Kuna nini Anglikana Sumbawanga??? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kuna nini Anglikana Sumbawanga???

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Rutashubanyuma, Jan 24, 2011.

 1. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #1
  Jan 24, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 85,149
  Likes Received: 60,358
  Trophy Points: 280

  Waumini wamzuia Askofu asiingie kanisani

  Imeandikwa na Peti Siyame, Sumbawanga; Tarehe: 24th January 2011 @ 07:54

  WAKATI kukiwa na hisia za kuibuka kwa udini nchini, kundi la waumini wa Kanisa Anglikana jana walimzuia Askofu wao kuingia kanisani kuongoza ibada, kwa kile wanachodai kuwa, hawamtambui na hana sifa ya kuwa kiongozi wa kiroho.

  Waumini hao maarufu kama watakatifu wote wa Jimbo la Ziwa Rukwa mjini Sumbawanga, kwa kutambua kuwepo kwa uwezekano wa kiongozi huyo kuingia kwa nguvu katika nyumba hiyo ya ibada, waliingia kanisani hapo na mawe katika mifuko ya plastiki na mikoba ya kinamama na fimbo kwa ajili ya kujihami.

  Kutokana na hali hiyo, Askofu huyo, Canon Kasagara na wafuasi wake walilazimika kubaki nje huku akiwa amevalia kiaskofu na mkononi ameshikilia fimbo ya kichungaji, wakati jitihada za kushawishi waumini hao ili akubaliwe kuingia kanisani hapo zikiendelea.

  Inadaiwa kuwa Askofu huyo alikutana na OCD wa Sumbawanga, Mohamedi Mbonde ambaye alimsihii asiende kanisani hapo kwa kuwa hali ni tete na waumini wa kanisa hilo wamesisitiza kutomtambua na hawatamruhusu kuingia kanisani.

  Akithibitisha kuwepo kwa mazungumzo na Serikali kuhusu hali hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Sumbawanga, Salum Shilingi alisema Mkuu wa Wilaya hiyo, John Mzurikwao alialikwa na Askofu huyo kuhudhuria misa hiyo, lakini aliona ni busara kutohudhuria ibada hiyo.

  Katibu Msaidizi wa Baraza la Wazee la kanisa hilo, Wandi Joseph alisema uongozi wa kanisa hilo ulimtaarifu Askofu wa Dayosisi ya Mbeya, John Mwela ili awasiliane na kiongozi mwenzake, Askofu Kasagara na kumsihi asifanye ziara hiyo.

  Kwa mujibu wa Katibu huyo, ujumbe huo ulifika na Askofu Mwela alimshawishi Askofu Kasagara asiende katika kanisa hilo kwa kuwa muda muafaka bado haujawadia lakini inadaiwa Askofu Kasagara alikataa ushauri huo.

  "Huyu Askofu Kasagara kwa kipindi chote cha miezi zaidi ya saba tangu asimikwe amekuwa akiishi mjini Mpanda na Jimbo hili lina ‘parishes’ 24 na kati hizo, 23 zinamuunga mkono isipokuwa sisi.

  “Sasa kwa nini anatufuata fuata, si awahudumie hao wengine wanao mkubali, kwanza mie hata kwa sura si mfahamu sina hakika kama wengi wenu mnamfahamu,“ alisisitiza Joseph.

  Akieleza sababu za waumini na uongozi wa kanisa hilo, linaongozwa na Baraza la Wazee kwa miezi saba sasa kumkataa askofu huyo, Joseph alisema kwanza hana sifa kwa kuwa alisababisha vurugu kanisani mjini Mwanza.

  “Askofu asiwe mtu mwenye kutuhumiwa na watu kwa lolote lile isipokuwa anapaswa kuwa kiongozi wa kiroho mwenye uwezo wa kupatanisha,” alisema Joseph huku akinukuu Bibilia.

  Wakati Askofu Kisangara na wafuasi wake wakiwamo baadhi ya wachungaji na waumini wakiwa nje, huku waumini wa kanisa hilo wakiendelea na ibada ndani ya kanisa, askari Polisi waliwasili wakiwa katika mavazi ya kiraia.

