waliongozwa na Naibu Spika, Job Ndugai, wamependekeza kampuni ya BAE System iliyouza rada hiyo ya kijeshi kwa Tanzania ichukuliwe hatua za kisheria na serikali ya Tanzania, iwapo hadi Septemba mwaka huu haitakuwa imelipa faini ya Pauni milioni 29.5 kama ilivyoomba na kuamriwa na mahakama ya Uingereza.
Timu hiyo ya wabunge ilitoa mapendekezo hayo mjini hapa jana walipozungumza na waandishi wa habari, baada ya kukabidhi ripoti yao kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Ndugai alisema kamati inapendekeza kwamba hata kama mahakama nchini Uingereza imekwishafunga jalada la kesi hiyo, Tanzania inayo fursa ya kuwafungulia kesi watuhumiwa wote waliohusika kwenye sakata la rada kwa kulipa malipo ya kupitiliza wakiwemo wafanyakazi wa BAE System na Watanzania.
Alisema watuhumiwa hao wanaweza kufunguliwa kesi nje ya Uingereza ambako suala hilo limekwisha kuhitimishwa.
Ndugai alisema pendekezo lingine ni kufungua akaunti maalum ya kutunza fedha hizo hadi hapo mvutano baina ya serikali na BAE System utakapokwisha.
Alisema kimsingi, ujumbe wake umebaini kwamba iwapo Tanzania itapewa fedha hizo, itakuwa kama haikununua rada kwa kuwa chenji hiyo ni nyingi kuliko fedha iliyotumika kununua chombo hicho.
Alisema wameeleza msimamo wa Serikali wa kutaka chenji hiyo irudishwe serikalini badala ya mpango wa BAE System wa kutaka kuzipitisha kwenye asasi za kiraia za Uingereza kwa kuwa kufanya hivyo ni kulidhalilisha taifa.
Ndugai alisema: Fedha hii ikirudishwa ni kama tumepewa rada bure kwa sababu tulinunua kwa pauni milioni 28, lakini sasa zinarudi pauni milioni 29.5 na riba juu...lakini naomba ieleweke kwamba hatushabikii wizi wala hatujabariki wizi uliofanyika.
Alisema wakiwa nchini Uingereza, walikutana na maofisa wa Kamati za Bunge la Uingereza za Hesabu za Serikali; Maendeleo ya Kimataifa; Mabunge ya Jumuiya ya Madola; Naibu Spika; Naibu Waziri anayeshughulikia misaada, asasi ya Transparency International, BAE System pamoja na asasi za kiraia zinazoshirikiana na kampuni hiyo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Zungu, alisema walisimama kidete kupinga mkakati wa BAE System, msimamo ambao umeungwa mkono pia na Kamati ya Maendeleo ya Kimataifa.
Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Kimataifa inakubaliana na sisi na tumepata fursa ya kuwasilisha kwao malalamiko yetu juu ya jambo hili na tumepewa muda hadi Julai 12, yenyewe itapeleka mahakamani malalamiko yetu na mapendekezo ni kwamba ifunguliwe akaunti maalum fedha hizi zihifadhiwe huko hadi sisi (Tanzania) na BAE System tutakapofikia muafaka wa jambo hili, alisema.
Alisema wamebaini kuwa mahakama ya Southwalk Crown, ilitoa hukumu na kufunga jalada la kesi kwa njama za kiujanja ujanja ziliyotumiwa na kampuni ya BAE System.
Hata hivyo, alisema Uingereza pia imeandaa mdahalo wa wazi utakaowakutanisha BAE System, Tanzania, SFO, wabunge wa Uingereza, asasi ya Transparency International na wadau wengine, utakaofanyika Julai 19, mwaka huu nchini Uingereza.
Hata hivyo, alisema ripoti yao imeibwa kabla hata haijafikishwa kwa Spika.
Hawa wenzetu ni wajanja kweli wa kuiba taarifa sijui wanafanyaje, wamechakachua hata ripoti yetu. Alisema Zungu bila kutaja watu walioiba ripoti hiyo.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Angela Kairuki, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa timu hiyo, alisema safari yao ilikuwa na changamoto nyingi ikiwemo hoja ya BAE System pamoja na baadhi ya asasi za kiraia zinazotaka serikali ichukue hatua kwa Watanzania waliohusika kwenye kashfa hiyo.
Alisema kumekuwapo pia na takribani watu 20 wanaoonekana ni Watanzania wanaowasiliana na Mwanasheria wa BAE System kumwelekeza kwamba kampuni hiyo isipitishe fedha hizo serikalini.