Kumbe Muungano ukivunjwa Zanzibar wana maili 10 tu kutoka nchi kavu

MSHINO

JF-Expert Member
Jul 26, 2013
1,067
709
Wanajamii hii nimeipata sehemu kwenye mtandao hapo chini, inaonyesha mipaka ya Zanzibar kabla ya Muungano ni maili 10 tu kutoka nchi kavu, je sehemu iliyobaki ni ya Tanganyika au Madascar au Kenya? soma kidogo baadhi ya hotuba ya maalimu seif ya Kiabanda maiti akithibitisha hilo.

…………………….. Katika miaka ya 1880 na 1885, Wakoloni walianza kuingia sehemu hizi... Wakaamua kugawana Afrika. Katika mkutano uliofanyika Berlin 1885 wakamnyang'anya mtawala wa Zanzibar (Sultan Hamad bin Thuwaini) sehemu yote ya Afrika. Zanzibar wakaachiwa visiwa pamoja na Mwambao wa maili kumi kwenda ndani. Kuanzia kaskazini mwa Kenya mpaka kusini ya Tanganyika. Ilikuwa yote hayo ni mamlaka ya Zanzibar. Wajerumani wakaamua kuununua ule mwambao wa maili kumi wa Tanganyika. Kenya Wajerumani hawakuinunua, mwambao wa Kenya ulibaki sehemu ya Zanzibar, Lamu ilikuwa sehemu ya Zanzibar mpaka mwaka 1963, Kenya ilipopata Uhuru wakakubaliana waache. Tukabaki na Unguja na Pemba kama nchi.


source: http://www.islamtanzania.org

Pia nimegundua kuwa kumbe Wanzazibar wanajua ukoloni ulianza 1885 baada ya mzungu kufika, kumbe Mwarabu alikuwa mwenzao japo alikuwa aliwauza kama wanyama. nafikiri hata maalimu Seif wakati anatoa hiyo hotuba alijisahau kwa kujifanisha na na mwarabu, angalia sentensi ya kwanza hapo juu" Katika miaka ya 1880 na 1885, Wakoloni walianza kuingia sehemu hizi...

Wakaamua kugawana Afrika. Katika mkutano uliofanyika Berlin 1885 wakamnyang'anya mtawala wa Zanzibar (
Sultan Hamad bin Thuwaini)............................................
Je Zanzibar ni warabu?

====================================

Hotuba ya Maalim Seif Kibanda Maiti

Waheshimiwa naomba niungane na Mwenyekiti wa Wilaya kuwashukuruni nyote ambao jioni hii mmeamua kushiriki kwa ukamilifu katika kikao hiki au mkutano huu ambao ni miongoni mwa mikutano yetu ya kampeni. Mimi nadhani ukikaa hapa kwenye jukwaa utadhani kuna bahari hivi sio watu.

Waheshimiwa, leo tumekutana hapa, ni mkutano maalum. Asubuhi leo nilikuwa na mkutano na waandishi wa habari, na ilikuwa mada yetu kubwa ni elimu, tayari nishazungumza na waandishi juu ya mada ya Uchumi na mkutano unaokuja tutazungumza na waandishi juu ya mada ya Afya. Sasa kuna suala moja ambalo ni muhimu sana sana nimehisi nilizungumze na wazanzibari moja kwa moja. Ndio maana ya mkutano huu. Na naamini Wazanzibari wengine ambao hawakuwahi kufika naamini wananisikiliza, naomba wanisikilize kwa makini.

Mada ya leo ni kuhusu hatma ya nchi yetu, hatma ya Zanzibar yetu, Zanzibar katika Muungano. Waheshimiwa, napenda nianze mada hii kwa kusema kwamba Zanzibar ina historia ndefu. Katika sehemu hii ya Afrika; Afrika mashariki na Afrika ya kati, Zanzibar ndio ilikuwa kwa kweli ni Dola ya kwanza. Dola hii ni Dola ambayo ilisambaa kuanzia hapa visiwani kwetu moja kwa moja... Tanganyika ilikuwa ni sehemu ya Dola ya Zanzibar, Kenya ilikuwa sehemu ya Dola ya Zanzibar, Uganda ilikuwa ni sehemu ya Dola ya Zanzibar, Mashariki ya Congo ilikuwa ni sehemu ya Dola ya Zanzibar, Kaskazini ya Malawi ilikuwa ni sehemu ya Dola ya Zanzibar. Kwa hiyo, Zanzibar ni nchi, sehemu au Dola yenye historia ndefu kabisa.

Katika sehemu hizi za Afrika Mashariki na kati dola ambayo ilitambulikana katika miaka ya karne ya 19 ni Zanzibar. Hapa Zanzibar palikuwa na Mabalozi wa nachi mbali mbali Wakiziwakilisha nchi zao.

Hii Zanzibar ilikuwa ni Dola kabla ya Tanganyika, Kenya, Uganda na katika nchi nyingine Afrika ya Mashariki na ya kati. Huo ndio utukufu wa Zanzibar.

