Kwanini namlilia Bi Sharifa Hussein Kalala, mama mlezi wa wanamarekani na Dkt. Ramadhani Dau

Rubawa

JF-Expert Member
Dec 25, 2015
2,055
3,239
Ilikuwa siku ya Ijumaa tarehe 21 Februari 2020 kiasi cha saa 4 usiku kwa saa za Malaysia wakati Mhe Balozi Asha Rose Shaaban Mtengeti-Migiro aliponipigia simu kutaka kuzungumza na mimi kuhusu mambo mawili.

La kwanza lilikuwa la kiofisi lakini la pili ilikuwa kunipa taarifa kuwa Bi Sharifa Hussein Kalala anaumwa na hali yake ni mbaya sana.

Kwa maneno yake Balozi Migiro, “kilichobaki ni Rehma ya Mwenyezi Mungu”.

Kwa hakika nilihuzunika na kushtuka sana. Nilihuzunika kwa sababu namfahamu Bi Sharifa kwa zaidi ya robo karne. Lakini nilishituka kwa sababu siku ya Alhamisi tarehe 13 Februari 2020, nilimtumia Mzee Yusuf Kalala (mume wa marehemu Bi Sharifa) ujumbe mfupi wa simu (sms) kumuarifu kuwa Mzee Iddi Simba amefariki dunia.

Mzee Kalala alinijibu kwa ufupi kusema “Innallillah Wainnaillahi Raajiuun,” kisha akaongeza kwa kuniarifu kuwa yupo kiwanja cha ndege cha Zurich akielekea Marekani kwa sababu Bi Sharifa anaumwa.

Haikunijia kabisa kuwa hali ya Bi Sharifa ilikuwa mbaya hadi aliponipigia simu Mhe Balozi Migiro siku moja tu kabla ya Bi Sharifa kufikwa na umauti.

Kwa huzuni kubwa, nilipoamka asubuhi ya Jumamosi tarehe 22 Februari nikakuta ujumbe wa simu uliotumwa kiasi ya masaa 3 yaliyopita kuniarifu kuwa Bi Sharifa Hussien Kalala amefariki dunia!

Nimewahi kusema mara kadhaa kuwa kuandika taazia ni jambo zito sana na haswa inapohusu mtu ambaye unaemfahamu sana.

Mara zote niandikapo taazia hutamani sana kuwa hiyo iwe ndio ya mwisho.

Kila niandikapo taazia (hii ni ya 7), hujikuta nabakiwa na majonzi kwa muda wa siku kadhaa baada ya kuichapisha kwa sababu kila inaposomwa, baadhi ya wasomaji hunipigia simu au kunitumia ujumbe kueleza hisia zao.

Jambo hili huwa linavuta hisia zangu (emotions) na inakuwa kana kwamba msiba ule ndio kwanza umetokea; ni sawa na kutonesha kidonda.

Hivyo basi, kwa kila taazia nilizoandika, msiba kwangu huwa haumaliziki mapema. Kutokana na sababu hii, mara hii niliamua nisiandike chochote kuhusu Bi Sharifa.

Hata hivyo, nafsi yangu inanisuta kuacha kuandika kuhusu Bi Sharifa kutokana na ukaribu wangu na familia yote ya Mzee Yusuf Kalala.

Ndipo leo ikiwa ni siku ya 5 tokea afariki Bi Sharifa, nilipoamua nibadili uwamuzi wangu kwa sababu ningekuwa sikumtendea haki Bi Sharifa na familia ya Mzee Kalala.

Katika mazingira haya, ni bora kwangu mimi kuendelea kuwa na majonzi kwa siku kadhaa baada ya kusomwa taazia hii, kuliko kuacha kuandika machache kati ya mema yake mengi aliyowafanyia binaadamu wenziwe.

Nimemfahamu Bi Sharifa tokea miaka ya 1990s wakati nilipokuwa Mkurugenzi wa Masoko katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA). Kipindi hicho nilikuwa nasafiri mara kwa mara kwenda Marekani kikazi na wakati huo Bi Sharifa na mumewe Mzee Yusuf Kalala walikuwa wanafanyakazi Washington DC.

Katika kumbukumbu zangu, mara zote nilipokwenda Washington DC ziara yangu inakuwa haijakamilika iwapo sijaenda nyumbani kwa Mzee Kalala ambapo mara kadhaa Mzee Kalala mwenyewe alikuwa ananifuata Baltimore Washington International (BWI) au International Airport Dulles (IAD) ambavyo ni viwanja vya ndege vinavyotumiwa sana na abiria wa Washington.

Marehemu Bi Sharifa pamoja na mumewe Mzee Yusuf Mtingwa Kalala ni watu wenye ukarimu usio na mfano. Nyumba yao ilikuwa nyumba ya Watanzania ambayo milango yake ilikuwa wazi muda wote kwa watu wa aina zote. Kama zilivyo familia nyingi za Marekani, familia ya Mzee Kalala haikuwa na mtumishi wa ndani.

