Loliondo ilivyowatia simanzi Wabunge | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Loliondo ilivyowatia simanzi Wabunge

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Dec 10, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Dec 10, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,449
  Likes Received: 81,496
  Trophy Points: 280
  Loliondo ilivyowatia simanzi Wabunge
  Imeandikwa na Shadrack Sagati; Tarehe: 7th December 2009 @ 07:16

  Habari Leo

  BINADAMU tumetofautiana kwa hulka na silika, wakati wananchi wa Loliondo waliofika mbele ya Kamati ya Bunge kutoa vilio vyao, baadhi yao walisikitika kwa simulizi zao za kutia simanzi, lakini baadhi ya Wabunge pia walisikika wakisema waziwazi kuwa wananchi hao ni waongo.

  Moja wa wananchi aliyefika mbele ya kamati hii alianza kwa kujitambulisha mbele ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuwa anaitwa Kinyenjui Kimeliani mkazi wa Kijiji cha Sointsambu kilichoko katikati ya pori tengefu la Loliondo.

  Akisimulia tukio la kuchomewa moto alisema, "Ilikuwa Julai mwanzoni siku ya Jumamosi, wakaja askari wakiwa kwenye magari matano katika kitongoji chetu cha Keitalo huku magari yakiwa na bendera nyekundu.

  "Walifika katika boma langu wakamwaga mafuta kisha wakawasha moto, mimi na familia yangu tukakimbia kuokoa roho zetu. Tulishangaa hatua hiyo kwani hatukuwa na ugomvi wowote na Serikali lakini pamoja na kuwa na mawazo hayo maboma yaliendelea kuteketea chini ya usimamizi wa Polisi.

  "Sikupata muda wa kuokoa kitu chochote, vitu vyote viliteketea kwenye maboma hayo kikiwemo chakula ambacho tulipewa kama msaada na Serikali kitusaidie wakati wa njaa," baada ya maelezo hayo Mwenyekiti wa kamati hiyo Job Ndugai akakatisha maelezo ya mwanakijiji huyo.

  Ndugai: Nasikia nyinyi mlifukuzwa huko kwa vile mlikuwa mnachunga na kisha mlikuwa mnaendesha kilimo jambo ambalo haliruhusiwi eneo hilo.

  Kinyenjui: Tulilazimika kulima kule kwa vile DC Msangi (Mkuu wa Wilaya) aliyekuwepo miaka ya nyuma alituagiza kuwa kila mtu alime ekari mbili katika eneo analokaa. Ndugai: Huyo DC aliagiza mlime kote?

  Kinyenjui: Hicho kilimo tulikuwa hatuendeshi eneo la malisho, kilimo kina eneo lake.

  Ndipo alisimama mwanamke aliyejitaja kuwa anaitwa Ndangali Najani ambaye anasema kwamba katika operesheni hiyo watu walioathirika zaidi ni watu wa kitongoji cha Keitalo ambacho anadai kuwa maboma 12 yalichomwa moto.

  "Sisi wanawake ndio tunaopata tabu kutokana na kuchomewa maboma yetu, angalia kwa sasa tunaishi chini ya mti na tunapikia chini ya mti.

  "Kwa kweli nilitamani niwaue wale vijana walichoma nyumba yangu, nilichanganyikiwa sana kutokana na tukio lile, sijui ninyi kamati ya Bunge mtatusaidiaje, lakini sina imani na ninyi yawezekana mmekuja kutuziba macho.

  Angalieni tumefukuzwa kwenye ardhi yetu, hatuna ardhi, hatuna ng'ombe na hatuna maziwa mwaka huu…na hiki ndicho chakula chetu tutaishije?

  "Mimi ni mwanamke wa Tanzania najiuliza kwa nini nichomewe nyumba yangu? Kwa kweli sitakubali tena kuteswa namna hii tena, hii ni ardhi yangu nitafia hapa hata kama watakuja kunipiga na mabomu siondoki tena.

  Sandeti Leya ni Leigwanani wa kijiji hiki cha Sointsambu chenye vitongoji saba, naye anapewa fursa ya kuelezea yaliyowakuta wake zake wakati wa operesheni ya kuwahamisha kutoka katika eneo la uwindaji.