Katika miaka ya 1880 na 1885, Wakoloni walianza kuingia sehemu hizi... Wakaamua kugawana Afrika. Katika mkutano uliofanyika Berlin 1885 wakamnyang'anya mtawala wa Zanzibar sehemu yote ya Afrika. Zanzibar wakaachiwa visiwa pamoja na Mwambao wa maili kumi kwenda ndani. Kuanzia kaskazini mwa Kenya mpaka kusini ya Tanganyika. Ilikuwa yote hayo ni mamlaka ya Zanzibar. Wajerumani wakaamua kuununua ule mwambao wa maili kumi wa Tanganyika. Kenya Wajerumani hawakuinunua, mwambao wa Kenya ulibaki sehemu ya Zanzibar, Lamu ilikuwa sehemu ya Zanzibar mpaka mwaka 1963, Kenya ilipopata Uhuru wakakubaliana waache. Tukabaki na Unguja na Pemba kama nchi.

Katika miaka ya 1950, 56, 57, Wazanzibari wakaunda vyama vya siasa, kumwondoa mkoloni.

Tukawa na Afro - Shirazi Party, Zanzibar Nationalist Party au Hizbu, Zanzibar and Pemba People's Party (ZPPP), tukawa na Umma Party.

Hivi ni vyama vilivyotafautiana kwa sera, kwa itikadi, lakini vyote vilishirikiana kumuondoa mkoloni Zanzibar.

Zanzibar ikapata uhuru tarehe 10/12/1963. Hapo Muingereza akaondoka. Alipoondoka Muingereza, Mkuu wa nchi akawa Sultani.

Zanzibar na Kenya zikajiunga na Umoja wa Mataifa kama wanachama kamili 13/12/1963 na bendera ya Zanzibar ilipanda katika Umoja wa Mataifa kama nchi nyingine.

12/1/1964 tukapinduana. Afro-Shiraz Party wakafanya mapinduzi, wakaipindua serikali ya Sultan, na Sultan akakimbia nchi.

Sasa, baada ya hapo ikaundwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ... ilikuwa ni serikali kamili, ni dola yake ya Wazanzibari. Tukawa na wimbo wetu wa Taifa. Tukawana Rais wetu Zanzibar.

Bahati mbaya uhuru huu wa Zanzibar ulidumu kwa siku 137 tu. Ilipofika tarehe 26/4/1964, Wazanzibari wakasikia ikitangazwa kuwa Zanzibar na Tanganyika zimeungana kufanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Siku 137 ikawa Zanzibar kama nchi, kama dola imekwisha, haipo tena.

Kwahivyo wazee wetu hawa wakaunganisha nchi. Lakini tuangalie nini kilitokea katika kuunganisha nchi.

Kwanza tujue tulikuwa na mkataba wa Muungano. Mkataba huo ulionesha kwamba kutakuwa na mamlaka tatu. Kwahiyo wakakubaliana yako mambo yatakuwa ni ya Muungano na yapo ambayo si ya Muungano. Kwahiyo wakakubaliana pawe na mamlaka tatu. Moja itasimamia mambo ya Muungano, mamlaka ya pili itasimamia mambo yasiyo ya Muungano kwa upande wa Zanzibar ikawekwa mamlaka yake tofauti (halikadhalika) Tanganyika. Lakini serikali zikawa mbili. Tukaambiwa ati Zanzibar watakuwa na serikali yao kusimamia mambo ambayo si ya Muungano.

Lakini Tanganyika mambo yao yatasimamiwa na serikali hiyo hiyo ya Muungano. Hapo ndipo kilipoanza "Kizungumkuti" hapo. Hapo ndio mwanzo wa "Kizungumkuti" hapo.

We una mamlaka, kwa serikali ya Muungano ilipaswa isimamie mambo ya Muungano. Na Tanganyika serikali yao isimamie mambo yao yasiyo ya Muungano. Lakini tukaambiwa kwamba, serikali ya Muungano ndiyo itakayosimamia (pia) mambo yote ya Tanganyika.

Sasa maana yake nini! Maana yake Tanganyika ikajivika joho la Muungano.


Na angalia baada ya Muungano, Katiba iliyoendelea kutumika ni katiba ya Tanganyika. Bendera iliyotumika ni bendera ya Tanganyika iliyofanyiwa marekebisho madogo. Nembo ile Adam na Hawa ni ile ile iliyokuwa ya Tanganyika ikaambiwa sasa ni ya Muungano.

Kwahiyo kila lililokuwa jambo la Tanganyika likafanywa la Muungano. Kwa hiyo sisi Zanzibar tukatoa madaraka yetu tukidhani tunaikabidhi serikali ya Muungano na Tanganyika watatoa madaraka yao wayakabidhi serikali ya Muungano, lakini lililotendeka, Tanganyika wakawa ndio Muungano. Kwahiyo tuliopoteza ni sisi Wazanzibari. Sio Tanganyika. Tanganyika ndio maana mpaka leo ukizungumzia serikali tatu wanakuwa wakali kweli kweli.

Kwasababu ikiwepo serikali tatu kutakuwa na chombo tofauti chakusimamia mambo ya Muungano. Na hapo watakuwa wao wametoa na sisi tumetoa.

