Lowassa atafufuka kweli?

Lowassa atafufuka kweli?

sifa ulizompamba zimefuta ubaya wooote unaojitahidi kutuaminisha, Lowasa ni msafi kama theluji uchafu huo mnaouorodhesha ni halali yake JK MRISHO,DR & PROF.ANAYEMALIZA NGWE YA NNE AKIWA CHOKA MBAYA.
 
aliekufa akafufuka ni yesu wa mariam peke yake huyo mamvi pangeni jinsi ya kwenda kuustiri mwili wake
 
Masikini pole yake lowasa aliwekeza kuliko na kauli zake za mwanzo
 
Mheshimiwa Edward Ngoyayi Lowasa ndio jina lililoteka hisia za wachambuzi wa mambo kwa kiasi kikubwa na hivyo kupata umaarufu mkubwa zaidi kuliko mwanasiasa yeyote katika siasa na wanasiasa wa Serikali ya awamu ya nne nchini Tanzania. Lowasa ameanza kuzungumzwa toka kipindi kile cha kusuka mtandao wa Kasi mpya, nguvu mpya na ali mpya, na baadaye akayakoroga na kutumbukia katika kashifa za Richmond, hadi sasa yuko katika mbio za kuusaka urais wa Tanzania. Jina la Edward Lowasa ni bahari ya habari.

Watu wengi wameandika na kusema mengi juu ya Lowasa. Leo ni zamu yangu kusema (japo kwa jumlajumla) machache juu ya mtu huyu anayesemwa kuutaka urais kwa gharama yoyote. Nianze na sifa nzuri za Lowasa. Lowasa alikuwa ni kiungo mhimu mno katika Serikali ya JK, kama ni gari basi ni injini. Hata kuyumba na kulegalega kwa Serikali ya JK inasemekana ni kwa sababu ya kuanguka kwa Lowasa. Lowasa alikuwa ni chachu ya ushindi wa kishindo wa JK katika uchaguzi mkuu wa 2005.Ndiye yeye aliyesuka na kusimamia kisayansi mtandao wa ushindi. Ni Lowasa huyuhuyu anayeweza kuusambaratisha mtandao huo akiamua.

Lowasa ana kila sifa za kuitwa a modern and strategic politician.Lowasa ana nguvu, haiba, mvuto na ushawishi wa kisiasa pengine kushinda wanasiasa wote walio katika mfumo sasa hivi Afrika Mashariki na Kati.Sioni wa kushindana naye katika sifa hizo Lowasa ana ubunifu wa hali ya juu katika uongozi.Hii inadhihirishwa na kuchukia viongozi wanaoendesha mambo kwa mazoea (business as usual).

Lowasa pia ni muibuaji mzuri wa misemo na vibwagizo vya kisiasa ambavyo hupumbaza wananchi. Sote tunakumbuka alipolaani tabia ya kumwambia mtu ‘pole na kazi.’ Lowasa alipendekeza watu wawe wanasema “Hongera kwa kazi”. Kasi mpya, nguvu mpya na ali mpya. Maisha bora kwa kila mtanzania. Hii yote ni kazi ya Lowasa.

Lowasa ni mchapa kazi hodari, mtendaji makini,na mwajibikaji asiye na mfano.Lakini ni kiongozi asiyeisema vibaya rushwa. Inasadikika hata alipokuwa Waziri mkuu alichukia zaidi uzembe au ugoigoi kazini kuliko rushwa. Hii inaashiria kwamba mbele ya Lowasa mtu aweza kuwa mla/mtoa rushwa alimradi ni mchapa kazi hodari. Kumbukumbu zinaonesha kwamba Lowasa hakuwahi kuwakemea wala/watoa rushwa bali alikuwa akiwakoromea mara kwa mara watumishi wanaofanya kazi kwa mazoea.

Lowasa ana mbinu za kisayansi za kukusanya na kutengeneza mtaji (scientific means and strategies for capital accumulation). Ni yeye anayejua hasa ni wapi hela za kampeni katika uchaguzi mkuu wa 2005 zilikotoka. Ndio maana Lowasa anatembea kifua mbele akijinasibu kwamba ana dawa ya tatizo la ajira kwa vijana nchini.

Lowasa ni jemadari asiyekufa kwa risasi moja! Ni mpambanaji asiyewaza kushindwa.Kutwa nzima anashinda na usiku mzima anakesha akiwaza namna ya kushinda. Lowasa alizaliwa kupambana na kushinda.Tangu kipindi cha Mwalimu Nyerere, Lowasa aliwekewa vizingiti lakini mwisho wa siku alishinda.

