Kwa hotuba hii ya Lissu, Prof. Kabudi ana mtego wa kuikana nafsi yake na maandishi ya taaluma yake

Nini hatma ya Kabudi dhidi ya kile alichokiamini na nafas aliyonayo leo?Umeisoma hotuba ya Lissu?Ameeleza mambo kwa facts tupu hapo na mifano.

Hatima ya kabudi ni kukana anachokiamin hyo inajuliana mm nimependa uwezo wake wa kujenga hoja
 
Mb
Uzuri wa Lissu ni kushameakili ya wasomi kama wanasahau akili madarasani wanapoenda Bungeni au laah!
Wakati fulani Lissu alijitapa kama mwasisi wa ile iliyoitwa list of shame na akawa tayari kututhibitishia uhalali wa hiyo orodha ya uchafu wa akina Lowasa. Lakini leo hii yuko tayari kumpigia magoti Lowasa na ni ndiyo mzee kwa kila lisemwalo na Edo. Kwa hivyo hana haja ya kushangaa lolote litakalofanywa na Prof. Kabudi.
 
Sawa kamanda Lissu ila sijaona ulipoongelea uteuzi wa makada wa ccm kwenye nafasi za wakurugenzi wa halmashauri ilihali watatakiwa kusimamia chaguzi kama wasimazi wakuu katika halmashauri husika. Sasa hapa ungeweka bayana sheria zinasemaje kuhusu hili suala, na fisi ataweza kuwalinda kondoo? Naomba hili litafutiwe namna na lijengewe hoja huko bungeni
Majibu yake yako kwenye katiba mpya ambayo ilipendekezwa na Tume ya jaji warioba. Imepiga pini hizo teuzi za aina hiyo.
 
Hio hamasa ilikuwa kwa sababu walikuwa ni wajumbe wa Tume ya Katiba mpya (maoni ya wananchi na msimamo wa wananchi kulingana na asilimia).

Ila kama ungeweza kuwatenganisha na ujumbe wa ile Tume ya Katiba basi wote hao ni waumini wa serikali mbili (msimamo na imani yao binafsi).
Ndg yangu, sio busara kushangilia na kusifu, hata watu kukosa msimamo. Kukosa msimamo sio MSIMAMO, bali ni kuganga njaa. HIVI, Kuna cha kujivunia hapo?
 
Maprofesa huwa na za kwao wakiwa nje ya system, wakiwa ndani ya system ni mapropesa nafsi kwanza Taifa baadae.
 
Inawezekana kamzidi that is fine.but ameonyesha kuwa mtu asiyesimamia itikadi na misimamo yake.kipindi yuko kwenye tume na baada ya ile ripoti tulikua tunamsikiliza kwenye midahalo mbali mbali kuhusu katiba mpya tena ilikua inaonyeshwa live na ITV alikua mkali sana na alidai katiba mpya kwa kusema wamepita nchi nzima wameona wananchi wanataka katiba mpya.asifikiri tumesahau tulimuona kwa macho yetu tena kipindi hicho waziri huyu wasira alikua anapingana nao sana kwenye midahalo but wao kina kabudi walishikilia sana misimamo yao.leo kapewa uwaziri anasema si muhimu simuelewi kabisa na amenifanya nisimuamini na kumfatilia tena kama gwiji wa sheria.lol anadhalilisha taaluma ya wanasheria
Wanaoweza kushinda mtihani wa njaa huku Africa, ni wa kutafuta saana. Mungu anatupenda sana kwa kuendelea kuwafunua hata wale tuliyodhani wanaaminika.
 
"even you Brutus" do you know this quote??@!
Ha ha ha ha hayo mambo ya kusalitiana ya Marcus Brutus na Julius Caiser
Alimpiga kisu cha mgongo,Julius anageuka anaona anyemuuwa ni rafiki kipenzi chake aliyemuamini...Julius akaishia kusema tu "Et tu,Brute?"....."Hata Wewe Brutus?"
 
Kuna watu humu wanashangaza sana mtu km mada ipo juu ya uwezo wako sio lazima uchangie.mbona watu wengi wanasoma na kupita kimya kimya?Acheni kujitoa akili kwenye mjadala wa mambo ya maana mnaboa sana. SIO LAZIMA KUCHANGIA MADA KHEEEEEE
Na wewe tayari ushachangia, ungekaa kimya tu kama haikupendezi
 
  • Thanks
Reactions: SDG
Wao walipaswa kuwa neutral by then,wamekusanya maoni,wameyawasilisha sio KUYASHABIKIA maoni yale na ndio maana leo wana aibika
Kama nao ulikuwa msimamo wao kwa ajili ya mustakabali wa taifa lao, sioni hilo swala la kuaibika linavyoingia hapa. labda kwa wale waliokuwa wanashabikia.
 
MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA, MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.) KUHUSU MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA 2017/2018
(Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2016)

UTANGULIZI​
Mheshimiwa Spika,
Hii ni mara yangu ya saba kusimama mbele ya Bunge lako tukufu na kutoa Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu kuhusu Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria. Tangu mwaka 2010 hadi mwezi uliopita, Wizara hii imeongoza kwa kuwa na mabadiliko mengi ya mawaziri kuliko Wizara nyingine yoyote. Kama utakavyokumbuka, Mheshimiwa Spika, mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, mtu wa kwanza kuteuliwa Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria alikuwa marehemu Mheshimiwa Celina Ompeshi Kombani. Hakumaliza mwaka mmoja, kwani nafasi yake ilikabidhiwa kwa mwanasheria Mathew Meindrard Chikawe.

Mheshimiwa Chikawe alidumu kwenye nafasi hiyo kwa takriban miaka mitatu. Ilipofika mwezi Disemba 2014, Waziri Chikawe aliondolewa na nafasi hiyo ikakasimishwa kwa mwalimu wangu wa sheria, Mheshimiwa Dkt. Asha-Rose Mtengeti-Migiro. Huyu alidumu kama Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria hadi mwezi Disemba, 2015, wakati nafasi yake ilipokasimishwa kwa mwalimu wangu mwingine wa sheria, Mheshimiwa Dkt. Harrison George Mwakyembe. Sasa, baada ya mwaka na miezi mitatu, nafasi ya Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria imekabidhiwa kwa kaka yangu na mwalimu wangu wa tatu wa sheria, Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi.