Suala la katiba hiyo ambayo ilikuwa ya Tanganyika ikaambiwa sasa ya Muungano, kwa mujibu wa makubaliano ya Muungano ni kwamba katiba hiyo ilikuwa idumu kwa muda usiozidi mwaka mmoja tu basi. Kabla ya mwaka kuisha ilikuwa Rais aunde Tume ya kuandaa mapendekezo ya katiba. Halafu aitishe Bunge maalum la katiba kufanya katiba ya Jamhuri ya Muungano. Mwaka ulimalizika halikufanyika hilo.

Tukaendelea na utaratibu huo (katiba ya Tanganyika) kuanzia 1964 mpaka 1977 baada ya TANU na Afro kuungana, ile ile kamati ya TANU na Afro ndio zikaambiwa sasa itayarishe katiba ya Jamhuri ya Muungano. Miaka 13 imeshapita. Na bunge lile lile ndio ikaambiwa litunge katiba mpya.

Kwa hiyo hata yale makubaliano ya muungano hayakufuatwa.

Kwa mujibu wa mkataba wa Muungano, ilikuwa baada ya huwekewa saini Muungano, basi bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar kila mmoja kwa upande wake lithibitishe makubaliano ya Muungano. Bunge la Tanganyika lilifanya hivyo, lakini kumbukumbu zote zinaonyesha Baraza la Mapinduzi halikufanya kazi hiyo, Baraza la Mapinduzi mpaka hii leo haijathibitisha makubaliano ya Muungano. Kwahiyo nataka mjue mazingira ya Muungano ni hayo, ujanja ujanja, ulaghai.

Tumeungana 1964 na mambo ambayo yamo katika mkataba wa Muungano, waasisi walikubaliana ni 11 tu.

Naona niwasomee myajue: Jambo la kwanza ilikuwa ni Katiba ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Tanzania.

La pili, mambo ya nchi za nje. Tatu, Ulinzi. Nne, polisi. Tano, mamlaka juu ya mambo yanayohusu kutangaza hali ya hatari. Sita, Uraia. Saba, Uhamiaji. Nane, mikopo na biashara ya nje.

Tisa, utumishi katika serikali ya Jamhuri ya Muungano. Kumi, Kodi ya mapato, ushuru wa forodha na kumi na moja Bandari, usafiri wa anga na posta na simu.

Lakini kuanzia hapo mpaka leo mambo hayo yamekuwa yakiongezwa hadi sasa yashafika 23. Na ukijayachambua moja moja yanafika 36. Na kama nilivyosema mwanzo, waliosarenda mamlaka ni Zanzibar.

Hiyo ni historia fupi tu. Nataka sasa nije kwenye kiini cha mazungumzo yangu.

Tuangalie athari gani zimepatikana kwa Muungano huu.

Athari ya kwanza ni kuviza na kudunisha uchumi wa Zanzibar. Kwanini. Kwa sababu chombo ambacho kinaweza kusimamia uchumi kwa ufanisi ni Benki Kuu ya nchi yoyote ile.

Tuiangalie Benki Kuu yetu. Kwanza niwaambie Wazanzibari hatuna Benki Kuu. Ndio kusema hatuna chombo cha kudhibiti, kuratibu uchumi wetu.

Benki Kuu iliyopo ni ya Tanzania. Na tuangalie Benki Kuu (hii) imepatikanaje.

Huko nyuma mambo ambayo yalikuwa yafanywe na Benki Kuu kwa Afrika Mashariki nzima, Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar yakifanywa na chombo kilichoitwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency Board).

Sisi kama nchi Zanzibar na mwanachama wa Bodi hiyo tulikuwa na mwakilishi wetu mwenye sauti.

Lakini baada ya muungano tu, viongozi wa Tanganyika wakafanya njama kumtoa mwakilishi wetu kwa kisingizio cha muungano.

Watu wa Bodi wakasema, hatuwezi kwani kwa mujibu wa Muungano wenu, mambo ya sarafu, mabenki, fedha za kigeni haya si mambo ya muungano. Wakakwama.

Lakini wakafanya mbinu wakahakikisha mambo ya sarafu, mabenki, fedha za kigeni yanaingizwa kwenye muungano. Nathubutu kusema yaliingizwa kinyemela. Ghafla likatiwa. Kwamba hili nalo ni jambo la muungano.

Baada ya hapo wakapata nguvu wakarudi katika bodi. Wakadai Zanzibar watolewe, hawana mamlaka juu ya sarafu na mabenki. Kwahiyo watolewe. Tukatolewa Zanzibar. Ikawa sasa sisi tunawakilishwa na Tanganyika katika hiyo Bodi.

Sasa ukaja wakati 1965 kila nchi ikataka iwe na Benki Kuu yake. Ile Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki ikaamua kuzisaidia nchi hizi kwakuzipa mitaji. Kenya wakapewa pesa zao, Uganda wakapewa pesa zao, Tanganyika wakapewa pesa zao. Pesa za Zanzibar je, wakazidai Tanganyika. Wakafanya mbinu mpaka wakazipata.

Ikaanzishwa Benki Kuu ya Tanzania. Kwa maana kwamba, mtaji ni fedha kutoka Tanganyika na Zanzibar.


