Kwanini Katiba mpya ni hitaji letu kuu kwa sasa

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,899
Suala la Katiba mpya haliepukiki nchini kwa mazingira ya sasa, na kujaribu kulizuia ni sawa na mtu kujaribu kutemea mate anga. Na kwa kufanya hivyo, hawezi kukwepa kujichafua uso wake mwenyewe. Au anajaribu kuzuia mafuriko ya mto kwa viganja vya mikono.

Historia ya nchi yetu inaonyesha kwamba, mabadiliko ya Katiba hayakwepeki kila panapotokea mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii; na hivyo kwamba, yanayoendelea nchini sasa yatashinikiza Katiba mpya. Kwa nini?

Katiba ya nchi ni ramani ya madaraka na ni kielelezo cha demokrasia nchini kwa sababu ni tunda la uamuzi wa dhati wa wananchi wenyewe. Kudumu kwa Katiba bila marekebisho ya mara kwa mara ni ishara ya Katiba makini; kinyume chake ni Katiba isiyozingatia matakwa ya wananchi na mabadiliko ya nyakati.

Katiba kama ile ya Marekani ambako ndiko tumeazima mfumo wa demokrasia wa sasa, imerekebishwa si zaidi ya mara nne katika kipindi cha miaka 229 tangu ianze kutumika rasmi mwaka 1788, tofauti na Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano ambayo katika kipindi cha miaka 13 pekee iliwahi kufanyiwa marekebisho 14, sawa na wastani wa rekebisho moja kila mwaka!

Dhumuni kuu la kurekebisha Katiba ya nchi ni kutaka kukidhi matakwa ya jamii inayobadilika kwa lengo la kutekeleza demokrasia, haki ya kijamii utawala wa sheria na maendeleo ya nchi. Misingi yote ya Katiba huongozwa na uzalendo na si kwa mizengwe ya siasa za vyama vya siasa kwani Katiba ya nchi iko juu ya vyama vya siasa.

Katiba inayozingatia malengo haya ina uwezo mkubwa wa kuhimili mitafaruku nchini inayoambatana na mabadiliko ya jamii ya mara kwa mara na kudumu kwa muda mrefu kuliko inayokiuka malengo haya, na hivyo kusababisha mabadiliko au marekebisho ya mara kwa mara. Katiba yetu iko katika Katiba za kundi la pili. Nitaelezea kwa nini tumefikia hapo.

Tangu tupate Uhuru Desemba 9, 1961 hadi sasa, Tanzania imepata kuwa na Katiba mpya tano ambazo katika uhai wake zimeweza kufanyiwa marekebisho mara kwa mara kwa kuzingatia mazingira ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ya nchi.

Kila Katiba mpya, na kila rekebisho au marekebisho ya Katiba yalitanguliwa na mitafaruku au migongano ya kijamii na kiuchumi iliyotishia mustakabali wa Taifa na uhusiano wa kimataifa.

Katiba ya kwanza iliyojulikana kama "Katiba ya Uhuru"[The Independence Constitution] ya mwaka 1961, ilitungwa na kutumika katika mazingira yaliyoashiria kumalizika kwa ukoloni mkongwe nchini Tanganyika.

Ilifuatiwa na Katiba ya Jamhuri [The Republican Constitution] ya mwaka 1962 iliyoashiria Watanganyika kuchukua madaraka ya nchi kutoka kwa wakoloni.

Nitafafanua kidogo. Katiba ya Uhuru ndiyo iliyotoa uhuru na ramani ya madaraka kwa Tanganyika huru bila madaraka kamili ya ndani kwa sababu nchi ilikuwa bado inasimamiwa na Uingereza kupitia mteule wake - Gavana wa Tanganyika.

Na kusema kweli, Katiba hiyo haikuwa tunda la Watanganyika; bali ilitungwa na kutolewa kwenye Ofisi ya Makoloni nchini Uingereza na kushushwa kwetu kama "Torati" yenye ukakasi bila kutoa uhuru kamili.

