Kwenu Watetezi wa Ufisadi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kwenu Watetezi wa Ufisadi

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by MwanaHaki, Sep 9, 2010.

 1. MwanaHaki

  MwanaHaki R I P

  #1
  Sep 9, 2010
  Joined: Oct 17, 2006
  Messages: 2,403
  Likes Received: 122
  Trophy Points: 145
  TANZANIA ni nchi yenye rasilmali nyingi sana. Nyingi sana. Lakini jambo la ajabu na kusikitisha, idadi kubwa ya watu wake ni masikini, tena masikini sana, fukara wa kufukarika, wasiokuwa na makazi stahiki kwa binadam (mpaka leo wengi wao wanaishi kwenye nyumba za kukandikwa na udongo unaowekwa kati kati ya miti na kuezekwa kwa nyasi); wasiokuwa na uhakika wa mlo mmoja kwa siku; wasiokuwa na elimu ya kuwawezesha kusoma na kuandika; wasiokuwa na fedha; wasiokuwa na nyenzo bora za kilimo; wasiokuwa na uwezo wa kupata huduma bora za afya (kutokana na kukosekana kwa wahudumu wa afya wa kutosha, dawa za kutosha, matabibu wa kutosha). Hii ni Tanzania ya leo, takriban miaka 50 baada ya Uhuru.

  Mwaka 2010, Tanzania itatimiza rasmi miaka 50 ya Uhuru wake. Jambo la ajabu, pia, na kusikitisha, ni kwamba, nchi hii haina lolote la kusheherekea kutimiza nusu karne ya Uhuru wake (wa bendera?). Mkakati mkubwa kama huu ulipaswa kuandaliwa – na kutangazwa kwamba umeandaliwa – kuanzia mwaka 2006, angalau. Tanzania ina mambo mengi ya kuuonesha ulimwengu; ina utajiri wa utamaduni wake wa asili, wa vyakula, michezo ya jadi, tamthilia (nyimbo, ngoma, mashairi, n.k.) na pia mavazi ya asili. Tanzania ina makabila zaidi ya 100, ambayo yote ni utajiri mkubwa wa kiasili, mpaka leo, hakuna mpango kamambe uliopangwa kutumia urithi huu mkubwa wa asili kama mtaji wa utalii wa kitamaduni (cultural tourism). Nchi za jirani wameendelea sana kwa hili; sisi bado usingizi ni mzito.

  Hata hivyo, si nia yangu kuzungumzia utajiri wetu wa asili – katika nyanja ya utamaduni. Nimekuja kuwazindua ndugu zangu, angalau mnaoishi kwenye miji mikuu, ili mjue kwamba tunapelekwa pabaya na uongozi uliopo madarakani. Nataka kuzungumzia suala la nishati ya umeme.

  Wakati ninaandika waraka huu, sichelei kuhofia ni wakati gani TANESCO watakata umeme, tena bila taarifa, na kurejesha wakati wowote wanaotaka wao. Sababu za umeme kukatika ghafla, bila taarifa, ni nyingi na nyingi hazina msingi wowote. Lakini hiyo ndiyo TANESCO – idara nyeti ya Serikali – isiyo na mipango thabiti ya udhibiti na usimamizi wa nishati hii muhimu kwa maendeleo ya watu.