Sasa kile kima ambacho kilitolewa ikawa kama ni mtaji wa Zanzibar, ni kama asilimia 11.4. Maana yake sisi ni Share holders. Benki ifanye shughuli zake mwisho wa mwaka tugawane faida kwa uwiano huo. Sisi tupate 11.4%. Nadhani kwa miaka zaidi ya 20 tulikuwa hatupati hata senti moja.

Sasa wameamua kutupa wametupa asilimia 4.5. Na anakuja Dkt, Omar anajisifu, Rais Mkapa anawapenda Wazanzibari, anawapa fedha sijui anawapanini.

Hatupi Bwana. Ile ni haki yetu tena tunadhulumiwa. Kwahiyo asizuke akasifu huyu mtu anaipenda sana Zanzibar. Haipendi hata kidogo.


Kama nilivyosema, Benki ndio inadhibiti mambo yote. Ikawa Waziri wetu wa Fedha wa Zanzibar yupo pale kama kusema "dignified clerk" karani aliyevishwa kilemba cha ukoka. Hana madaraka juu ya sera za fedha, sasa atawezaje kujenga uchumi wa Zanzibar.

Na ushahidi upo. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilishaamua kuanzisha kitu kinachoitwa "Off shore Companies" . Ilitumia dola laki moja kwa kazi hiyo. Lakini Waziri wa Fedha wa Tanganyika akasema No. Hakuna ruhsa.

Hili ni suala ambalo lingetumika kujenga uchumi wa Zanzibar kwa mashali ya Wazanzibari. Lakini wenzetu wanasema No. Hivyo nawaambieni uchumi umeathirika kiasi kikubwa.

Sheria iliyoanzisha Benki Kuu ya Tanzania kuna kipengele katika sheria ile kinasema: "Any Political Sub-division in the United Republic is just like a local government." Yaani mgawanyo wowote wa madaraka kisiasa unaofanywa ndani ya Jamhuri hii, basi kama serikali ya mtaa tu basi.

Kwahivyo, kwa sheria ya Benki Kuu serikali ya Zanzibar ni serikali ya mtaa tu basi.

Wakati ule waziri wa Fedha Zanzibar alikuwa marehemu Abdul-Aziz Twala. Marehemu Twala alipigania sana sana haki za Zanzibar. Na yeye alitaka kuanzisha Benki Kuu ya Zanzibar. Wakapigwa stop. Wakaambiwa hapana sheria hairuhusu. Wakataka waanzishe State Bank or National Bank, wakaambiwa hapana. Hii people's Bank mnayoiona hii, waliambiwa anzisheni kama kampuni ya kawaida tu.

Waliambiwa anzisheni kama kampuni ya kawaida tu, halafu watapewa leseni wafanye shughuli za kibenki. Kwahiyo Zanzibar People's Bank imeanzishwa kama kampuni sio kama benki.

Lakini kwanini kwa Zanzibar tu? Wakati Bara walipotaka kuanzisha mabenki yao walitunga sheria maalum ya kuanzishwa mabenki hayo.

Hii benki ya Taifa ya Biashara ilianzishwa kwa waraka au kwa sheria ya 1967, hivyo hivyo kwa CRDB na Mabenki yote. Lakini ya Zanzibar wakaambiwa hapana. Kwahiyo muone jinsi tulivyobanwa. Muone jinsi gani hatuwezi kufurukuta. Hatuwezi kujenga uchumi wetu kwa namna tunavyotaka sisi wenyewe. Hapo ndipo tulipofikishwa Wazanzibari. Hiyo ndiyo hali yetu.

Tunaambiwa kama nilivyosema kabla, kama serikali mbili. Lakini hebu nambieni jamani, mambo ya muungano yanajulikana ni machache tu.

Wizara zinazojulikana za muungano ni nne tu, Mambo ya Ndani, Wizara ya Ulinzi na Wizara ya Elimu ya Juu na Teknolojia.

Hizi ni wizara za Muungano. Lakini nambie, Wizara ya Kilimo Bara, kilimo si suala la Muungano. Waziri wa (kilimo) mwisho wake Chumbe, hawezi kuingia huku. Lakini huyu anaitwa Waziri wa kilimo wa Muungano. Kaipata wapi hii?

Waziri wa Elimu - Sekondari na primari, mamlaka yake yanamalizika Chumbe. Lakini anaitwa Waziri wa Elimu na Utamaduni wa Muungano. Waziri wa Afya wa Bara, yeye ni kwa ajili ya Bara tu, sisi tuna Waziri wetu wa Afya huku. Lakini mbona yule mmoja anaitwa wa Muungano? Kapata wapi mamlaka hayo? Mnakiona kizungumkuti hicho? Mnakiona mkizungumkuti hicho?


Sasa matokeo yake nini. Tanzania ni mwanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloitwa UNESCO, ambalo linaloshughulika na mambo ya elimu na utamaduni. Na kila mwaka mawaziri wanakutana. Anayeiwakilisha Tanzania ni nani? Ni waziri wa bara sio wa Zanzibar.

Tanzania ni mwanachama wa shirika la Afya Duniani (WHO). Kila mwaka wanakutana mawaziri. Anayeiwakilisha Tanzania ni nani? Ni Waziri wa Afya wa Bara, sio wa Zanzibar.