Kwa hiyo ilizua nguvu ya hoja kwamba uhuru kwa Watanganyika bila kuwa na Serikali yenye madaraka ya ndani [Jamhuri] lilikuwa debe tupu, na huo ukawa msingi wa kudai Serikali hiyo na Katiba mpya; madai ambayo ndiyo yaliyozaa Jamhuri.

Kwa bahati mbaya, Katiba zote mbili za kwanza; Katiba ya Uhuru na Katiba ya Jamhuri, tofauti na Katiba za nchi zingine zilizokuwa zilizokuwa makoloni ya Uingereza, hazikuwa na tamko kuhusu Haki za Binadamu.

Huo ndio ulikuwa mwanzo wa mfumo wa utawala wa rais dikteta, mwenye imla [imperial presidency],asiyeambilika au kushaurika; kwani chini ya kifungu cha 3 (3) cha Katiba hiyo, Rais alipewa mamlaka na uwezo wa kuongoza nchi atakavyo kwa vile hakulazimika kusikiliza au kupokea ushauri kutoka kwa mtu yeyote kuhusu masuala ya uongozi wa nchi.

Hali hiyo haijabadilika hadi sasa kama inavyobainishwa kwa maneno yale yale katika ibara ya 37 (1) ya Katiba yetu ya 1977 inayoendelea kutumika.

Kama kweli tunataka demokrasia ionekane kufanya kazi, tunapendekeza Rais atende kazi kwa ushauri wa Baraza la Mawaziri, na Bunge la nchi [sauti ya watu] lipewe mamlaka zaidi ya kutoa maelekezo kwa Rais bila hofu ya kuvunjwa na yeye kwa mamlaka aliyo nayo chini ya ibara ya 97 (4) ya Katiba ya sasa.

Katiba ya tatu [nayo ilikuwa ya muda] ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya 1964, ilianzishwa kwa kusudi la kukidhi matakwa ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, pale nchi mbili hizo zilipoungana, Aprili 26, 1964.

Katiba hii ilikuwa ni maboresho tu ya Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika ya 1962 kupitia Agizo la Rais [Presidential Decree] na kuitwa "Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano", wakati huo Jamhuri ya Muungano ikijiandaa kupata Katiba yake kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na Mkataba wa Muungano pamoja na Sheria ya Muungano.

Katiba ya Nne iliitwa "Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar" ya mwaka 1965 ambayo, kwa kutumia Kikao cha kawaida cha Bunge la kawaida [badala ya Bunge la Katiba kama ilivyotakiwa], ilipitishwa na kuanzisha Utawala wa Chama kimoja cha siasa badala ya vyama vingi, tofauti na ilivyokuwa kwa Katiba zilizotangulia.

Na chini ya marekebisho ya Katiba hiyo yaliyofanywa mwaka 1975, Chama cha Tanganyika African National Union [TANU], kilitangazwa "kushika hatamu" za uongozi wa nchi, ambapo vyombo vyote vya Serikali vilifanywa kuwajibika kwa Chama.
 
Mwanahabari Huru,
Unachanganya mambo na inaelekea hata ulichokiandika haukielewi, Marekani haijawahi kuandika Katiba mpya bali inarekebisha iliyopo, hakuna nchi Dunia hii inayoandika Katiba mpya bila ya kuwa na crisis of some kind halijawahi kutokea, na TZ hatuna crisis yoyote ile, hakuna tulipokwama, hivyo labda ungesema mabadiliko ya Katiba iliyopo lkn siyo Katiba mpya, hakuna uhitaji wa hilo TZ na yoyote anayefikiri kutakuwa na Katiba mpya TZ anajidanganya!
 
Ni muhimu sana kwa sasa ili tuweze kumdhibiti uchwara
Mmeshindwa kumtoa Mwenyekiti wa Maisha ndani ya chama ndo mtaweza kukitoa chama kilichoshikilia Dola! Amin amin nawaambia, mnapoteza muda wenu na kupigania matumbo ya viongozi wenu
 
Tunataka maendeleo kwa sasa haya mambo mengine yatakuja yatakapohitajika.......tushachoshwa na mambo ya siasa kila siku,,,,,,huu sasa ni mda wa kuendeleza nchi kama mtaendelea na hizo kelele sawa ni maamuzi yenu
 
Back
Top Bottom