  Kila mwaka, TANESCO hupandisha gharama za manunuzi ya umeme kwa wateja wake, na kila mwaka, wateja wa TANESCO hulazimika “kubana mikanda” zaidi ili kuweza kumudu gharama hizo kubwa. Hii ni kwa kuwa mpaka sasa hakuna kampuni nyingine kubwa – zaidi ya Artumas inayofanya kazi kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara pekee – iliyoruhusiwa kushindana na TANESCO. Sababu ya kutokuwapo kwa kampuni shindani ni moja tu – ufisadi wa kulinda maslahi ya wakubwa, ambao hunufaika na “mgao wao wa fedha” usio rasmi, wakati wa mchakato wa kuwathamini wazabuni wanaopewa zabuni za kuingiza na kujenga vinu vya kuzalishia umeme kwa nishati ya mafuta ya petroli (fossil fuel technology), ambayo, licha ya kwamba ina gharama kubwa, lakini bali pia ina athari kwa mazingira kutokana na uchafuzi wa hewa kupitia moshi wenye kemikali zinazoathiri tabaka la ozoni unaozalishwa na vinu hivyo. Tabaka la ozoni ni kinga mojawapo kwa dunia yetu hii, ambayo husaidia kufifisha nguvu za miale ya jua yenye kiwango kikubwa cha joto. Kinga hii imekuwa ikipotea mwaka hadi mwaka, chanzo cha matatizo mengi kwenye ardhi yetu; kubadilika kwa tabia-nchi, mvua za maafa, ukame, uharibifu wa mazingira, kuyeyuka kwa miamba ya barafu Ncha ya Kaskazini na Ncha ya Kusini, n.k.

  Wakati yote haya yakiendelea, nchini hapa hakuna mkakati wowote ule ulioandaliwa kuacha kabisa kutumia nishati hii yenye athari kubwa kwetu wote. Hakika, mikakati iliyopo ni kuongeza matumizi ya nishati ya mafuta ya petroli kuzalishia umeme, badala ya kuweka mikakati ya matumizi ya nishati ya upepo, ambayo, licha ya kwamba haina madhara ya aina yoyote kwa mazingira, haina pia gharama kubwa za manunuzi ya nishati ya msingi – UPEPO HAUNA BEI YA MANUNUZI!

  Wadau waliopo kwenye vyombo husika vya serikali vinavyosimamia uzalishaji wa nishati ya umeme hawawezi kuanzisha mikakati hii, kwa kuwa, mosi, wanategemea sana “twenty percent” zao wakati wa kupitisha zabuni, na pia, wanategemea “ten percent” wakati wa manunuzi ya mafuta ya dizeli yanayotumika kwenye vinu vilivyosambazwa nchini kote, licha ya madai kwamba sehemu nyingi zinafikiwa na umeme wa “grid”.

  Ukitaka kuupata ukweli, chungua maisha na mienendo ya Makamishna wanaofanya kazi kwenye Wizara ya Nishati na Madini, utagundua mambo kadhaa. Watumishi hawa wa umma wanaishi maisha ya kifahari mno, kana kwamba wao si Watanzania, bali ni wageni tu hapa. Nenda kachunguze.

  Gharama ya kununua na kujenga kinu cha kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo kwa kiwango cha megawatt 1, kinachoagizwa nje ya nchi, ni takriban dola za Marekani 500,000, takriban sawa na Shilingi za Tanzania 750,000,000. Gharama ya kuunda na kujenga kinu kama hicho hapa nchini ni takriban Shilingi za Tanzania 50,000,000, sawa na asilimia 7 ya bei ya kinu kutoka nje ya nchi. Tanzania tayari ina wataalam – wazawa, wazalendo – wenye uwezo wa kujenga vinu hivi vya kuzalisha umeme, pamoja na kujenga mfumo wote wa kuusambaza bila athari kwa watumiaji wake. Sehemu za wapi nishati ya upepo inapatikana kwa kiwango kinachotakiwa si mjadala; taarifa hizo zipo, zimetokana na utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 20! Wizara ya Nishati na Madini pia ina taarifa hizi.

