Kwako mheshimiwa rais

NGULI

JF-Expert Member
Mar 31, 2008
4,803
637
KWAKO MHESHIMIWA RAIS

Niandikapo barua hii nafikiria, natafakari na kutafakuri kwa uwingi wa mawazo usiokuwa na ukingo wala kufungwa kwa itikadi tena isiyo mgando,
Hivi karibuni yaliyotokea kule Arusha, yaliyojiri kule Mbeya na yaliyokupata k...utokea tukadhani yashakuwa historia kumbe mabichi kama kidonda kilichoachwa pasipo japo kumwagiwa maji yasiyo dawa japo nzi kupunguzia kule Temeke,

Mauaji ya Raia tena wasio hatia, hata hawaokuwa na yeyote iitwayo silaha, wakaitwa wachochezi, wakosefu wa amani, walipewa ufedhuli wa kutokutii Mamlaka na zile bado natingwa tena kwa wingi wa lindi la mawazo ziitwazo sheria,
Alipouwawa mwananchi kule katika kata ya Ubaruku Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kwa kutetea maslahi aitwae Mwekezaji, apewae lukuki haki, agaiwae ardhi mwanzo tulizokuwa tukiziita maeneo yaliyo hifadhi, au ya waitwao wananchi, hakuwa japo na mkuki, pinde, mundu au chochote cha kudhuru alichokuwa akitetea mzawa yake haki, mauti yakamfika kwa risasi yakawekezwa kwa kumtetea yule atukuzwaye haki kwa mbwembwe na kila hali apewae, nawaza sana sipati jibu, nafikiria mno sipati la japo kusadiki achana mbali na kusadifu,

Kwa ufupi japo nikijaribu kudurufu kile wananchi hao walichokiarifu kwa vyombo vya habari tukapata taarifu:
“Tunakuambia Mkuu sisi tunataka shamba letu na huyo polisi aliyefanya mauaji kwa sababu tunamfahamu. Nyie serikai ndiyo mmechangia haya mauaji kwani mmekuwa mkitunyanyasa sisi wazawa na kuwapendelea wageni. Sasa tunasema tumechoka, tupo tayari kufa kwa lolote hivyo tunalitaka shamba letu na huyo polisi aliyeua,” walilalamika.
Kabla hata sijamaliza hizi mbili kubwa kuziona tafakuri, kuzinyumbulisha kwa umakini napata nyingine nazo zaniacha na lindi la mawazo, wingi ukwazo na changamoto isiyo upago,

Mtoto Juma Malomo miaka kumi na miwili tu, labda alie na wingi wa ndoto kutimiza tena kwa maslahi ya lake Taifa akwamishwapo, risasi kwa kiumbe hiki kule Keko Molemo wilaya Temeke, TMK waitapo, katelekezwa na jeshi husika, ameachwa na yake familia isiyo na uwezo wa gharama zilizoletwa kwa labda ukosefu wa umakini, uharaka wa maamuzi na utumiaji wa nguvu pasipo yakinifu iliyojaa wake upembuzi na tafiti ya tele chunguzi. Eti walikuwa wanasakwa watuhumiwa na wengine waliokuwa tulivu ndani wakapewa uhusika na hata mdogo huyu kiumbe tarehe 24 Oktoba 2010 ikawa mwanzo wa kutunukiwa ulemavu usio rasmi, mzigo ulio mzigo wala si mithili bali zaidi ya zigo la kuni, masikini aulizapwo ndoto zake bado zingali zilizo huku machozi ya uchungu yammiminikapo kuwa Rais ama Rubani irukapo ndege angani apatapo angalizo.
Uwapi Mheshimiwa Rais, ziwapi sauti zisipwezwa kwa wingu la uzandiki wala upazo usio na thibitisho bali ukanushi usio thibitisho?

Kwako Mheshimiwa Rais, je tunahitaji mtu wa kutoka kimataifa, ughaibuni tuwapau utukuka hata kama hawastahili japo tuzo kuwatuza, hao juzi jana na leo tukaambiwa binadamu wa kwanza kuvumbua mlima Kilimanjaro, kiumbe wa kwanza kugundua wakafanya likaitwa kwa jina la Malkia lililo leo Victoria? Ingali miaka nenda rudi wakalikaa wenyeji na kudumisha uangalizi wa hizo tunzi lakini leo tusioohoji uwepo wa historia zisizo japo tija wala uhakiki wa ukweli usiohitaji darubini wala wingi wa tafakuri kuuhini?
Je kwa kukubali haya tuyaonayo, kwa kuyabeba hayo tuyasomayo na ukweli tuufichao kwa kuita kibwaya mkasema sarawili, kwa kutulisha shubiri wakataka tusifia tamu zaidi ya asali tena irutubishayo mwili,

Je tunahitaji mgeni aje kwa kumchezea sindimba, kumpigia gwaride na hotuba nzuri kumsomea kutuambia kuwa tuelekeako siko na 2015 yaweza kuwa maafa kwa sababu tunaachia sio tu nyufa bali pandikizi za chuki, ubinafsi, uzandiki, ubadhirifu, uhasama, unafiki na wingi wa dhuluma pasipo haki wala huruma? Je twahitaji huyo ili tuje nae tumuandike kwenye vitabu vilivyotukuka tele vya historia kwamba alikuja fulani kutoka nchi ile kubwa tamalani, alieona mbali na akawa wa kwanza kuona yatakayojiri katika nchi yetu isiyo ongofu bali tuliyoionea fahari kwa miaka nenda iliyo zaidi ya kenda kama kisiwa cha Amani?

Kwako Mheshimiwa Rais,
Kwa uchaguzi uliokuweka madarakani, ni uaminifu wa jamii iliyo imani na kukupa wewe unahodha kwa kuamini tuendako tutafika, Iweje leo, chombo kiendapo mrama, upepo uzidipo kadhia na wala si tu kwa kuona mbali udhia, wangaliao wasaidizi wa chombo wakaweka uadilifu kando, maslahi ya Taifa yakawekwa kwa kibindo na fedhuri, kebehi na dhihaka isiyo na chembe ya kweli kutaka kutamka kuwa hakuna kilicho mrama wala chombo hakiendi zama,
Kwako Mheshimiwa Rais,

Imekuwa leo ikawa werevu ni kwa kiasi gani mtu ameiba mali ya umma, uyakinifu ukawa ni kwa kasi gani mtumishi wa umma kaweza kulimbikiza si utambuzi wa uchapa kazi au umakini ulio na wingi wa ujuzi bali kasi ya kuchuma yaliyo mbivu na wanaostahili kuwatupia zisizo japo mbichi bali kuwapoka hata kidogo walichostahimili miaka nenda rudi kusubiri?

Uwapi wetu utaifa, nani aliyesema kila mmoja haki yake itapimwa kwa itikadi, utiifu na upofu wa hali halisi bali uanachama wa chama au kada fulani, je kweli hatutambui mamilioni ya walio wananchi wasio na chama na wengi waliochoshwa na ahadi na mbwembwe za itikadi zilizokosa utekelezwaji, uendelezaji bali kila ifikapo kipindi kunadiwa kwa midundo, shamirisho zisizo komo wala uhakiki ushindi ufikiwapo?
Hoja ya wagombea binafsi ipigwayo kumbo na kebehi kumilikishwa, kwani wote wafilisio na kuhujumu mengi wazi yaliyowekwa na mengine tusojua wamiliki lakini madeni tukaambiwa twapaswa kulipa, kwani hao walikuwa binafsi au bado wengine watukuzwao kwa itikadi na wingi wa heshima wengine hata mfano bora wa kuigwa twaambiwa?

