Kwani wewe umeamua nini?

Amani Dimile

JF-Expert Member
Jul 27, 2022
243
395
Wewe umeamua nini?

By Amani Dimile

Mimi nimeamua kuendelea kuwa mwema mbele yao hata kama watanilipa mabaya, najua ikiwa hapa duniani hakuna anaethamini wema wangu basi yupo mbinguni anaeubariki. Wewe je, umeamuaje?

Mwenzio Mimi nimeamua kukubali kuonekana mshamba kwenye ardhi ya dhambi za vijana wa sasa, nimeamua kuonekana wa mwisho ili kuzikwepa fashion zisizo na utu wala kitu za binadamu hawa wa sasa?

Mimi binafsi, nimeamua kuwa mwanafunzi kwenye kila jambo ambalo silifahamu, sita sita kunyoosha mkono wangu kuuliza yale yote yenye ukakasi mbele ya ufahamu wangu.

Kwani wewe umeamuaje? Mwenzio nimeamua kumtumaini aliyeniumba tu. Hata kama nitakosana na hawa viumbe wa sayari hii kwa kuishi maisha yasiyowapendeza, ila najua nitamfurahisha aliyenijaalia pumzi kwa kuishi maisha aliyoyaagiza.

Zaidi ya yote nimeamua kuwa kiziwi, yale maneno yote yenye uchungu yaliyojaa kashfa na kejeli nimeamua nisiyaruhusu kupita kwenye masikio yangu. Acha waendelee kuongea, mbwa hazuiwi kubweka.

Nimeamua kutunza heshima yangu, nimeamua kuufumbata uaminifu ili nisishangazwe na usaliti. Nimeamua kuishi vyema ili kila ninapopita wazazi wangu wasifike kwa malezi bora.

Kwani wewe umeamua nini? Maana mi nimeamua kua kimya mbele ya watu ambao hata nisipojielezea sipotezi chochote kile. Nimeamua kua samaki mfumba mdomo, ili nisikamatwe kirahisi na ndoano za majini.

Nimeamua kuuzuia moyo wangu dhidi ya tamaa zisizo na kikomo. Nimeamua kuifunza nafsi yangu itosheke ili maisha yanisitiri na aibu zisizoelezeka.

Aaanh! Nimeamua mengi. Sijui wewe mwenzangu umeamua nini? Maana mi nimeamua kuamini Muda na Mungu na wala si ushindani na chuki.

Nimeamua kua mpole, nimeamua kujishusha mbele ya kila kitu ili nisichafue utu wangu. Sababu najua uaminifu, utu na heshima ni vitu vitatu vinavyoenda sambamba hivyo ukikikosa kimoja basi huwezi kupata vingine.

Ndugu yangu, we umeamuaje kwani?

Muandishi Amani Dimile
 
Back
Top Bottom