Kwa nini CHADEMA wameiliza CCM? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kwa nini CHADEMA wameiliza CCM?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Apr 6, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Apr 6, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 58
  Trophy Points: 145
  Mwandishi Wetu


  [​IMG]


  Joshua Nassari


  USHINDI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika kinyang'anyiro cha ubunge Arumeru Mashariki wa Jumapili iliyopita kwa kiasi kikubwa msingi wake ni makosa ya kimkakati ya Chama cha Mapinduzi (CCM), pamoja na tuhuma za ufisadi zinazowaandama baadhi ya viongozi wa chama hicho,Raia Mwema, limeelezwa.

  Ushindi huo wa CHADEMA pia ni pigo kwa Kamati Kuu ya CCM ambayo ilifanya uteuzi wa mgombea kwa kuzingatia matarajio ya maslahi ya kisiasa (political expedience) badala ya kuzingatia msingi ya kikanuni (principles) ya chama hicho.

  Uteuzi wa Siyoi Sumari uliofanywa na Kamati Kuu ya CCM, hata hivyo, unatajwa kuzua malumbano makali miongoni mwa vigogo wa CCM, baadhi wakitajwa kuona dalili za mapema za kushindwa endapo mgombea huyo angepitishwa.


  Lakini kwa upande mwingine, ushindi huo wa CHADEMA moja ya nguzo zake pia ni baadhi ya wa wananchi kuchoshwa na viongozi wa CCM na Serikali, ambao, kwa mfano, katika Kata ya Kiwira, mkoani Mbeya ambako CHADEMA ilishinda udiwani dhidi ya CCM, malalamiko ya wananchi dhidi ya ufisadi wa viongozi wa kitaifa katika mgodi wa makaa ya mawe Kiwira yalizidisha chuki dhidi ya chama hicho tawala.


  Mara kadhaa, gazeti hili pia liliwahi kuripoti kuwapo kwa wafanyakazi wa mgodi wa makaa ya mawe Kiwira kutolipwa mishahara yao kwa miezi takriban 18 huku familia zao zikitaabika, wakishindwa kulipia karo za watoto wao. Malalamiko hayo pia yaliwahi kufikishwa bungeni na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, lakini hali ya utekelezaji wa ahadi za Serikali kuhusu kadhia hiyo ya mgodi wa makaa ya mawe Kiwira hazikutekelezwa kiasi cha kuridhisha.


  Lakini kwa upande wa Jimbo la Arumeru Mashariki ambako Joshua Nassari wa CHADEMA ameshinda dhidi ya Siyoi Sumari wa CCM, pengine wakazi wa jimbo hilo pia iliwashangaza kuwaona viongozi wale wale waliopaswa kutatua matatizo yao ya awali kama ardhi na huduma ya maji, wakiibuka na ahadi za kutatua kero hizo bila kujali kuwa walikuwa na nafasi hiyo miaka kadhaa iliyopita lakini walishindwa kupata ufumbuzi.


  Mbali na hayo, gazeti hili pia limeelezwa kuwa ushindi huo wa CHADEMA maana yake si tu ni kukimaarisha chama hicho katika safari yake ya kisiasa, na hasa ya kusafisha njia yake kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, bali pia ni kuwaimarisha viongozi wake wakuu, akiwamo Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Slaa.


  Dalili za CCM kushindwa Arumeru Mashariki zilijibainisha mapema baada ya kuanza kuhesabu kura kati ya saa 10 alasiri na saa 12 jioni. Ilipofika saa tatu usiku, matokeo mengi katika vituo yaliashiria CCM kushindwa.


  Uchunguzi wetu ulibaini kuwa, baada ya kusambaa kwa taarifa hizo hakuna kada hata moja kutoka timu ya kampeni ya CCM aliyesubiri matokeo ya mwisho. Wengine waliondoka usiku huo huo na kwenda kulala mjini Moshi.


  Miongoni mwa ‘waliokimbia' kabla mapambazuko ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM, Martin Shigela, na Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Beno Malisa.


  Kwa upande wake, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde aliondoka siku moja kabla ya kampeni kumalizika. Viongozi hao waliondoka wakimwachia ‘utawala binafsi' Siyoi mithili ya mtu aliyetelekezwa.


  Sababu za kushindwa CCM

  Kati ya sababu zilizomwangusha mgombea wa CCM, Siyoi ni mgombea huyo kujengewa taswira ya mtu anayetaka ‘kununua' ubunge.

  Siyoi alikuwa anahusishwa kisiasa na mtandao wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Kampuni ya Richmond, Edward Lowassa, ambaye pia ni mkwewe, na mtandao huo unadaiwa kuendesha siasa za matumizi makubwa ya fedha katika kufanikisha malengo yake, ikiwa ni pamoja na siasa za ndani ya CCM, mkoani Arusha na hata kitaifa.


  Kwa hiyo, kete mbili za ubunge si uongozi wa kurithishana (Siyoi alikuwa anapambana kurejesha jimbo la baba yake) na ile ya ubunge haununuliwi, ndizo zilizochangia kumwangusha Siyoi.