Kwa ushahidi huu, Mheshimiwa Spika, tangu niwe Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, tumekuwa na Waziri tofauti wa Mambo ya Katiba na Sheria kwa takriban kila baada ya mwaka mmoja na miezi mitatu. Kwa vyovyote vile inavyoweza kuelezewa, hii ni rate of turnover kubwa sana katika uongozi wa Wizara yoyote ile. Na kama nilivyosema mwanzoni, katika kipindi hicho, hakuna Wizara nyingine yoyote katika Serikali hii ya CCM ambayo imekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara namna hii.

Mheshimiwa Spika,
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, mabadiliko haya ya mara kwa mara ya Mawaziri wa Mambo ya Katiba na Sheria yanaashiria kitu kimoja kikubwa: Mawaziri husika walishindwa, ama kwa sababu zao binafsi ama kwa sababu za mfumo wetu wa kisiasa na kikatiba, kuiongoza nchi yetu katika kutatua matatizo makubwa ya kisiasa na kikatiba ambayo yameikabili nchi yetu kwa miongo kadhaa. Tumeyazungumza matatizo haya kwa kipindi chote ambacho nimekuwa Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika,
Mheshimiwa Prof. Kabudi anaweza kuwa mgeni katika Bunge lako tukufu na katika Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria. Hata hivyo, Mheshimiwa Prof. Kabudi sio mgeni hata kidogo katika uelewa wa matatizo makubwa ya kisiasa na ya kikatiba ya nchi yetu. Mwaka 1984, Mheshimiwa Prof. Kabudi akiwa mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliandika Thesis yake kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, The International Law Examination of the Union Between Tanganyika and Zanzibar. Katika Thesis yake, Prof. Kabudi alikuwa mtu wa kwanza kuweka hadharani ushahidi wa nyaraka wa chanzo cha ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar’ mwaka 1983-84, kulikopelekea kung’olewa madarakani kwa Rais wa Pili wa Zanzibar, Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi.

Mheshimiwa Spika,
Utaalamu wa Mheshimiwa Prof. Kabudi haukuishia kwenye uelewa wake wa masuala ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Mwaka 1985, Prof. Kabudi na Dkt. Aggrey K.L.J. Mlimuka walikuwa wasomi wa mwanzo kabisa kuelewa na kuelezea historia ya jinsi chama kimoja, kwanza TANU na baadae CCM, kilivyotumika kulimbikiza madaraka makubwa kikatiba na kisheria kwa Serikali na, ndani ya Serikali, kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Makala yao, ‘The State and the Party’, yaani ‘Dola na Chama’, katika The State and the Working People in Tanzania, kitabu kilichohaririwa na Prof. Issa G. Shivji na kuchapishwa mwaka 1985, ilikuwa andiko la kwanza la kisomi kuelezea dhana ya ‘chama-dola’ katika mfumo wetu wa kisiasa na kikatiba, na jinsi chama-dola hicho kilivyovunja nguvu ya Bunge kama chombo kikuu cha maamuzi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,
Kwa sababu ya utaalamu na uelewa wake mkubwa wa masuala muhimu ya kikatiba na kisheria ya nchi yetu, mwaka 2012 Mheshimiwa Prof. Kabudi aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, maarufu kama Tume ya Warioba. Kama inavyofahamika, Tume hiyo ndiyo iliyokusanya maoni ya waTanzania, kuandaa Ripoti na Rasimu ya Katiba Mpya kwa ajili ya nchi yetu na kuiwasilisha mbele ya Bunge Maalum mnamo mwezi Aprili, 2014.

Kama mwanafunzi wake na mmoja wa wale ambao tumefuatilia maisha ya kitaaluma ya Mheshimiwa Prof. Palamagamba Kabudi kwa karibu, ninaweza kusema bila wasi wasi wala shaka yoyote kwamba Ripoti ya Tume ya Warioba na Rasimu ya Katiba Mpya ina alama za vidole vya kitaaluma vya Prof. Kabudi kuliko, pengine, vya mjumbe mwingine yeyote wa Tume hiyo. Na kusema hivyo hakuna maana ya kudharau michango ya Wajumbe wengine wote wa Tume ya Warioba, bali ni kutambua mchango mkubwa wa Waziri wa sasa wa Mambo ya Katiba na Sheria katika mchakato huo wa kihistoria katika nchi yetu.

Kwa sababu zote hizi, wakati ni halali kabisa kumpongeza Mheshimiwa Prof. Kabudi kwa kuteuliwa katika nafasi yake hii mpya, ni vizuri kumkumbusha juu ya majukumu makubwa na mazito ambayo nafasi yake hii inamlazimisha kuyabeba. Na ni vizuri zaidi kumkumbusha kwamba mazingira ya utekelezaji wa majukumu hayo yanamlazimisha kuchagua kati ya kusimamia maslahi ya kweli na ya kudumu ya nchi yetu – ambayo yanajionyesha katika maandiko yake ya kitaaluma na katika Ripoti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba – na maslahi ya muda ya kisiasa ambayo mara nyingi hayana na maisha marefu. Tutaanza na suala la Katiba Mpya.


YA KATIBA MPYA

Mheshimiwa Spika,
Katika Taarifa yake kwa Kamati ya Kudumu ya Katiba na Sheria ya mwezi uliopita, Mheshimiwa Prof. Kabudi amezungumzia suala la Katiba Mpya kwa aya moja tu yenye kichwa cha habari ‘Mambo ya Katiba.’ Kwa mujibu wa Mheshimiwa Waziri, “Serikali ya Awamu ya Tano inatambua umuhimu wa nchi kuwa na Katiba Mpya. Hata hivyo, ikumbukwe kuwa mara baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani ilianza kazi kwa kuunda Serikali na kufanya mapitio ya kina ya miundo na mifumo ya kiutendaji. Kwa sasa, baada ya kazi hiyo kukamilika Serikali inapitia sheria zinazohusika na mchakato wa mabadiliko ya Katiba kwa madhumuni ya kubaini utaratibu mzuri wa kuendelea na mchakato huo kutoka pale ulipoishia.”

Mheshimiwa Spika,
Taarifa hiyo imeainisha mambo saba ambayo Mheshimiwa Waziri ameyaita ‘maeneo mahususi ya kipaumbele.’ Kati ya hayo, hakuna jambo hata moja linalohusu Katiba Mpya, ambayo hata haijatajwa kabisa. Aidha, katika ‘mchanganuo wa matumizi ya bajeti kwa kila Fungu’, hakuna Fungu hata moja linalohusu Katiba Mpya. Vile vile, katika vitabu vya Randama kwa Mafungu yote sita yaliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria, hakuna kasma hata moja ambayo imetengwa kwa ajili ya Katiba Mpya.

