu sana itakuwaje hasa wakihitaji kuzaa je itakuwaje?
 
Allah Akbar.
Mimi huwa najiuliza tu, akifa mmoja itakuwaje?
Mwenzie pia atakufa au itakuwaje?

Naamini watoto walioungana kama hawa wanazaliwa wengi sana, ila kwa imani potofu zilizotujaa wengi huuwawa wakiwa angali wachanga.
 
Allah Akbar.
Mimi huwa najiuliza tu, akifa mmoja itakuwaje?
Mwenzie pia atakufa au itakuwaje?

Naamini watoto walioungana kama hawa wanazaliwa wengi sana, ila kwa imani potofu zilizotujaa wengi huuwawa wakiwa angali wachanga.
wanakufa wote kwa sababu kuna organs zingine wanakua wanashare so ni ngumu mmoja kusurvive pindi mwenziwe akiaga dunia
 
Allah Akbar.
Mimi huwa najiuliza tu, akifa mmoja itakuwaje?
Mwenzie pia atakufa au itakuwaje?

Naamini watoto walioungana kama hawa wanazaliwa wengi sana, ila kwa imani potofu zilizotujaa wengi huuwawa wakiwa angali wachanga.
Hili swali hata mimi najiulizaga ila naishia kuona chenga tu, yapo maswali mengi ya kujiuliza ila Mungu ndio anajua.
 
wanakufa wote kwa sababu kuna organs zingine wanakua wanashare so ni ngumu mmoja kusurvive pindi mwenziwe akiaga dunia
Mungu Mkuu sana aisee. Ila mmoja akifa na mwingine atakufa kwa sababu maiti lazima apelekwe mortuary baadae akazikwe. Mungu apishe mbali siku hiyo ikbidi wafe wote kwa wakati mmoja maana atakayekufa baadae sijui mateso atakayoyapata mwilini na rohoni. Mungu keshaweka utaratibu kabla hawajazaliwa ila kibinadamu itabidi aliyehai nae aupate umauti tu kwa namna yoyote maana hawezi kuwa anaoza halafu mwingine analala nae.
 
wanakufa wote kwa sababu kuna organs zingine wanakua wanashare so ni ngumu mmoja kusurvive pindi mwenziwe akiaga dunia
Sio lazima wafe wote siku moja. Inategemea wanachangia viungo gani.

Unajua MTU hufa nini kati ya ubongo na moyo?
Kawaida mtu hufa ubongo, ndo maana babu zetu hukagua kama mtu amekufa kwa kuvuta nywele za utosini.
Kama ubongo umekufa, nywele hunyofoka upesi.

Naongelea natural death
 
Sio lazima wafe wote siku moja. Inategemea wanachangia viungo gani.

Unajua MTU hufa nini kati ya ubongo na moyo?
Kawaida mtu hufa ubongo, ndo maana babu zetu hukagua kama mtu amekufa kwa kuvuta nywele za utosini.
Kama ubongo umekufa, nywele hunyofoka upesi.

Naongelea natural death
wale wameungana tumbo kama mmoja ikatokea amefariki unadhani huyo mwingine ataishi kwa muda gani?!!
 
ILA natamani wakate roho kwa wakati mmoja sababu kukaa na mwenzio kafa duh itaumiza,.. ila Mungu ndiye anayejua
Huyo mwingine atakufa kwa sababu ya loneliness na mawazo ya mwenziwe au mmoja akifa mwingine hawezi kuishi hata kumtenganisha itakuwa ngumu

Maan kuna wale walikuwaga wameungana halafu wakubwa nchini kama Sio Sri Lanka basi ni Indonesia waliweza kuishi kwa muda wa miaka 28 wakawa walikufa theatre room Operation kubwa kuwahi kutokea duniani n madaktari bingwa walikua wanajaribu kuwatenganisha.
 
Back
Top Bottom