  Lakini pia baadhi ya wanasiasa wanaopinga siasa za matumizi ya fedha walitafsiri kuwa ushindi wa Siyoi ungeweza kuzidi kupandikiza tabia ya CCM kuamini katika siasa za fedha.


  Kutokana na mazingira hayo, baadhi ya wanaCCM wa Arumeru wamelithibitishia gazeti hili kuwa hakuwa tayari kumpigia kura Siyoi ili kuonyesha ari yao ya kupinga siasa za kutegemea nguvu ya fedha ndani ya chama chao. Miongoni mwa wanaCCM hao ni wale waliokuwamo katika kambi nyingine za wagombea waliochuana na Siyoi katika kura za maoni, ambako walizua malalamiko ya matumizi ya fedha lakini Kamati Kuu ya CCM iliwapuuza.


  "Kamati Kuu ilipuuza malalamiko ya wagombea wengine (kura za maoni CCM) ambayo yalikuwa yanatiwa nguvu na taarifa za kiuchunguzi za vyombo vya usalama, lakini viongozi wa juu wa chama walipuuza malalamiko hayo," alieleza mmoja wa wapiga kura ambaye ni mwanaCCM Arumeru Mashariki.


  Kiongozi mwingine wa CCM Arumeru Mashariki alisema; "Kampeni zilifanyika katika mazingira magumu hasa kutokana na wanachama wengi kutoridhia uteuzi wa Siyoi. Kulikuwa na mgawanyiko ulio wazi katika kata nyingi , kampeni zetu zilikosa hamasa kiasi cha kutosha."


  Sababu nyingine za kushindwa zinatajwa kuwa ni udhaifu wa mgombea katika jukwaa la kisiasa, hali iliyochangia kutowavuta wapiga kura ipasavyo. Hata hivyo, madai hayo yanapingwa na Mratibu wa Kampeni hizo wa CCM, Mwigulu Nchemba, ambaye amelieleza gazeti hili kwamba, mgombea huyo ni mwanasheria kitaaluma na kwa hiyo si rahisi kwake kushindwa kujieleza.


  Mbali na hayo, inaelezwa kuwa udhaifu mwingine uliosababisha anguko la CCM ni baadhi ya wapiga debe wake kutumia lugha zisizo za staha hadharani, wakiwashambulia viongozi wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Dk.Wilbroad Slaa pamoja na Meneja wa Kampeni wa chama hicho, Vicent Nyerere.


  Lowassa amfunika Siyoi CCM Arumeru

  Katika hali isiyo ya kawaida,ushiriki wa Edward Lowassa binafsi kwenye kampeni hizo unatajwa kuinyang'anya ushindi CCM huku ikidaiwa kuwa wapo baadhi ya wana CCM waliopinga Lowassa kushiriki wakiamini tuhuma zinazomkabili zitakuwa mtaji wa ziada wa kuimarisha jukwaa la siasa la CHADEMA.

  Wakati vigogo wa kampeni wakilumbana, CHADEMA waliendelea kujisafishia njia ya ushindi.


  "Uamuzi wa kumruhusu Lowassa uliwagawa makada, kikaoni walifikia hatua ya kutiana masumbwi baada ya watu waliokuwa wakimtetea kuelezwa kuwa ‘mtu' wao bado amezungukwa na wingu la ufisadi," anaeleza mtoa habari wetu aliyeshiriki kikao hicho.


  Taarifa zinaeleza kuwa siku nne kabla ya ujio wa Lowassa kulikuwa na kikao cha ndani kufanya tathmini ya ujio na ushiriki wake katika kampeni.


  "Makada waliokuwa wanamuunga mkono Lowassa wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Beno Malisa na Katibu Martin Shigela walishinikiza wakisema, Lowassa anakubalika Arumeru hivyo anapaswa kusimama jukwaani kumnadi mgombea wao.


  Baada ya kikao hicho kilichofanyika katika Hoteli ya Gate Ways, kuelekea kuridhia ushiriki wa Lowassa, mmoja wa wabunge aliwaeleza wajumbe wenzake:

  "Naomba muandike kwenye muhtasari wa kikao hiki kuwa mimi nimesema sikubaliani na ujio wa Lowassa kwenye kampeni hii. Namheshimu sana Lowassa lakini hapa si mahala pake na naomba msimamo wangu ueleweke hivyo."


  Katika hatua nyingine, ndani ya kikao hicho mbunge mmoja (jina linahifadhiwa) anadaiwa ‘kumkwida' shati na kumzaba vibao mjumbe mwingine ambaye ni mfanyabiashara maarufu aliyekuwa anashinikiza Lowassa ashiriki kampeni hizo.


  Viongozi wa dini

  Zipo taarifa kuwa tofauti miongoni mwa wana CCM waliokuwa Arumeru zikichemka, kulikuwapo mikutano ya ndani ya vigogo wa CCM na viongozi wa dini, hasa madhehebu ya kikristo na wazee wa jamii ya Wameru, kuwashawishi wamkubali Siyoi.

