Kufanikiwa sio Kujidanganya

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,340
51,901
UKITAKA KUFANIKIWA "USIJIDANGANYE"

Na, Robert Heriel

Yapo mafanikio ya aina nyingi na ya nyanja tofauti tofauti. Wapo waliofanikiwa kupata elimu kubwa kuanzia shahada mpaka Phd. Wapo waliofanikiwa kuwa matajiri, wapo waliofanikiwa kuwa watu mashahuri, wapo waliofanikiwa kuwa viongozi wakubwa wa nchi na dunia, wapo waliofanikiwa katika fani zao kitaaluma, wapo waliofanikiwa kimuziki ni wanamuziki wakubwa, wapo waliofanikiwa kuwa wachezaji wakubwa wa mpira miongoni mwa mafanikio mengine.

Watu wote wenye mafanikio unaowajua na usiowajua, wanafanana kwa tabia kadha wa kadhaa, moja wapo ni "KUTOKUJIDANGANYA" Mtu yeyote aliyefanikiwa hana desturi ya kujidanganya.

Kama kuna makosa ambayo watu wengi hasa waliomasikini wanayafanya basi moja wapo ni kosa la kujidanganya. Watu wengi kama sio wote wanapata shurba za maisha, waliofeli kwenye jambo lolote lile, iwe ni kielimu, kimali, kidini, kimichezo, kisiasa, kijamii, kivita, n.k wote waliojidanganya waliangukia pua.

Ni vigumu sana kwa mtu kujidanganya, hivyo mpaka mtu ajidanganye basi lazima apitie michakato mbalimbali na afanye maamuzi magumu ya kutoitumia akili yake vizuri. Jambo lolote ambalo halipatani na akili yako lakini unalilazimisha liingia akili kwa lazima huko kunaitwa kujidanganya.

DALILI ZA MTU ANAYEJIDANGANYA NI KAMA IFUATAVYO;

1. KUCHUKULIA MAMBO KIRAHISI.
Watu wote wanaojidanganya hupenda kuchukulia mambo rahisi rahisi. Hii huwafanya kupuuzia mambo na kuwa na dharau. Mtu yeyote mpuuzi na mwenye dharau anatabia ya kujidanganya. Kitendo cha kuchukulia mambo kirahisi kunamfanya akose maandalizi ya kutosha.

Hii ni tofauti na Mtu asiyejidanganya, ambaye yeye hachukulii mambo kirahisi, mara zote huona kila jambo linaugumu wake, na hata kama jambo ni rahisi kwake kwa namna gani yeye huuona huo urahisi ndio ugumu wenyewe. Tabii hii humfanya mtu kujiandaa vya kutosha, bila kupuuzi jambo lolote lile, hii huwafanya watu wa namna hii kufanikiwa katika mambo wayafanyayo.

Waimbaji wakubwa wote unaowajua duniani waliofanikiwa, ni watu wasiochukulia mambo kirahisi, Hata huyu Diamond platnum hapa bongo ni moja ya wasanii wanaofanya mazoezi ya kutosha. Muangalie Bondia Hasan Mwakinyo, Hata Marehemu Michael Jackson alikuwa mtu wa maandalizi, yeye kila siku ni kujiandaa. Muangalie Christian Ronaldo, Muangalia Mayweather, hawa watu hawachukulii mambo kirahisi na ndio maana muda mwingi huutumia kujiandaa katika fani zao.

Lakini wale wenzangu na miye, utakuta anajisifu anajua kuimba, anajua kupigana, anaakili darasani, au anapesa lakini yanapotokea mashindano anapigwa vibaya mno kutokana na kuwa hafanyi mazoezi, anachukulia mambo kirahisi. Anajidanganya. Hata waliofeli shule kidato cha nne wengi wao hujidanganya kwa matokeo ya mitihani ya ndani, sasa NECTA inapokuja wao hufukiria kirahisi rahisi tuu, wengi walifeli.

2. HUJIWEKA KWENYE WINGI BADALA YA UMOJA.
Watu wanaojidanganya huwa na tabia ya kujiweka kwenye wingi. Hupenda kujifariji kwa kutumia wingi badala ya umoja. Huathiriwa na makundi ya watu wengine. Hujisifu na makundi ya watu wengine, hivyo naye hujiweka katika kundi hilo.
Kwa mfano,
Mtu huweza kusema kuwa kwao wanapesa wakati yeye hana.
Mtu huweza kusema kabila lao wamesoma wakati yeye hajasoma.
Mtu huweza kusema kabila lao ni wazuri au warefu wakati yeye sio mrefu au mzuri.
Mtu huweza kusema Mjomba wake ni kiongozi mkubwa wakati Baba yake au yeye mwenyewe hana lolote.