Lowasa ni kiumbe wa kuthubutu kufanya mambo makubwa hata yaliyo nje ya uwezo wake.Katika hili Lowasa ni mchwa, kiumbe anayethubutu kutafuna hata jiwe.Tabia moja husababisha nyingine. Lowasa ni jasiri asiyeogopa kitu au mtu yeyote.Tabia hii imesababisha baadhi ya watu waseme: “Lowasa hana hata hofu ya Mwenyezi Mungu.”

Katika mchakato wa Uchaguzi wa Urais wa 1995, Mwalimu alimuonya Lowasa na wenzake, “Ikulu sio mahala pa kukimbilia” lakini Lowasa hakuhofia onyo hilo. Ndio kwanza alianza kujipanga kwa kusuka mtandao wa ushindi.

Kabla sijaendelea mbele naomba nikiri kwamba, Lowasa ni jabari. Lowasa ni mahiri wa siasa. Lowasa ana akili ya kufanya siasa safi na chafu. Kama umetumwa kushindana naye, itabidi ujipange, tena ujipange sana. Kama vipi yakupasa uchimbe kaburi lako kwanza ndio uingie katika ulingo wa mapambano.

Lowasa ni mwepesi wa kusoma uzito na mwelekeo wa upepo wa masuala. Ni mwepesi vilevile wa kufanya maamuzi na kuchukua hatua juu ya masuala au matatizo yanayowakabili wananchi. Tabia hii huwapa faraja wananchi hata kama hakuna kilichobadirika.Sote tunakumbuka siku mheshiwa Lowasa alipopaa kwenda Thailand kutafuta watalaamu wa kutengeneza mvua.

Kitu kingine kinachombeba Lowasa ni umahiri wake katika fani ya mashairi. Lowasa hutoa hotuba zake kwa vionjo vya kimashairi. Kwa mtindo huu, ni rahisi mno kwa Lowasa kuteka hisia na mawazo ya wasikilizaji. Hata wabaya wake hujikuta wamelainika baada ya kumsikiliza Lowasa.Siasa ni mchezo wa kucheza na hisia au akili za watu. Lowasa anauweza mchezo huo.

Kinachomponza Lowasa ni kuwa na uchu wa mafanikio katika nyanja zote za maisha – yaani kiuchumi, kisiasa na kijamii. Ana nguvu inayomsukuma siku zote kuwa namba moja katika nyanja hizo. Anatamani mwisho wa siku aitwe baba wa mafanikio.Hapo ndipo hata baba wa Taifa alihitilafiana na Lowasa. Enzi hizo za siasa za ujamaa na kujitegemea, Lowasa alionekana kama kijana mbinafisi anayependa kujilimbikizia mali. Kuna wakati Mwalimu alitahadhalisha, “Huyu ni kijana wa kwenda naye kwa umakini sana.” Lakini enzi za leo ni za siasa za Kipepari ambapo mwenye mali nyingi ndio kila kitu.

Kitu kingine kilichomponza Lowasa ni kuacha ama kwa makusudi mazima au kwa njia yoyote ile vidole vyake vikachovya damu ya Richmond.Ni dhahiri kwamba tuhuma za kuhusika na kampuni feki ya kufua umeme ya Richmond zilimchafua sana Mheshimiwa Lowasa - ni vigumu kumsafisha.

Baada ya kubainishwa na kamati teule ya Bunge kwamba Kampuni ya Richmond, iliyokuwa ikilipwa mamilioni ya shilingi kwa siku, ilikuwa ni utapeli mtupu, wananchi wengi wamebaki na maswali lukuki vichwani mwao.Watu wakawa wanajiuliza: Kumbe mheshimiwa Lowasa ni mbinafisi hivi? Kumbe Mheshimiwa Lowasa hana huruma kiasi hiki? Kumbe Mheshimiwa Lowasa ni tapeli hivi? Kumbe Mheshimiwa Lowasa ni mhuni hivi? Kumsafisha Lowasa ni pamoja na kujibu maswali haya.

Hata staili yake ya kujiuzulu nayo haikuwapendeza watu wengi. Ilizidi kumchafua badala ya kumjenga. Bado naikumbuka sana siku hiyo. Siku hiyo Lowasa alikuwa na gahazabu na jaziba kali mno. Alifoka utafikiri Volcano za Mlima Oldonyo Lengai.Uamuzi wa kujiuzulu ulikuwa wa busara mno. Laiti kama angelitumia busara hiyohiyo na kuwa muungwana na mnyenyekevu mbele ya watanzania wakati wa kuwasilisha hotuba yake ya kujiuzulu, Lowasa angelihurumiwa na kila mtu.