  Baadhi ya maofisa hao wa Polisi walichanganyika na waumini kanisani na wengine walionekana kuranda randa nje ya kanisa hilo Muda mfupi baadae askari wa kuzuia na kutuliza fujo, FFU wakiwa na silaha waliwasili hali iliyowatisha baadhi ya waumini hasa akina mama na watoto waliokuwa ndani ya kanisa hilo, kuamua kukatisha ibada na kutoka nje lakini waumini wengine wanaojiita wafia dini waliendelea na ibada bila ya hofu.

  Baada ya waumini hao kushikwa na hofu na wengine kuanza kutoka nje, Kiongozi aliyekuwa akiongoza ibada hiyo, Mchungaji mstaafu John Mazingaliwa aliwatoa hofu kwamba Yesu Kristo hawezi kuwaacha na badala yake atawapatia ulinzi wa kutosha.

  Askari Polisi na baadhi ya waandishi wa habari waliokuwa ndani ya kanisa hilo walishuhudia fimbo zilizowekwa chini ya viti vya kukalia waumini ambazo zilidaiwa kuwa ni kwa ajili ya kujihami kwa lolote litakalotokea.

  Pamoja na ulinzi huo, ibada hiyo iliendelea kwa utulivu chini ya Mchungaji Mazingaliwa aliyewasihi waumini wake, waliofurika kwa rika zote wawe na moyo wa ushupavu kufia dini yao kwa kutetea haki yao.

  Mmoja wa askari hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alidai kuwa baadhi ya akina mama waliokuwa wakiendelea na ibada kanisani humo walikuwa na mawe waliyoyaficha kwenye mifuko ya plastiki na wengine kenye mikoba yao.

  Alisema baadhi yao walisita kuingia kanisani na silaha hizo za jadi na wengine polisi waliwagundua na kuwanyang’anya silaha hizo ili kuepusha uvunjifu wa amani.

  Kwa kawaida kanisa hilo lina ibada moja tu ya Misa Takatifu ambayo huanza saa tatu, lakini jana alfajiri taarifa aza ujio wa Askofu huyo zilipowafikia baadhi ya viongozi na waumini, kulifanyika mkutano na taarifa za kuwahi kanisani zilisambazwa.

  Baada ya kusambaa kwa taarifa hiyo, waumini hao walifika kanisani hapo na ibada ilianza mapema kuliko ilivyo kawaida, kwenye saa mbili asubuhi, ili kuhakikisha kuwa Askofu huyo haingii kanisani humo kwa kuwa kiongozi huyo na ujumbe wake walitarajiwa kuanza ibada saa tatu asubuhi.

  Hata hivyo tofauti na walivyotarajia, Askofu Kasagara hakuwasili saa tatu badala yake kiongozi huyo ambaye kwa miezi saba aliweka makao yake Mijini Mpanda baada ya waumini wa kanisa hilo ambalo ndilo lenye ofisi yake kumkataa, aliwasili katika kanisa hilo saa sita mchana akiongozana na kwaya kutoka Mpanda mjini na wachungaji wapatao 17. Wachungaji hao walitoka katika makanisa ya Namanyere, Mpanda mjini, Mishamo na Nduruma.

  Lakini walikwaa kisiki kuingia kanisani kwa kuwa waumini wa kanisa hilo walisisitiza kuwa hawamtambui na kwamba hana sifa na mchakato wa kumchagua uligubikwa na rushwa.

  Kutokana na mgomo huo, baadhi ya waumini wanaomuunga mkono Askofu Kasigara ambao ni wachache, waliendelea kukaa nje na kiongozi huyo.

  Mgogoro huo ulianza miezi saba iliyopita ambapo waumini hao walimzuia Askofu Mkuu wa Anglikana, Dk. Valentino Mokiwa kumsimika Askofu huyo katika kanisa hilo ambalo ndio makao makuu, ikabidi tarehe za kazi hiyo kusogezwa mbele na alisimikwa Juni 16 mwaka jana Mpanda mjini.

  Katibu Tawala wa Wilaya, Shilingi akiwa anamwakilisha Mkuu wa Wilaya, Mzurikwao alimtaka Askofu huyo na ujumbe wake wasiingie kanisani na jitihada ifanyike ili pande hizo mbili zikae na walioko tayari ndani ya kanisa waachwe waendelee na ibada.

