Hashpower7113
JF-Expert Member
- Sep 26, 2011
- 1,353
- 2,144
Hebu vuta picha, umetembelea mahali ambapo hujawahi kufika lakini unagundua kwamba kuna kitu cha ajabu, unatazama kushoto unamuona mtu mmoja lakini ukigeuka upande mwingine, unamuona mtu mwingine lakini amefanana kwa kila kitu na yule uliyemuona upande wa pili, unagundua kwamba ni mapacha.
Unatazama mbele unamuona mwingine lakini unapogeuka upande mwingine, unamuona mwingine aliyefanana sana na yule uliyemuona ulipogeuka nyuma, mapacha wengine. Unaendelea na ‘hamsini’ zako, lakini mita chache mbele unakutana na hali kama ileile, watu wawiliwawili wamefanana kwa kila kitu!
Kadiri unavyozidi kusonga mbele unazidi kukutana na mapacha wengine, wengi zaidi na wamefanana kwa kila kitu, wawiliwawili! Unaweza kudhani umechanganyikiwa si ndiyo? Basi kwa taarifa yako, hali kama hiyo unaweza kukutana nayo utakapoenda kwenye Kijiji cha Kodinhi, Wilaya ya Kerala nchini India.
Kwa makadirio, katika kijiji hicho kuna jozi zaidi ya 400 za mapacha katika familia 2000 tu zinazoishi kwenye kijiji hicho na idadi hiyo inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mujibu wa utafiti, mwaka 2008, kijiji hicho kilikuwa najozi za mapacha 280 na idadi imezidi kuongezeka siku hadi siku.
Taarifa za mamlaka za afya, zinaonesha kwamba katika kila watoto 1000 wanaozaliwa, 45 ni mapacha.
Oktoba 2016, timu ya wataalamu kutoka taasisi mbalimbali, ikiwemo Chuo Kikuu cha Kerala, Chuo Kikuu cha London na wengine kutoka Ujerumani, walianza kufanya utafiti kutaka kujua ni kwa nini watoto mapacha wanazaliwa kwa wingi zaidi katika kijiji hicho kuliko sehemu nyingine yoyote duniani.
Japokuwa majibu ya kitaalamu bado hayajatoka, wapo wanaohusisha kiwango hicho cha uzazi wa watoto mapacha na madini fulani yanayopatikana kwenye maji na hewa ya kijiji hicho, kwamba huenda ndiyo yanayosababisha kuzaliwa kwa watoto mapacha kwa wingi.
Hoja hiyo inapewa uzito kutokana na ushahidi mwingine kwamba wanawake ambao wamekulia kijijini hapo, hata wanapoolewa na kwenda kuishi sehemu tofauti kabisa, wengi wao hujifungua mapacha, hali inayoonesha kwamba huenda kuna madini ambayo walikuwa wakiyapata tangu wakiwa wadogo ndiyo yanayosababisha hali hiyo.
Unapoingia kwenye kijiji hicho, kuna bango kubwa linalosomeka Karibu Kwenye Kijiji cha Mungu cha Mapacha, Kodinhi. Maelfu ya watalii wamekuwa wakifunga safari kila mwaka kwenda kwenye kijiji hicho kuwashangaa mapacha hao, wakubwa kwa wadogo.
Sameera na Femeena ni miongoni mwa mapacha waliozaliwa kijijini hapo ambapo katika mahojiano maalum na shirika moja la utangazaji, wanaeleza kwamba wakiwa shuleni, darasa lao lilikuwa na jozi nane za mapacha, achilia mbali madarasa mengine ambapo kwa wastani, kila shule inakuwa na jozi 24 za mapacha.
Kitu kingine kinachozidi kuumiza vichwa vya wanasayansi wengi, ni kwamba mapacha karibu wote wanaozaliwa katika kijiji hicho, wanakuwa ni wale wanaofanana kwa kila kitu (identical twins), yaani kama ni wa jinsia ya kiume, wote wanakuwa hivyohivyo na wanafanana kwa kila kitu na kama ni wa jinsia ya kike, vivyo hivyo.
Hayo ndiyo maajabu ya Kijiji cha Kodinhi, Kijiji cha Mungu cha Mapacha.
Hashpower7113