Kwa maneno mengine, Mheshimiwa Spika, mchakato wa Katiba Mpya, ambayo Mheshimiwa Waziri anataka tuamini kwamba haujauawa na Serikali ya Awamu ya Tano, haujatengewa hata senti moja katika bajeti inayopendekezwa kwa Bunge lako tukufu mwaka huu. Na huu ni mwendelezo wa bajeti ya mwaka jana ambayo nayo haikutenga hata senti moja kwa ajili ya mchakato wa Katiba Mpya.

Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yangu juu ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2015/2016, nilielezea kwa kirefu jinsi ambavyo ‘Katiba Mpya imekwama.’ Tarehe 26 Aprili, 2014, yaani The Golden Jubilee ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambayo Rais Jakaya Kikwete aliwaahidi wa Tanzania kuwa ndiyo tarehe ya nchi yetu kuwa na Katiba Mpya, ilifika na ikapita bila ya nchi yetu kuwa na Katiba Mpya.

Tarehe 30 Aprili, 2015, ambayo Rais Kikwete aliwaahidi wananchi kuwa ndiyo ingekuwa siku ya kufanyika kwa kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa - ahadi ambayo ilirudiwa rudiwa na kila kiongozi wa CCM na Serikali yake ndani na nje ya Bunge hili tukufu – ilifika na kupita bila kura ya maoni kufanyika.

Baada ya hapo, na kwa kipindi kilichobakia cha utawala wa Rais Kikwete, viongozi wa CCM na Serikali waliendelea kusisitiza, ijapo kwa sauti za kinyonge, kwamba kura hiyo ya maoni ingefanyika katika tarehe ambayo, hata hivyo, hawakuwa tayari kuitaja tena. Haikufanyika hadi wakati Rais Kikwete anaondoka madarakani na Rais Magufuli anaingia madarakani. Ndio maana nilisema, katika Maoni yangu ya mwaka juzi, kwamba, “kwenye signature issue ya utawala wake, yaani Katiba Mpya, huyu ni Rais aliyeshindwa (na) hii ni Serikali iliyoshindwa.”

Mheshimiwa Spika,
Rais John Pombe Magufuli ameshatangaza hadharani kwamba Katiba Mpya sio kipaumbele cha Serikali yake. Rais amedai kwamba wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015, yeye hakutoa ahadi yoyote kwa waTanzania kwamba atawaletea Katiba Mpya akichaguliwa kuwa Rais. Kwa hiyo, kwa msimamo huo wa Rais Magufuli, mchakato wa Katiba Mpya ambao, hadi ulipoishia kwa kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa, ulikwisha kugharimu jumla ya shilingi bilioni 121.463, umekwishakufa na kuzikwa.

Mheshimiwa Prof. Kabudi ni mtu mwelewa sana wa siasa za kikatiba za Tanzania. Kwa uelewa wake mkubwa wa masuala haya, Prof. Kabudi anafahamu vema kivuli kirefu cha ‘Urais wa Kifalme’, ambayo ndiyo imekuwa ‘the organizing principle’ ya katiba na siasa za Tanzania tangu mwaka 1962 ilipotungwa Katiba ya Jamhuri. Kwa uelewa wake huo, Mheshimiwa Prof. Kabudi anafahamu, au anatakiwa kufahamu, kwamba, kwa Katiba na Sheria za Tanzania, na kwa mila na desturi zake za kisiasa na kikatiba, Rais akishasema hawezi kubishiwa na Waziri wake. Ni suala la – kama wasemavyo Wakatoliki - *Roma locuta*, *causa finite*, yaani Roma ikishasema, ndio mwisho wa mashauri!

Kwa sababu hiyo, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inataka kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, Serikali ya Awamu ya Tano inatambuaje umuhimu wa nchi yetu kuwa na Katiba Mpya wakati Rais Magufuli amekwishasema Katiba Mpya sio kipaumbele cha Serikali yake? Na, je, kama kweli Serikali hii ina mpango wa kuuendeleza mchakato wa Katiba Mpya kutoka pale ulipoishia, ni kwa nini Serikali hii haijatenga hata senti moja kwenye bajeti hii kwa ajili ya jambo hili muhimu?

Bila majibu ya kweli kwa maswali haya, Waziri Kabudi atakuwa ameangukia kwenye shimo lile lile walimoangukia watangulizi wake wanne: kushindwa kutekeleza matakwa na matarajio ya waTanzania ya kupata Katiba Mpya na ya kidemokrasia itakayokidhi mahitaji ya kizazi hiki na vizazi vijavyo. Na sio ajabu, maisha yake kama Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, yakawa mafupi kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake.

YA HAKI ZA BINADAMU
Mheshimiwa Spika,
Katika Taarifa yake kwa Kamati, Mheshimiwa Prof. Kabudi alidai kwamba “Wizara iliendelea kuimarisha na kusimamia uzingatiwaji wa misingi ya haki za binadamu kama ilivyoainishwa na kuhifadhiwa katika Katiba na sheria za nchi....” Madai haya hayaelezi hali halisi ya haki za binadamu katika nchi yetu. Ukweli ni kwamba kauli ya Mheshimiwa Prof. Kabudi inapotosha ukweli juu ya haki za binadamu katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,
Badala ya kupungua, matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na, hasa, vyombo vya ulinzi na usalama, ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu imeyapigia kelele kwa muda mrefu, yameendelea kuongezeka. Aidha, matukio ya nyuma ya ukiukwaji wa haki za binadamu hayajatatuliwa wala wahusika kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria zetu. Kwa mfano,

 Mauaji au mashambulio dhidi ya viongozi wa kidini na waumini wao na sehemu zao za ibada yaliyotokea Zanzibar kati ya mwaka 2012 na 2013 hayajatatuliwa hadi leo;

 Hakuna aliyetiwa hatiani wala kuadhibiwa kwa kuhusika na shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki Olasiti Arusha lililoua watu watatu na kujeruhi wengine wengi na wala Serikali hii ya CCM haijatoa taarifa yoyote rasmi hadharani au Bungeni juu ya wahusika wa mauaji na mashambulio hayo na sababu zake;