Aliposimama kujibu mapigo, mimi ningemshauri aanze hivi: Ndugu zangu watanzania, maji yakishamwagika hayazoleki. Kuteleza si kuanguka.Napenda niweke wazi kwamba kuhusika kwangu katika Kampuni ya Richmond lilikuwa ni jambo la kuteleza kimaamuzi. Nimesikitika sana kuona kwamba kamati teule haikunipa hata dakika moja ya kusema ninayoyajua kuhusu Richmond lakini walipata mda wa kwenda Boston – Marekani kusaka ushahidi…Naomba niwajibike hata kama mhusika mkuu hakuwa mimi ili kulinda heshima ya Serikali ya chama changu! Kwa bahati mbaya sana Lowasa hakuomba ushauri, na kama alishauriwa basi alishauriwa vibaya.

Lowasa aliishia kulalamika kwamba ameonewa, hajaulizwa, mara hajatendewa natural justice.Kwa maneno yake Lowasa alilalamika: “...nimefadhaika sana, nimedhalilishwa sana, nimeonewa sana katika hili.” Na alijiuzulu huku akitamka: “Nimeamua kumwandikia Rais barua ya kumwomba niachie ngazi.” Maneno hayo “niachie ngazi” yalitafsiriwa kama ya ‘ukichwangumu’ zaidi kuliko uungwana.Wakati huo wanamtandao watiifu waliokuwa wamekunywa damu ya Lowasa na kuapa kufa naye, na waliokuwa wameonja ladha ya matunda ya mtandao, walikuwa wakibamiza meza zao kwa kushangilia kila alichosema Lowasa.

Kumbukumbu ya kashifa za Richmond bila shaka ni kumbukumbu mbaya sana kwa mheshimiwa Lowasa (a haunting experience).Ni kumbukumbu ambayo ilimtesa sana Edward, na ambayo yaweza kuendelea kumtesa yeye na kizazi chake kwa siku za usoni.Kwa sasa Edward walau amepona kidogo na asingependa akumbushwe ya Richmond. Lakini mimi naomba nikumbushie kidogo. Hata hivyo natanguliza samahani kama nitamkwaza mheshimiwa Lowasa.

Kumbukumbu zangu zinaanzia tarehe 13 Novemba 2007 pale bunge la tisa chini ya Spika Samwel Sitta lilipolidhia kuundwa kwa kamati teule kuchunguza mchakato wa zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura uliofanyika mapema 2006.Mwenyekiti wa kamati ile ya kihistoria alikuwa ni mheshiwa Harrison Mwekyembe. Jioni ya siku ile, mara baada ya spika Sita kuliahirisha Bunge lililolidhia kuundwa kwa kamati teule ya Bunge, kikundi cha mawaziri waliokuja kujulikana baadaye kama mafisadi wa Richmond, kilionekana na nyuso za taharuki (worried faces). Waziri mmoja alimuuliza Lowasa, “Vipi tutatoka hapa kweli mheshimiwa?” Lowasa alimjibu Waziri yule bila kumwangalia usoni, “hawa ni wachache mno.” Jibu hilo la Lowasa liliashiria jambo moja; alikuwa amejipanga kiustadi na mbinu za kisayansi kuituliza na kuimeza tume huru ya bunge.

Kwa bahati nzuri au mbaya akina mwakyembe walilijua hilo mapema maana wanamjua Edward, mtu mahiri katika mikakati, mweledi, na zaidi ya yote jasiri asiyekubali kushindwa kirahisi.Kwa hiyo walimchunguza Lowasa kwa kimyakimya staili – hawakutaka kubwabwaja kwa kila mtu. Waliamini katika misemo ya Kiswahili; Simba mwenda pole ndio mla nyama.Ukitaka kumuua nyani usimwangalie usoni.

Baada ya mikikimikiki ya kubaini nani ni nani katika zabuni ya kuzalisha umeme hatimaye ukafika wakati wa kamati teule kuwasilisha taarifa yake bungeni.Kamati teule bila ya kutafuna maneno iliweka wazi kwamba Lowasa hawezi kukwepa kashifa za kuipendelea na kuiwezesha kampuni hewa ya Richmond Development LLC kuingia mkataba wa kuzalisha umeme nchini Tanzania.Tuhuma zote zilielekezwa kwake mheshimiwa Lowasa, kwamba alikuwa ndiye injinia wa mipango na mikakati ya uwepo wa Richmond.

Baada ya kuwa Mwakembe ameharibu kila kitu kuhusu Richmond, ukafika wakati wa Lowasa kujibu mapigo. Bila shaka huu ulikuwa wakati mhimu sana kwa Lowasa – kila mtu ndani ya bunge alikuwa kimya, nchi nzima ilikuwa kimya ikisubiri kwa hamu atasema nini Lowasa.Ni wachache waliobashiri atasema nini Lowasa. Yawezekana ni watu wawili tu walikuwa wanajua nini Edward atasema asubuhi ile; Regina na JK. Maana mshituko wa Samwel Sitta ulionesha waziwazi kwamba hakujua. “Tamko hilo ni zito sana, na sikutegemea. Sasa ningeomba ushauri tuendeleeje?” alisikika Sitta.

