Kiwango cha ugonjwa wa Malaria chapungua kwa zaidi ya asilimia 50 ndani ya miaka miwili

Suley2019

JF-Expert Member
Oct 7, 2019
1,815
4,563
1576849284816.png

Kiwango cha ugonjwa wa Malaria nchini, kimepungua zaidi ya asilimia 50 ndani ya miaka miwili kutoka asilimia 14 hadi kufi kia asilimia 7.3. Pia, vifo vitokanavyo na ugonjwa huo, vimepungua kwa asilimia 75.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Leonard Subi wakati wa kikao kazi cha kanda. Kikao hicho cha waganga wakuu wa mikoa, wilaya, wafamasia na waratibu wa malaria kutoka kanda, kilijumuisha mikoa ya Dodoma, Singida, Njombe, Iringa na Morogoro.

Alisema hatua hiyo imefikiwa kutokana na utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP).

“Tumedhamiria kuitokomeza na kuondoa malaria Tanzania na mafanikio yameanza kuonekana, kwa kipindi cha miaka kumi sasa kwani mwaka 2010 kiwango cha malaria kilikuwa asilimia 18, lakini ndani ya miaka miwili ugonjwa huo umepungua kutoka asilimia 14 mwaka 2015 hadi sasa tunaongelea asilimia 7.3 mwaka 2017” alisema.

Dk Subi alisema kuwa vifo vitokanavyo na malaria navyo vimepungua kwa zaidi ya asilimia 75 kwa kipindi cha miaka 10. Watu wanaougua na maambukizi mapya ya ugonjwa huo, nao wamepungua kwa zaidi ya asilimia 67.

“Katika nchi 10 za Afrika, Tanzania bado tunatajwa kuwa ni miongoni mwa nchi zenye kiwango kikubwa chenye malaria, lakini ila bado tunayo fursa ya kuiondosha malaria hapa nchini” alisema.

Dk Subi alisema kuwa kama nchi, hivi sasa wanataka kuwa na mpango endelevu wa kuondoa malaria ambao utasaidia kuondoa malaria kuanzia viluwiluwi na mbu wapevu.

“ Hawa mbu tukipambana kuwaondosha tutaweza kuiondoa malaria nchini kwani tunayo fursa kwa kutumia Kiwanda chetu cha Kibaha ambacho kinazalisha viuadudu, hivyo tutaendelea kununua pia kusambaza viadudu kwenye ngazi za halmashauri na kutumia njia ya jamii kwa kila mtaa na vijiji” alisema.

Aidha, Dk Subi alisema kupitia mpango huo, kila mtanzania atakayeenda kwenye kituo cha kutoa huduma za afya akipimwa na kugundulika na malaria kupata tiba atafuatiliwa “Tunataka kila atakayeenda kituo chetu cha huduma ya afya apimwe, apate tiba sahii na baada ya tiba afuatiliwe maana watu wengi tukiwapatia dozi hakuna anayejua kama mtu huyo kiwango cha malaria kimeisha na anaendelea vizuri ili watu katika familia yake wasiambukizwe” alisema.

Aidha, Dk Subi aliitaka mikoa kutenga fedha kwa ajili ya udhibiti wa wadudu waharibifu na kuzingatia miongozo ya wizara katika kudhibiti ugonjwa wa malaria nchini, kwani lengo lililoweka ifikapo mwaka 2020 ni kufikia angalau kuwa na asilimia moja ya ugonjwa huo.


Chanzo: Habari Leo
 
Back
Top Bottom