 Mauaji na mashambulio ya waandishi wa habari na wanaharakati wengine kama madaktari yaliyotokea kati ya 2012 na 2013 hayajatatuliwa pia. Waliohusika kumteka nyara na kumtesa Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka, hawajakamatwa hadi leo licha ya majina yao kujulikana;
 Hakuna aliyekamatwa wala kuadhibiwa kwa kumteka nyara na kumtesa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Absalom Kibanda, na wala Serikali hii ya CCM haijatoa taarifa yoyote rasmi hadharani au Bungeni kuhusu shambulio hilo linalofanana na shambulio dhidi ya Dk. Ulimboka;

 Hakuna askari polisi aliyekamatwa wala kuadhibiwa kwa kushambulia mikutano halali ya CHADEMA kwa mabomu na risasi za moto ambako watu wengi waliuawa au kujeruhiwa katika miji ya arusha na Morogoro;
 Ukiachia Mawaziri wa wa Ulinzi, Mambo ya Ndani, Maliasili na Utalii na Mifugo waliolazimishwa kujiuzulu nyadhifa zao, wale walioua, kutesa na kulemaza Watanzania na kuwaibia au kuharibu mifugo na mali zao nyingine wakati wa Operesheni Kimbunga na Operesheni Tokomeza Ujangili hawajakamatwa wala kuchukuliwa hatua zozote za kisheria;

 Serikali hii ya CCM haijatoa hadharani wala bungeni taarifa ya Tume ya Uchunguzi ya Jaji Msumi iliyoundwa na Rais Kikwete kupitia Tangazo la Serikali Na. 131 la tarehe 2 Mei, 2014, ili kuchunguza matukio haya ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Kwenye Maoni yangu ya mwaka 2014, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu ilisema kuhusu mmojawapo wa Makamishna wa Tume hiyo kuwa “... ana rekodi ya kutumiwa na Serikali hii ya CCM kuisafisha Serikali kwa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na watendaji wa Serikali.”

 Maafisa wa Jeshi la Polisi na watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa walioshirikiana kuwabambikizia viongozi na wanachama wa CHADEMA kesi za uongo za ugaidi zilizopelekea wengi kuteswa kwa ukatili mkubwa baada ya kukamatwa na kuhojiwa katika vituo vya polisi hawajachukuliwa hatua yoyote;

Mheshimiwa Spika,
Katika mazingira haya ya impunity, Katika Maoni yangu ya mwaka 2014, nililiambia Bunge lako tukufu kwamba “Serikali hii ya CCM imeitia demokrasia kitanzini na inatishia kuinyonga na kuiua.”
Miaka miwili baadae, yaani mwaka jana nilirudia tena kauli hii. Katika Maoni yangu ya mwaka jana, nilisema yafuatayo kuhusu hali ya demokrasia katika nchi yetu: “... [P]ale serikali inapoamua kunyamazisha upinzani, inakuwa na njia moja tu ya kupita, nayo ni njia ya kuongezeka kwa vitendo vya kikandamizaji, mpaka serikali hiyo inakuwa chanzo cha hofu kwa wananchi wake wote na inatengeneza nchi ambapo kila mmoja anaishi kwa hofu.”
Nilitoa mifano ifuatayo kuthibitisha kauli yangu hiyo:

 Mbunge wa Jimbo la Kilombero, Mh. Peter Ambrose Lijualikali, aliyekuwa “... anakabiliwa na mashtaka ya jinai mahakamani kwa kosa la kutetea demokrasia na utawala wa sheria na kukataa utawala wa mabavu na udikteta.”

 Jiji la Tanga ambako baada ya CCM kukataliwa na wananchi, Serikali hii ilitumia ghilba na mabavu ya kila aina kuhakikisha CCM inanyakua Umeya wa Jiji hilo, na baadae viongozi wa vyama vya UKAWA na madiwani waliochaguliwa na wananchi kufunguliwa mashtaka ya uongo kwa sababu tu ya kukataa kwao kutawaliwa na watu ambao hawakupata ridhaa ya wananchi;

 Mkakati wa kunyamazisha vyombo huru na binafsi vya habari kwa kufuta magazeti na kufungia vituo binafsi vya radio vinavyotoa habari zisizowapendeza watawala, na kutishia hatua hiyo hiyo kwa vyombo vingine vya habari;

 Mkakati wa kulinyamazisha Bunge ili lisiendelee kuwa chombo cha kuiwajibisha Serikali kwa kufuta matangazo ya moja kwa moja ya televisheni, kuingilia utaratibu wa kupanga wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge, kupuuzwa kwa uhuru wa wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na Bunge kuongozwa kwa maagizo ya Ikulu na ya Mawaziri kama tunavyoshuhudia kila mara ndani ya Ukumbi huu wa Bunge lako tukufu;

 Kupigwa marufuku kwa shughuli za kisiasa, kama mikutano ya hadhara na maandamano, ambazo ni halali kwa mujibu wa Katiba yetu na Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni zake;

Mheshimiwa Spika,
Yaliyotokea kabla na wakati ninatoa Maoni yangu ya mwaka jana yalikuwa ni madogo ikilinganishwa na yaliyokuja kutokea baada ya Maoni hayo. Hata kabla ya Bunge la Bajeti la mwaka jana halijamalizika, wabunge wengi waandamizi wanaounda Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, walisimimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa vipindi virefu ambavyo havipo hata kwenye Kanuni za Kudumu za Bunge lako tukufu.

Baada ya hapo, kwa kutumia Sheria za kikandamizaji zilizotungwa na Bunge hili, kama vile Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, 2010, Sheria ya Makosa ya Mtandaoni, 2015, na Sheria ya Magazeti, 1976, Serikali ilianzisha wimbi kubwa la kuwakamata, kuwaweka mahabusu kwa vipindi virefu na kuwatesa wale wote waliokuwa wanatumia mitandao ya mawasiliano ya kijamii kutoa mawazo ambayo yalikuwa yanakosoa au kulaani matendo ya Serikali, hasa ya Rais Magufuli, na Serikali yake.

Mheshimiwa Spika,
Wimbi hili la kamata kamata lilihusisha kila aina ya watu. Fulgence Mapunda alias Mwanacotide, mwanachama na msanii maarufu wa CHADEMA, alikamatwa Dar es Salaam pamoja na watengeneza muziki (producers) Mussa Sikabwe na Benjamin Nzogu. Kosa lao lilikuwa kuimba na kurekodi wimbo wenye maneno ‘Dikteta Uchwara.’ Wote watatu walikamatwa tarehe 26 Agosti, 2016.