Watu wa namna hii hupenda kujipa ujiko kwa sifa za watu wengine. Wengi huishia kujisifia vitu visivyo vyao wao wakiishia kuwa masikini.
Pia watu hawa hujiweza kukutisha na kupata madhara kwa kujidanganya kwao.
Kwa mfano.
Mtu anaweza akakuchokoza alafu akakutisha kuwa yeye anawashikaji wahuni kibao. Yaani anakutishia kwa mgongo wa vikundi mshenzi vya kihuni. Wengi hupasuka, huchapika na kujikuta hakuna aliyemteta.
Pia wanafunzi wanaoandamana, wengi huandamana kwa kujua wapo wengi lakini matokeo yake wanaoathirika ni wachache hasa wale viongozi.

Hii ni tofauti na watu wasiojidanganya ambao wao hawajiweki kwenye wingi bali kwenye kundi la Umoja. Hupenda kutumia nafasi ya kwanza umoja wakijisemea wao wenyewe.
Hawa hawajisifii kwa mali za ndugu wakati yeye ni choka mbaya
Hawa hawajisifii kwa mafanikio ya kabila lao wakati yeye hajasoma
Wao hawachokozi watu kisa wanategemea kikundi mshenzi cha kihuni. Akikuchokoza ujue mtamallizana na yeye na wala hatamshirikisha mtu.

Wengi waliofanikiwa hutafuta mali zao wenyewe bila kutegemea msaada wa ndugu. Wakati wanaojidanganya hutegemea cha nduguye mwishoe huishia kuwa fukara.

3. HUPENDA KUJIKWEZA.
Watu wanajidanya hupenza kujikweza sana. Kuanzia kwenye maneno. uvaaji, chakula miongoni mwa mambo mengine. Wengi huwa na ile falsafa isemayo "Umaridadi wa mavazi huficha umasikini" Hivyo wengi huhakikisha wanavaa vizuri na kupendeza ili kuwadanganya watu kuwa wao mambo safi, pia hujidanganya kuwa wao ni mambo safi lakini mwishowe huangukia pua.
Kujikweza ni tabia ya kupenda kuheshimika kwa lazima, hali inayopeleka mtu kujitukuza, kujionyesha anacho hata kama hana.
Mtu yeyote anayependa kuheshimiwa kwa lazima huyo anajidanganya, huwezi ukajidanganya unaheshimiwa kwa kujikweza nawe ukaona unaheshimika.
Watu wa namna hii huvaa nguo zisizoendana na vipato vyao. Hutumia simu za gharama zisizoendana na vipato vyao, hupanga nyumba zisizoendana na kipato chao. Unajua nini kitatokea? Njia ya mwongo ni fupi, hawezi kudumu hivyo kwa miaka kumi lazima apasue matairi. Mara nyingi umri ukifika miaka 40+ ndipo mtu hujua kuwa alikuwa akijidanganya na wala sio kuwa alikuwa akidanganya watu.

Hii ni tofauti na watu wasiojidanganya, wao hawajikwezi, wapo tuli wanafanya mambo yao. Umuheshimu usimuheshimu utajua mwenyewe hilo halimuhusu. Watu wa namna hii hawanaga mbwembwe nyingi labda awe kwenye fani inayohitaji mbwembwe kama U-MC, uchekeshaji, Muziki wa kisasa n.k
Watu wasiojidanganya huvaa kulingana na kipato chake, sio kwa lengo la kutafuta heshima au sifa bali kujisitiri kulingana na hali yake ya kipesa.
Hupanga nyumba kulingana na uchumi wake.
Hutumia usafiri au simu kulingana na uchumi wake.
Watu wa Hivi mara nyingi hutoboa mapema sana, kwani anaishi kulingana na hali yake.

4. WENGI HUMTEGEMEA MUNGU/SHETANI
Watu wanaojidanganya wengi humtegemea Mungu kama sio shetani. Wao kila kitu wanadhani Mungu ndiye amepanga, Huamini kuwa umasikini wao unatokana na Mungu kuwa ndio kawapangia. Wengi humuomba Mungu zaidi kuliko kufanya kazi, na hata akifanya kazi basi hafanyi kwa maarifa ya kufanikiwa. Wengi hutumia falsafa kama " Riziki mafungu saba" "Ipo siku yangu" Kesho yangu itakuwa bora" Masikini ataenda mbinguni" n.k. Tabia hii imewafanya kubweteka, kutojishughulisha, kutofanya kazi kwa bidiii, kutoweka akiba au kuwekeza kwani wanadhana kuwa kama Mungu/shetani hajapanga hata ufanyeje huwezi fanikiwa. Watu hawa hulaumu wengine, pia humlamu Mungu au shetani kuwa ndiye chanzo cha umasikini wao. Wengine husema wamelogwa. Kumbuka wao hutumia falsafa ya nafsi ya wingi, na wala sio umoja. Wengi husema; "Kuna Baba yangu asiyeshindwa kamwe" Mtetezi wangu Yu hai" lakini mpaka wanazeeka hawana la maana kwani hawajui kuwa kufanikiwa sio kujidanganya. Jukumu la maisha ya mtu lipo mikononi mwake mwenyewe.

