Kumbukumbu ya uhuru wa tanganyika 9 desemba 1961

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,923
30,272
KUMBUKUMBU YA UHURU WA TANGANYIKA 9 DESEMBA 1961 2
KISA CHA FUNDI MUASHI, FUNDI CHERAHANI NA WASOMI WA CHUO KIKUU CHA MAKERERE 1955 SEHEMU YA KWANZA

Katika sehemu ya kwanza tumeoa jinsi wananchi wawili wa kawaida kabisa tena wasio na elimu kubwa walivyoweza kuweka mipango ya kufungua tawi la TANU Dodoma ili kupigania uhuru wa Tanganyika.

Fikra ya Mzee Edward Mwangosi ilikuwa harakati hizi ziwashirikishe wasomi wa Makerere ambao walikuwa waalimu Kikuyu Secondary School.

Bahati mbaya hawa hawakuweza kwa sababu ya kufikiria kazi zao ambazo waliogopa watasipoteza endapo DC Mwingereza Mr. Smith angetambua kuwa walikuwa wanashiriki katika siasa za TAA.

Jukumu hili likawa chini ya wananchi wa kawaida wakiongozwa na fundi muashi wa PWD Haruna Taratibu na fundi cherehani Omar Suleiman.

Endelea kusoma sehemu ya mwisho.

Kwa bahati nzuri katika gari moshi lile lile ambamo Taratibu na wenzake walikuwa wakisafiri kulikuwa na wajumbe wa TANU kutoka Kigoma, Bukoba na Mwanza wakisafiri kwenda Dar es Salaam kuhudhuria mkutano mkuu wa kwanza wa mwaka wa TANU.

Hii ilikuwa mwaka wa 1955.

Wahudumu ndani ya gari moshi walipofahamu kuwa walikuwa na wajumbe wa TANU kwenye gari moshi lile, waliwafanyia heshima kubwa.

Mmoja wa wahudumu wale alijitolea kumpa malazi Salum Mussa nyumbani kwake Dar es Salaam.

Mahdi Mwinchumu aliwapeleka Haruna Taratibu na Said Mussa makao makuu ya TANU New Street ambako walifanya mazungumzo na Nyerere pamoja na Rupia.

Uongozi wa makao makuu ulielezwa kwa ufupi matatizo yaliyokuwa yakikabili Dodoma katika kufungua tawi la TANU.
Papo hapo Nyerere alimwalika Taratibu kuhudhuria mkutano mkuu Hindu Mandal Hall kama mjumbe wa Jimbo la Kati.

Mkutano ule ulimchagua Taratibu kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU.

Taratibu na ujumbe wake walirudi Dodoma washindi, walikwenda Dar es Salaam watu wasiojulikana na walirudi nyumbani wakifuatana na mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa wa TANU, chombo cha juu kabisa katika chama.

Nyerere alimpa Taratibu dafari ya tasjili ya wanachama, kadi mia moja hamsini za uanachama wa TANU na nakala hamsini za ''Bill of Rights.''

Kazi ya kuwahamasisha na kuwaingiza watu TANU alipewa Omari Suleiman, na fundi cherahani mwingine aliyejulikana kwa jina la Abdu Mohamed Mkamba.

Mara tu baba mwenye nyumba wake alipopata habari za kuwa mpangaji wake, Haruna Taratibu alikuwa mwanachama wa TANU, alimfukuza kutoka kwenye nyumba yake.

Baada ya kupata kikundi kidogo cha wanachama, Taratibu alipiga simu makao makuu ya TANU na kuzungumza na kaimu katibu, Elias Kissenge akaomba ruhusa ya kufanya uchaguzi.

Kissenge hakuweza kutoa uamuzi wowote wa maana kuhusu tatizo la uongozi wa TANU Dodoma.

Taratibu alifanikiwa kumpata Kambona ambae aliidhinisha uchaguzi ufanyike kwa shuruti moja la kuwa Hassan Suleiman na Ali Ponda waruhusiwe kushiriki na kugombea uongozi wa chama.

Kusisitiza kwa Kambona juu ya uongozi wa zamani wa TAA kuongoza chama kipya huenda kulishawishiwa na mafanikio ya zamani ya uongozi wa Hassan Suleiman mbae alimfahamu huko Dodoma wakati Kambona alipokuwa mwalimu akifundisha Kikuyu Secondary School.

