KITANDA CHA MPANGAJI MWENZANGU - 9
ILIPOISHIA
"Hamna bwana, mwenzio najisikia," alisema Halima akimshikashika kijana huyo na kumvutia kwake.
"Halima unatangaza kwa watu mimi nalala na huyo kijana mbona na wewe upo kwake tena usiku huu?" sauti ya mama Tina ilisema mlango ukiwa wazi.
Wote walishtuka mle chumbani, mama Tina alisimama. Halafu alivyo jasiri alipenyeza mkono wake na kuwasha taa ya ukutani, tap! Kukawa na mwanga mkubwa.
ENDELEA SASA… "
Mi nimekuja tu mara moja," alijitetea Halima…
"Ungekuja mara moja kungekuwa na giza?"
"Hatukutaka kuwasha taa."
"Mmmh! Jamani, muwe wakweli, siyo mnawasingizia wenzenu kumbe na nyie ni mulemule," alisema mama Tina akiondoka kwa hasira.
Hasira zake zilikuwa mara mbili, kwanza Os Anjelus ni ‘mtu' wake, pili Halima ameingilia penzi lake, aliumia sana, basi tu.
Hakwenda chooni, alirudi chumbani kulala huku akiwa anasonya kila wakati…
"Vipi, una nini?" mume wake alimuuliza baada ya kushtuliwa na sonyasonya nyingi.
"Si hao wapangaji, sijui nani kaingia chooni wala hajamwaga maji!"
"Atakuwa nani, labda huyo mpangaji mgeni, maana hiyo tabia sijawahi kuiona wala kuisikia."
"Mm! Yule wala, sidhani kama anaweza kuwa na ustaarabu sifuri kama huo."
"Atakuwa yeye tu, mbona unamtetea au unamjua aliyefanya hivyo?"
"Mimi simjui mume wangu na wala simtetei, ila nasema haoneshi kama ana ustaarabu mbovu kama huo."
Walilala baada ya mazungumzo hayo.
***
Halima aliamka kwake baada ya kutoka kwa Os Anjelus usiku ule hata bila ya kucheza mechi, mama Tina alimtibulia ingawa pia haijulikani kama kijana huyo angemkubalia au la!
Alifikicha macho akiwa uani huku kaaibu kwa mbali kakimtawala usoni.
Mama Tina alichomoka kwake na kutokea uani, hakumsalimia Halima licha ya kwamba alimkuta…
"Za asubuhi mama Tina?"
Kimya…
"Mama Tina nakusalimia."
"Kwani lazima kuitika salamu yako Halima?"
"Khaa! Mke wangu kwani kuna nini? Mtu anakusalimia unasema kwani lazima? Mna ugomvi? Eti Halima kuna ugomvi?"
"Hatuna ugomvi," alijibu kwa haraka mama Tina. Aliamini kwamba kama angechelewa kusema lolote, Halima angeweza kufichua yaliyofichika ambapo yeye asingetaka mambo yafikie huko…
"Sasa kwa nini unakataa salamu yake? Eti Halima kuna ugomvi?" baba Tina alirudia tena kumuuliza Halima maana awali alimuuliza akajibu mke wake…
"Muulize mkeo, si anajua mimi niko singo sijaolewa, yeye kaolewa, muulize sasa," alisema Halima kauli iliyojaa utata wa kutosha kumfanya baba Tina ahisi kuna jambo hasa kwa kauli hii…
"…si anajua mimi niko singo sijaolewa, yeye kaolewa…"
"Mama Tina kuna nini?"
"Hakuna kitu mume wangu, amesema tu. Salama Halima mdogo wangu jamani, umeamkaje?"
"Mimi sijambo."
Baba Tina ambaye alikuwa akienda kazini alifungua mlango mkubwa na kutoka, lakini akili ikakumbuka mazungumzo yake na mkewe usiku uliotangulia kuhusu chooni…
"Si hao wapangaji, sijui nani kaingia chooni wala hajamwaga maji!"
"Atakuwa nani, labda huyo mpangaji mgeni, maana hiyo tabia sijawahi kuiona wala kuisikia."
"Mm! Yule wala, sidhani kama anaweza kuwa na ustaarabu sifuri kama huo."
"Atakuwa yeye tu, mbona unamtetea au unamjua aliyefanya hivyo?"
"Mimi simjui mume wangu na wala simtetei, ila nasema haoneshi kama ana ustaarabu mbovu kama huo."
"Hili suala la leo asubuhi lina jambo zito ndani yake, Halima na mke wangu sijawahi hata kuwasikia wako kwenye mgogoro wowote, ni nini kipya kimetokea?
"Halafu kwa nini Halima amekimbilia mambo ya kuolewa na kutoolewa, ina maana msingi wa mzozo wao ni huo?" alijiuliza mwanaume huyo hata alipokuwa amefika kazini…
"Lazima nianze ufuatiliaji, hapa penye ndoa na usingo pana kitu, mimi ni mtu mzima na ule ni ujumbe nilipewa kwa akili," alisema moyoni baba Tina.
Akiwa katika harakati za kazi, simu ya baba Tina iliita, namba ngeni…
"Halooo," alipokea baba Tina.
"Halo, wewe ni baba Tina?"