Life in Tanzania is so Uncertain | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Life in Tanzania is so Uncertain

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by TANMO, Sep 13, 2012.

 1. TANMO

  TANMO JF-Expert Member

  #1
  Sep 13, 2012
  Joined: Apr 12, 2008
  Messages: 8,914
  Likes Received: 214
  Trophy Points: 160
  Nimekosa maneno ya kutumia kwa Kiswahili fasaha kwenye heading.


  Changamoto ni nyingi, mvua zikinyesha kidogo tu basi kila mahali panakuwa hapapitiki, yaani ni tope, maji machafu, pamoja na harufu mbaya kila kona (nazungumzia hasa kwenye miji mikubwa nchini). Unajiuliza hivi si tuna Manispaa? Umefika nyumbani unategemea kujipumzisha huku unatazama ni habari gani zinazojiri kwenye Luninga kumbe Umeme hakuna. Unajiuliza hivi si tuna nishati kibao pamoja na gesi? Wakati huo huo unafikiria jinsi ulivyoipitisha siku yako unakumbuka rafu ulizokumbana nazo kwenye baadhi ya maeneo unayokuwa umepita kwa siku hiyo.


  Kama ulipita Hospitalini basi unakumbuka juu ya wagonjwa uliokuta wamelazwa kitanda kimoja wawili wawili huku wengine wakiwa wamelala sakafuni kutokana na ukosefu wa vitanda pamoja na ufinyu wa wodi za kulaza wagonjwa. Unajiuliza hivi bajeti za wizara ya Afya huwa zinafanya nini hasa? Unaelekea kumuona Daktari napo unakutana na Foleni ndefu ya kukatisha Tamaa huku waliokutangulia wakiwa kimya huku wameshika Tama, hawana matumaini ya kumaliza vipimo vyao. Mara anakuja mtu anatoa simu mfukoni anapiga na mara Daktari anatoka kwenda kumlaki na kuingia naye ndani, unajaribu kuhoji wenzako wanakushangaa na cha kushangaza wengine wanakukejeli kana kwamba unamkosea adabu Daktari. Unajiuliza hivi Takukuru inafanya kazi wakati wa uchaguzi tu?


  Umetoka Hospitalini basi unaamua kwenda kwenye Ofisi Fulani ya Serikali kushughulikia masuala yako. Uko kwenye daladala na foleni ni ndefu, mara unasikia king’ora, mkubwa anapita. Magari ya Kifahari yasiyopungua kumi yanapita kwa kasi ukiuliza unaambiwa ni Waziri Mkuu anaenda kushiriki Mazishi ya nani sijui. Unajiuliza hivi angetumia Helkopta si angeokoa muda na nguvu nyingi sana zinazotumika?


  Basi unafika unapoelekea kwa bahati mbaya unakuta ni muda wa chai hivyo unalazimika kusubiri. Mara Mhusika anafika huku amezongwa na watu kibao wote wanamueleza shida zao na yeye kwa mbwembwe kabisa anapiga mluzi, kila mtu anamnyenyekea. Unaambiwa alivyotoka kunywa chai kuna waliomsindikiza eti wanapiga naye stori. Basi “washikaji” wa Bwana Mkubwa wanamaliza shida zao, sasa ni zamu yako. Unanyanyuka kumfuata anakuambia samahani naomba unisubiri kidogo Bosi ameniita Ofisini kwake mara moja. Unasubiri tena, anaelekea Ofisini kwa Bosi wake, mara unasikia wanaanza kupiga stori kwa sauti na vicheko juu. Unajiuliza hivi hawa ndiyo tumewapa dhamana ya kutukwamua dhidi ya umasikini?


  Unaendelea kusubiri, baada ya nusu saa anajitokeza tena kuelekea kwenye kiti chake na wewe unajisogeza kumweleza shida yako, mara unaambiwa naomba ueleze shida yako haraka manake ninatakiwa niwahi kwenye kikao. Unajitambulisha na kuanza kueleza shida yako, hujamaliza unaambiwa hilo suala tunalishughulikia siku za Jumatatu. Njoo Jumatatu! Huna jinsi, unajiondokea zako. Unajiuliza mbona wenzangu walikuwa na shida kama yangu lakini amewahudumia?