Mkewe Bi Sharifa alikuwa anafanyakazi Benki ya Dunia na akirudi nyumbani jioni anakuta kundi la wageni nyumbani kwake. Bila kujali uchovu, Bi Sharifa huwapokea kwa bashasha na kuingia jikoni kuanza kupikia wageni.

Wakati mwingine, mara tu baada ya kumaliza kula, kundi lingine la wageni huwa linaingia na Bi Sharifa anaingia tena jikoni. Hayo yalikuwa ni maisha yao ya kila siku.

Bi Sharifa alikuwa akiyafanya hayo kwa furaha ambayo ilidhihiri kwa watu wote kiasi cha kuwafanya wajione wapo nyumbani.

Yapo mengi sana mazuri ambayo Bi Sharifa na mumewe Mzee Kalala wameyafanya katika kusaidia jamii ya Watanzania.

Nakumbuka katikati ya miaka ya 1990s Bi Sharifa na Mzee Kalala walianzisha utaratibu wa kuwasaidia vijana wa Kitanzania kwenda kusoma Marekani.

Chini ya mpango huo, vijana hao walikuwa wanakwenda kuanza masomo kwenye Community Colleges kwa sababu ada ya masomo zilikuwa chini sana ukilinganisha na ada za vyuo vikuu.

Walipofika Marekani, vijana hao walikuwa wanafikia kwenye nyumba ya Bi Sharifa na Mzee Kalala hadi watakapoweza kujikimu na kupata makazi yao ya kudumu.

Vijana wengi sana wamenufaika na mpango huu na wamesoma hadi kupata shahada za Chuo Kikuu huko Marekani.

Baadhi yao wamerudi nyumbani na wengine hadi leo wanaishi Marekani na wanafanyakazi kwenye makampuni makubwa kwenye fani mbalimbali kama vile Wahasibu, Wahandisi, Wanasheria nk.

Baadhi yao leo wanamiliki kampuni zao binafsi Marekani na zinafanya vizuri sana.

Msingi wa yote haya ni mapenzi na ukarimu mkubwa uliooneshwa na marehemu Bi Sharifa na mumewe Mzee Yusuf Kalala.

Miongoni mwa sifa zake kubwa Bi Sharifa ni kutokuwa na kinyongo na mtu hata pale ambapo utamkosea.

Nakumbuka vyema mwezi Januari 2001 kuna kijana mmoja alikwenda Marekani na kama ilivyokuwa kwa wengi waliotangulia kabla yake, nae alifikia nyumbani kwa Bi Sharifa.

Baada ya miezi minne tu yule kijana akapata marafiki Uingereza ambao walimshawishi aende huko kwa kuambiwa kuwa kuna fursa nyingi zaidi kuliko Marekani.

Kwa bahati mbaya sana yule kijana aliondoka bila kuwaaga wenyeji wake ambao walipata taharuiki sana waliporudi nyumbani na kuona kijana ameondoka bila kuacha taarifa yoyote.

Siku ya pili tu baada ya kuondoka Marekani, nilipata taarifa kuwa yule kijana amehamia Uingereza na ameondoka bila kuaga. Bila kusita nilimpigia simu Bi Sharifa na kumtaka radhi sana kwa yaliyotokea. Jibu lake lilinituliza sana moyo wangu na kuona kuwa Bi Sharifa alikuwa na moyo wa pekee kabisa.

Kwa kifupi tu aliniambia “Bwana Dau (kama alivyozoea kuniita), fulani (kamtaja jina) ni kijana mdogo sana. Amefanya makosa na katika maisha yake ataendelea kufanya makosa. Wajibu wetu sisi kama wazazi ni kumsamehe na kumuongoza, haifai kabisa kumkasirikia.”

Huyo ndiyo Bi Sharifa!

Binafsi nimeumizwa sana na msiba huu kwa sababu Bi Sharifa alikuwa mzungumzaji wangu sana.

Kila niendapo Marekani lazima nifike nyumbani kwao kuwatembelea na mara nyingi hulala hapo hapo.

Mke wangu ameshakwenda Marekani mara kadhaa na mara zote amefikia nyumbani kwa Bi Sharifa.

Walipoamua kurudi Tanzania zaidi ya miaka 10 iliyopita, mara nyingi tumekuwa tukitembeleana.

Pamoja na ukarimu wake mkubwa, Bi Sharifa atakumbukwa kwa ucheshi wake usio kifani.

Katika mazungumzo yetu, mara kwa mara nimekuwa nikimtania kuwa amruhusu mumewe aoe mke wa pili ili bi mdogo amsaidie kazi ya kumlea Mzee Kalala.

Kwa kusisitisa suala hili, nimekuwa namkumbusha ule wimbo maarufu wa taarabu kuhusu ukewenza ulioimbwa na Sami Haji Dau na Bi Mwapombe na haswa pale Sami Haji Dau aliposema, “Ukewenza ndio wenye maliwaza, kazi na mwenzio atakupokeza.”

