Kumbukumbu ya Ramadhani 5

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,268
KUMBUKUMBU YA RAMADHANI 5

MFUNGO WA RAMADHANI MUSCAT 1999, SALA YA EID NDOGO TILBURY 1992, SALA YA EID KUBWA TILBURY PORT 1992 NA SALA YA EID KUBWA REGENT PARK MOSQUE LONDON 1993

Muscat, Oman 1999
Tuanze na Ramadhani Oman.

Nimefunga Ramadhani siku chache Muscat Oman mwaka wa 1999.
Muscat ya mwaka wa 1999 si Muscat ya hivi sasa.

Nilipokwenda Muscat mwaka wa 2016 nimeikuta Muscat nyingine kabisa iliyochangamka.

Nilikuwa nimefika Dubai mwaka huo huo kama miezi mitatu iliyopita ndipo nikaenda Muscat.

Tofauti niliyoiona nikifananisha na Dubai ilikuwa kubwa mno ni kama vile Muscat mji hauna watu.

Kwa mtu aliyefika Dubai na kushuhudia vurugu iliyopo Dubai ya watu walivyokuwa wengi mitaani na barabara zilizojaa watu na magari ataelewa ninachokisema.

Ramadhani ya Muscat ilikuwa imetulia sana.

Ilikuwaje nikarudi London mwaka wa 1993 na kusali Eid al Adha msikiti wa Regent Park?

Kisa cha kushindwa kusali Eid Ndogo Regent Park mwaka wa 1992 nikaenda kusali Msikti wa White Chapel East London nimeshakieleza.

Nilikuwa Le Havre mji Kaskazini ya Ufaransa nikaja Paris kisha London nikikusudia kwenda Cardiff.

Ikasadif kuwa Eid Kubwa imenikuta London ndipo nikaamua kwenda kusali msikiti wa Regent Park, msikiti ambao mwaka uliopita 1992 sikuweza kusali.

Allah ni muweza.

Kanirudisha London Regent Park Mosque kuja kusali Eid Kubwa.
Baada ya sala nimesimama nje ya msikiti barabarani.

Najiuliza niende wapi asubuhi hii London hii isiyokuwa na habari kuwa leo ni Siku ya Eid?

London siku ya Eid na kama siku nyingine yeyote ya kazi.
Ghafla nasikia sauti inaita, ''Sidney, Sidney, Sidney...''

Nimeshtuka sana.
Nani analijua jina langu hili hapa London?

Hata hapo Dar es Salaam si wengi wanalijua jina hili ila wale waliokuwa karibu sana na mimi toka udogoni.

Nageuza shingo namuona anaeniita ni Shufaa Zialor mke wa rafiki yangu Yusuf Zialor yuko upande wa pili wa barabara na wanae na mama mkwe wake mama yetu Bi. Asha.

Ndugu zangu hawa kutoka Dar es Salaam lakini kwa miaka mingi wamehamia London na kwao nikienda wakati niko Cardiff.

Nyumba yao iko jirani na kwangu Masaki.
Furaha yangu ilikuwa kubwa sana.

Tilbury Port, 1992

Mwaka uliopita 1992 nilisali Eid Kubwa Tilbury.
Huu mji ni bandari ndogo kilomita chache nje ya London.

Eid ilinikuta nikiwa katika mji huu.

Asubuhi mimi na wanafunzi wenzangu wote kutoka Nigeria tukaamua kwenda kusali Eid lakini toka kufika mji ule hatukupata kuona msikiti popote.

Tukatoka kuelekea mjini.

Tilbury ulikuwa mji uliohamwa kwa kuwa hekaheka za sera za uchumi za Margaret Thatcher ziliuathir sana.

Wakazi wake wakitegemea bandari na bandari ilikuwa inachechemea.
Mji ulikuwa mfano wa ''Ghost Town.''

Katika maisha yangu yote sijapatapo kuona mji kama huu.

Maduka ya mji yamefungwa unachokiona ni kufuli katika madirisha makubwa ya vioo ya maduka na milango yenye kufuli na nje matangazo ya biashara yaliyopauka.

Barabara nzima ukitembea unajikuta uko peke yako kisha wewe ni mgeni.
Mji hauna msikiti.

Tukiwa tunahangaika kutafuta msikiti akapita mzee mmoja wa Kihindi ndani ya gari na naamini kilichomfanya asimame ni yale mavazi ya Kinigeria waliovaa wenzangu.

Akatuuliza kama tulikuwa tunatafuta msikiti wa kusali Eid.

Alituchukua hadi kwenye shule ya msingi ambako ndani ya darasa moja ndipo sala ya Eid ilikuwa inasaliwa.

John Hopkins University, Maryland 2011

Mwaka wa 2011 nikiwa Washington DC nikaja kwa mara nyingine tena kusali Sala ya Ijumaa ndani ya darasa, John Hopkins University.

Hapa nataka niongeze kitu ingawa hakihusiani na Ramadhani wala Eid.

Nilikwenda Washington DC kumtembelea rafiki yangu Dr. Harith Ghassany mwaka wa 2011.

Ijumaa imefika akanichukua kwenda kusali.
Tulisali Sala ya Ijumaa John Hopkins University ndani ya darasa.

Hakika kutembea ni elimu tosha.

Picha: Nje ya msikiti Muscat na Ismail ''Gigi'' Bahdor, Mwana Kariakoo mwenzangu.

Ismail Bahdor alifurahi sana kuniona.

Mimi na mwenyeji wangu tulikuwa tunatoka msikitini na yeye alikuwa ndiyo anaingia kusali Dhuhr.

1710535049151.png
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom