Miongoni mwa maneno ya watu wa zamani wenye hekima ambao kwa jina moja huitwa wahenga, waliwahi kusema kuwa Uzee nyumba ya Magonjwa, wakimaanisha kuwa na umri mkubwa yaani Uzee ni kuwa karibu mno na magonjwa ya aina mbalimbali. Moja ya magonjwa ambayo uzee humsababishia yule aliyezeeka ni pamoja na ugonjwa wa kupungua kwa akili, yaani mtu kutowaza sawasawa, kuwaza pungufu ama kutowaza kabisa.
Miongoni mwa jamii yetu tunao wazee.,wazee hawa wamegawanyika katika makundi mbalimbali na pia walikuwa watu wa aina tofauti waliopitia na wenye uzoefu wa kada mbalimbali za kiutendaji. Ingawa kauli nyingine inayowataja wazee inawataja kuwa ni nyumba ya hekima kwa maana kuwa umri mkubwa unanasibishwa na uzoefu na kujua mambo mengi ambayo hawa wazee huwa wameyapitia katika maisha yao.
Jina lingine ambalo mtu akizeeka anaitwa kutokana na umri wake ni BABU.,mimi ninao mababu na nawajua mababu wengine wengi, ila yupo babu mmoja ambae pamoja na Uzee wake na kuchoka bado anatamani kuyafanya yale ambayo babu hapaswi kuyafanya, anayasema yale ambayo yanatoa tafsri tofauti na yanapingana na falsafa ya weledi na hekima ambazo mtu mzima mwenye umri mkubwa yaani babu anastahili kuwa nao.
Naomba nimtambulishe Babu huyu ninayemfahamu, ambae ni miongoni mwa viongozi waandamizi wa Chama cha Siasa Cha Upinzani. Babu huyu anazeeka vibaya sana.,na niliwahi kulisema hili hapo nyuma kuwa mtu mzima huyu amekuwa wa hovyo sasa na kauli yangu hiyo imeendelea kuthibitishwa na maneno na matendo ya Babu huyu.
Hivi karibuni Babu ametoa kauli si tu ya kupotoka bali yenye ziada ya Uongo Mkuu, ya fitina na uchonganishi, yenye kulenga kushawishi chuki, hasira, hasadi na utengano ndani ya jamii yetu ya kitanzania. Kauli ya Dr Slaa kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Mwenyekiti wa Chama Makini Chenye kuongoza Dola CCM Ndugu Jakaya mrisho Kikwete ni muasisi wa Udini hapa nchini, ni kauli mbaya kuwahi kutolewa na KIONGOZI hasa wa kisiasa hapa nchini.
Kauli hii si tu ya uongo,bali pia haikupaswa kutolewa na kiongozi mwenye umri wa Slaa katika wakati huu ambao nchi imekaa pamoja kujenga umoja na mshikamano baina ya watu wa dini mbalimbali. Aidha, Kauli hii ni mfululizo wa kauli nyingine za uchochezi na zenye kuhamasisha chuki za kidini hapa nchini.
Kauli hii ni ya mtu asiyeweza kufikiri sawasawa ama mjinga asiyeelewa athari za kauli hiyo, ni ushahidi wa kukosa weledi wa kisiasa, hekima na zaidi ni kukosa Uzalendo na Utaifa. Ni mtu asiyelipenda taifa lake tu ndio ataishabikia kauli hiyo na kuipongeza lakini yeyote mwenye kufikiri sawasawa ameshtushwa na ataalaani vikali kauli hiyo na zingine mfano wa hiyo zenye kuhatarisha AMANI ya nchi hii.
Nisingelienda mbali zaidi na kufikiri juu ya Uzee na kufahamu kwangu kuwa Uzee unasababisha Ugonjwa na hasa wa Akili basi ningeliishauri dola kumchukulia hatua kali za kinidhamu mzee huyu. Bali naelewa kuwa Babu anazeeka vibaya, uzee wake unamjia vibaya sana. Kama ameyasema hayo kwa minajili ya kujiletea umaarufu wa Kisiasa katika kipindi kama hiki ambacho makanisa yanalipuliwa, misikiti inachomwa moto, masheikh na maaskofu wanajeruhiwa na kuuawa, basi nadiriki kusema ni siasa mbaya sana kuwahi kufanywa hapa nchini, na kama maneno hayo yatahalalishwa katika jamii kwa kuwa tu yametolewa na mwanasiasa na kubebwa kisiasa basi sasa siasa hii inaelekea kutuangamiza.
Babu hana sifa achilia mbali ya kuongoza nchi bali hata kuongoza taasisi yenye hadhi ya chama cha siasa, ni mtu wa hovyo, asiyejitambua, ni mtu ambae anaweza kusema ama kufanya lolote popote bila kujali chochote.
Kiongozi wa watu kamwe hawezi kutoa kauli kama hizi zenye kuharibu murua hata wa mzungumzaji mwenyewe. Ni kauli za kimbayuwayu zenye kujaa upotoshaji. Ni UCHOCHEZI ulio dhahiri, hii ni kauli nyingine iliyozifuata zile za awali kama "..NCHI HAITATAWALIKA.." na "..DAMU ITAMWAGIKA.."
Ni wazi akili ya Babu imechoka,ni vema tukawa washauri bora kwake kumshauri Babu kupumzika Siasa. Ni wakati wa kusataafu na kuwapisha vijana wafanye siasa. Mimi binafsi naamini Chadema inao vijana wanaofikiri, tena wasomi wazuri wanaoweza kuleta chachu na changamoto ya kuleta mwelekeo na taswira inayokubalika ya Chama hicho na viongozi wake ndani ya Jamii yetu.