Tanzania ni mwanachama wa shirika la chakula duniani, FAO. Anayewakilisha Tanzania ni nani? Ni waziri wa kilimo wa Bara.

Sasa anakwenda kule huu Utanzania kaupata wapi? Ajaaliwe tu amfikirie mwenziwe amchukue katika safari yake basi. Lakini mwenye mamlaka ni yeye. Akiamua asimchukue mtu kutoka Unguja hachukui. Na hakuna wa kumuuliza.

Mashirika hayo yanasaidia sana maendeleo ya nchi hizo. Sisi Waziri wetu hana mamlaka kule. Kinachotoka atakipata?

Unasema serikali mbili hizi hizi, unajua kubaki kwa serikali mbili ni kuendelea kuonewa, kupunjwa, kudhulumiwa na kudhalilishwa Zanzibar? Unajua hayo wewe? Unajua hivyo wewe?

Tunaendelea kudhalilishwa. Ndio maana tunasema ukitaka kuondoa matatizo ya muungano mbadili mfumo wa muungano waserikali mbili uwe wa serikali tatu.


Mimi sifahamu kwanini wenzetu wa Tanganyika hawalitaki hili. Wataathirika nini wao. Wakiwa na serikali yao wataathirika nini wao! Nini litawaathiri hamna.

Mfano mwingine.

Suala la michezo si suala la muungano. Sisi tunayo wizara yetu ya michezo huku nao wanayo yao. Au hatuna? Lakini leo hata sisi kuwakilishwa katika vyombo vya kilimwengu vya michezo, wenzetu hawataki. Ndio maana ZFA wanataka iwe mjumbewa FIFA lakini Bara wameweka mguu wao. Hawataki. Jamani kwani sisi Zanzibar tukiwa wajumbe na nyinyi mkawa wajumbe, nyinyi mtaathirika nini hasa? Nini wataathirika wenzetu hawa!

Waangalieni wenzenu Waingereza. United Kingdom. Uingereza nchi moja. Lakini Scotland inawakilishwa pale, ile Uingereza yenyewe au England inawakilishwa, Wales inawakilishwa na ni nchi moja; Ireland inawakilishwa. Wana timu nne. FIFA nne, wapi nne kila pahali nne, nne. Wenzetu wanaona choyo, hata sisi kuwa wanachama wa FIFA, mnaona choyo! Jamani; jamani!

Sasa mnapotaka serikali mbili ziendelee mnataka yaendelee haya? Unataka yaendelee kunyanyaswa kwa Zanzibar? Ndio maana yake.

Nasema kwahiyo basi matokeo ya muungano ni kwamba hatuna chombo cha kusimamia uchumi wetu. Ni lazima tukapige magoti kwa wenzetu Bara. Waziri wa Fedha wetu hana mamlaka yoyote. Sasa nchi itaendeelaaje kama huwezi kudhibiti uchumi wako.

Sasa hivi kuna shirika hili linaloitwa TRA. Shirika la kod la Tanzania. Sasa hawa wana branchi yao Zanzibar. Na hapa pana Kamishna na Msaidizi wa TRA. Ilikuwa fedha zinazokusanywa hapa zinakwenda People's Bank; Benki ya Watu wa Zanzibar ambayo ni Benki ya Serikali ya Zanzibar.

Kwa hiyo zile pesa zikitiwa Zanzibar serikali ya Zanzibar inaweza kuzitumia. Lakini kuanzia mwezi uliopita Agosti, mwezi wa nane mwaka huu, Bwana Mkapa anatoa amri, fedha zote zinazokusanywa na TRA ziende BoT yaani Benki Kuu ya Tanzania.

Serikali ya Zanzibar haina madaraka katika Benki Kuu ya Tanzana. Jamani kimebaki nini!

Bendera hatuna, wimbo wa Taifa hatuna, sarafu hatuna, hata kuamua mambo ya nje hatuna uwezo. Basi jamani hata hizi fedha ambazo zinakusanywa katika nchi yetu, hata kuzitumia hatuna ruhusa? Hata kutumia kodi hatuna ruhusa? Maana hata baraza la mji likikusanya manispaa taxes (kodi) wana uwezo wa kuzitumia wenyewe. Leo fedha zinakusanywa katika nchi yetu, serikali ya Zanzibar hawana ruhusa ya kuzitumia. Kumebaki nini jamani? Kumebaki nini?

Juzi nasikia wameleta watu kutoka Bara kuja kuwasimamia hawa wafanyakazi wa TRA akiwemo huyu Kamishna msaidizi, yaani hawa wamepewa madaraka waendeshe shughuli zaolakini hawaaminiwi. Kwahivyo wameletwa wanyapara kuja kuwasimamia.

Jamani tuna nchi? Mna nchi? Wazanzibari mna nchi? Ndio hali tulipofikishwa.

Wamesema Rais Mkapa anaipenda Zanzibar. Lakini mapenzi haya sijui mapenzi gani. Maana mapenzi haya tukiamka viboko. Tukilala bakora, ukitembea jela! Sasa haya mapenzi gani? Kwanini Mkapa anatoa amri sisi wana CUF tuteswe hapa, kwanini hasa? Kwanini. Mimi nasema amri hii niya Mkapa moja kwa moja. Kwasababu Mkapa ndiye Jemedari Mkuu wa majeshi yote. Usalama wanamwarifu mambo yanayofanywa Zanzibar na yeye anasema endeleeni.

