Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,322
33,127
Tabaruku

Na mtaujuwa ukweli na ukweli utawaweka huru. – Biblia Yohane 8:32

Na sema: Ewe Mola wangu! Nipitishe kunako mlango wa ukweli na hishima, na nitowe kupitiya mlango wa ukweli na hishima. Na unipe nguvu kutoka kwako zenye ushindi zinisaidie. – Qur’ani 17:80


Kwa wananchi wote wa Zanzibar, kwa Wazanzibari na marafiki wa Zanzibar popote pale walipo duniani, ili watoke katika kiza totoro cha upotoshaji wa historia ya Mapinduzi ya Zanzibar, mojawapo ya matukio makubwa kutendeka katika nchi yao, Afrika Mashariki na Kati, na kusudi waelekee kwenye mwangaza wa kudumu utakaoyaimarisha na kuyangarisha maridhiyano yao na kufunguwa kitabu kipya cha kujijuwa na kujitambuwa.

Kwa Alhajj Rais Amani Abeid Karume kutokana na hikima, busara na ustahamilivu wa kibinaadamu na wa kisiasa anaouonyesha kwenye medani za Utawala wa leo Zanzibar, kuanzia kutochukuwa hatua ya kuyarejesha yaliyopita hadi kifo cha baba yake aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar baada ya mapinduzi, na kwa kujitahidi kwake kupatanisha kambi zilizofarakana kwa nusu karne, ni ushahidi unaotosha wa dhamira ya kuelekeya kwenye Zanzibar Mpya inayotamaniwa na kila mwananchi wake na kila mpenda amani duniani.

Ni majuzi tu ambapo katika historia ya nchi ya Zanzibar, Alhajj Rais Amani Abeid Karume na Alhajj Maalim Seif Sharif Hamad wameitekeleza ahadi waliyoitowa mbele ya ulimwengu ya kuyaweka maslahi ya nchi na utaifa wa Zanzibar mbele kuliko utashi wa kisiasa. Ahadi hiyo imepata baraka kamili za Baraza la Wawakilishi kutafuta suluhu ya kudumu itakayoungwa mkono na nguvu za wananchi wote ili kuumaliza mpasuko na mnaso wa kisiasa Zanzibar.

Kwa ajili ya ndugu zetu wa iliyokuwa Tanganyika, leo Tanzania Bara, ili kiwafunguwe minyororo ya utumwa wa nafsi iliyowafanya wawaone ndugu zao wa Zanzibar kuwa ni mahasimu zao wanaopaswa kuendeleya kudhibitiwa kwa nguvu zote. Hii leo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya utawala wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, imepata Raisi ambaye anapopata nafasi hupenda kukumbusha namna viongozi wa Kizanzibari walivyompaliliya na leo hii ni mmoja kati ya Marais vijana wenye utawala mzuri na umaarufu barani Afrika.
Furaha yangu ilifikiya kilele pale Rais Kikwete alipoizuru 1600 Pennsylvania Avenue, Washington DC, kama Rais wa Kiafrika wa kwanza kuonana na Rais Barrack Obama wa Marekani, ambaye mwenyewe ana asili ya jirani zetu wa Kenya. Inafahamika kuwa babu yake Rais Obama amewahi kuishi Zanzibar na kusoma ilimu ya dini ya Kiislam.

Kwa ajili ya Wazanzibari na Watanganyika kwa ujumla wao ili kitabu hichi kiwawezeshe kuzibadilisha nafsi zao. Waweze kuona fursa za mapenzi na neema zilizopo kwao wao na kwa ndugu na majirani zao wa jadi, na kisha wafanye kazi kwa pamoja katika kujenga Muungano Mpya na uhusiano mkongwe baina ya Waafrika na Waarabu—Afrabia—utakaosimama juu ya ukweli na hivyo kuimaliza kabisa mitikisiko na misukosuko ya muda mrefu.

Sina jengine la kuwatunukiya Watanzania Wazanzibari, Watanzania Bara, Waomani na Watanzania, Waafrika na Waarabu (Waafrabia) isipokuwa kitabu hichi ambacho ni tunda la fursa nyingi za ilimu ya bure ya msingi na ya sekondari niliyotunukiwa na Dola ya Zanzibar, pamoja na fursa za ilimu ya juu nilizotunukiwa na Dola ya Oman.

Namshukuru Mungu Muweza kwa wema na ukarimu nnaotunukiwa katika maisha yangu na ya aila yangu na kufaidika nao kutoka Serikali ya Sultan Qaboos bin Said Al Said kiongozi ambaye anautambuwa na kuuhishimu wajibu wa Oman na taarikh zetu kwa Zanzibar. Sultan Qaboos bin Said Al Said anasifika duniani kwa kujitenga na mizozano na kwa siasa yake ya urafiki na kila nchi, na amekuwa tegemeo la kimataifa katika jitihada za kuleta mapatano ya kudumu katika migogoro mikubwa ya kimataifa na kwa kulinda amani duniani.

Kwa unyenyekevu mkubwa nauomba uongozi na viongozi wetu adhiim wa pande mbili za Muungano na za uhusiyano mkongwe baina ya Waafrika na Waarabu—Afrabia, hadi raia kwa jumla, wake kwa waume, wakubwa kwa wadogo, vijana wa leo hadi Taifa letu la kesho, mkipokee kitabu chenu hichi kama ni kielelezo cha uzito wa nchi adhiim tuipendayo kwa dhati ya Zanzibar. Kwa wote hao, na kwa yote hayo natabaruku.
Nawaomba tusome kwa pamoja kutoka historia ya Zanzibar ya nusu karne iliyopita juu ya umuhimu wa kuishi na kuongeza mapenzi baina ya watu wa Tanzania Zanzibar, Tanzania Bara, Oman na Khaleej, na Afrika Mashariki na Kati. Muhimu katika kufanikiwa katika kheri ni kujipa nguvu za kuweza kutazama mbele na kusamehe juu ya kuwepo uwezo wa kulipa kisasi. Tusiuwachiye uchungu wa mitihani iliyotukumba kuzigeuza shingo zetu kuangaliya nyuma tulikotoka.Yaliyopita si ndwele tugange yajayo.
Mwisho, kabla hujaendelea kusoma kurasa zilizomo kwenye weblog hii ya Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!, unaombwa ubonyeze hapa ili kusoma maelezo yanayohusu hatimiliki na fursa zinazokhusu toleo hili la kwenye mtandao.
 
Back
Top Bottom