  Ninawashangaa wachumi wanaoishauri Serikali. Mimi ni mchumi. Sijapata nafasi ya kuishauri Serikali, lakini ningeipata, ningeishauri kwamba tuachane kabisa na suala la uzalishaji umeme kwa kutumia nishati ya petroli, kwani, inachangia kwa kiwango kikubwa athari kwa mazingira na pia kwa watumiaji wake. Wakazi wa Dar es Salaam wanaoishi eneo la Ubungo Maziwa, iliyopo mitambo ya Aggreko, ni mashuhuda katika hili. Wengi wao wameathirika na athari mbaya kwa mazingira inayotokana na mitambo hiyo ya kuzalisha umeme kutokana na gesi asilia ya Songo Songo. Mtambo huo ulipaswa kujengwa eneo ambalo halina wakazi, la, wakazi hao walipaswa kutafutiwa eneo lingine la makazi, kulipwa fidia na kuhamishwa. Lakini Serikali haikujali kwamba kulikuwa na athari kwa mazingira na binadam wanaoishi hapo. Hili halikuwa la msingi.

  Yapo madai kwamba nishati ya kuzalisha umeme kwa upepo ina gharama kubwa. Kama wapo Watanzania wenye utaalam wa kuunda vinu vya kuzalisha umeme kwa kiwango kikubwa, kupitia nishati ya upepo, tena kwa gharama nafuu sana, madai hayo ya mitambo kuwa na gharama kubwa yanatokana na takwimu gani? Au ni lazima mitambo hiyo iwe imeagizwa nje ya nchi ili kuweza kutumika hapa nchini? Kwani kila kitu kinachotakiwa kutumika hapa ni lazima kiagizwe nje ya nchi?

  Busara ni kwamba, nchi inapaswa kujenga uwezo wa kujitegemea, hususan katika mambo muhimu yahusuyo maendeleo yake, kama vile kujenga uwezo wa kitaaluma na uzalishaji wa nishati ya umeme, kutegemea mifumo ya ndani – iliyo endelevu – kuliko ile inayoagizwa nje ya nchi, ambayo inajenga utegemezi wa teknolojia za nje ya nchi, kuliko zile za ndani ya nchi. Mjadala huu upo pia kwenye sekta ya kilimo; ingawa sasa Tanzania tuna uwezo wa kuunda matrekta yetu wenyewe, bado wapo wato wanaodharau uwezo huu, wakipendelea zaidi “power tillers” na trekta kutoka nje! Kasumba hii ya kudharau kilicho chetu na bora zaidi ITAISHA LINI?

  Mafisadi hawataki kabisa nchi hii iwe na uwezo wa kujitegemea kwenye suala la nishati ya umeme. Hawataki! Hawataki Watanzania wengi zaidi waweze kutumia nishati hii kujiendeleza kibiashara. Hawataki Watanzania wengi zaidi waweze kujiajiri kupitia nishati hii. Viwanda vidogo vidogo, karakana, mafundi seremala, mafundi wanaounda mageti na “grill”, vyote vinahitaji umeme mwingi wenye gharama nafuu.

  Mafisadi wako radhi Watanzania waendelee kuwa maskini, waendelee kuwa tegemezi, wasiinuke kutoka kwenye lindi la umaskini. Hawa mafisadi ndio wanaosababisha gharama ya umeme kwa mtumiaji kupanda mwaka hadi mwaka. Hawa mafisadi ndio wanaosababisha umeme – licha ya kuonekana kuwa anasa – kutopatikana kwa uhakika, kutokana na ukweli kwamba, usimamizi wa mfumo wa umeme uliopo sasa ni duni. TANESCO haina wahandisi wa umeme wa kutosha; sidhani kama nchini kuna chuo chochote kile kinachofundisha uhandisi wa umeme katika ngazi ya vyuo vya ufundi (VETA), au hata chuo kikuu.

  Tunawajua mafisadi. Tunawajua maswahiba zao. Tunawajua makuwadi wao. Tunawajua washirika wao. Lakini wanaowatetea wanataka kuwaghilibu wananchi – ambao ndio wenye ridhaa ya kuwaweka madarakani – waendelee kuwapigia kura na kuwaweka madarakani. Hawa ni WAKOLONI WEUSI! Hawa hawana uchungu na nchi hii, hawaitakii mema nchi yetu.