Wote watatu walikaa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam kwa zaidi ya wiki tatu. Sheria yetu inayohusu mwenendo katika makosa ya jinai inalazimu watuhumiwa waliokamatwa na Jeshi la Polisi wafikishwe mahakamani ndani ya saa 24 tangu kukamatwa, au haraka iwezekanavyo kama haiwezekani kuwafikisha mahakamani ndani ya saa 24.

Aristotle Mgasi na Hosia Mbuba walikamatiwa Vwawa, Mkoa wa Songwe, mnamo tarehe 25 Agosti, 2016. Siku hiyo hiyo Ignasia Mzenga alikamatwa Wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro; na Shakira Abdallah Makame alikamatwa Kinondoni, Dar es Salaam. Siku iliyofuata, yaani tarehe 26 Agosti, Dkt. David Nicas, aliyekuwa mgombea ubunge wa CHADEMA Jimbo la Busega kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, alikamatwa Tunduma mkoani Songwe. Mdude Nyagali wa Vwawa, Songwe, Juma Salum Mtatuu wa Dar es Salaam na Suleiman Said alias Mpemba wa Pemba, Zanzibar, nao walikamatwa siku hiyo hiyo ya 26 Agosti, 2016.

Wote hawa walikusanywa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam, ambako waliwekwa mahabusu kwa zaidi ya wiki tatu. Kosa lao kubwa lilikuwa kutuma ujumbe kwenye mitandao wa whatsapp uliokuwa una maneno yasiyopendeza kwa Rais Magufuli. Wote walidai kwamba wakati wakiwa mahabusu walikuwa wakichukuliwa nyakati za usiku na kupelekwa katika nyumba moja iliyoko maeneo ya Mikocheni ambako walikuwa wakiteswa kwa kupigwa wakati wakiwa wamevuliwa nguo zote.

Baada ya mawakili wao kupiga kelele juu ya ukiukwaji huu wa sheria, watuhumiwa hawa walirudishwa mahali walikokamatiwa ambako walishtakiwa kwa makosa ya mtandaoni chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na ya Posta. Nyingi ya kesi hizo zimekwisha kufutwa na mahakama kwa sababu ya washtaki kutopeleka ushahidi mahakamani.

UTEKAJI NYARA NA UTESAJI

Mheshimiwa Spika,
Katiba yetu imepiga marufuku vitendo vya utekaji nyara na utesaji wa wasiokubaliana na Serikali. Vifungu kadhaa vya Katiba vinathibitisha jambo hili:

 Ibara ya 9(a): “... Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha kwamba utu na haki nyinginezo zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa.”Ibara ya 13(1): “Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.”

 Ibara ya 9(f): “... Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha ... kwamba heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata Kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu Haki za Binadamu.”

 Ibara ya 9(h): “... Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha ... kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini.”

 Ibara ya 13(6)(e): “... ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha.”

 Ibara ya 14: “Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria.”

 Ibara ya 15(1): “Kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru.”
 Ibara ya 15(2): “Kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kuwa huru na kuishi kwa uhuru, itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini, kuhamishwa kwa nguvu au kunyang’anywa uhuru wake vinginevyo, isipokuwa tu ... katika hali na kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria; au ... katika kutekeleza hukumu, amri au adhabu iliyotolewa na mahakama kutokana na shauri au na mtu kutiwa hatiani kwa kosa la jinai.”

Mheshimiwa Spika,
Pamoja na makatazo haya ya kikatiba, sheria zetu za jinai pia zimesisitiza kwamba utekaji nyara kwa lengo la kuua au kuumiza mtu ni kosa kubwa la jinai. Chini ya kifungu cha 248 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kwa mfano, “mtu yeyote anayemteka nyara mtu kwa lengo la mtu huyo kuuawa au kuwekwa kwa namna inayoweza kusababisha mtu huyo kuuawa anakuwa ametenda kosa na anaweza kufungwa jela kwa miaka kumi.” Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 250 cha Sheria hiyo, kuteka nyara kwa lengo la kumuumiza mtekwa nyara ni kosa la jinai vile vile na adhabu yake ni kifungo jela kwa muda wa miaka kumi.

Mheshimiwa Spika,
Sambamba na wimbi la kamata kamata ya wanaomsema vibaya Rais Magufuli au Serikali yake, limeibuka wimbi lingine la kutisha zaidi la utekaji nyara na kuwatesa wanaomkosoa Rais. Katika hili tunaomba kuweka rekodi sawa. Sio Ben Rabiu Saanane wa CHADEMA, wala mwanamuziki Ney wa Mitego, wala mwanamuziki Roma Mkatoliki aliyekuwa wa kwanza kutekwa nyara.

Mtu wa kwa kutekwa nyara alikuwa Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema, Mbunge wa Arusha Mjini. Mheshimiwa Lema alitekwa nyara na watu waliojiita askari polisi nje ya geti la Bunge lako tukufu, na kusafirishwa usiku kwa usiku hadi Arusha alikoishiwa kuwekwa mahabusu kwa karibu miezi minne.

Mheshimiwa Lema hakuwahi kuambiwa kosa lake wakati anakamatwa. Hakuonyeshwa arrest warrant. Waliomkamata hawakujitambulisha kwake, na wala hawakumruhusu kuwasiliana na wakili wake au na familia yake. Na ijapokuwa alikamatwa wakati wa vikao vya Bunge lako tukufu, waliomkamata hawakutoa taarifa kwa, wala kuomba na kupata ruhusa, ya Spika. Yote haya ni matakwa ya Sheria zetu zinazohusu mwenendo wa jinai.

Mheshimiwa Spika,
Yaliyomtokea Mheshimiwa Lema yamenitokea na mimi mwenyewe kati ya Agosti mwaka jana na mwezi uliopita. Jioni ya tarehe 2 Agosti, 2016, nilikamatwa nikihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Ikungi, jimboni kwangu Singida Mashariki. Nilisafirishwa usiku kwa usiku hadi hapa Dodoma, nikalazwa katika mahabusu ya Kituo cha Polisi Chamwino na kesho yake nikasafirishwa hadi Dar es Salaam ambako nilishtakiwa kwa kumwita Rais Magufuli Dikteta Uchwara.

Jioni ya tarehe 6 Februari ya mwaka huu nilikamatwa tena, mara hii nje ya geti la Bunge lako tukufu wakati nikitoka kwenye kikao cha Bunge lako tukufu. Nilisafirishwa usiku kwa usiku hadi Dar es Salaam ambako niliwekwa mahabusu kwa siku tatu kabla ya kupelekwa mahakamani kushtakiwa kwa madai ya uchochezi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mdogo wa Mbunge wa Jimbo la Dimani Zanzibar mwezi Januari ya mwaka huu.