Sasa mnajua maana yake? Maana yake moja ni kumsaidia mtu wake ashinde. Ati nyinyi wana CUF mtavunjika moyo mtachoka.

Ya pili ni kwamba anataka mateso yazidi ili Wazanzibari wafike pahala, waseme, si basi hiyo serikali moja ije? Maana nakumbuka wakati wanataka kuunganisha vyama vya Afro na TANU, Zanzibar walishawishiwa na mipango ikafanywa, ikawa hali ya maisha ni ngumu kweli kweli Zanzibar.

Kwahiyo lilipokuja pendekezwa kuunganisha vyama watu wakasema afadhali huenda tukapata ahueni. Na hivyo Wazanzibari wengi wakaunga mkono Afro-Shiraz na TANU vikaunganishwa. Ili kuona vipi, watapata ahueni. Mwalimu Nyerere mwenyewe akasema hapo Amani, kwamba ile furaha aliyoiona katika nyuso za Wazanzibari hajapata kuonapo, kwa kuunganisha vyama.

Mkakati ulikuwa vipi, wataabishe, wapate taabu, baada ya hapo ukija na pendekezo hili watakubali.

Wanadhani wakiwatesa kiasi walichowatesa mtachoka wakisema, basi si afadhali tuwe na serikali moja mtasema ndiooo.

Wazanzibari nimesema hapa kwanini wenzetu ukiwatajia serikali tatu hawataki. Hawa Bwana nitawaambieni sasa hivi hapa. Nchi yenu Zanzibar ni tajiri sana.

Kwa ule ule ulaghai, suala la mafuta na gesi lilitiwa kama ni jambo la muungano.Lakini dhahabu si jambo la muungano. Almasi si jambo la Muungano, mkaa wa mawe si jambo la muungano.

Kitu cha muungano ni mafuta. na kwanini walifanya hivyo. Walifanya vile walishajua Zanziba kuna mafuta mengi sana.

Mwaka 1996/97, serikali ya Muungano iliiomba shirika moja la Canada kufanya uchunguzi. Shirika hilo likagundua mafuta mengi sana.

Sasa ikawa wafanye mipango yachimbwe chini ya serikali ya Muungano. Serikali ya Zanzibar wakachachamaa. Wakatafuta kampuni nyingine ya Kimarekani. Sikilizeni ripoti yao. Wanasema Zanzibar mafuta yaliyopo yakianza kuchimbwa, yatachimbwa kwa miaka 80. Kila mwaka Zanzibar inaweza ikapata dola za Kimarekani bilioni 100.

Sasa kwa mpango wa sasa kwavile ni suala la muungano, wakiyachimba wao sisi tutapata asilimia 4.5 tu. Zilizobaki zote wachukue wao.

Basi hiyo ndiyo sababu mnapigwa. Hiyo ndiyo Bwana Mkubwa (Mkapa) anashikilia lazima mtu wake (Karume) apite ili amalize kazi.
 
"Kuanzia kaskazini mwa Kenya mpaka kusini ya Tanganyika" Hapa sijaelewa maana nijuavyo ni kuwa; Kaskazini mwa kenya ni Sudan na Ethiopia, Kusini mwa Tanganyika ni Msumbiji
 
"Kuanzia kaskazini mwa Kenya mpaka kusini ya Tanganyika" Hapa sijaelewa maana nijuavyo ni kuwa; Kaskazini mwa kenya ni Sudan na Ethiopia, Kusini mwa Tanganyika ni Msumbiji

Ana maana kaskazini mwa kenya upande wa bahari ilikuwa zanzibar lakini baada ya mkutano wa Berlin 1885 walinyanganywa wkabaki na maili 10 tu. ni hii ndiyo mipaka mipya tunayoitumia, hata Malawi wanang'ang'ania ziwa kupitia mipaka hii.
 
Tumia akili sio kila kitu unameza tu, jiulize Tanganyika wakati inapata uhuru mipaka yake ilikuwa ipi, na Zanzibar wakati inapindua Sultani mipaka yake ilikuwa wapi. kama huwezi kujibu hayo tafuta katiba ya Tanzania na uone mipaka ilivyo. Sio story zenu za kijinga vijiweni huko mnaleta JF.
 
Tumia akili sio kila kitu unameza tu, jiulize Tanganyika wakati inapata uhuru mipaka yake ilikuwa ipi, na Zanzibar wakati inapindua Sultani mipaka yake ilikuwa wapi. kama huwezi kujibu hayo tafuta katiba ya Tanzania na uone mipaka ilivyo. Sio story zenu za kijinga vijiweni huko mnaleta JF.


weka hqpq katiba ya Tanganyika achana na ya Tanzania. utapata jibu.
 
Tumia akili sio kila kitu unameza tu, jiulize Tanganyika wakati inapata uhuru mipaka yake ilikuwa ipi, na Zanzibar wakati inapindua Sultani mipaka yake ilikuwa wapi. kama huwezi kujibu hayo tafuta katiba ya Tanzania na uone mipaka ilivyo. Sio story zenu za kijinga vijiweni huko mnaleta JF.