Kwa bahati mbaya, wanachama wa TANU waliokuwa wanainukia na chama pale mjini Dodoma waliwaona Hassan Suleiman na Ali Ponda kama wasaliti kutokana na kutokushirikiana na wenzao katika kuanzisha TANU.

Wakati ametatizwa na tatizo la uchaguzi wa TANU, Taratibu alijulishwa na makao makuu kuwa makamo wa rais, John Rupia, atapita Dodoma kwa gari moshi akiwa njiani kwenda Tabora kushughulikia mambo ya chama.

Gari moshi liliposimama Dodoma Rupia alishangazwa kuona kundi la wanachama wa TANU wakimsubiri katika kituo cha gari moshi wakimtaka avunje safari waende mjini kujadili na kutatua tatizo la uchaguzi.

Rupia aliwaeleza wanachama wa TANU wa Dodoma kuwa yeye hakuwa na idhini kutoka makao makuu kufanya shughuli yoyote ya chama mjini Dodoma.

Wanachama wa TANU hawakutaka kusikia lolote na walimwambia Rupia kuwa wamechoshwa na makao makuu kwa kushindwa kwake kutoa uamuzi wa tatizo la uchaguzi.

Mizigo ya Rupia ilishushwa chini kutoka kwenye gari moshi na Rupia akawa hana khiyari isipokuwa kuwafuata wale wanachama wa TANU hadi mjini.

Ghafla mji mzima ukavuma tetesi kuwa makamu wa rais wa TANU, John Rupia, yupo mjini kufungua tawi la TANU.

Rupia alimwita Hassan Suleimna na akamtaka alete hati ya tasjili ya TANU Hindu Mandal siku inayofuata, mahali ambako mkutano utafanyika.

Hassan Suleiman hakutokea mkutanoni lakini alimtuma mtu apeleke ile hati.

Ali Ponda alihudhuria mkutano ule. Rupia alikuwa mwenyekiti wa mkutano na TANU ikafanya uchaguzi wake wa kwanza.

Alexander Kanyamara alichaguliwa Rais; Haruna Taratibu Makamu wa Rais, Abdu Mohamed Mwamba, Katibu na Omari Suleiman Mweka Hazina.

Miongoni mwa wanachama waasisi alikuwa mwanamke mmoja wa Kimanyema, Binti Maftah Karenga; wengine walikuwa Bakari Yenga, Maalim Khalfan, mwanachuoni wa Kiislamu aliyekuwa akiheshimawa sana, Idd Waziri na Said Suleiman.

Wale wasomi wa Makerere hata mmoja hakujitokeza kwenye mkutano huu wa kuasisi TANU.

Ali Juma Ponda, mwanasiasa mkongwe alipuuzwa na hakuchaguliwa kushika wadhifa wowote.

Walipoona hawakupewa wadhifa wowote katika TANU, Ali Ponda na Hassan Suleiman walijiunga na UTP kuipinga TANU.

Baada ya uchaguzi huo, wale mafundi cherahani wawili, Abdu Mohamed Mkamba na Omari Suleiman, walianza kuhamasisha wananchi wazi wazi kujiunga na TANU ili wapiganie uhuru wa Tanganyika.

Tawi la TANU la Dodoma baada ya kujizatiti pale mjini, lilituma wanaharakati kuwahamasisha watu wa Kondoa ili wafungue tawi la TANU katika wilaya hiyo.

Abdallah Jumbe alizipenyeza kadi za TANU na kuzipeleka kwenye wilaya hiyo kwa siri akaanza kuandikisha watu.

D.C. wa Singida alikuwa jeuri sana kiasi kwamba ni baada ya Mkutano Mkuu wa Tabora wa mwaka 1958 ndipo Abdallah Jumbe aliweza kufanikiwa kufungua tawi mjini Singida.

Wakati huo TANU ilikuwa na nguvu sana ikiwa na wajumbe wake katka Baraza la Kutunga Sheria.
Kwa ajili hii hakuna Mzungu aliyethubutu kuwa fedhuli kwa TANU na kuwabughudhi wanachama wake.

Picha ya kwanza Julius Nyerere akifungua mkutano wa kwanza wa TANU Ukumbi wa Hindu Mandal, Dar es Salaam tarehe 24 Oktoba 1955.

Picha ya pili wa kwanza kushoto ni Ali Juma Ponda.

Picha ya tatu ni John Rupia kama alivyokuwa mwaka wa 1955.

Screenshot_20211102-070433_Facebook.jpg
 
Back
Top Bottom