Namuwaza mwananchi kule Mbinga, Muheza matunda aliyowekeza kuvuna shambani muda ukifika kumuozea nyumbani na kwa machache bei ya chini kuuza shurutika, kule Wete ahangaikae na jahazi mkono mmoja kupiga kadhia mwingine samaki chomboni kumvizia, vijijini mpaka mashambani, maziwani mpaka baharini, ukadhani mjini afadhali waishio maisha yasiyo tija wala staha wengi na hali za kustaajabisha,

Nisikiapo leo hii kizazi kilicho kichanga, kilichojaa kina beyonce na kutowatambua tena kuwabeza kina Zawose, Sinti Binti Saad, Shaaban mwana wa Robert, wapi alipo Bi Kidude sanaa leo sahaulika wakajaa kina minaj, lil fulani hata biz sijui wazi?
Japo labda chozi latiririka, nikitafakari tulikotoka, tulikopita na sasa tuelekapo kama meli iliyokumbwa na wingi wa upepo na kukosa stamilivu himili, lakini naamini bado hatujachelewa ingali tu wewe nahodha uliekabidhiwa chombo utapoamua si kusikiliza nyimbo nzuri za sifa na wingi wa tukufu ripoti za utekelezaji usio na chachu endelevu bali kutafakari zile pia zilizo chungu, pinganifu na zilizojaa mapendekezo yakinifu,

Nataka kucheza bado kwa furaha wapi mdundo ulipo mdundiko, wapi nijitupe na kujimwaya iitwayo sindimba, nicheze kwa fahari ritungu, huku taratibu nikinesa nisikiapo vanga, mnanda, mganda kwa mbali nasikia kibati nipisheni niingie katikati, kwetu Tanzania isifike kipindi afunguae mdomo kuitikia mpigo jadidu wake manju akaulizwa si kwa wake ustadi au tungo zilizo na jumbe kusema wazi mapungufu kwa kutakia heri na kujenga yaliyo sadifu bali akaulizwa ametokea wapi eti yeye si Raia wa nchi, historia yake leo ikakosa angalifu,

Ndimi,
Matukio OleAfrika Aranyande Chuma
16/01/2011
 
Naona umeanza kuongea mwenyewe! kweli maisha yamekuwa magumu. Pole sana, subiri miaka mitano ijayo.
 
Mkuu hili andiko linahitaji "kichwa" kulipata kisawasawa. Nimekuelewa vizuri sana. Kwa jinsi ninavyomfahamu jk, lazima ujumbe huu utamfikia kwa kusoma yeye mwenyewe au kupewa na wasaidizi wake. Jambo moja nina uhakika nalo, atasoma kama anavyosikiliza taarabu na muziki wa kizazi kipya. Usitarajie atachukua hatua yoyote ya maana pamoja na mazuri uliyogusia.
 
Jaribu kutumia lugha iliyo rahisi, naona una ujumbe mzuri lakini namna unavyoileta sidhani kuwa inaeleweka kwa wengi
 
Naona umeanza kuongea mwenyewe! kweli maisha yamekuwa magumu. Pole sana, subiri miaka mitano ijayo.

Tumia angalau busara kidogo kushirikisha ubongo wako katika mambo muhimu tafadhali
 
Hivi usha waandikia na wale waliochochea maandamano haramu?
 
Uheshimiwa wake ni wapi hasa? Katika cheo " Rais" au "yeye binafsi". Kama ni cheo nadhani hastahili kwani hakushinda kwa haki. Kama ni binafsi (personal) sawa.

Ila vyovyote vile, the guy is an absolute stinker of president!
 
Zomba umeandika vizuri na ujumbe wako unaeleweka. Kutokana na post (pamoja na comment zako) za nyuma imenilazimu kurudia mara tatu mada yako. Nimetambua kwamba mara nyingine huwa unafanya kusudi. Hatimaye umekubali kwamba Raisi hayupo!! Umeamua kumtafuta kupitia JF!! Hatimaye umeelewa tatizo tulilonalo ni kukosa Raisi! Hatujui alipo!
 
Zomba umeandika vizuri na ujumbe wako unaeleweka. Kutokana na post (pamoja na comment zako) za nyuma imenilazimu kurudia mara tatu mada yako. Nimetambua kwamba mara nyingine huwa unafanya kusudi. Hatimaye umekubali kwamba Raisi hayupo!! Umeamua kumtafuta kupitia JF!! Hatimaye umeelewa tatizo tulilonalo ni kukosa Raisi! Hatujui alipo!
Enzi hizo mtu

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Back
Top Bottom