Sokomoko
JF-Expert Member
- Mar 29, 2008
- 1,915
- 127
Kuna njama za kuwachafua zaidi Karamagi, Msabaha
Peter Nyanje
Source: Tanzania Daima
Peter Nyanje
KWA mantiki ya kawaida, choki huwa safi baada ya kuoshwa kwa maji safi. Chombo kilicho safi, iwapo kitaoshwa na maji machafu, basi matokeo yake chombo hicho huambukizwa uchagu kutoka katika maji yaliyotumika kukioshea. Hatimaye, chombo hicho nacho huchafuka.
Kama chombo ni kichafu, halafu kikaoshwa na maji machafu, uwezekano mkubwa ni kuwa uchafu wa chombo unaweza kuondoshwa, lakini uchafu wa maji machafu ukabaki katika chombo, hivyo kukifanya chombo hicho kiendelee kuwa kichafu.
Kwa mantiki hiyo, ili chombo kiwe kisafi kikioshwa na maji machafu, huishia kuwa kichafu.
Haya ndiyo serikali inayotaka kuyafanya kwa waliowahi kuwa mawaziri katika Wizara ya Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha, waliolazimika kujiuzulu Februari, mwaka huu, kutokana na kashfa ya Richmond.
Walipokuwa wanajiuzulu, walikana kuhusika kwa namna yoyote na aina yoyote ya ukiukwaji wa sheria na taratibu, katika mchakato wa kuipatia Richmond kandarasi ya kufua umeme wa dharura.
Hii haiwezi kuwafanya Karamagi na Dk. Msabaha kuwa wasafi kwa sababu kukana kwao bado hakujathibitishwa na chombo kingine huru.
Inagwa sehemu ya tuhuma dhidi yao zimethibitishwa na baadhi ya vyombo, lakini hatuwezi pia kusema kuwa Karamagi na Msabaha ni wachafu kwa sababu chombo cha kutoa haki hakijalipitia suala hilo na kutoa maamuzi yake.
Kwa hiyo, Karamagi na Msabaha wanaweza kuwa wachafu au wasafi, lakini hatua ya serikali kuitumia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuwachunguza wanasiasa hawa, itakuwa ni kutowatendea haki.
Hii ni kwa sababu usafi wa TAKUKURU yenyewe kama ilivyo kwa akina Karamagi na Msabaha, nao upo mashakani kutokana na yale yaliyobainishwa na Kamati Teule ya Bunge.
Kamati hiyo, iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe (CCM), katika mapendekezo yake, ilitaka TAKUKURU ifanyiwe mabadiliko makubwa.
Kana kwamba hiyo haitoshi, kamati ilipendekeza; Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU awajibishwe kwa manufaa ya umma na maofisa wa TAKUKURU walioshiriki kwenuye zoezi la uchunguzi na kuandaa Taarifa ya Richmond Development Company LLC iliyoficha ukweli nao pia wawajibishwe kwa manufaa ya umma.
Lakini katika taarifa yake ya kuonyesha jinsi serikali ilivyoyatekeleza mapendekezo hayo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akiripoti bungeni, alisema vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi wa kina kwa lengo la kutaka kujua kama kuna rushwa yoyote iliyojitokeza wakati wa mchakato huu inayomhusisha Karamagi, katika suala hili.
Sote tunafahamu kuwa chombo cha dola chenye mamlaka ya kufanya uchunguzi wa masuala ya rushwa nchini hivi sasa ni TAKUKURU, ambayo Dk. Mwakyembe na wenzake walitueleza kuwa inahitaji kufanyiwa marekebisho makubwa kutokana na upungufu uliobainika ndani yake.
Tangu mapendekezo hayo yatolewe hadi sasa hatujasikia mabadiliko yoyote kufanyika kwa TAKUKURU. Zaidi sana, Pinda alizidi kuionyesha taasisi hiyo kama yenye usafi wa kutilia mashaka pale alipoeleza kuwa hata Mkurugenzi wake mkuu, Edward Hosea, ni miongoni mwa maofisa wa serikali ambao wametakiwa kujieleza, kutokana na tuhuma zinazowakabili.
Hizi zinaweza kuwa tuhuma tu, lakini sidhani kama chombo kinachotuhumiwa kinaweza kutumika kumchunguza mtuhumiwa mwingine. Hii ni sawasawa na kutumia maji machafu kuosha chombo. Hata kama chombo hicho ni kisafi, hatimaye kitachafuliwa na yale maji machafu.
Tukiiachia TAKUKURU ifanye uchunguzi dhidi ya Karamagi na Msabaha, itakapotoa matokeo yake na kubainisha kuwa mawaziri hao wa zamani walijihusisha na rushwa, wapo watakaohoji iwapo hiyo si njama ya TAKUKURU kutaka kujisafisha na udhaifu iliouonyesha awali?
Pia, kama TAKUKURU ikisema mawaziri hao waliojiuzulu hawakujihusisha na rushwa, wengi watasema walitarajia hivyo kwa sababu TAKUKURU ilishasema tangu awali kuwa hakukuwa na rushwa katika suala hilo.
Hadhi ya Karamagi na Dk. Msabaha katika sakata hili lote itawekwa sawa na uchunguzi utakaofanywa na chombo ambacho usafi na uadilifu wa viongozi wake hauna mashaka. TAKUKURU hii tuliyo nayo sasa, ambayo kiongozi wake mkuu naye yupo chini ya uchunguzi, haina sifa hiyo hata kidogo.
Source: Tanzania Daima