Kesi hiyo ilifutwa baada ya mwezi mmoja. Tarehe 6 Machi, 2016, siku ambayo kesi hiyo ilifutwa, nilikamatwa tena nikiwa mahakamani kumwakilisha Bi Shakira Makame Abdallah aliyekuwa amekamatwa katika wimbi la kamata kamata ya mwaka jana. Mara hii sikushtakiwa kwa kosa lolote la jinai lakini simu yangu binafsi ilinyang’anywa na polisi waliokaa nayo hadi Ijumaa ya wiki iliyopita.

Baada ya hapo, nikiwa katikati ya mgogoro wa Uchaguzi wa Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika, tarehe 16 Machi, 2017, nilikamatwa nyumbani kwangu hapa Dodoma wakati najiandaa kwenda Mahakama Kuu kusikiliza uamuzi wa shauri lililofunguliwa kupinga kufanyika kwa Uchaguzi huo. Nilisafirishwa hadi Dar es Salaam ambako niliwekwa mahabusu ya Kituo Kikuu cha Polisi hadi kesho yake nilipopelekwa mahakamani na kushtakiwa kwa makosa yale yale yaliyofutwa na waendesha mashtaka wa Serikali hii ya CCM siku 11 kabla.
Nilipopata dhamana ya mahakama nilienda moja kwa moja Uwanja wa Ndege wa Julius Kambarage Nyerere na, kama wanavyosema Waingereza, the rest is history.

Mheshiwa Spika,
Kama ilivyokuwa kwa Mheshimiwa Lema, kwa mara zote nne ambazo nimekamatwa sijawahi kuonyeshwa arrest warrant na, mpaka nafikishwa Dar es Salaam, sijawahi kuambiwa nimekamatwa kwa kosa gani. Na wala Spika wa Bunge hakujulishwa wala kuombwa ridhaa kabla sijakamatwa kwenye viunga vya Bunge. Vitendo vyote hivi ni utekaji nyara, na ni kosa la jinai kwa mujibu wa Sheria yetu ya jinai.

Mheshimiwa Spika,
Kwenye Maoni yangu ya mwaka jana nilisema kwamba kwa vile nchi yetu imeingia katika mteremko wenye utelezi mwingi kuelekea kwenye dola la kidikteta, “... hakuna aliye salama....” Maneno haya pia yametimia. Katika kipindi cha mwaka mmoja tu tangu niyaseme maneno hayo, wabunge watatu wa CCM nao wamekamatwa na kuwekwa mahabusu kwa mtindo huu huu au, kama ilivyokuwa kwa Mheshimiwa Nape Nnauye, kutishiwa silaha hadharani mchana kweupe.

Katika kipindi hicho hicho, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alias Daudi Bashite, akiongozana na watu wenye silaha za kivita waliovalia sare za Jeshi la Wananchi na Jeshi la Polisi amevamia kituo cha kurushia matangazo ya radio na televisheni cha Clouds Media Group jijini Dar es Salaam. Kwa muda mrefu, kituo cha radio na televisheni cha Clouds Media kilikuwa ni cheerleader mkubwa wa utawala huu wa Rais Magufuli. Kujipendekeza kwao kwa Magufuli hakukuwapatia ulinzi wowote. Kwenye utawala wa kidikteta hakuna aliye salama.

Kama wabunge wanatekwa nyara na mapolisi au usalama wa taifa nje ya viunga vya Bunge na kusafirishwa usiku wa manane kama ilivyofanyika kwa Mheshimiwa Lema au kwangu mimi maana yake ni kwamba, chini ya utawala wa Rais John Magufuli, uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge uliowekwa na ibara ya 100 ya Katiba yetu ni kejeli tu kwa wabunge na kwa waTanzania na kwa watu wengine wanaoamini katika uhuru wa mawazo na majadiliano.

Kama vyombo vya habari vinavamiwa usikuwa wa manane na watu wenye silaha wakiongozwa na viongozi waandamizi wa Serikali, maana yake ni kwamba maneno ya ibara ya 18(a) ya Katiba yetu kwamba, “kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake” ni ya mapambo tu. Kama alivyosema Rais Magufuli mwenyewe siku chache baada ya shambulio la Clouds Media, ‘hakuna uhuru wa aina hiyo.’

Na kama Rais anaweza kupiga marufuku shughuli halali za kisiasa za vyama halali vya kisiasa bila kuwa na uhalali wowote kikatiba wala kisheria, maana yake ni kwamba maneno ya ibara ya 3(1) kwamba, “Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia ... yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa”; au ya ibara ya 3(2): “Mambo yote yahusuyo uandikishaji na uendeshaji wa vyama vya siasa nchini yatasimamiwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii _na ya sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo”, ni maneno matupu tu.

Mheshimiwa Spika,
Tuligusia mwanzo suala la kukamatwa na kushtakiwa kwa Mbunge wa Kilombero, Mheshimiwa Lijualikali. Kama inavyofahamika, kwa sababu ya kujaribu kuhudhuria kikao ambacho alikuwa Mjumbe wake halali, Mh. Lijualikali baadae alipatikana na hatia ya kufanya vurugu na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela kabla hajaachiliwa huru na Mahakama Kuu ya Tanzania, mwezi mmoja uliopita. Mahakama Kuu iliridhika kwamba sio tu kwamba hati ya mashtaka dhidi yake ilikuwa ni magumashi, bali pia hakukuwa na ushahidi wowote kwamba Mh. Lijualikali alifanya vurugu yoyote. Aidha, Mahakama Kuu ilitamka kwamba kwa vyovyote vile Mh. Lijualikali alikuwa mjumbe halali wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero na, kwa hiyo, ilikuwa ni makosa kumzuia kuingia kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo.

Mheshimiwa Spika,
Kitu ambacho hakijulikani na wengi ni kwamba kesi dhidi ya Mh. Lijualikali ilikuwa imepangwa hata kabla hajafanya kosa lenyewe. Kwa ushahidi uliotolewa katika Mahakama ya Wilaya ya Kilombero, kulikuwa na barua iliyoandikwa na Katibu Mkuu TAMISEMI iliyotamka kwamba Mh. Lijualikali hakuwa mjumbe halali wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, hivyo asiruhusiwe kuingia kwenye kikao hicho.