  Njaa imekubana unaamua kupita kwenye kibanda ujipatie chochote, unapita kwa muuza chipsi, ile unataka kuagiza chipsi mayai basi unakumbuka kuhusu mayai ya kichina pamoja na ishu za mafuta ya Transfoma kutumika kukaangia chipsi. Unaamua kuagiza ugali nyama, unaletewa ugali wako unaufakamia haraka haraka unaagiza kinywaji na unaletewa soda, inafunguliwa unakutana na uchafu kama kutu kwenye mdomo wa chupa, unaweka kamgomo ka kuinywa basi unaletewa Glasi huku muuzaji akijitetea kuwa hausiki na huo uchafu. Unajiuliza hivi si tuna Mamlaka ya viwango Tanzania?


  Mara simu inalia, meseji imeingia, kuangalia unaambiwa Asante kwa kuchangua ***** mlio wako wa sijui nini umewezeshwa na umekatwa kiasi kadhaa, kuangalia salio, kweli limepungua unabaki kujiuliza ni lini na ni vipi nilijiunga na milio ya simu? Jibu unakosa, basi unaamua kuachana nalo. Kichwani unajiuliza, hivi mamlaka inayosimamia mawasiliano iko kwa ajili gani?

  Uko barabarani unataka kuvuka tena sahemu ya pundamilia mara Boda boda hiyo inakukosa kosa, basi unamshukuru Mungu kwa kukunusuru. Maisha yanaendelea, uko Stendi Teja anaanza kukuzengea, “Kariakoo, Kariakoo” anaita, unaamua kushikilia kwa umakini ulichoshika mkononi, Hamadi pembeni yako mama mtu mzima anapiga yowe, mwiiiziii. Teja anajitahidi kupenya watu inashindikana, wanaanza kumpiga, damu zinaruka, dakika tatu hazijaisha Teja yuko chini chali, pumzi zimemtoka!! na watu wanatawanyika wote. Mama aliyeibiwa bado ameduwaa, teja kafa na bado mali yake hajaipata, Unajiondokea zako usijechukuliwa ukaisaidie Polisi. Unajiuliza hivi kuua vibaka kutakomesha tabia ya ukwapuaji? Mbona kama vile ndiyo inazidi kuongezeka?


  Uko kwenye pilika pilika mara unasikia akina nani sijui wanaandamana, barabara haipitiki, mabomu ya machozi yanavurumushwa mtindo mmoja. Unaamua kukimbia kunusuru roho yako. Ile unaingia Jamii Forums unakutana na habari watu wawili wamekufa na wanne kujeruhiwa na kile kinachoaminiwa kuwa ni Risasi za moto kwenye maandamano ya akina nani sijui na Polisi wakaamua kuyazuia. Unajiuliza, kulikuwa na ulazima wa Polisi kuingilia mandamano hayo?


  Unaanza kufanya tathmini ya afya yako kiujumla unajigundua kuwa unakonda zaidi. Mawazo juu ya mawazo, na hapo hujafikisha hata miaka Thelathini. Unawaza kuhusu maisha ya kuishi kwa Mtanzania kwa mujibu wa akina nani sijui, unakumbuka kuwa ni miaka 45, mara mamlaka sijui ya vitu gani inakuja na hoja kuwa ili uje kupata mafao yako ni lazima utimize miaka 55 na kuendelea, unajiuliza hivi hiyo miaka waliifikiria vyema kweli? Mbona tumeshahakikishiwa kuwa Umri wetu wa kuishi ni miaka 45? Sasa hiyo 55 itatoka wapi? Unaamua kuachana na kuwaza sana manake wanasema mawazo nayo yanapunguza umri wa kuishi.


