Kwa muda mrefu sasa wazo la kuasili mtoto limekuwa likinivutia sana.
Limekuwa likinivutia hadi kunifanya nilifanye kuwa ndo moja ya baadhi ya azma zangu maishani.
Kwamba, ipo siku ambayo si mbali sana kutoka sasa ambapo nitauanza huo mchakato wa kuitimiza hiyo azma.
Msukumo wangu kwenye hili unatokana na ukweli kwamba mimi napenda sana watoto. Na kwa mtaji huo huwa sipendi kabisa kuona watoto wakiteseka kwa namna yoyote ile au kukosa fursa ya kuishi maisha mazuri yenye furaha tele.
Ni ada kwangu kabla sijafanya maamuzi yenye athari ya/za kuweza kudumu kwa muda mrefu, kutulia na kwenda taratibu huku nikitafakari kwa kina yaliyo chanya na hasi, changamoto zilizopo na ambazo zaweza kujitokeza mbeleni na kama naweza kukabiliana nazo bila kuyumba, na kadhalika.
Kwa ufupi, huwa napenda kufanya tathmini kamilifu halafu ndiyo naamua la kufanya.
Sasa hili la wazo la kuasili mtoto nimekuwa nalo kwa muda mrefu. Nimelijadili sana na watu wa kada mbalimbali. Na kusema ukweli majadiliano mengi yamekuwa ni ya chanya na kutia moyo.
Kwa manufaa ya uwazi kuhusu hali yangu ya kindoa, mimi ni kapera. Hali hii ndo moja ya sababu inazonifanya nikawie kufanya kweli.
Manake huwa nafikiria, unapomleta mtoto mdogo kuwa chini ya himaya yako na kumlea pasipo na mlezi wa kike, sijui hayo malezi yanaweza kuja kuathiri vipi makuzi yake. Hilo ndo moja ya changamoto za mbeleni nilizozigusia hapo juu.
Lakini ima fa ima, ipo siku tu nitafanya kweli. Nisipofanya kweli nitajiona kuna kitu kimepungua katika uwepo wa uhai wangu hapa duniani. Na sitaki kuwa na hiyo hali maana itanisumbua kwa kiasi chake. Huwa sipendi kushindwa kutimiza malengo yangu niliyojiwekea.
Sasa basi, kwa vile JF-MMU ni jamvi la wengi na kama wahenga walivyonena, penye wengi pana mengi. Hayo mengi ni pamoja na tajiriba mbalimbali na tofauti za kimaisha.
Na hiyo ndo sababu mahsusi ya mimi kuamua kuuleta huu mjadala hapa. Inawezekana mpo ambao mmeshawahi kuasili watoto. Kama mpo basi naomba mtupe mliyokutana nayo na mnayokumbana nayo.
Au pia huenda kukawepo na watu ambao mliasiliwa. Kama mpo na nyie fungukeni mtupe mliyoyapitia na mnayoendelea kuyapitia.
Hata kama haupo kwenye hayo makundi mawili lakini una mawaidha au mausia mawili matatu ambayo unaweza kuchangia, nasema ahlan wa sahlan.
Ni mimi wenu mtiifu,
Nyani Ngabu bin Kibadiru.