Kwa mujibu wa ushahidi huo, barua hiyo ilinakiliwa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kilombero kwa maagizo kwamba atekeleze msimamo huo kwa kumkamata na kumfungulia mashtaka ya jinai. Kwa hiyo, hata kabla Mh. Lijualikali hajakanyaga kwenye eneo la mkutano, tayari alishaundiwa njama na Serikali hii ya CCM ya kumkamata na kumfunga. Haya ndio mambo yanayofanyika katika nchi zinazotawaliwa kidikteta.

Mheshimiwa Spika,
Katika makala yake ya mwaka 1985, Mheshimiwa Prof. Kabudi alisema yafuatayo kufuatia kutungwa kwa the Human Resources Deployment Act, 1983, maarufu kama Sheria ya Nguvukazi, 1983, na the Economic Sabotage (Special Provisions) Act, 1983, yaani Sheria ya Uhujumu Uchumi, 1983: “The enactment of the two legislation ... clearly shows that once the ruling class is facing a major crisis and it can no longer bury itself in its populist ideological cacoon (sic!), it will resort to the only alternative – the use of the repressive state apparatus. Thus it will use the logic of force rather than the force of logic.”

Yaani, “kutungwa kwa sheria hizi mbili kunaonyesha dhahiri kwamba pale tabaka la watawala linapokabiliwa na mgogoro mkubwa na linaposhindwa kujificha nyuma ya utando wa kiitikadi ya maneno matamu, huanza kutumia mbadala pekee – matumizi ya vyombo vya ukandamizaji vya dola. Hivyo litatumia hoja ya nguvu badala ya nguvu ya hoja.” Kwa haya ambayo yametokea katika tangu Rais Magufuli aingie madarakani mwaka mmoja na nusu uliopita, nani anayeweza kubishia ukweli wa maneno ya Waziri wa sasa wa Katiba na Sheria, hata kama aliyasema zaidi ya miaka thelathini iliyopita?

UENDESHAJI WA MASHTAKA YA JINAI

Mheshimiwa Spika,

Mamlaka ya uendeshaji wa mashtaka ya jinai imekasimiwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa mujibu wa ibara ya 59B(2) ya Katiba. Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 59B(4), katika kutekeleza mamlaka yake, “Mkurugenzi wa Mashtaka atakuwa huru, hataingiliwa na mtu yeyote au na mamlaka yeyote na atazingatia ... nia ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki na maslahi ya umma.” Kanuni hii kuu imetamkwa pia na kifungu cha 8 cha Sheria ya Utumishi wa Mashtaka ya Taifa, Na. 27 ya 2008 (National Prosecutions Service Act, 2008) ambayo pia imefafanua na kutilia nguvu mamlaka haya ya kikatiba.

Kwa mujibu wa Sheria hii, Mkurugenzi wa Mashtaka ana mamlaka sio tu ya kudhibiti mashtaka yote ya jinai bali pia kuratibu shughuli za upelelezi wa makosa ya jinai [kifungu cha 16(1)]. Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 17(1) na (3), Mkurugenzi ana uwezo wa kutoa maelekezo ya maandishi kwa ofisa yeyote wa umma ili apatiwe taarifa yoyote inayohusu upelelezi au uendeshaji wa mashtaka ya jinai na ofisa huyo anatakiwa kutii maelekezo hayo.

Mheshimiwa Spika,

Ili kumwezesha Mkurugenzi wa Mashtaka kutekeleza wajibu wake wa kikatiba kwa uhuru kamili na bila woga au upendeleo, Mkurugenzi wa Mashtaka amewekewa kinga ya ajira yake. Kwa mujibu wa kifungu cha 19(1) na (2) cha Sheria ya Utumishi wa Mashtaka ya Taifa, sifa, masharti na mafao ya ajira ya Mkurugenzi wa Mashtaka yatakuwa sawa _ay a_e ya ajira ya Jaji wa Mahakama Kuu.

Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 19(3), Mkurugenzi wa Mashtaka hawezi kuondolewa kwenye madaraka yake isipokuwa kwa kushindwa kutimiza wajibu wake kwa sababu ya ugonjwa au kwa kukiuka Kanuni za Maadili ya Kitaaluma ya Maafisa wa Sheria, Mawakili wa Serikali na Wanasheria Walioko kwenye Utumishi wa Umma chini ya Sheria ya Utekelezaji wa Mamlaka ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268 ya Sheria za Tanzania.

Hii ndio kusema kwamba, kwa mujibu wa Sheria Na. 27 ya 2008, utaratibu wa kumwondoa Mkurugenzi wa Mashtaka kwenye ajira yake hauna tofauti na utaratibu wa kumwondoa Jaji wa Mahakama Kuu kwenye ajira yake.

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba utaratibu huu wa kikatiba na kisheria umempa Mkurugenzi wa Mashtaka nyenzo za kutosha kisheria za kupambana na uhalifu mkubwa hapa nchini na vile vile kuzuia matumizi mabaya ya mfumo wa uendeshaji na utoaji haki na hasa hasa ya mfumo wa mashtaka ya jinai. Licha ya kuwa na mamlaka na kinga hizi za kisheria, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka imeshindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.

Hii inathibitishwa na kitendo cha kutowachukulia hatua za kijinai Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alias David Bashite kwa vitendo vya kijinai alivyofanya katika uvamizi wake wa Clouds Media Group. Inathibitishwa pia na kitendo cha kushindwa kuwachukulia wale wote waliteka waTanzania na kuwatesa kama ambavyo tumeelezea humu kwa kirefu; na wale waliomtishia Mheshimiwa Nape Nnauye silaha hadharani mbele ya waandishi habari. Na hii inathibitishwa na kushindwa kwake kuchukua hatua za kijinai dhidi ya wale wote waliokula njama za kumfungulia mashtaka ya uongo na kumfunga Mheshimiwa Lijualikali.

Mheshimiwa Spika,
Katika mazingira haya, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inataka Mheshimiwa Waziri alieleze Bunge lako tukufu, kama bado Mkurugenzi wa Mashtaka anastahili kuendelea kushikilia nafasi hiyo muhimu wakati ni wazi hana uwezo wala nia ya kutekeleza majukumu yake ya kikatiba na kisheria.

YA KAIMU JAJI MKUU

Mheshimiwa Spika,
Mahakama ya Tanzania haina kiongozi wake kamili, yaani Jaji Mkuu. Hii ni kwa sababu, tangu Jaji Mkuu Mohamed Chande Othman astaafu tarehe Mosi Januari ya mwaka huu, Rais John Pombe Magufuli hajateua Jaji Mkuu mpya kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Jaji Mkuu Chande Othman. Badala yake, Rais Magufuli amemteua Jaji wa Rufaa Prof. Ibrahim Hamisi Juma kuwa Kaimu Jaji Mkuu.