Hii ni tofauti na watu wasiojidanganya ambao huamini kuwa Maisha yao yanategemea jitihada zao wenyewe. Watu wote waliofanikiwa hawaamini kuwa Mungu/shetani ndio kawapa mafanikio hayo. Wengi wanaamini ni mipango, mikakati, uthubutu, utekelezaji, mtandao mzuri wa watu, mazingira rafiki ndivyo vilivyowafanya wafanikiwe. Wengi huamini kuwa Mungu/shetani alichosaidia ni 10%.
Tabia hii inawafanya watu wa namna hii kufanya kazi kwa bidii, kuweka akiba, kujishuhulisha, kuunda kila siku mtandao mzuri wa watu wenye pesa,
Watu wa namna hii wakifeli huwa hawamuhusishi yeyote yule, wanajilaumu wao wenyewe, Kumbuka wao hutumia falsafa ya nafsi ya umoja na wala sio wingi.


5. KILA SIKU NA IJUMAA(siku zinafanana)
Watu wanaojidanganya wanatabia nyingine ya kuona kuwa kila siku ni ijumaa. Wapo hufikiri kuwa siku zote ni sawa. Hata wakipata leo atakula kila kitu asiache akliba au kuwekeza. Wanafikiri kwa vile kapata leo basi na kesho atapata. Au kwa vile kakosa leo basi kesho anamuachia Mungu.
Huko ni kujidanganya,

Wakati wasiojidanganya wao wanajua siku huwa tofauti hivyo ni jukumu lao kuzifanya zifanane vile watakavyo. Kama leo alikuwa na furaha basi atahakikisha kesho inakuwa kama leo. Ndio maana watu wa namna hii huwa na nidhamu kubwa kwenye matumizi, huweka akiba, huwekeza, kwa kuihofia kesho wasioijua. Ili kesho ikaja na mambo yake basi mtu hutumia akiba kuikabili hiyo kesho.

6. KUTEGEMEA WATU.
Watu wanaojidanganya wanatabia ya kutegemea sana watu. Hutegemea ndugu, Baba, kaka, mjomba n.k. Wao wanaamini kuwa mtu fulani yupo kwa ajili ya maisha yake. Hawa usishangae akakaa tuu alafu anategemea kakaake, au Baba yake amtafutie kazi, au ampe pesa ya kujikimu mahitaji yake. Watu hawa hupenda kupiga vizinga kwa ndugu zao kama vile kaka, baba, wamama wadogo, na ole wako usimpe hela ndio utamfahamu vizuri. Wengi hutoa lawama, laana na maneno ya shombo kwa watu wasiowasapoti.
Watu wa namna hii hupenda kung'ang'ania urithi ikiwezekana huweza kuua kabisa.
Wengi huweza kwenda kwa waganga ilimradi tuu amuweke kiganjani mtu mwenye pesa ili apewe yeye.
Hili pia lipo kwa baadhi ya wazazi, unakuta mzazi hajahangaika kwenye malezi, wengine ni wababa wametelekeza watoto lakini siku ya siku wengi huwapiga virungu watoto na kuwatishia maisha kama sio kuwalaani kabisa.

Hii ni tofauti na watu wasiojidanganya, wao falsafa yao ni maisha yao yapo juu yao wenyewe. Hakuna aliyepo kwa ajili ya maisha yao. Wao hutafuta uhuru wa maisha yao kwa kumiliki mali zao wenyewe. Wengi hawategemei msaada wa ndugu, mwanzoni ndio hutaka msaada lakini wasipopewa msaada huachana na ndugu na kuanza kuhangaika wao kama wao.
Watu wa namna hii hawapigi virungu, hawapigi vizinga watu. Wala hawatoi lawama kwa ndugu zao endapo hawatasaidiwa. Bali huona maisha yao ni jukumu lao kuyafanya kuwa mazuri.
Hawamtegemei mtu bali wanaamini kwa nguvu zao wenyewe.

WITO: Watu wasijadanganye, watu wajiambie ukweli tuu.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
 
Dalili zote ulizoandika kuanzia namba 1 hadi hiyo 6 sifa zote anazo rais wa zamani wa Dar ndugu Bashite
 
Back
Top Bottom