ANAANDIKA Askofu Bagonza PhD
DUNIA BILA MUNGU na WAPINZANI BILA CHAMA
Ukipenda ubishi, jiepushe kuwa na hasira. Siku moja nusura nizichape na rafiki yangu Mwislamu. Akaniuliza; nyie Wakristo mnasema Yesu alikufa na kufufuka siku ya tatu? Nikajibu ndiyo. Akaongeza, “na mnasema Yesu ni Mungu kweli? Nikasema ndiyo. Akamalizia, “kwa hiyo Mungu wenu alikufa na dunia ikabaki bila Mungu kwa siku mbili?
Hasira zangu zikapanda. Mjadala ukaisha.
Ukweli ni kuwa, Dunia ilikuwepo, Ukristo ulikuwepo na Mungu alikuwepo. Mungu wetu ana nguvu hata kifoni. Natafakari:
1. Sasa tuna wapinzani wasio na chama. Hawa ni fursa au tumekunywa uji wa mgonjwa? Bora ukose nguvu lakini upate akili.
2. Wabunge, madiwani, wenyeviti wa vijiji na mitaa wa chama kilichopelekwa likizo bila malipo, wana uhalali wa kufanya kazi?
3. Polisi, madaktari, madreva, wahudumu wa mortuary na wapishi wa viongozi wenye itikadi ya upinzani moyoni, waende likizo pia? Mnafikiri hawapo? Mnanibishia? Kuna Mserikali mmoja kaniambia mkewe alihama chumba aliposikia kanisa la Ufufuo limefungiwa kufufua! Upinzani tunao mpaka bedroom.
4. Kwa nini tunatazamiana majibu? Aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama kilicho likizo, kama angesaini kanuni za uchaguzi, Msajili akaja kumtengua, sahihi yake ingetenguliwa? Kwa nini mahakama inapeleka chama likizo baada ya chama kufungiwa ruzuku? Mnafikiri hayana uhusiano?! Kalaghabao! Huu ni umoja wa mihimili.
5. Ukizaa watoto wanakufa, usiwahi kuwapa majina. Subiri wakuekue. Umezaa wa 1, kapelekwa jela kwa uhaini. Ukazaa wa 2, akafungiwa asishiriki uchaguzi hata kama alikuwa hataki. Ukazaa wa 3 akanyimwa ruzuku ya bill ya maziwa. Ukazaa 4 akazuiwa asicheze na watoto wenzake. Ukazaa wa 5, akazuiwa asitoke chumbani na ndoo ya kujisaidia kapelekewa huko. Huyu hatutamkuta amegeuka paka shume?
6. Mchakato wa kufikia “upinzani usio na chama” umejaa ukweli wenye macho kodo bila kupepesa:
✅Ubaya wa Yanga hauongezi uzuri wa Simba.
-✅Likizo ya Yanga haimwamshi Simba kuingia kazini.
-✅Simba bila Yanga kwenye ligi, hata Chimpumu ya bure inadoda.
✅Simba bila Yanga, marefa, vibendera, waganga wa kienyeji na wanajimu wanakosa soko.
✅Yanga bila Simba, walalahoi wanajitambua na kudai haki zao. Mapenzi yanahamia kwenye siasa.
✅Simba bila Yanga, wanazaliwa Yanga wadogo ndani ya Simba. Kwani Gwaji katoka wapi?
7. Tulikofikia, tujifunze kutunza na kulinda amani bila kutumia silaha. Amani ya silaha na kiota cha machafuko yaliyoahirishwa.
Mnakwepa kurudi mezani? Mtakapokumbuka kurudi mezani, viti vya kukalia vitakuwa havipo. Mtakaa chini.
Wasiojulikana wanajulikana na hawapendi kujulikana. Waliotumwa wanapenda kufuta ushahidi; waliotuma wanapenda kufuta ushahidi. Dhambi isiyotubiwa hudhoofisha afya ya akili.