Mheshimiwa Spika,
Ibara ya 118(4) ya Katiba yetu, Rais anaruhusiwa kuteua Kaimu JAji Mkuu iwapo itatokea kiti cha Jaji Mkuu kitakuwa wazi; au Jaji Mkuu hayupo Tanzania; na au Jaji Mkuu atashindwa kutekeleza kazi yake kwa sababu yoyote, na Rais ataona kuwa kwa muda wa tukio lolote kati ya hayo matatu inafaa kumteua Kaimu Jaji Mkuu. Kaimu Jaji Mkuu aliyeteuliwa kwa utaratibu huu “... atatekeleza kazi za Jaji Mkuu mpaka atakapoteuliwa Jaji Mkuu mwingine....”

Mheshimiwa Spika,
Pamoja na kuwapo kwa ibara ya 118(4), Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inaamini kwamba Rais Magufuli anavunja Katiba ya nchi yetu kwa kushindwa kuteua Jaji Mkuu kamili takriban miezi mitano tangu kustaafu kwa Jaji Mkuu Chande Othman. Hii ni kwa sababu, ibara ya 118(4) haikutungwa kwa lengo la kumwezesha Rais kuteua Kaimu Jaji Mkuu bila kikomo cha muda.

Kama ilivyo kwa sheria zote, ibara ya 118(4) ina sababu yake maalum. Ibara hiyo imewekwa kwa makusudi ya kuhakikisha kwamba kwa muda wote kunakuwa na kiongozi wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania pamoja na kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, wakati Jaji Mkuu kamili anasubiriwa kuteuliwa. Kaimu Jaji Mkuu ni sawa ni kile kinachoitwa na wanasheria ‘interlocutory position.’ Kaimu Jaji Mkuu ni nafasi ya muda inayoshikiliwa na mtu mwenye sifa za kuwa Jaji Mkuu kabla nafasi hiyo haijajazwa na Jaji Mkuu kamili.

Swali halali linahitaji majibu ni, je, Kaimu Jaji Mkuu anastahili kuwapo madarakani kwa muda gani? Hili ni suala la tafsiri ya Katiba linalohitaji kujibiwa na Mahakama. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, miezi mitano ni muda mrefu mno wa kuwa na Kaimu Jaji Mkuu. Hii ni kwa sababu, katika historia yetu yote tangu uhuru, haijawahi kutokea Rais wa nchi yetu akashindwa kuteua Jaji Mkuu kamili kujaza nafasi iliyo wazi ya Jaji Mkuu.

Mheshimiwa Spika,
Bunge lako tukufu, kama mmojawapo wa mihimili mikuu ya dola ya Tanzania, lina kiongozi wake mkuu muda wote: Spika au Naibu Spika. Serikali, kama mhimili mwingine mkuu, ina kiongozi wake mkuu muda wote: Rais au Makamu wa Rais. Kwa Mahakama ya Tanzania, mhimili mkuu wa tatu wa dola ya Tanzania, kutokuwa na kiongozi wake kamili miezi mitano baada ya kustaafu kwa Jaji Mkuu Chande Othman, kunatoa taswira potofu kwamba Mahakama ina hadhi hafifu au ya chini ikilinganishwa na mihimili mingine mikuu ya dola ya Tanzania.

Kitendo hiki vile vile kinatoa taswira potofu kwamba pengine Kaimu Jaji Mkuu wa sasa hatoshelezi nafasi hiyo; au kwamba miongoni mwa Majaji wote wa Rufaa au wa Mahakama Kuu ya Tanzania au mawakili na wanasheria wengine wa nchi hii pamoja na wale wa nchi za Jumuia ya Madola hakuna hata mmoja wao mwenye uwezo au sifa za kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.

Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inamtaka Mheshimiwa Waziri amshauri Rais Magufuli, kwa heshima zote anazostahili, amthibitishe Kaimu Jaji Mkuu Prof. Juma katika nafasi hiyo au, vinginevyo, ateue mwanasheria mwingine anayemwona ana sifa za kuwa Jaji Mkuu kamili wa Tanzania. Hali ilivyo hivi sasa inawatia aibu wanasheria wote wa Tanzania na inaitia aibu nchi yetu katika jumuia ya kimataifa.

Mheshimiwa Spika,
Naomba nimalizie maoni yangu haya kwa kusema yafuatayo. Watanzania hawastahili Serikali ya aina hii. Kama alivyosema Baba wa Taifa katika kitabu chake Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania: “Hatulazimiki kuendelea na uongozi mbovu wa Chama na Serikali. Wala tukiendelea na hali hii, bila kubadili uongozi wa Chama na Serikali, sina hakika kama tutafika huko salama.

Masuala muhimu ya nchi yetu hayatashughulikiwa.... Na masuala mengine muhimu ... yataachwa yajitatue yenyewe. Nasema katika hali kama hiyo sina hakika kama tutafika salama; na tukifika salama tukiwa na uongozi huu huu wa Chama na Serikali mbele kutakuwa ni giza tupu. Majuto ni mjukuu, huja baadaye.”

---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, SHERIA NA KATIBA
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
25/04/17
Watu vichwa viva lisu.
 
Tundu anashindwa kutofautisha kati academic discussion na political practitioner na matokeo yake he goes astray.
 
Kabudi hawezi kuwa tofauti NA Kitila, ni hao hao NJAA MWANAMALEGEZA. Kitila alilaani wasomi kuondolewa vyuoni, leo anakubali kuondoka chuoni , anakula uharo wake! Si rahisi kumpata University lecturer wa kweli, ni wachache. Amekubali kutoka, njaa baba!
 
Tundu anashindwa kutofautisha kati academic discussion na political practitioner na matokeo yake he goes astray.
Nadhani mpo ambao hampendi mambo ya msingi katika kujenga taifa bora, yasemwe na kuzungumzwa kwa uwazi. Tundu Lisu anastahili pongezi kwa kuanzisha mijadala hii ambayo wote, bungeni na hata kwa wananchi tukishiriki kwa uzalendo wa kweli, tutajenga taifa lenye haki, hekima na umoja wa kweli. Tusikwepe, tusiogope wala kuchukia hoja za Lissu na hata za wengine wenye mawazo mbadala ya kuleta maendeleo kwenye nyanja zote: jamii, siasa etc.
 
Back
Top Bottom