WAKATI alipokubali kuzungumza na waandishi wa habari kutokea Kilimanjaro Hotel kuhusu mchakato wa kumpata mgombea urais mnamo Machi 14, 1995, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alionya mwanzoni mwa hotuba yake kuwa kama waandishi walikuwa wametarajia kuwa katika tukio hilo angetaja majina au jina la mtu anayedhani kuwa anafaa kuwa rais wa Tanzania katika uchaguzi wa mwaka 1995, walikuwa wanekosea.
Alisema kuwa alichokuwa amejiandaa kukifanya ni kuzungumzia sifa ambazo mtu anayepaswa kuwa rais wa Tanzania anapaswa kuwa nazo.
Mwalimu Nyerere alipanga sifa hizi kulingana na changamoto na matatizo ambayo Tanzania, kama taifa, ilikuwa inayapitia wakati huo. Baada ya hotuba hiyo, katika uchaguzi uliofuata, Benjamin Mkapa alichaguliwa kuwa rais akimrithi Ali Hassan mwinyi.
Kama Mkapa alikuwa chaguo zuri au la kulingana na sifa alizozieleza Mwalimu Nyerere bado ni suala la kubishaniwa hadi hii leo. Wapo watu wanaamini kuwa Mkapa ni mmoja wa viongozi waliofanya vizuri sana katika nafasi ya urais wakati kundi jingine likimuona Mkapa kama mtu ambaye ameisababishia nchi matatizo makubwa kutokana na aina ya uongozi wake.
Nimeyakumbuka maneno ya Mwalimu Nyerere kutokana na baadhi ya maoni niliyotumiwa na wasomaji wa safu hii wiki iliyopita.
Katika makala hiyo, niliishauri serikali kufuata ushauri uliowahi kutolewa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, katika suala la elimu. Kiufupi, niliiunga mkono hoja ya Lowassa na kuisihi serikali kuiweka elimu kama kipaumbele cha kwanza badala ya kilimo.
Niliandika makala hiyo kwa kuitumia hoja ya Lowassa na wala sikuwa na fikra za kumhusisha Lowassa kama mtu aliyeitoa hoja hiyo. Nilichokiangalia ni hoja yenyewe na si mtoa hoja.
Lakini inaelekea kuna baadhi ya wasomaji ambao walielewa zaidi ya kile nilichokusudia kukieleza katika makala hiyo. Wakiwa na tafsiri zao hizo, baadhi yao walinitumia ujumbe wakinituhumu kuwa katika makala ile nililenga kumpigia debe Lowassa kama mtu anayefaa kuwania urais mwaka 2015. Wengine wakasema kuwa ninajipendekeza kwa Lowassa.
Mmoja aliandika: "Habari ndg Peter? Hakuna cha zaidi cha kuongeza, mnatumia nguvu kubwa kumnadi Lowassa. Tukubaliane kuwa ameshafanya kazi nyingi sasa ni wakati wake wa kupumzika na kula pesa zake. Hafai kuwa rais, kachoka."
Wakati nikitafakari maudhui ya ujumbe huo kwa lengo la kutaka kumpigia aliyeniandikia ili tuzungumze kwa kina, ukaingia ujumbe mwingine ukisema: "Hivi tumepewa nini na Lowassa tunamfanyia kampeni kiasi hiki?"
Nikaanza kupatwa na wasi wasi kuwa kuna baadhi ya watu hawakusoma kwa makini nilichokiandika na wameamua kuja na tafsiri yao.
Mara ujumbe mwingine ukaingia: "Sijui ni mimi au nini lakini Lowassa huyu si ndiye alikuwa Waziri Mkuu? Ni lipi alilifanya kuhusu elimu japo tuone tu? Si huyu walioanza kuifilisi nchi na kuiingiza kwenye mikataba mibovu. Ni ujiko tu anautafuta na wewe naona kama unajikomba kwake! Hana jipya, lakini unaweza kumbeba."
Ilipofika hapo nikakata shauri kuwa ingawa sikupanga kuliandikia hili, basi ni vema nitoe ufafanuzi ili tuwekane sawa kuhusiana na Lowassa, urais wa 2015 na ninachokifikiria mimi kuhusiana na suala hilo.
Msimamo wangu hautofautiani na maneno aliyoyatoa Mwalimu Nyerere pale Kilimanjaro Hotel. Naamini kuwa tutafanya kosa kubwa sana iwapo tutaanza kumjadili mtu anayefaa kuwa rais wa nchi mwaka 2015.
Ninaamini kuwa tunachotakiwa kukijadili ni changamoto zinazotukabili kama taifa. Kutokana na changamoto hizo tutapata sifa za mtu anayefaa na baada ya hatua hiyo ndipo tunaweza kuanza kuangalia ni nani anakidhi haja ya sifa hizo.
Kuanza kumjadili mtu hivi sasa wakati hata hatujakubaliana kuhusiana na changamoto na matatizo ya msingi ambayo rais ajaye anapaswa kuyavalia njuga, tutakuwa hatulitendei haki taifa letu.
