Kutana na kijana Issa Haruna, mke wake na mwanae

MSAGA SUMU

JF-Expert Member
May 25, 2015
6,477
20,383
Mbali na jina lake Issa Haruna, jijini Mwanza, hasa eneo la Kirumba anafahamika kama Issa Mapilau kutokana na uwezo aliyonao wa kula chakula kingi.

Kwa sababu hiyo, pia mitaani wamempa majina mengi, baadhi humwita Matonge na wengine Mapleti. Issa mwenye uzito wa kilo 85 na umri wa miaka 27, ni mzaliwa Kigoma ambaye kwa sasa anaishi jijini Mwanza alikohamia na wazazi wake. Kwa sasa anaishi na baba yake, Mzee Haruna Mnazi.

Ukikutana naye alivyo mpole na mtaratibu, unaweza usiamini kazi anazozifanya kwenye jamii na amekuwa maarufu na hupendwa na wengi.

Ukiacha ulaji wake, mitaani anaelezewa kama mtu mwenye nidhamu, muaminifu, mcheshi na muongeaji kwa kila mtu anayekutana naye. Kutokana na uwezo huo, pia amejaaliwa nguvu za kubeba vitu na kufanya kazi pia ana uwezo wa kuimba na kuchekesha.

Hata hivyo, licha ya shughuli kubwa anazofanya kwenye milima ya Kirumba, lakini uhalisia wa maisha yake na familia kwa ujumla bado ni duni na kilio chake ni mtaji wa kufanya biashara hata ya mayai.

Mwananchi lilimtembelea nyumbani kwake na kuweka kambi ya siku nzima, kushuhudia maajabu ya kijana huyo. Baada ya kufika majira ya saa 2:00 asubuhi Mapilau Waandishi wa Mwananchi walishuhudia katika kifungua kinywa chake akila chapati 45 na chai chupa moja na nusu (vikombe 9).

Ilipofika mchana sasa 7:00 katika mlo wake wake wa siku hiyo Mapilau alikula wali uliotokana na mchele kilo nne na maharage kilo moja, kisha akashushia maji glasi mbili.

Jioni, ingawa Mwananchi halikushuhudia, Mapilau alisema anakula kiwango kama hicho cha wali na maharage. Katika mazungumzo alisema anaweza kula ugali kilo nne; kunywa lita tano za maji; chapati 70 na kisado cha dagaa. “Nina uwezo wa kula kilo nne za wali ukiwa na maharage kilo mbili. Maji nakunywa jagi mbili kubwa, kifungua kinywa napiga hadi chapati 70 na chupa mbili za chai na kama ni vitumbua nakula deli mbili,” anasema.

Lakini mbali na hayo, Issa alionesha uwezi katika kuimba taarabu, mashairi, kuchezesha macho, kubeba wanaume watano na kulia milio ya wanyama paka au mbuzi.

Pamoja na hayo, Issa hakusita kuelezea visa na mikasa vilivyowahi kumtokea kutokana na mazingira yake, zikiwamo changamoto na faida anazopata kupitia uwezo wake, huku akiomba sapoti kwa Serikali na jamii kumtambua.

Nini faida yake?
Kwanza kijana huyu anabainisha kuwa licha ya kula kwa kiwango hicho, hafanyi fujo mtaani na ulaji wake umemuweka karibu na jamii kwani kila mmoja ameweza kuelewa maisha yake.

Anasema kama ambavyo watu wengine wanavyolewa na kufanya vurugu au kuwasumbua raia mitaani, yeye hutumia nguvu zake kwa shughuli za kijamii.

“Mimi sipigani wala kusumbuana na mtu barabarani au hapa mtaani, ninachoshukuru majirani na watu hapa Kirumba wananifahamu tabia yangu, mimi nguvu zangu ni kusaidia jamii,” anaeleza.

Pamoja na kula hivyo, anasema huwa anakubaliana na hali pale anapokosa chakula cha kumtosha.

Hasara anayopata
Issa anasimulia kutokana na ulaji wake amejikuta akitengwa na ndugu, jamaa na marafiki kwani wengi wameshindwa kuhimili hali yake.
Anasema hata mama yake mzazi naye amefika hatua ameanza kumkwepa kwani anapopanga kwenda Igoma kumsalimia, huwa anamkwepa muda mwingine akidai amesafiri.

