Elias Msuya
Senior Member
- Dec 23, 2011
- 175
- 681
Wakati Chama chama ACT Wazalendo kikiwa kimesaini kanuni za maadili ziliztolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), sasa kimetangaza kampeni ya kuzipinga mahakamani kwa madai kuwa zina upungufu mkubwa.
Chama hicho kilikuwa miongoni mwa vyama 19 vilivyosaini kanuni hizo Aprili 12, 2025 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu amesema wamesaini kanuni hizo sio kwa kukubali yaliyomo bali ni kutimiza matakwa ya kiuchaguzi.
Chadema ndio chama pekee ambacho hakikusaini kanuni hizo kutokana na msimamo wake wa kutaka mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi kabla ya uchaguzi maarufu ‘No Reforms No Election.’
Sababu ya kusaini
Akizungumza na Jamii Africa leo Aprili 14, Ado amesema wametia saini kutekeleza matakwa ya kisheria.
“Kwa maoni yangu kisheria, kusaini sio kuafiki kila kilichomo, bali ni kutekeleza matakwa ya kisheria, kwa sababu sharia hii ambayo kwa kweli ni kandamizi, inavitaka vyama vyote ili vishiriki uchaguzi mkuu na chaguzi zote kwa miaka mitano, ni lazima visaini. Unapenda unasaini, kwa miaka yote ya mageuzi hivyo ndivyo ilivyo,” amesema.
Amesema bado wanaamini kuwa wanaweza kupinga kanuni hizo mahakamani.
“Tumefanya uchambuzi wa vile vifungu tukagundua maeneo Zaidi ya 20 ambayo yanachangamoto, tukayawasilisha kwa tume lakini hayakupewa uzito.
“Hivyo wanasheria wetu wanafanya tathmini kuona kama tuna kesi ya msingi. Ndio maana kiongozi wa chama akasema amewaagiza wanasheria wetu kufanya uchambuzi, kwa sababu moja ya changamoto, vitendo vya tume havihojiki mahakamani,” amesema.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 74(12) inasema, "Hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka yakuchunguza jambo lolote lililotendwa na Tume ya Uchaguzi katikakutekeleza madaraka yake kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii."
Alipoulizwa sababu ya kutaka mahakamani ilihali wanajua mambo ya Tume ya Uchaguzi hayahojiki mahakamani, amesema:
“Sisi tafsiri yetu ni kwamba kipengele hicho (cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano) kinamaanisha vitendo, hakimaanishi tafsiri ya vifungu.
“Tunamini kwamba mahakama inaweza kupima mazingatio ya kikatiba. Mahakama inafanya tafsiri ya vifungu viwe vya kikatiba, kisheria na kikanuni,” amesema.
Mambo sita
Awali ACT Wazalendo walitoa mambo sita wanayotaka yafanyiwe kazi kuelekea uchaguzi mkuu, hata hivyo hawakueleza watatumia njia gani kuhakikisha yanatekelezwa, au watafanya nini yasipotekelezwa.
Mambo hayo ni pamoja na Makamishna wa Tume ya Uchaguzi wapatikane kwa ushindani, Wakurugenzi wa Halmashauri wasiwe wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo, mawakala wa vyama wafanye shughuli zao bila bugudha na wasizuiwe, wagombea wasienguliwe, pasiwe na kura feki na vyombo vya ulinzi na usalama visiingilie mchakato wa uchaguzi.
Alipoulizwa utekelezaji wa mambo hayo, Ado amesema, wamezindua operesheni Linda Demokrasia kupitia makongamano yanayofanyika mikoani.
“Tunafanya mawasiliano na wadau ikiwemo jumuiya ya kimataifa na asasi za kiraia na hivi karibuni tutazindua ziara za majimboni kwa ajili ya mikutano ya hadhara kwa ajili ya kuleta msukumo wa mambo sita tunayoyapigania,” amesema.
Je, yasipotekelezeka?
“Tutauvuka mto tutakapoufikia. Chama chetu kina kamati ya uongozi ambayo kila jambo tunalitathmini kwa hatua zake. Ndio maana hivi karibuni tutajifungia kutoa dira yetu ya uchaguzi,” amesema Ado.
Awali Ado aliandika katika ukurasa wake wa X kuhusu sababu ya chama hicho kusaini kanuni hizo.
“Ingawa ni muhimu kwa kiongozi wa kisiasa kukonga nyoyo za umma na kufurahisha wafuasi, lakini ni muhimu kwa kiongozi kujua uongozi ni zaidi ya kukonga nyoyo.
“Kiongozi lazima awe tayari kufanya maamuzi kwa kuzingatia hali halisi hata kama maamuzi hayo, katika wakati husika yanaweza kuwa yasiyofurahiwa sana lakini yakawa na matokeo makubwa na ya mbali katika siku za usoni.”
Dorothy Semu
Mbali na Ado, Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu amezungumzia msimamo wa chama hicho kupinga maadili hayo mahakamani, akisema zina upungufu mkubwa.
“Kanuni za maadili zimewalazimisha vyama kusainisha maadili kwa makubaliano yanayokiuka katiba. Kwamba chama ambacho hakitasaini kanuni za maadili hakitashiriki uchaguzi, hii ni kuwanyima haki wananchi wa Tanzania kushiriki uchaguzi.
“Hii ni uvunjwaji wa wazi wa haki za kisiasa, kwamba kila Mtanzania ana haki ya kushiriki uchaguzi, haki ya kuchaguliwa, haki ya kugombea na haki ya kupigiwa kura.
“Kwa hiyo naomba niwaarifu kwenye mkutano huu, kwamba chama cha ACT Wazalendo kwa kushirikiana na asasi za kiraia kitafungua kesi ya kisheria kuzipinga kanuni hizi pingamizi,” alisema.