Kutokana na ninachokiamini sijawahi hata siku moja kuanza kumfikiria mtu fulani kuwa anafaa kuwa rais; si Lowassa au mtu mwingine yeyote yule. Kwa maana hiyo, wale wanaodhani kuwa niliandika makala ile ili kumpigia debe Lowassa au kujikomba kwake, napenda wafahamu kuwa wamekosea.
Na kama wanataka kuthibitisha kuwa wamekosea, nawashauri warudie kuisoma makala ile kwa utulivu ili wanionyesha hata sehemu moja ambapo, hata kwa maudhui tu, nilionyesha kuwa Lowassa anafaa kuwa rais mwaka 2015.
Kwanza hao wanaonilaumu mimi kuwa ninampigia debe Lowassa wanaweza kuwa wanafanya kosa lile lile wanalolipiga vita. Kwa kuwa sikuzungumzia suala la Lowassa na urais, nimeamini kuwa wao ndiyo wanawaza waza sana kuhusiana na Lowassa na urais kiasi kuwa kila wanapoona jina lake limeandikwa, wanasoma kwa ajili ya kutafuta kitu cha kuwalaumu walioandika maandishi hayo.
Ndiyo maana, ingawa sikuzungumzia suala la urais, wao waliweza kuliona hilo.
Kwao hao na wengine wenye msimamo kama huo, naomba kuwaeleza kuwa wanatupotezea muda wenye thamani kubwa sana kwa kutulazimisha kujadili watu. Kuna mambo mengi muhimu ya kujadili likiwamo hili la urais wa 2015.
Lakini, tunaweza kufanya makosa makubwa sana iwapo aina yetu ya mijadala itakuwa ya aina hii ya kuanza kuwaangalia watu badala ya hoja.
Sipingi mtu kuwa na msimamo wa kumuunga fulani mkono katika kuwania urais mwaka 2015. Lakini kama wao wana haki ya kumuunga mkono huyo wanayemuunga mkono, hata kama hawamtaji, kwa nini iwe kosa kwa wengine kumuunga mkono Lowassa?
Nadhani suala siyo kumuunga mkono au kutomuunga mkono Lowassa au mtu mwingine yeyote. Suala tunalopaswa kuliangalia kwa makini ni changamoto zinazotukabili kama nchi na kisha kuorodhesha sifa za mtu anayefaa kukabiliana na changamoto hizo. Sifa hizo ndizo tuzitumie kumpata mtu anyefaa kuwa kiongozi wetu.
Kama kwa kutaja tu suala la elimu kama lilivyozungumzwa na Lowassa kunamaanisha kuwa nimemvalisha Lowassa moja ya sifa za kuwa rais, napenda mambo kadhaa yaeleweke.
Kwanza, sifa ya kuwa rais haitatokana na suala moja tu la elimu. Nchi ina changamoto nyingi zaidi ya elimu. Lakini, msimamo wangu wa kuona kuwa Lowassa analiwakilisha vema suala hili la msisitizo wa elimu haimaanishi kuwa ni yeye tu ndiye mwenye wazo zuri kuliko wote katika suala la elimu.
Niwasihi watanzania wenzangu hawa kuwa wasipofushwe macho na wanasiasa. Iwe ni Lowassa au mwingine yeyote, tunapaswa kufahamu kuwa wote ni wanasiasa na kuwa kipimo tutakachowapimia kinapaswa kuwa sawa.
Inavyoelekea wanamuogopa Lowassa ingawa hajatangaza mwenyewe kuwa atagombea urais. Haya yanayosemwa kuwa atawania urais yanaweza kugeuka baadaye kuwa kweli.
Kama kweli itakuwa hivyo, ushauri wangu kwa hao ambao wanadhani hafai ni kuwa kama wanataka kuuthibitishia umma wa watanzania kuwa Lowassa hafai, basi waje na wagombea wao ambao wana sifa zinazomzidi Lowassa.
Hata mimi, siku nitakapoamua kumuunga mkono mtu fulani, sidhani kama nitajihangaisha na kuangalia upungufu wa wapinzani wake kuwa ndiyo msingi wa kumpa nafasi mgombea ninayemuunga mkono.
Kama kweli nina dhamira ya dhati ya kumfanya mgombea wangu ashinde, basi nitajikita katika kuelezea sifa zake na kwa nini anafaa kuwa rais wa nchi yetu. Kuanza kumponda mpinzani ni dalili za kuonyesha kuwa umeishiwa na hoja za kumsifia mgombea wako.
Napenda kuwathibitishia wasomaji wangu hawa ambao wamenishutumu kuwa ninatumiwa au ninajipendekeza kuwa sina tabia hiyo na wala sitarajii kuwa nayo kwa sababu walionifundisha jinsi ya kuishi hawakunifunda niwe mtu wa kujipendekeza iwapo ninataka mafanikio.