  Ninyi mnaowatetea mafisadi, kumbukeni kwamba historia itakuja kuwahukumu.

  Leo hii mnatunga uongo, mnapoteza dira kwa hoja zinazohusu maisha binafsi ya wakombozi wetu, huku ninyi wenyewe mnaishi kwenye nyumba za vioo. Mnarusha mawe. Lakini sisi – ingawa tunao uwezo huo – hatutarusha mawe. Hatutashiriki kwenye siasa hizo chafu, za maji ya ******, maji taka! Hapana. Hatutapoteza dira yetu.

  Mijadala hiyo potovu ipelekeni mahakamani, kama mnadai haki hiyo ya kusafishwa.

  Mimi namcheka sana huyu anayedai kuporwa mke. Alikuwa wapi mpaka aporwe mke? Basi nina mashaka na urijali wake. Labda hakumtosheleza mkewe, mpaka akakimbia kwa KIDUME wetu! Hahahahaah!

  Mnayataka maendeleo? Mnautaka umeme nafuu utakaowaleteeni maendeleo lukuki na kuwajazeni mapesa? Mnataka kuondokana na umaskini WA KUTENGENEZWA unaolindwa na mafisadi hawa? Jiungeni sasa na Mchakato wa Mabadiliko (Movement for Change) unaoletwa kwenu na CHADEMA.

  Napenda kutoa tahadhari. Kuunga chama cha siasa cha upinzani SIO LAZIMA uwe mwanachama wa chama hicho. Mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa, lakini ninaiunga mkono CHADEMA. Hiki ndicho chama kilicholetwa kutukomboa sisi wanyonge. Hiki ndicho chama kilicho na uchungu na nchi hii. Nabii hupingwa daima nyumbani kwake, lakini fisadi hufanyiwa sherehe kubwa kubwa na kutukuzwa kama Mungu Mdogo. Kisa? Pesa zake!

  Siku ya Hukumu – imeandikwa – wale wote waliopokea rushwa kuwachagua viongozi fisadi wataulizwa wajieleze ni kwa nini waliwasaliti wenzao na kukiuka amri ya Mwenyezi Mungu. Wataulizwa. Wakishindwa kujibu, wataoneshwa mlango wa kushoto – Jahanam. Kwa hili, hakuna jibu litakalotosha kuwaokoa na Jahana. Hakuna.

  CCM ina kiapo cha uanachama. Rushwa ni adui wa haki. Sitatoa wala sitapokea rushwa. Lakini VIONGOZI wa CCM ndio wamekuwa mstari wa mbele kukiuka kiapo hiki! Ya Firauni haya; ya Musa hayastaajabishi tena!

  Wabillah Tawfiq. Wa Rahmatullah, Taala Wabarakatuh!

  Eid Mubarak!
   
 2. WomanOfSubstance

  WomanOfSubstance JF-Expert Member

  #2
  Sep 9, 2010
  Joined: May 30, 2008
  Messages: 5,465
  Likes Received: 72
  Trophy Points: 0
  THIS IS POWERFUL.............Food for thought.Ni Chama cha siasa kitakachotuletea ukombozi au ni mtu ndani ya chama au ni mtu nje ya chama?


  Will come back to discuss..Im stepping out for now.
   
 3. MwanaHaki

  MwanaHaki R I P

  #3
  Sep 9, 2010
  Joined: Oct 17, 2006
  Messages: 2,403
  Likes Received: 122
  Trophy Points: 145
  Ina manaa wewe peke yako ndio umeona umuhimu wa kuchangia mada hii? LOL

  Basi tuendelee na haya maumivu ya umeme wa bei mbaya wa TANESCO, wakati jirani zetu wa Kenya wameanza kufaidi matunda ya nishati ya umeme itokanayo na UPEPO!
   
Loading...