Siku zote jibu la Bi Sharifa lilikuwa “Jambo zuri kama hili bora uanze wewe Bwana Dau”.

Baada ya jibu hilo tunaishia kucheka!

Kifo ni siri kubwa sana ambayo Mwenyezi Mungu Ameiweka. Aidha maisha baada ya kufa ni siri kubwa zaidi ambayo hakuna mwanadamu anaejua.

Hata hivyo katika mafunzo Yake, Bwana Mtume (SAW) Anatumbia kuwa binaadamu wenyewe ndio mashahidi wakubwa wa hatma ya mtu anapokwenda baada kifo.

Iwapo mtu ameishi vizuri na binaadamu wenziwe, hao binaadamu wenziwe ndio mashahidi wa wema aliyoyafanya.

Kwa wale waliotenda mabaya wakati wa uhai wao, binaadamu kuwa mashahidi wa hayo.

Kwa sisi tuliomfahamu Bi Sharifa, tunashuhudia kuwa wakati wote wa uhai wake aliwafanyia wema watu wengi ambao kwa kupitia wema wake, leo wamepata msingi mzuri wa maisha.

Pamoja ya kuwa hakuna binaadamu mwenye haki ya kuhukumu hatma ya binaadamu mwenziwe baada ya kufa, lakini sisi ambao tumeamiliana na Bi Sharifa, tuna dhana njema kuwa amepata mapokezi mema huko Barzaq.

Dhana hii inathibitishwa na kauli ya Bwana Nassor Basalama ambaye alimuuguza Bi Sharifa kwa kuwa nae muda wote mpaka alipoaga dunia.

Kwa maneno ya Bwana Nassor, siku za mwisho za uhai wake, Bi Sharifa alikuwa katika hali mbaya sana kiasi ambacho muda wote alikuwa amefumba macho.

Kwa muda wote huo Bwana Nassor alikuwa hospitali na kumsomea visomo mbalimbali ikiwemo Sura Yassin na Swalat Naria huku akiwa amemshika mkono.

Hata hivyo muda mchache kabla hajaaga dunia kwa mara ya kwanza Bi Sharifa alikunjua mkono wake na akawa anaupigapiga (tap) mkono wa Bwana Nassor kumpa ishara kuwa amtazame.

Alipomtazama usoni, akamuona Bi Sharifa akiwa na tabasamu kubwa sana kisha akamwambia kwa sauti ya chini kuwa “nimefurahi sana kukuona.”

Muda mchache baadae alifariki dunia saa 8 dakika 32 mchana akiwa amezunguukwa na mumewe wa zaidi ya miaka 40 Mzee Yusuf Kalala, binti zake wawili Bi Farida na Bi Rahima, wadogo zake wawili Bi Zahra na Bi Shekha wote wakiwa na waume zao.

Kwa mujibu wa Bwana Nassor, Bi Sharifa ameiaga dunia huku akiwa na utulivu na tabasamu kubwa usoni mwake.

Alifariki akiwa hana hofu wala huzuni. Na hizo ndizo sifa za watu wema wakati wanakata roho kama Alivyosema Mwenyezi Mungu kwenye Quran Sura ya 41 Aya 30:

Hakika waliosema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu, Kisha wakadumu katika waliloliamini, hao huwateremkia Malaika (wakati wa kukata roho) wakawaambia: msiogope, wala msihuzunike; furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu Azithibitishe amali za Bi Sharifa, Ampe Makaazi Mema Peponi na Amuongezee Ucheshi wake aliokuwa nao hapa duniani awe nao katika Barzaq na siku ya Hesabu. Tunamwomba Mwenyezi Mungu Atupe sisi wafiwa subira njema.

Aaaamin, Yaa Rab!
FB_IMG_1582956945047.jpeg


Sent using Jamii Forums mobile app
 
Pole nyingi kwa Familia, pole nyingi kwa wadau wote waliopitia mikono ya mama huyu. Zama hizi familia mithili ya huyu Mama yetu aliyetangulia mbele za haki imekuwa adimu sana. Apumzike kwa amani Mama yetu, sisi wenye ndoto za kufika Ughaibuni tumepoteza nuru.
Ujaaliwe Mwanga wa Milele....Aaamin
 
Poleni sana kwa wote walioguswa kwa namna yoyote na huu msiba. Pole sana na wewe mkuu. MUNGU awapeni wepesi kipindi hiki kigumu. Bwana ametoa na Bwana ametwaa,jina lake lihimidiwe. Amina

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Poleni sana kwa wafiwa.
Mwandiko naona kama ni wa mzee wetu maarufu hapa JF.
Nje ya mada, huyu mzee ana connection nyingi nisingekuwa mgalatia ningemtafuta.
 
Inna lillah wa inna ilayhi rajiuun.
Usiache kuandika unatoa hamu ya waja kuwafanyia waja wenzao mema na mazuri na kwamba watu wema hawajesha bado wapo hata leo.
 
Back
Top Bottom