  Katika maelezo yake anasema, "Ng'ombe ni wangu na watu ni wangu, wote hawa wameshambuliwa na moto, tukalazimika kuhamisha mifugo kutoka huko malishoni, matokeo yake mifugo yetu imekufa kwa wingi kutokana na kukosa malisho.

  "Mimi kama Leigwanani nilishituka na operesheni ile, nilihoji watu wangu kufa kama ng'ombe walivyokufa baada ya operesheni.

  Kwa ufahamu wangu kijiji hiki ndio kwetu na tumezaliwa hapa, tangu 1959 tulivyohamishwa kutoka Serengeti.

  "Mwaka 1972 OBC walikuja kuwekeza hapa, walikuwa marafiki zetu hatukuwa na shida nao kwani yule Mkurugenzi wa kwanza aliyekuwepo (Akamtaja kwa jina la Mohamed) alikuwa anaongea na sisi wanakijiji mara kwa mara.

  "Mwaka 1999 Mohamed aliondoka akaja Mkurugenzi mpya, kwa kweli tangu wakati huo hakuna maelewano, tumekuwa tunavurugana na hakuna amani tangu kipindi hicho jambo mbalo mimi naona si zuri.

  Kwa hiyo nyinyi Wabunge msiondoke bila kutuachia amani, kama mnashindwa tuchukueni tupelekeni kwa Rais.

  Ndugai: Wewe mzee wa kimila, unataka kumwona Rais, je, ukibahatika kukutana naye, utamweleza nini Rais wako? Leigwanani: Tutamweleza hali halisi Rais wetu jinsi tunavyonyanyasika ndani ya ardhi yetu.

  Kiteto Mako ni mwanamke mwingine anayejitokeza mbele ya kamati hii kueleza yaliyomsibu. Yeye ni mkazi wa kitongoji cha Mwandosi na anasema kwamba hajui idadi ya maboma yaliyochomwa kwani ni mengi katika eneo analoishi.

  "Wakati tunachomewa tuliamini kuwa baba yetu ni Serikali wangekuja kulia pamoja na sisi katika shida hii, lakini hakuna kiongozi yeyote kutoka wilayani aliyekuja kutupa pole.

  "Tumekuwa kama yatima ndani ya nchi yetu, tumekuwa kama wanyama kwani hakuna aliyejali shida yetu tuliyopata…tunaamini kuwa tungekuwa ni watu basi wangefika viongozi wetu kutufariji.

  Naye Losingo Eliada anasema wakati askari hao wanafanya operesheni pia walichukua mbuzi wake na kuondoka nao kwenye gari, hajui walikopeleka hao mbuzi na walichoenda kuwafanyia.

  "Baada ya kuchukua mbuzi wangu walinipiga huku wakiniambia kwamba mimi ni Mkenya na wakahoji kwa nini nalima mashamba eneo hilo nami nikawajibu nafanya hivyo kwa vile kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu," anasema Eliada.

  "Sisi akina mama tumeumia sana kwa kutuchomea nyumba zetu, watoto wetu wamehangaika pamoja na sisi na wameshindwa kwenda shule kwani sare zao ziliungulia kwenye maboma yaliyochomwa, lakini watoto wa mwekezaji kutoka Dubai (OBC) wananufaika na rasilimali yetu.

  "Huko tulikofukuzwa ndiko mategemeo yetu na mifugo yetu, kamwe hatutakubali kuondoka na tuko tayari kufia huko kwani hii ni ardhi yetu. Mzee Olkosikos Yiele alichomewa maboma tisa na anadai kwamba ndama wake 90 walipotea pamoja na watoto wa mbuzi 40.

  Anasema binti yake mimba iliharibika na wakati wanachoma moto boma lake walipiga risasi juu hali iliyowafanya watoto na wajukuu zake kukimbia na kutokomea porini na mmoja wa binti zake aliyekuwa mjamzito mimba ilitoka.

  "Pale nilipochomewa ndipo nilipozaliwa, wazazi wangu na mababu zangu walifia pale na wamezikwa eneo hilo. Nami nataka niwaambieni nyie wabunge kwamba nikifa nitazikwa pale ambako nimefukuzwa na polisi.