Majuha wamekua wengi mno kutokana na elimu mbovu wanayo soma watoto na vijana wetu! Na watakurupuka wengi kucomment kijuha juha kama mleta uzi alivyo.
 
Nchi hii ni moja jamani, na tunapakana na nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Kongo, Zambia, Malawi, Msumbiji n.k. Zanzibar na Tanzania bara ni nchi moja na sisi wote ni wamoja.
 
Majuha wamekua wengi mno kutokana na elimu mbovu wanayo soma watoto na vijana wetu! Na watakurupuka wengi kucomment kijuha juha kama mleta uzi alivyo.

wewe uliye mwelevu na usiye juha si ulete hoja hapa mezani tujadiri badala ya kuzungumza kijumla jumla tu? leta utetezi hapa. Nashangaa hata hoja ya kuwa Zanzibar ni Oman hujajibu kwaani tumesoma kuwa Zanzibar alikuwepo mkoloni mwarabu muda mrefu sana, lkn seif anadai mkoloni alianza kufika zanzibar 1885, je na hili ni ujuha?
 
Nchi hii ni moja jamani, na tunapakana na nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Kongo, Zambia, Malawi, Msumbiji n.k. Zanzibar na Tanzania bara ni nchi moja na sisi wote ni wamoja.


Nakubaliana na wewe kuwa nchi hii ni moja ndani ya Muungano lkn nje ya Muungano kuna nchi mbili zenye mipaka (territories)
 
Ana maana kaskazini mwa kenya upande wa bahari ilikuwa zanzibar lakini baada ya mkutano wa Berlin 1885 walinyanganywa wkabaki na maili 10 tu. ni hii ndiyo mipaka mipya tunayoitumia, hata Malawi wanang'ang'ania ziwa kupitia mipaka hii.


Thanks got u
 
hoja hapo ni kuvunja muungano, idadi ya maili chache siioni kwa sababu Zanzibar yenyewe ina idadi ya watu wachache hata milioni mbili sidhani ka wanafika.

wakati mwingine idadi ya watu huenda sambamba na ukubwa wa eneo.
 
Mimi sioni tatizo hata kama zingekuwa chini ya maili 10. Kuna nchi inaitwa LESOTHO iko katikati ya Afrika ya kusini kama ilivyo Dodoma kwa Tanzania lakini ni nchi huru na inayotambuliwa kimataifa haina hata hizo maili 10 pande zote. Mbona Marekani ni nchi tajiri duniani lakini haina madini na migodi mingi kama Tanganyika? Tanganyika inaweza kuwa na kilometa nyingi za maji ya bahari na maziwa lakini ikawa masikini kuliko Zanzibar. Hata sasa angalia Tanganyika ina mito, mabwawa, maziwa bahari na vyanzo vingi vya maji lakini wananchi wake wanashida kubwa ya maji na umeme kuliko hata nchi zilizopo jangwani kama Libya na nchi nyingine za kiarabu. Ukubwa wa kichwa sio wingi wa akili mkuu. Unaweza kukuta ndani kimejaa matope tu kama baadhi ya ving'ang'anizi wanaoendesha bunge la katiba!
 
hoja hapo ni kuvunja muungano, idadi ya maili chache siioni kwa sababu Zanzibar yenyewe ina idadi ya watu wachache hata milioni mbili sidhani ka wanafika.

wakati mwingine idadi ya watu huenda sambamba na ukubwa wa eneo.
Canada Vs Nigeria
 
wewe uliye mwelevu na usiye juha si ulete hoja hapa mezani tujadiri badala ya kuzungumza kijumla jumla tu? leta utetezi hapa. Nashangaa hata hoja ya kuwa Zanzibar ni Oman hujajibu kwaani tumesoma kuwa Zanzibar alikuwepo mkoloni mwarabu muda mrefu sana, lkn seif anadai mkoloni alianza kufika zanzibar 1885, je na hili ni ujuha?

Hapa wote mmesahau au hamuijui vizuri historia ya Zanzibar.
Zanzibar ilianza kutawaliwa na wakoloni kabla ya hiyo 1885.
Iran&Other Arabs waliitawala Zanzibar toka BC hadi AD. Walitawala hadi mwaka 1504. Baada ya hapo waliitawala Wareno (Portuguese Empire) hadi 1668 Alipochukua Sultani wa Oman na kufanya Makao Makuu ya Oman (Stone Town). Huyu alitawala hadi Tanganyika.
Mwaka 1885 wakoloni wakarudi na kugawa bara la Afrika nakuiweka hii mipaka yao.
Mwaka 1890 Sultani alinyang'anya mamlaka kamili na Uingereza ila wakamweka kama kibaraka wao.
Mwaka 1963, British wakampa tena Uhuru Sultan kuitawala Zanzibar, lakini alipinduliwa mara tu British walipo ondoka Zanzibar.
Kwa hiyo historia ya Zanzibar haianzii 1885 bali toka zama za kale. Wakoloni (Waarabu na Wazungu) waliipenda Zanzibar kwa sababu ilikuwa kitovu cha biashara zao na ni rahisi kujilinda.
Wazanzibari ni mchanganyiko wa Waarabu, Wareno na Wabantu.
 
