The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,800
USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU.jpg

Hivi karibuni matukio ya usafirishaji haramu yameonekana kuzidi kushika kasi na kuibuka katika mazingira ambayo watu wengi wasingeweza kudhani. Makala ya hivi karibuni iliyorushwa na kituo cha televisheni cha BBC ilionesha jinsi baadhi ya watu wenye ulemavu wanavyorubuniwa na kupelekwa nchini Kenya ambapo wanatumikishwa kwa kuwa ombaomba kwa ajili ya watu au magenge ya kihalifu.

Si muda mrefu baadaye pia kuliibuka taarifa za kuwa takriban ombaomba 78 kutoka katika vijiji vya Tanzania walikamatwa jijini Nairobi katika operesheni iliyolenga kuvunja mtandao wa siri wa biashara hiyo haramu ya kuwalazimisha watu kuingia katika maisha ya kuombaomba. Lakini pia kuna matukio mengi ya watu kurubuniwa au kulazimishwa kwenda maeneo mbalimbali ambako hujikuta wakifanya kazi ambazo hawapo tayari kuzifanya, mara nyingi ikiwa ni katika mazingira magumu ambayo yanawaathiri kwa kila namna.

Mabilioni haramu

Biashara hii inahusisha usafirishaji haramu wa watu (mmoja mmoja au kikundi) kwa nguvu au udanganyifu kwa madhumuni ya kuwatumikisha kikazi au kingono, kwa lengo la kuwaingiza katika ndoa za lazima, kuvuna viungo vya mwili n.k. Makadirio ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) yanaonesha kuwa watu milioni 50 walikuwa wakiishi katika utumwa wa kisasa mwaka wa 2021. Kati ya watu hao, milioni 28 walikuwa katika kazi za kulazimishwa huku milioni 22 wakinaswa katika ndoa za kulazimishwa. ILO pia inakadiria kuwa kazi za kulazimishwa (forced labor) ni biashara haramu inayoingiza dola bilioni 150 kwa mwaka.

Waathiriwa wa usafirishaji mara nyingi wanakabiliwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika nchi wanazopelekwa. Hii inatokea pale ambapo waathirika hutengwa kabisa na mifumo ya usaidizi na wanajikuta wakiwa chini ya udhibiti wa watesi wao kwa muda mrefu.

Sera nyingi za serikali zinatoa kipaumbele kuwaweka kizuizini, kuwafungulia mashtaka na kuwafukuza nchini kwa makosa yanayohusiana na hali zao, ikiwa ni pamoja na ukiukaji wa sheria za uhamiaji, ukahaba au ombaomba. Sera hizi ‘zinamdhulumu mwathiriwa,’ na kusababisha ukiukaji zaidi wa haki za binadamu.

Kujinasua utumwani

Hata hivyo, kutokana na nguvu isiyotosha katika mapambano ya janga la biashara hiyo, waathiriwa wengi hulazimika kujinasua wenyewe mikononi mwa watesi wao na baadaye kuripoti kwa mamlaka. Hii ni kwa mujibu wa Ripoti ya Usafirishaji Haramu wa Binandamu (Global Report on Trafficking in Persons, 2022) ya mwaka 2022 iliyozinduliwa Januari 24, 2023 na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC). Kesi nyingine huanzishwa na vyombo vya kusimamia sheria kama vile polisi, maafisa uhamiaji n.k, huku zingine zikitolewa ripoti za awali na wanajamii pamoja na asasi za kiraia.

Hata hivyo, waathirika wengi wanaweza wasijitambue kuwa wapo katika mazingira ya kitumwa.

Kutotosha_kwa_juhudi_dhidi_ya_biashara_ya_usafirishaji_haramu_wa.jpg

Madhila kwa waathiriwa

Waathiriwa mara nyingi hukabiliwa na hali mbaya ikiwa ni pamoja na kazi nyingi bila mapumziko, kufanya kazi bila ulinzi na vifaa vya usalama au ukatili wa kimwili unaotekelezwa na wasafirishaji wao. Kwa kuongezea, waathiriwa wanaweza kukabiliwa na hatari za kiafya kama vile magonjwa ya zinaa au kujikuta wakiingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

Pia, mara nyingi walionusurika hupata hatari kubwa za afya ya akili kutokana na kusafirishwa kwa mateso, ukosefu wa usalama, hofu, n.k. Tafiti nyingi zinaonesha viwango vya juu vya tatizo la mfadhaiko unaotokana na matukio ya kutisha na kuumiza – yaani Post-traumatic stress disorder (PTSD) kwa walionusurika. Usafirishaji haramu unaweza pia kusababisha kupoteza kumbukumbu, unyonge, na hata kujiua.

Watoto wanaosafirishwa huwa hatarini zaidi kutokana na umri wao. Usafirishaji haramu wa binadamu wa aina yoyote huathiri sana ukuaji mzuri wa kihisia, kimwili na kiakili kwa ujumla. Wanaposafirishwa kimataifa, wanaweza kushindwa kuomba usaidizi au kujaribu kukimbia kutokana na changamoto za lugha, vizuizi vya kijiografia n.k

Juhudi zaidi zinahitajika

Biashara haramu ya binadamu haitokei tu. Ni matokeo ya dhuluma zingine zinazoendelea na ukosefu wa usawa katika jamii yetu na uchumi wetu. Wasafirishaji huwarubuni waathirika kwa kujifanya wana lengo la kuwapa kitu wanachotaka au kuhitaji sana. Wakati mwingine ni kazi. Wakati mwingine ni upendo, au mahali salama pa kulala.

Ni muhimu haki za binadamu ziwe msingi wa mkakati wowote wa kupambana nabiashara hii. Mkakati unapaswa kulenga kutambua na kurekebisha mila za kibaguzi na kuhakikisha kuna mgawanyo sawa wa huduma za kijamii. Ni vema mataifa kuwekeza katika utambuzi wa haraka wa waathiriwa kupitia uchunguzi unaozingatia haki za binadamu, na kutoa ulinzi mara tu viashiria vya msingi vya usafirishaji haramu wa binadamu vinapogunduliwa.

Pia kuna haja ya nchi kukuza jukumu la ulinzi wa kijamii ili kukabiliana na suala hili, yaani, kusisitiza kuwa yeyote anayeona viashiria vya kutokea kwa tatizo hili anapaswa kutokaa kimya. Serikali zinapaswa kuboresha mifumo ya kuripoti uhalifu kwa siri mtandaoni. Wadau wote – yaani Serikali, taasisi binafsi na jumuiya ya kimataifa zinapaswa kushirikiana ili kuongeza uelewa wa tatizo hili kwa kuongeza sauti dhidi yake kupitia majukwaa mbalimbali na vyombo vya habari.
 
Back
Top Bottom