Taarifa nilizonazo ni kwamba sababu za wananchi hao kutoka kijiji cha ITUNUNU umbali kama km 5-6 toka Mugumu mjini walifikia hatua hiyo baada ya kuona jeshi la polisi linaendelea kuhujumu jitihada zao za kukabiliana na uhalifu kijijini kwao na wilayani kwa ujumla. Kumekuwa na tabia ya polisi kuwaachia wahalifu pasipo kuwafikisha mahakamani ili wakakabiliane na tuhuma zinazowahusu, mara nyingi polisi wamegeuka kuwa ndio mahakimu na kumalizia kesi zote kituo cha polisi mugumu wakati matukio ya wizi, majeruhi na mauaji yakiendelea kila mara.
Katika tukio la jana kulitokea wizi kijijini ITUNUNU na katika tukio hilo watu wawili wakauawawa na hao wezi, na kama kawaida polisi walitaarifiwa na kwakuwa kuna watu waliokuwa wanahisiwa kwamba ndio wezi wakakamatwa. Kwa upande wa pili wananchi hao walijitokeza kwa wingi kufuatilia ng'ombe waliokuwa wameibiwa na kufanikiwa kuwakamata.Sasa wakati wanarudi nyumbani ndo wakapata taarifa kwamba wezi na wauaji wamekamatwa wako kituo cha polisi mugumu, ndipo wakaamua kupita hapo ili kuja kinachojiri na kutokana na kuchoshwa na vitendo vya uhalifu vinavyojirudia rudia kila mara na pasipo polisi kuchukua hatua zinazostahili ndipo baadhi yao wakataka wakabidhiwe watuhumiwa hao wa wizi na mauaji ili wawashughulikie wenyewe kwa kuwa polisi imeshindwa kufanya kazi yake ipasavyo.
Polisi kuona hivyo, ghafla tu bila hata kutoa tahadhari wakaanza kupiga risasi za moto bila mpangilio hali ikiyopelekea watu wengi kujeruhiwa na kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa rasmi kwamba kuna watu watatu wamefariki katika mtafaruku huo. Kibaya zaidi polisi walianza kuzunguka mji mzima na kupiga watu hovyo hata wasiojua kinachoendelea ambao hawakuwepo eneo la kituo cha polisi. Watu walikuwa kwenye shughuli zao, wakavamiwa huko na polisi na kuanza kupigwa; kuanzia sokoni, stendi hadi mitaani kote watu walikuwa wanapigwa tu hovyohovyo, hii hali ni ngumu kuieleza lakini kwa hali iliyopo mugumu, wananchi hawana imani kabisa na jeshi la polisi.
Kwa jinsi hali ilivyo, jeshi la polisi linatakiwa kujipanga upya, watafute mbinu mpya za kukabiliana na uhalifu na zaidi sana watafute weledi wa kushughulikia malalamiko ya wananchi, lakini kwa utaratibu huu wa sasa wa polisi kujigeuza mahakama, na kibaya zaidi kuchukua fedha toka kwa wahalifu na kushindwa kuwafikisha mahakamani kwa kisigizio cha kukosekana kwa ushahidi, hili ni jambo ambalo lazima litazamwe upya na kwa umakini wa hali ya juu, na katika hili IGP Mwema ana kazi kubwa sana ya kubadili mtazamo na utendaji wa polisi.
Kwa mtazamo wangu kwa kuangalia matukio mbalimbali yanayotokea yakihusiana na jeshi la polisi kuwaua wananchi, kuwajeruhi na kuwapiga, ni dhahiri kuwa wananchi wamepoteza na wanaendelea kupoteza imani na jeshi la polisi, kuanzia tarime, arusha, mbarali, iringa, tabora na kila kona ya nchi hii polisi wanalalamikiwa, na katika hili JESHI LA POLISI NI LAZIMA WAJIVUE GAMBA!!