Anadai ndugu zake na ukoo wameshindwa kumvumilia wakidai hawana uwezo wa kumlisha hadi kushiba kama anavyotaka yeye.
Hata hivyo, pamoja na kuishi na baba yake, huwa hawapiki nyumbani bali hula magengeni na baba yake humsaidia pale anapokwama kupata chakula cha kutosha.

“Huwa tunaenda kula kwenye migahawa, kama sina pesa nakula sahani nne ila baba huniongezea nyingine nne kisha nasukumizia maji jagi mbili basi natulia,” anasema.

“Mjomba wangu wa Tabora alifikia hatua akanifukuza kwake kwa sababu alikuwa amenipa kazi ya kumwagilia shamba la nyanya chungu, lakini chakula kikawa hakinitoshi hadi nikawa nachuma ndoo mbili nakula,” anasimulia kwa msisitizo.

Atumika kubeba abiria
Mapilau hutumika kama gari huko mitaani kama njia ya kutumia nguvu za msosi anaokula. Inapotokea maji yamekatika mtaani maeneo ya mlimani, yeye huingia kazini kwa kubeba ndoo mbili kubwa za maji zinazoitwa diaba kichwani na kuwapelekea wananchi.

Anasema mbali na kusomba maji, pia ikitokea mjamzito akapatwa na uchungu yeye muda wowote husakwa ili kumbeba hadi kwenye barabara ya lami kisha huchukuliwa na gari.

Kama haitoshi, Mapilau anaeleza kuwa yeye ana uwezo wa kubeba wanaume watano na kazi hiyo humuingizia kipato kwani kutokana na mlima uliopo, hujikuta akikusanya Sh500 kwa kila mtu kuwapandisha.

“Hata nyumba unazoona huku juu mlimani nimehusika sana kubeba matofali na vifaa vya ujenzi,” anasema.

Mke kama yeye
Issa Mapilau anasema Mungu alimjalia kupata mke ambaye wanaendana sana katika familia, hasa katika suala la ulaji, licha ya kwamba hawajafanikiwa kufunga ndoa. Anasema wakati wa mashindano ya kula mkoani Mwanza alipata faida kubwa ukiachana na nafasi ya pili aliyoshika akizidiwa na Salala aliyeshika namba moja, aliibuka pia na mke.

Anasema katika shindano hilo lililofanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, alimpata mke huyo ambaye alikuwa mshiriki na mshindi wa tatu kwa kula mikate 35 na kreti moja ya soda.

“Katika mashindano hayo, mimi nilikuwa mshindi wa pili kwa kula mikate 50 na kreti mbili za soda, aliyenifuata alikuwa mwanamke (Mariam) ambaye alikula mikate 35 na kreti moja ya soda na kuanzia hapo tukapanga kuoana,” anasema.

Anasema licha ya kwamba hawajafunga ndoa, tayari wamepata mtoto mmoja (Haruna) ambaye naye amefuata nyayo za wazazi wake.
Ndani ya familia yao, mlo wa siku hupika ugali kilo nane, ambapo yeye hula kilo nne, mke wake kilo tatu na mtoto wao mwenye umri miaka minane hupiga kilo moja.

“Bahati mbaya mke wangu hayupo Mwanza kwa sasa, ila kikawaida tunapika kilo nane za unga wa dona, mtoto amefuata nyayo zetu kwa sababu anakula kilo moja,” anasema.

Itaendelea kesho
Imeandikwa na
Saddam Sadik na Johari Shani, mwananchipapers@mwananchi.co.tz
 
F2E396F4-D267-4AA7-8EE5-75D2E60CFD65.jpeg
 
daah..nimecheka kingese ni kwamba alipata mke kwenye shindano so nice kwa kweli Mungu hukupa yule unae endana nae. Ila jamaa ni noma mpka mjomba alimtimua kisa kala ndoo mbili za nyanya chungu dunia ina mambo mazuri kweli.

Usisahau kuleta Part 2 Mkuu
 
kuna jamaa huku mtaa unga limitedii ye anakula ndo kubwa imejaa ugali.siku alikuta hom kwake imebaki unga nusu debe akaona hautoshi akaupika tu anywe uji..
 
Back
Top Bottom