  “Tumieni busara hii Baba Askofu, kuwa tayari kurudi nyuma katika hili na hao waumini tuwaache waendelee na ibada kwa muda wote waliosema,“ alisisitiza.

  Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa vikali na baadhi ya waumini wanaomuunga mkono Askofu Kasagara na kudai kuwa suluhu ni kanisa hilo lifungwe ili kupisha mjadala.

  Akizungumzia sakata hilo, Askofu Kasagara akiwa amezungukwa na umati mkubwa nje ya kanisa hilo, alisema baadhi ya waumini hao wanaomkataa wana sababu zao lakini aliwataka wajitenge na waabudu mahali pengine na kwamba yuko tayari kuwapatia msaada wowote ule watakaouhitaji.

  Hata hivyo baada ya kuona waumini hao wamegoma kabisa kutoka kanisani, Askofu huyo aliondoka kanisani hapo kwa ahadi kwamba atarudi baadae na waumini waliokuwa kanisani waliamua kukaa ndani ya kanisa hilo kwa madai wanataka kuona mwisho wa jambo hilo.

  Waumini hao walifikia hatua ya kutuma ujumbe majumbani kwao na kuletewa chakula kanisani hapo ili kuhakikisha hata Askofu huyo atakaporudi kama alivyoahidi, asipate nafasi ya kuingia kanisani.

  Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, Askofu huyo alikuwa ameondoka kanisani hapo lakini waumini hao waliendelea kuimba na kusali huku wakiletewa chakula ndani ya kanisa hilo.
   
 2. U

  Uwezo Tunao JF-Expert Member

  #2
  Jan 24, 2011
  Joined: Nov 14, 2010
  Messages: 6,948
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  Kwani vipi tena??
   
 3. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #3
  Jan 24, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 85,149
  Likes Received: 60,358
  Trophy Points: 280
  Macho ya watanzania yamefunguka na sasa wanaelewa ya kuwa kumbe wana sauti juu ya viongozi wao kila mahali...........hali hii ni njema kabisa.........................hatua ya pili ya kudai uhuru wetu ambao waswahili wenzetu wametupora............
   
 4. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #4
  Jan 24, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 85,149
  Likes Received: 60,358
  Trophy Points: 280
  Si usome hilo purukshani za waumini kumkataa Baba Askofu ya kuwa hana sifa za kuendesha ibada...............
   
 5. U

  Uwezo Tunao JF-Expert Member

  #5
  Jan 24, 2011
  Joined: Nov 14, 2010
  Messages: 6,948
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  Akina Masanja na Joti hili sakata la Askofu na waumini wake huko Sumbawanga (au kwa lunga nyingine Tupa Uchawi) ni bonge la picha ya bure. Lazima kuna ufisadi fulani chini ya bahari ya mambo huko.
   
 6. Mahesabu

  Mahesabu JF-Expert Member

  #6
  Jan 24, 2011
  Joined: Jan 27, 2008
  Messages: 4,938
  Likes Received: 507
  Trophy Points: 280
  tabia za dini nyingine zikianza kuingia kanisani ni za kutiliwa shaka....!
   
 7. Gama

  Gama JF-Expert Member

  #7
  Jan 24, 2011
  Joined: Jan 9, 2010
  Messages: 7,768
  Likes Received: 722
  Trophy Points: 280
  Biashara+ maslahi= ngumu+ virungu.
   
 8. Gama

  Gama JF-Expert Member

  #8
  Jan 24, 2011
  Joined: Jan 9, 2010
  Messages: 7,768
  Likes Received: 722
  Trophy Points: 280
  Biashara+ maslahi= ngumi+ virungu.
   
 9. Pastor Achachanda

  Pastor Achachanda JF-Expert Member

  #9
  Apr 21, 2014
  Joined: May 4, 2012
  Messages: 3,006
  Likes Received: 932
  Trophy Points: 280
  Tumefika huku?Kwa hiyo askofu hakuendesha ibada ya pasaka makao makuu?Du karibu kwenye kalamu!
   
 10. Aadilu

  Aadilu JF-Expert Member

  #10
  Apr 21, 2014
  Joined: Mar 20, 2013
  Messages: 625
  Likes Received: 131
  Trophy Points: 60
  Ndio ugundue hakuna tabia za dini fulani linapokuja suala la kudai haki.
   
Loading...