CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka serikali pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kufanya uchunguzi wa ufisadi wa kutisha wa zaidi ya Sh bilioni 1, uliofanywa na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, chini ya Mkurugenzi wake, Sara Linuma, ili wafikishwe katika vyombo vya sheria.
Fedha hizo zilitolewa na Serikali Kuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hali iliyowafanya madiwani wa halmashauri hiyo kuandika barua kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ili amhamishe Mkurugenzi huyo na kuamuru fedha hizo zilirejeshwe kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Turiani, wilayani Mvomero juzi jioni, Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye, alisema malalamiko ya wizi wa fedha hizo yamekuwa mengi na katu hayawezi kuachwa bila kuchukuliwa hatua zozote.
Nape alisema kuna baadhi ya watumishi wa Halmashauri nchini wamekuwa mchwa wa kutafuna fedha za umma ambazo ni mali ya walipa kodi ambao kila kukicha wamekuwa wakitegemea kupata neema ya maendeleo katika maeneo yao.
Awali Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Jonas Vanzeland, alisema kuwa uchunguzi wa awali ulifanywa na mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo na Tume iliyoundwa Januari mwaka huu umebaini jumla ya Sh bilioni 1.42 zimeibwa katika akaunti za halmashauri kwa awamu tofauti katika tawi la benki ya NMB Mvomero.
Alisema uchunguzi huo ulionesha kuwa siku moja Idara ya Uhasibu ya
Halmashauri hiyo ilitoa zaidi ya awamu 20 fedha kwa kutumia vocha tofauti za kughushi na kuzipeleka kusikojulikana.
"Takwimu zinaonesha sehemu ya fedha hizo zililetwa katika Halmashauri ya Mvomero kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, lakini badala yake zote ziliishia mifukoni mwa wajanja wachache.
"Mchanganuo wa fedha zilizoibiwa na wajanja wachache, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ni Sh milioni 290 zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi wilayani Mvomero, Sh milioni 300 za miradi ya kilimo, Sh milioni 83 za ujenzi wa barabara, Sh milioni 72 za ujenzi wa Daraja la Kisala lililopo katika Kata ya Sungaji na Sh milioni 400 za kodi ya uvunaji wa miti aina ya mitiki iliyopo katika wilaya yetu hii," alisema.
Vanzeland alisema hata kikao chao cha Baraza la Madiwani wameazimia kwamba hawamtaki Mkurugenzi huyo na kwamba tayari walikwisha muandikia barua Waziri Mkuu Pinda kuhusu suala hilo.
---
via gazeti la MTANZANIA
Source:
wavuti.com - wavuti