  Ukiangalia vijana wenzako wengi wanatumia ulevi, unajiuliza, hata Nanii naye siku hizi anakunywa? Ukiwahoji wanakuambia unywe usinywe mishahara yenyewe haikutani. Ni kweli kauli yao, lakini unaamua uwe mjasiria mali, unaamua kuanzisha kamradi kako mara TRA hao, tupe chetu, mara Manispaa, tupe chetu, lakini miundo mbinu iko vile vile, hali ikiwa mbaya mnachangishana wenyewe mnakodisha Greda angalau lifukie fukie mashimo. Unajiuliza, hivi hawa Manispaa ushuru wanaupelekaga wapi?


  Unafikiria hivi mbona watanzania wengi wamekata tamaa? Ni kwa nini siku hizi yanaibuka madhehebu mengi ya dini na yanapata waumini sana? Unahisi labda baadhi ya Viongozi wa dini wajanja wameamua kuwekeza kwenye kukata kwetu tamaa na wanajichumia mali kiulaini kwa kuwahadaa waliokata tamaa kuwa watawaondolea matatizo yao na kuwaponya magonjwa ambayo yangewezekana kutibika mahosipitalini kama huduma za afya zingeboreshwa. Unajiuliza hivi Vitabu vya dini vilisemaje juu ya kuibuka kwa manabii wa uongo?


  Unaamua kutafakari mustakabali wa maisha yako unaona kiza zaidi. Unawaza kuwa ukitembea barabarani muda wowote unaweza gongwa na magari yaliyofeli Breki, au Boda boda ambayo kijana amejifunza asubuhi, jioni yuko barabarani. Ukisafiri, muda wowote unaweza kufa manake imekuwa desturi sisi kufa kwa ajali za barabarani. Ikulu nadhani walishaandaa kabisa salamu za Rambirambi kwa ajili ya watanzania wenzetu wanaopoteza maisha kwa ajali kila kukicha, manake ikitokea tu, utasikia Mheshimiwa Rais ametuma salamu za rambirambi. Anasubiri ajali nyingine itokee, atume tena salamu!!


  Unajifikiria hizi bidhaa tunazonunua nyingi hazina ubora stahiki kwa ajili ya matumizi ya binaadamu. Unaweza kununua bidhaa kumbe ndiyo umejinunulia kifo. Serikali iko bize kutafuta madawa dhidi ya vifua vikuu, kansa, malaria n.k. Unajiuliza hivi tunachohitaji ni Tiba au ni njia ya kudumu kukomesha haya matatizo?


  Unafikiria kuwa unaweza kuwa unatembea barabarani ukakutana na Umati wa watu wameamua kufanya maandamano ya amani kudai haki zao mara Polisi wanatokea na kuanza kumimina Risasi za moto. Unaweza kuwa mmoja wa watakaokufa kwa hizo risasi. Unajiuliza hivi Polisi wasipoua hawajisikii raha?


  Hoja yangu hapa ni kuwa ukiishi Tanzania jiandae kufa wakati wowote. Kwa mantiki hiyo ni wajibu wetu sote kusimama kutetea maslahi yetu na ya nchi yetu manake hata usipofanya hivyo, mfumo uliopo umeshakujengea mazingira ya kufa anytime. Tuamke dhidi ya Mafisadi wanaojinufaisha kwa kututoa roho.


  Mapendo.
  TANMO
   
 2. Neiwa

  Neiwa JF-Expert Member

  #2
  Sep 13, 2012
  Joined: Feb 17, 2012
  Messages: 730
  Likes Received: 44
  Trophy Points: 45
  TANMO mkuu, Kiswahili heading nadhani ingekuwa "Maisha ya Tanzania ni ya kubabaisha/bangaiza". Mkuu umegusa penyewe kabisa.
   
 3. h

  hippocratessocrates JF-Expert Member

  #3
  Sep 13, 2012
  Joined: Jul 1, 2012
  Messages: 3,612
  Likes Received: 26
  Trophy Points: 135
  what a story TANMO..
   
 4. K

  Kaldinali JF-Expert Member

  #4
  Sep 14, 2012
  Joined: May 25, 2012
  Messages: 264
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Duuuh

  Kweli tupu TANMO. Nashauri ungetengeneza ka documetary ka dakika 15 kuhusu haya yote uliyoandika na upost youtube (two version swahili and english version).

  yaani hayo ndio maisha ya asilimia 85 ya watanzania
   
Loading...