Edward alianza kuongea taratibu huku akichagua maneno kwa umakini mkubwa. Mwanzoni tu mwa hotuba yake, Edward alimpongeza kinafiki Mwakyembe: “Nimpongeze Dr. Harrison Mwakyembe, mwenyekiti wa kamati teule kwa kuwasilisha kwa mbwembwe nyingi sana taarifa yake, mbwembwe zilikuwa nzuri kweli.” Ukimwangalia usoni, Mheshimiwa Lowasa alikuwa amebadirika kabisa – alikuwa amebeba uso mzito uliojaa hasira, ghazabu, jaziba na majuto kwa mbali. Ukivichanganya vitu hivi sijui unapata kitu gani? Sijawahi kumuona Edward katika sura ile. Ukimuona mtu mweupe anabadirikabadirika rangi kama kinyonga ujue kuna jambo zito linamsibu.

Asubuhi ile ya tarehe 7 Februari 2008 baridi ilitawala bungeni. Baridi iliwatafuna hasa wanamtandao walioshuhudia Lowasa akisurubiwa bila huruma. Haikuwa rahisi kwao kuamini kirahisi. Nyuso zao hazikuwa tofauti na za waombolezaji. Tunaambiwa kwamba Wiki nzima wafuasi watiifu wa Lowasa walienda nyumbani kwake kumpa pole. Lakini Edward aliwajibu tofauti na walivyofikiria: “Msinililie mimi, bado sijafa. Jililieni ninyi na nafsi zenu” Jibu hilo la Lowasa lilikuwa na maana moja tu; Lowasa aliamini alikuwa bado na nguvu ya kupambana na kurejea kileleni.Maana, bila kupoteza mda, Edward alionekana akihaha kujisafisha kwa juhudi kubwa.
Inasadikika ni watu wa dini waliomuonya Edward, “tulia mheshiwa, utachafuka zaidi ya hapo kama utakurupuka…..” Mimi naona waliomshauri hivyo walifanya jambo jema sana.

Kwa upande mwingine wabaya wa Lowasa walikesha wakisherehekea kuanguka kwake. Walimmiminia sifa kedekede mwenyeketi wa kamati teule. Miongoni mwao walikuwa mwendo wa kinyonga kazini ambao Lowasa aliwahi kuwachachafya. Waliamini kwamba Richmond imemzika katika kaburi la chuma, na kwamba asingelifufuka kabisa. Na hata kama angefufuka basi asingefurukuta kutoka. Nionavyo mimi, waliodhani Lowasa amekufa kisiasa walijidanganya.

Kiuhalisia, Lowasa anafufuka, anachipua, na anajiandaa kuruka mbali zaidi ya hapo alipokuwa. Hata wapinzani wake ambao amefanikiwa kuwavuruga na kuwasambaratisha, wanalijua sana hilo.Maswali ya kujiuliza ni, je, Lowasa akishatoka itakuwaje? Atawasamehe wabaya wake? Swali jingine ni, je, wabaya wa Lowasa ndani ya CCM wakibahatika kushika dola itakuwaje? Watamrudisha Lowasa kaburini? Tusubiri.

angeweza kupata nafasi akapiga magwanda mbona angewamaliza.
 
Tunavyomuweka Lowasa kwenye Kashfa ya Richmond hakika tunamuweka Magufuli kwenye kashfa ya uuzaji wa n yumba za Serikali!!
kitu ambacho bado ni mwiba mkubwa. Ambao bado unauma tukijaribu Watanzania kutembea
 
Ningekuwa mm ningetumia michuzi mingi kuwashawishi wapitishaji wa mwisho;Maana kwa historia ya nchi hii,alopitishwa ndo mshindi

Haya maneno hautayakana kwamba sio yako? Magufuli sasa hivi ni kama kifaranga kimekoswa na mwewe!
 
Jemedari asiyekufa kwa risasi moja, kama na hili pigo utajaribu kufufuka comred wangu basi mimi simo kwenye ufalme wako. Pumzika kwa amani...

Aisee, mduawo kama si mshangao. Nitadandia chopa hata kwa mbele. Come what may. Hakuna namna nyingine kama Lema anakuita Rais itakuwa mimi niliyekuandika vyema hivyo. Hata kupanga mafaili ya ikulu tu itatosha!!!
 
Back
Top Bottom