  "Kwa mfano katika kikao kimoja ambacho mmoja wa vigogo wa CCM, Lowassa, alishiriki na viongozi wa madhehebu ya KKKT, Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Meru, Mhashamu Paul Akyoo, alimhoji Lowassa sababu za kushinikiza kuwachagulia wananchi wa Arumeru mbunge na kutafsiri hatua hiyo kuwa ni dharau kwa Wameru," kinaeleza chanzo chetu cha habari.


  Akimkariri Askofu Akyoo mtoa habari wetu anaeleza: "Wewe (Lowassa) uliwahi kuwa kiongozi wa juu wa nchi na ni mbunge wa Monduli, tunakuheshimu sana lakini unapata wapi ujasiri wa kutuchagulia kiongozi wa eneo letu? Na kwa nini kama una nia njema hujatushirikisha mapema kabla ya kufanya uamuzi huo?"


  Taarifa hizo zinaeleza kuwa, kwa unyenyekevu mkubwa Lowassa anadaiwa kuomba msamaha kwa kujibu kuwa ilikuwa ni kwa bahati mbaya tu lakini uamuzi wa kuwashirikisha viongozi na wazee ulikuwapo na kwamba tofauti hizo ndogo zisiathiri kampeni za mgombea wa CCM.


  Sababu nyingine ya kuanguka kwa CCM inatajwa kuwa ni maisha magumu yanayowakabili wananchi wa Arumeru Mashariki, wakiamini msingi wa hali hiyo ni viongozi wa CCM.


  Kauli za viongozi wa CCM

  Akizungumza na Raia Mwema kwa njia ya simu Meneja kampeni wa CCM, Mwigulu Nchemba alisema; "Suala la mgombea wetu kutokuwa na uwezo wa kujenga hoja siafikiani nalo kabisa.

  "Kwa ufahamu wangu Siyoi ni mwanasheria na kwa kawaida hao huzungumza kwa utaratibu sana ili aweze kueleweka, hivyo mgombea wetu alikuwa na uwezo mkubwa tu wa kuzungumza na wapiga kura.


  "Kuhusu malalamiko juu ya ushiriki wa Lowassa katika kampeni hii nayo si hoja kwa kuwa katika Kata ya Kikatiti ambayo alipiga kampeni, CCM tulishindwa kwa kura 300 na ilikuwa ni kati ya kata ambazo tulishindwa kwa idadi ndogo ya kura kuliko kata nyingine, kwa hiyo hizo hoja mufilisi," alisema Mwigulu.


  Baadhi ya wanasiasa waliozungumza na Raia Mwema wanasema kuanguka kwa CCM safari hii kutakuwa ni fundisho kubwa kwake kwamba waelewe kwamba huu ndio mwanzo wa mwisho wa siasa za fedha na matusi.


  " Hili litakuwa ni fundisho kubwa kwa CCM. Wajue kwamba sasa siasa za fedha na matusi si mali kitu, zimefika kikomo. Lakini pia kwa jinsi walivyopokea matokeo hayo tuseme pia kwamba wanastahili pongezi, maana wamekubali moja kwa moja.


  " Katika siku zijazo CCM wasidharau chuki ya raia kwa vitendo vya kifisadi. Hiki ni kizazi kipya cha wapiga kura, kinachukia ufisadi ambao kinaona unasaidia kukididimiza. Lakini vyama vingine navyo vijifunze. Ni vyema pia kuipongeza Tume ya Uchaguzi. Ni mwanzo mzuri kwa mzee Jaji Damian Lubuva lakini hata Polisi nao wapongezwe maana ile mikiki yao safari hii haikuonekana sana," anasema mchambuzi mmoja.


  Ushindi wa Joshua Nassari

  Tofauti na mgombea wa CCM, Nassari alikuwa na uwezo wa kujieleza mwenyewe mbele ya wananchi na kuomba kura.

  Ushindi huo wa Nassari pia ulitiwa chachu na matatizo ya wanaArumeru hususan matatizo ya ardhi na huduma ya maji.


  Katika ajenda ya maji, Nassari alihoji sababu za kukosa maji wakati maji yanayotumiwa na wananchi wa miji ya Arusha na Monduli yanatokea Arumeru na hoja iliyowagusa sana wapiga kura wengi.


  Uchaguzi huo mdogo ulifanyika Jumapili ya Aprili Mosi, mwaka huu, katika jimbo hilo ambapo mgombea wa CHADEMA Joshua Nassari alibuka na ushindi wa kura 32,699 dhidi ya Sioi Sumari wa CCM, aliyepata kura 26,757.
   
 2. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #2
  Apr 6, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 58
  Trophy Points: 145
  Na bado watachanganyikiwa kabla ya 2015...
   
 3. m

  mgeni wenu JF-Expert Member

  #3
  Apr 6, 2012
  Joined: Jan 2, 2012
  Messages: 3,669
  Likes Received: 614
  Trophy Points: 280
  Nina imaani na Sumaariii oyaaah,oyaah oyaah x2 sumarii kweeliii,kweli,kweelii, kwelikwelikweli Sumariii..by. BWM(aka)fupi lao
   
Loading...