Kitila: Bunge la hoja vs Bunge la kanuni | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kitila: Bunge la hoja vs Bunge la kanuni

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by sir.JAPHET, Aug 9, 2012.

 1. sir.JAPHET

  sir.JAPHET JF-Expert Member

  #1
  Aug 9, 2012
  Joined: May 18, 2012
  Messages: 700
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Na Dr. Kitila Mkumbo | Raia Mwema

  KATIKA siku za hivi karibuni majadiliano katika Bunge letu yamepata ufuasi mkubwa kutoka kwa wananchi wanaofuatilia kupitia luninga na redio. Kuna Mwalimu mwenzetu mmoja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye kwa muda sasa amekuwa akirudi nyumbani kila ifikapo saa nne asubuhi na saa kumi na moja, jioni kwenda kutazama kipindi cha Bunge. Imefika mahala anamshindwa kuacha kwenda kutazama majadiliano bungeni na anaporudi hutusimulia yaliyojiri kwa furaha na hamasa kubwa.

  Hata hivyo, katika siku za karibuni ameacha kwenda kutazama Bunge kama ilivyo kawaida yake, kwa sababu anazodai kuwa Bunge letu limegeuka kuwa Bunge la Kanuni badala ya Bunge la Hoja ! Kwamba Bunge letu limekuwa likitumia muda mwingi kulumbana juu ya matumizi ya kanuni za Bunge, badala ya kujadiliana hoja zinazohusu maisha ya wananchi na taifa kwa ujumla. Na kuna wabunge ambao wameamua kubobea katika kutoa miongozo kiasi cha kupachikwa jina la ‘Mbunge wa Mwongozo' mitaani.

  Kwa mujibu wa maoni ya wananchi yaliyochapishwa katika magazeti ya Jumapili iliyopita, ni wazi kwamba wananchi wengi wameanza kukosa hamasa na hamu ya kutazama majadiliano bungeni kama ilivyo kwa mwalimu mwenzangu niliyemtaja. Maoni ninayoyatoa katika makala haya yana lengo la kujaribu kuwakumbusha wabunge, na hasa viongozi wa Bunge, juu ya wajibu wao ili warudi katika mstari na kuwapa wananchi kile wanachokitarajia kutoka kwao.

  Katika Jumuiya ya Madola, Bunge lina kazi kubwa nne za msingi. Kazi ya kwanza ni kujadili, kutathmini na kusimamia utendaji wa serikali. Kazi ya pili ni kujadili na kupitisha sheria mbalimbali. Kazi ya tatu ni kuiwezesha serikali kupandisha kodi kupitia bajeti za kila mwaka. Kazi ya nne ni kujadili na kutoa mwelekeo juu ya jambo lolote zito lililotokea katika nchi ambalo linaweza kuchukuliwa kama dharura.

  Ukiwa mfuatiliaji wa Bunge letu utakubaliana nami kwamba Bunge letu limefanya kazi nzuri sana katika maeneo mawili, ambayo ni kupitisha sheria na kuiwezesha serikali kupandisha kodi mbalimbali kupitia bajeti za kila mwaka. Kwa maoni yangu, Bunge letu halijafanya kazi yake sawa sawa katika kujadili, kutathmini na kusimamia utendaji wa serikali. Hata lugha ambazo wabunge wetu wanazitumia bungeni ni kielelezo cha kutosha juu ya wao kupwaya katika kuelewa au kuzingatia uzito wa mamlaka yao dhidi ya serikali ambayo yapo wazi kikatiba.

  Kwa mfano, wabunge wengi wanapowasilisha maoni au mahitaji yao kuhusu jambo fulani wana tabia ya kusema kwamba ‘ninaiomba au ‘ninaishauri' serikali. Sasa hata kama mimi nilikuwa ndiye serikali ukishaniambia ‘unaomba' au ‘unanishauri' ni wazi kwamba nina hiari ya kukubali au kukataa ombi au ushauri wako. Serikali ina washauri chungu nzima ambao wameajiriwa kwa ajili hiyo wakifanya utafiti na uchambuzi kwa ajili ya kuishauri serikali kitaalamu, ambao ni muhimu zaidi kuliko ushauri wa mbunge unaotolewa katika dakika 10 anaposimama bungeni.

  Kwa sababu wabunge wetu wamekaa kiushauri zaidi kuliko kiuwajibikaji, wamefika mahala hawawezi kujadili jambo lolote zito hadi serikali ikubali kushauriwa. Na ni bahati mbaya kwamba viongozi wa Bunge wanaisikiliza serikali zaidi kuliko wanavyowasikiliza wabunge. Na serikali nao wamebuni mtindo unaowasaidia kukwepesha mijadala mizito kwa kutumia kanuni. Kwa hivyo serikali, badala ya kujiandaa kujibu hoja, inajiandaa kwa kutafuta kanuni ya kukwamisha mjadala ! Matokeo yake ni kwamba Bunge letu lipo ‘busy' kulumbana juu ya kanuni badala ya kulumbana juu ya hoja, na hatimaye upande wa serikali hushinda-kwa kukwamisha mjadala.