Wanajamii hii nimeipata sehemu kwenye mtandao hapo chini, inaonyesha mipaka ya Zanzibar kabla ya Muungano ni maili 10 tu kutoka nchi kavu, je sehemu iliyobaki ni ya Tanganyika au Madascar au Kenya? soma kidogo baadhi ya hotuba ya maalimu seif ya Kiabanda maiti akithibitisha hilo.
Mkuu Mshino, asante kulizungumzia hili!, wakoloni walipokutana Berlin mwaka 1884 kugawana bara la Afrika miongoni mwao, baadhi ya tawala za kifalme za Kiafrika zenye nguvu ikiwemo Zanzibar, Uganda, Ethiopia na Afrika ya Kati, hazikutawaliwa, bali ziligawiwa maeneo, wakati huo Zanzibar ikiwa ni dola lenye nguvu lenye hadi sarafu yake. Zanzibar ilinyanganywa aneo lake na kubakishiwa eneo lote la visiwa vya bahari ya Hindi na ukanda wa pwani wa kilomota 10 kuingia huku bara, inamaa miji ya Dar, Bagamoyo, Kilwa, na pwani yote ilikuwa mali ya Zanzibar.

Mkataba ule ndio uliweka mipaka yakatikati ya maji kwenye miziwa makuu!. Tanzania ilipewa Ujerumani, Kenya ilipewa Uingereza Rwanda na Burudi, Ubelgiji, Msumbiji na Angalo, Ureno etc!.

Baada ya vita kuu ya kwanza kwa Ujerumani kushindwa, ikapokwa makoloni yake yote, hivyo Tanzania kugaiwa kwa Uingereza sio kama koloni, bali Protectorate na ili kuvilinda visiwa vya Zanzibar, pia Zanzibar nayo ikapewa ulinzi, kile kipande cha ukanda wa maili 10 za pwani ya Tanganyika kikarudishwa Tanganyika, Kamuzu Banda akapewa zawadi nchi ya Nyasaland pamoja na kumpa ziwa lote la Nyasa!.

Hivyo sasa hiyo 10 mile costal strip ni mali yetu!.

Ila pia hakuna kumbukumbu zozote zinanozoonyesha Mwarabu alipokuja Zanzibar aliingia mkataba wowote na wazawa ili awatawale!. Hivyo huyo Mwarabu naye ni mvamizi tuu wa visiwa vile, vilikuwa ni sehemu ya Tanganyika kabla ya kumegeka na kuchukuliwa na maji, ndio maana mimi nasisitiza tuwe nchi moja, chini ya na serikali moja, rais mmoja na taifa moja!, Huyo Mwarabu mvamizi kama hataki, afungashe virago vyake, yeye na vizalia vyake arudi kwao Oman!.

Thanks.

Pasco
 
Wanajamii hii nimeipata sehemu kwenye mtandao hapo chini, inaonyesha mipaka ya Zanzibar kabla ya Muungano ni maili 10 tu kutoka nchi kavu, je sehemu iliyobaki ni ya Tanganyika au Madascar au Kenya? soma kidogo baadhi ya hotuba ya maalimu seif ya Kiabanda maiti akithibitisha hilo.

…………………….. Katika miaka ya 1880 na 1885, Wakoloni walianza kuingia sehemu hizi... Wakaamua kugawana Afrika. Katika mkutano uliofanyika Berlin 1885 wakamnyang'anya mtawala wa Zanzibar (Sultan Hamad bin Thuwaini) sehemu yote ya Afrika. Zanzibar wakaachiwa visiwa pamoja na Mwambao wa maili kumi kwenda ndani. Kuanzia kaskazini mwa Kenya mpaka kusini ya Tanganyika. Ilikuwa yote hayo ni mamlaka ya Zanzibar. Wajerumani wakaamua kuununua ule mwambao wa maili kumi wa Tanganyika. Kenya Wajerumani hawakuinunua, mwambao wa Kenya ulibaki sehemu ya Zanzibar, Lamu ilikuwa sehemu ya Zanzibar mpaka mwaka 1963, Kenya ilipopata Uhuru wakakubaliana waache. Tukabaki na Unguja na Pemba kama nchi.


source: http://www.islamtanzania.org

Pia nimegundua kuwa kumbe Wanzazibar wanajua ukoloni ulianza 1885 baada ya mzungu kufika, kumbe Mwarabu alikuwa mwenzao japo alikuwa aliwauza kama wanyama. nafikiri hata maalimu Seif wakati anatoa hiyo hotuba alijisahau kwa kujifanisha na na mwarabu, angalia sentensi ya kwanza hapo juu" Katika miaka ya 1880 na 1885, Wakoloni walianza kuingia sehemu hizi...

Wakaamua kugawana Afrika. Katika mkutano uliofanyika Berlin 1885 wakamnyang'anya mtawala wa Zanzibar (
Sultan Hamad bin Thuwaini)............................................
Je Zanzibar ni warabu?

====================================

Maalimu ni alishababu
 
Back
Top Bottom