Mwaka mwingine wa maisha yetu sasa umepita. Mwaka mpya u mbele yetu. Je! kumbukumbu yake itakuwaje?
Kila mmoja wetu ataandika nini juu ya kurasa zake nyeupe?
Jinsi tunavyoitumia kila siku itaamua suala hili.
Hebu na tuingie katika mwaka mpya tukiwa na mioyo iliyotakaswa kutokana na uchafu wa uchoyo wetu na kiburi chetu. Hebu na tuweke mbali nasi kila anasa ya dhambi, na kutafuta kuwa waaminifu, na wanafunzi wenye bidii katika shule yake Kristo. Mwaka huu mpya unafungua mbele yetu kurasa mpya, nyeupe. Je! tutaandika nini juu yake?
Tafuteni jinsi ya kuuanza mwaka huu mkiwa na makusudi mema na nia safi, kama viumbe vinavyowajibika kwa Mungu wao. Daima kumbukeni kwamba matendo yenu yanapita kila siku na kuwa historia mbele ya kalamu ya malaika atunzaye kumbukumbu zetu. Mtapaswa kukutana nazo tena hapo hukumu itakapowekwa na vitabu vitakapofunguliwa. TUOMBE ombi hili Katika zaburi *Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima*. Zaburi 90:12
Iwapo tunajiunganisha na Mungu, aliye Chimbuko la amani, na nuru, na kweli, basi, Roho wake atabubujika kupitia kwetu, sisi tukiwa kama mfereji, kuwaburudisha na kuwabariki wote wanaotuzunguka.
Huu unaweza kuwa mwaka wa mwisho wa maisha yetu. Je! tusingeuingia tukiwa tunautafakari kwa makini? Je, unyofu, heshima, na ukarimu, visingekuwa shabaha ya mwenendo wetu kwa watu wote? Hebu na tusizuie kitu cho chote kwake Yeye aliyetoa maisha yake kwa ajili yetu....
*Wapendwa ndugu na dada zangu, Nawatakia kila mmoja wenu na wote, Heri ya Mwaka Mpya!*