  Ndivyo ambavyo mijadala mizito kama ya utekwaji wa Dk. Steven Ulimboka na kuzama kwa meli ya MV Skagit ilivyozimwa. Kwa kutumia kanuni za Bunge, viongozi wa Bunge wametukosesha fursa muhimu na adimu ya kujua kilichomkumba Dk. Ulimboka na sababu hasa za matukio yanayofuatana ya kuzama kwa meli huko Zanzibar. Bunge letu limeingia katika historia isiyotukuka kwa kukubali kukatazwa kutekeleza kujadili mambo mazito katika jamii.

  Ni muhimu viongozi wa Bunge wakazingatia kwamba watazamaji na wasikilizaji wa vipindi vya Bunge hawapo kwa ajili ya kushuhudia umahiri wa kuzijua kanuni za Bunge. Wana hamu na hamasa ya kutazama na kusikiliza jinsi ambavyo wabunge wao wanaibua hoja zinazohusu maisha yao na nchi yao. Na hili ndilo lililoleta hamasa kubwa kwa wananchi kupenda mijadala ya Bunge.

  Kama viongozi wa Bunge wataendelea kuikumbatia serikali kwa kuiruhusu itumie kanuni kuzima mijadala yenye maslahi mapana kijamii, Bunge litapoteza mvuto na maana katika jamii. Na ikifika hapo Bunge letu litasuswa sio tu na watazamaji/wasikilizaji ,lakini pia hata na wabunge wenyewe kama tulivyoshuhudia hivi karibuni.

  Tunamshauri Spika wa Bunge atumie kanuni za Bunge katika kufanikisha badala ya kukwamisha mijadala ya wabunge. Tunataka Bunge la Hoja na sio Bunge la Kanuni!
   
 2. Kaa la Moto

  Kaa la Moto JF-Expert Member

  #2
  Aug 9, 2012
  Joined: Apr 24, 2008
  Messages: 7,666
  Likes Received: 164
  Trophy Points: 160
  Hata hapa umevunja kanuni ya kulisema bunge gazetini.
  Kaa chini!
  Teh teh teh teh teh eee
   
 3. Anna Mghwira

  Anna Mghwira Verified User

  #3
  Aug 9, 2012
  Joined: Mar 9, 2012
  Messages: 203
  Likes Received: 332
  Trophy Points: 80
  Nilianza kufikiri pengine bunge hili lingeweka historia ya kuifikisha Tanzania mahali pa kukataliwa na wananchi...
  Kuna ambo ya msingi yanaleta shaka kuliko matumaini, pengine kuna haja ya kupiga kura ya imani na bunge - yaweza kupunguza mapungufu tunayoyaona bungeni.

  Kuna haja ya mabadiliko kuletwa na wananchi endapo viongozi wawakilishi wataonekana kushindwa kumudu majukumu yao. Katika mfumo wa jumuiya ya madola na hasa wa Kiingereza (common law) tuliorithi sisi hatuna mabunge mawili kwa maana ya bunge la matajiri (house of lords) na bunge la watwana (house of commons) na historia zake zilizoletea mapinduzi ya miaka ya 1800, ambapo bunge la watwana lilishinda na kutoa fursa kwa wawalikishi kuwa na nguvu katika usimamizi wa serikali.

  Mijadala ya bunge letu inaonesha kuwa kuna wabugne wanotetea mfumo tu kwa hali yoyote ile, bila kujali kama kuna hoja za msingi za utetezi na hasa pia bila kujali kuwa misimamo hiyo wakati mwingine haiisaidii serikali yenyewe kujiona na kujirekebisha kama inavyotegemewa baada ya kila mjadala.

  Kuna wakati maswali na majibu ni kama hayachukuliwi kutoa dira na mwelekeo wa serikali inavyofikiri inataka kulipeleka taifa. kuna haja ya bunge kujipima na kuona ubora na uthamani wa hoja zinazoletea mabadiliko ya msingi katika utendaji yanazingatiwa. Kwa raia dhamana ya ubunge inapoteza sura yake vigezo hivi vinapopungua.
   
 4. M

  Mngendalyasota Senior Member

  #4
  Aug 10, 2012
  Joined: Jan 22, 2011
  Messages: 171
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Unategemea nini kama speaker aliwekwa na akina andrew chenge hapo alipo.
   
Loading...