  "Katibu tawala alikuja siku moja akanitaka nihame eneo hilo, nami nikamwambia kama anataka nihame aniandalie makazi mapya kabla ya ya kuhama. Hivyo nilimgomea kwa vile hakuniambia kwamba kuna mahali ameniandalia pa kwenda kuishi.

  "Baada ya kugoma kuhama siku chache wakaja polisi wakanichomea maboma yangu pamoja na nyumba zangu tatu za bati na zile za mila jumla yake ni nyumba 23.

  "Pamoja na unyama huu wa kuchomewa, bado naishi eneo hilo nimegoma kuondoka kwani ni nyumbani kwangu siwezi kuhama kwa sababu mwekezaji hataki kuniona.Nitaendelea kuishi huko na kulima kwani sitakubali watoto wangu wafe kwa njaa, na nyinyi wabunge naomba mniokoe kwa vile sina pa kwenda," anasema Mzee Yiele.

  Mzee mwingine aliyesimama kuelezea kadhia waliyopata wakati wa operesheni hiyo ni Kilusu Koipa ambaye anasema wamechomewa nyumba na vijana wanaume (polisi) tena kwa makusudi.

  Katika simulizi lake anasema boma lake lilikuwa na nyumba 12 "Wakati nikiwa nje mara nikaona wanaume wanakuja na magari mengi huku wameshika bunduki.Kufika wakaniamuru nitoke nje mimi na familia yangu.

  "Kuona hivyo nikashika majani (kimila kushika majani ni kutoa ombi wasifanye uchomaji huo) kuwaomba wasichome maboma yangu hadi nimalize sherehe ya kimila niliyokuwa nayo katika familia yangu. Hata wake zangu walitoka ndani wakawalilia wasiwachomee hadi wamalize sherehe hiyo.

  "Siku hiyo walichoma kidogo maboma, wakaingia na tochi kwenye nyumba zangu zingine wakatoka na kisha wakaamua kuondoka kurudi walikotoka.

  Kesho yake saa tatu asubuhi wakarudi wakaja na mafuta na wakayamwaga kwenye nyumba zangu zote.

  "Nilikasirika baada ya kuona nyumba zangu zinaungua, nilitaka kuingia kwenye ule moto ili nami niungue lakini mmoja wa watoto wangu wa kiume alinishika kwa nguvu nisifanye hivyo.

  Hivyo nikabaki mikononi mwa kijana wangu huku nikishuhudia maboma yangu yanateketea kwa moto.

  "Baada ya hapo nilitengeneza tena maboma sita, lakini walikuja tena wakayachoma moto na wakanitaka niondoke eneo hilo nami nikawaambia siondoki kwani hapo ndipo kwangu na watoto wangu.

  "Tukio hili la kuchomewa lilitushitua na hasa mke wangu mkubwa alichanganyikiwa akawa kichaa na akawa anakimbia ovyo huko msituni bila kujali kama kuna wanyama wakali.

  "Kwa sasa sina nyumba naishi chini ya mti, ninachowaomba nyinyi Wabunge mnirudishe pale kwangu ili niweze hata kukaribisha wageni wakija nyumbani kwangu. Kwa sasa sina pa kuishi wala sehemu ya kukaribisha wageni wangu.

  Hicho ni kilio cha kijiji kimoja tu cha Sointsambu ambacho wananchi wake walitoa yale wanayodai ni unyama waliofanyiwa na Polisi wakati wa kuwahamisha ili kuipisha kampuni ya OBC kufanya uwindaji ndani ya pori tengefu la Loliondo.

  Vilio vya namna hivi viko vingi katika vijiji vitano kati ya vijiji saba vilivyoko Tarafa ya Loliondo.

  Kiukweli simulizi zao ziliwatia simanzi baadhi ya Wabunge, lakini baadhi ya Wabunge waliwaona wananchi hao masikini kuwa ni waongo.

  "Huu ni uongo, wamefundishwa cha kusema hawa," alisikika Dk. Charles Mlingwa ambaye ni mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo wakiwa katika kijiji hicho cha Sointsambu.
   
Loading...