Kumbukumbu ya Ramadhani 7

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,923
30,272
KUMBUKUMBU YA RAMADHANI 7: FUTARI KWA AZIZ ALI MTAA WA MBARUKU NA CONGO 1940s

Aziz Ali alikuwa tajiri na akaupamba utajiri wake kwa ukarimu.

Yeye alikuwa mjenzi wa majumba na alikuwa akimjengea mtu nyumba na akashindwa kumlipa alimpa muda alipe kwa taratibu.

Kwa wema wake huu watu wa Dar es Salaam wakampa jina la ''Aziz'' yaani ''Kipenzi.''

Lakabu hii ikaua jina lake la Ali Kidonyo akafahamika kwa jina la Aziz Ali.

Nyumbani kwake Mwezi wa Ramadhani kuanzia tarehe mosi hadi mwisho wa mfungo ikiingia magharibi watoto wake wa kiume Waziri (Dossa), Ramadhani na Hamza na watoto wa jirani walikuwa wanajumuika kufagia uwanja na kutandika majamvi kwa ajili ya watu watakokuja kufuturu barazani kwao.

Nyumba yake ilikuwa Mtaa wa Mbaruku na Congo jirani na nyumba ya babu yangu Salum Abdallah.

Miezi ya kawaida Aziz Ali nyumbani kwake ikiingia magharib mwanae Hamza alikuwa na kazi ya kuwasha karabai na kuzitawanya katika misikiti yote ya Kariakoo.

Baada ya sala ya Isha Hamza atazipitia karabai zote kuzirejesha nyumbani kwa matayarisho ya siku ya pili.

Hii ndiyo ilikuwa kazi yake Hamza Aziz na haya kanieleza mwenyewe kwa kinywa chake.

Miaka hiyo misikiti ya Kariakoo ilikuwa haina umeme.

Misikiti mingi ya Dar es Salaam ilijengwa na Aziz Ali na alipofariki Tanganyika Standard liliandika kwa wino uliokoza: ''Aziz Ali Mjenga Misikiti Amefariki.''

Aziz Ali alikataa kumpeleka mwanae mkubwa shule Dossa kuanza darasa la kwanza hadi kwanza aingie chuoni ahitimu mashafu.

Haya kanieleza mwenyewe Dossa nyumbani kwake Mlandizi mbele ya Ally Sykes.

Mzee Dossa anasema kwa ajili hii alianza darasa la kwanza akiwa na miaka 14 na ndiyo sababu yeye kusoma darasa moja na Abbas Sykes ambae kwake alikuwa mdogo kwa umri.

Akanambia na ndiyo sababu ya urafiki wake na Abbas Sykes kuwa mkubwa kuliko urafiki aliokuwanao na kaka zake Abdulwahid na Ally.

Aziz Ally alijenga jumba la fahari la vioo na vigae Mtoni na sehemu ilipo nyumba yake hii inaitwa Mtoni kwa Aziz Ali hadi leo.

Kwa miaka ile hakuna Mwafrika alikuwa na nyumba kama ile.

Nyumba mfano wa hiyo zilikuwa Oyster Bay makazi ya Wazungu.

Aziz Ally barza yake kubwa ya maongezi ilikuwa Mtaa wa Stanley na Sikukuu nyumbani kwa Kleist Sykes na ndipo lilipokuwa duka lake la vifaa vya ujenzi.

Hii ilikuwa barza maarufu ya wazee wa Dar es Salaam.

Barza hii ilififia baada ya kifo cha Kleist Sykes mwaka wa 1949.

Aziz Ali alikufa muda mfupi baada ya kutoka safari ya Hijja mwaka wa 1951.

1710760501628.png

Aziz Ali​
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom