Kitabu kidogo cha busara

Shayu

Platinum Member
May 24, 2011
608
1,653
Hiki ni kitabu kidogo cha busara. Ni matokeo ya tafakuri kuhusu maisha na mwenendo ulio bora. Kitabu hiki ni nuru na mwongozo uliobora. Kitaongeza ufahamu kwa wasio na ufamu na kukuza uelewa wao. Ni matokeo ya fikra katika kazi.
Mtu akaaye na kutafakari mawazo yake hutembea na kufika katika kona za mwisho wa dunia. Huchambua giza na kutenga na nuru.


Kwa kitabu hiki utajifunza kulinda na kuongoza mwenendo wako katika njia zilizo sahihi. Moyo wako utajawa na matumaini na kujiongezea kujiamini na kujitambua. Kitabu hiki ni zao la fikra.

Katika binadamu kuna hazina iliyojificha ndani kabisa ya roho ya binadamu, ni kazi ya fikra kuitafuta kwa kutafakari, na kwasababu pasipo kutafakari hazina hii haitofichuka. Ni wajibu wetu kutafakari kila siku ili kupata majibu ya matatizo yanayo tutatiza kila siku katika maisha yetu. Pasipo kutafakari hatuta tambua muelekeo wa safari ya maisha yetu hapa duniani.


Matatizo mengi ambayo binadamu anayoyapata ni kwasababu hakai na kupata muda wa kutafakari. Kutafuta suluhisho la matatizo yake ya kila siku. Kama ikiwa tabia yetu ya kila siku kukaa katika kiti na kutafakari basi haitochukua muda kwetu kuyashinda maisha.


Ndani kabisa ya roho ya kila mmoja wetu kuna suluhisho la matatizo yetu kama tutakaa na kutafakari. Tutakapo kaa na kutafakari tutajua ni njia gani tunapaswa kupita. Kwasababu sio kila njia ni sahihi kwetu. Ni wajibu wetu kutafuta njia iliyosahihi. Na hatuwezi kuipata njia hii kama hatutafakari.


Ni haki ya kila binadamu kuishi maisha ya furaha hapa duniani. Ni haki ya msingi ya kila mtu. Lakini kwa wengi maisha yamekuwa kitu cha shida na dhiki. Wengi hawafurahii maisha yao hapa duniani wala uwepo wao katika hii dunia. Lakini hatukai na kutafakari kwanini maisha yamekuwa hivyo? Utakapo kaa na kutafakari utajua kwanini. Ni jukumu la kila mtu kutafuta ukweli na wala tusitegemee watu wengine kukaa na kutafakari na kuja na ukweli. Ukweli uko ndani ya kila mmoja wetu. Furaha ni hazina ambayo wachache wanayo. Furaha ni zao la busara. Usipoenenda kwa busara huwezi kupata furaha. Ni wajibu wetu kukaa na kutafakari kila wakati. Furaha sio ya maskini wala ya matajiri. Msingi wake ni jinsi tunavyo fikiri. Msingi wake ni mtizamo wetu kuhusu maisha.


Wengi wetu tunachanganya kati ya furaha na starehe. Lakini ukiangalia kwa ukaribu sana utagundua kwamba starehe uhusisha mwili lakini furaha ni akili na moyo. Kwa mtu mwenye busara akiambiwa achague kati ya furaha na starehe atachagua furaha. Na ukiangalia Zaidi starehe huondoa kabisa uwezekano wa binadamu kupata furaha na humtumbukiza katika shimo. Kwa miaka mingi wanafalsafa wamekuwa wakiujiuliza kuhusu furaha chanzo chake ni nini na binadamu atawezaje kupata furaha ya kudumu. Lakini wasi wasi wa maisha na utafutaji wa mali umefanya watu wengi kukosa furaha. Wengi wetu tunadhani mali ndio zitakazo tuletea furaha. Lakini kinachotufanya tusiwe na furaha ni kutoridhika kwetu kwa kile kidogo tulicho nacho. Tunapojifunza kuridhika kwa kile kidogo tulicho nacho furaha taratibu huanza kurudi.



Binadamu tunapaswa kutambua binadamu ukuaji wake ni hatua, lazima azaliwe na akue kufuata taratibu ambazo zimepangwa. Usiporidhika na ulichonacho hutaweza kupiga hatua katika ukuaji wako wa ndani wa kiroho ni lazima ukuaji wa ndani na wa nje uende sambamba. Hii ndio siri iliyopo; na tusiwe na wasiwasi kuhusu mali. Kwa asili ya mali huwa haitoshi kwa mtu anayeijua mali anafahamu hili, na kama tutaweka akili yetu katika mali kama ndio msingi wa furaha kamwe furaha hiyo hatutaipata. Watu wengi tunaifuata mali kama ndio kitu kilichotuleta duniani kuitafuta, na kwamba tutakapoipata ndio tutakuwa tumekamilisha malengo yetu ya kuwepo hapa duniani. Mali sio mbaya kama ni katika kusaidia katika kurahisisha maisha yetu. Kwenye mambo yale ambayo ni muhimu. Lakini mali inapotumiwa vibaya humuangamiza aliyonayo. Kwahiyo mali inahitaji busara kuitumia. Tunatakiwa kuitawala mali na sio mali kututawala sisi na kuitumia sivyo kukandamiza haki za wengine. Na wala mali haipaswi kutumiwa kwa starehe bali kwa kufanya mabadiliko katika maisha ya watu. Dunia ina maskini wengi sana na kama umebarikiwa saidia. Pata muda wa kutafakari unapotafakari ndipo unapokua.



Watu wengi wanakua kimiaka lakini ukuaji wao wa kiakili unaendelea kuwa mdogo. Je tunaitumiaje senti ndogo tunayoipata kila siku hili ndio suala tunalopaswa kujiuliza je tunaitumia kwa faida au kwa hasara? Tunapaswa pia kujua utumiaji wa pesa zetu. Lazima tuwe na busara ya utumiaji wa pesa. Tutakapokuwa na busara ya utumiaji wa pesa ndipo tutakapoendelea. Jinsi gani tutaweza kusimamia pesa zetu katika njia ambazo ni za busara. Tunapojua kukusanya pesa tujue na kuzitunza na kuziongeza kwa kutumia fikra na sio tamaa kwakuwa tunajua tutakapokuwa na mtazamo hasi kuhusu pesa utafanya kudhuru wengine hasa tunapokuwa na tamaa ya pesa kupita kiasi. Kama pesa itatumiwa vizuri itatuongezea furaha lakini sio chanzo halisi cha furaha. Fikra zetu ni chanzo cha furaha yetu; jinsi tunavyoongoza fikra zetu.

Tunajua kwamba tusipokuwa na busara tutatenda mambo yasiyo sahihi na tunapotenda mambo yasiyo sahihi furaha yetu umong’onyoka. Pesa peke yake haiwezi kufanya mambo yote haya. Kwa hiyo busara ni ya msingi sana katika maisha ya binadamu. Busara hutengeneza mienendo yetu katika usahihi. Na mahusiano yetu yanategemea sana busara. Kama hatutakuwa na busara mahusiano yetu yatakuwa ni mabovu. Na mahusiano ni msingi mkuu kwa binadamu. Hatuwezi kuuumizana kama tuna mahusiano mazuri. Matatizo yote ambayo binadamu anayopata ni kutokana na kutofikiri sawasawa. Vurugu, fujo na vita vinatokana na fikra mbovu. Hatukai na kutafakari matendo yetu. Hatufikiri tunavyatuka katika matendo na maneno. Unapokaa na kutafakari unaona kabisa sisi binadamu ni wajinga na wapumbavu. Na kwamba dunia ilijengwa njema na sisi tumeiharibu kwa fikra zetu mbovu. Hatufikiri sawasawa ni wapumbavu. Hatutafuti busara ituongoze. Na kwamba busara ingetufanyia yaliyo mema kama tungekaa na kutafakari. Tusipotumia akili zetu tutakuwa hatuna tofauti na nyani.


Kamwe hatutaweza kupata amani kama hatufikiri sawasawa; na kama tutatenda sawa sawa tutakuwa na amani. Hatutakuwa na amani miongoni mwetu kama hatutafikiri sawasawa. Kama hatutashughulisha akili zetu tusahau kuhusu amani. Hakuna kitu kinachofanyika kwa kubahatisha katika hii dunia kikadumu kila kitu ni zao la fikra kazini. Misingi imara ya taifa lolote hujengwa na fikra sahihi. Taifa lolote imara hujengwa na mtu anayejua anachokifanya na jamii inayojua inachokitenda.



Je ni nani anayestahili kuongea? Ni yule anayejua. Ili maneno yake yanufaishe wengine, ili maneno yajenge wengine. Mwenye maarifa anastahili kuongea kwenye hadhara ili maneno yake yawe faida kwa wengine. Kwanini mijinga ung’ang’anie kuongea? Je kipofu anaweza kumuongoza kipofu mwenzake? Kupewa mdomo haina maana ya wewe kuongea yoyote hata yale yasiyo na maana. Tega sikio sikiliza maneno ya hekima yakusaidie katika maisha yako. Mwenendo wako ni kila kitu kwako uangalie kwa makini. Nawe utakuwa na matumaini na siha njema. Kwa mtu mwenye akili huogopa kuongea na anapoongea huongea ukweli.

Uovu wetu hutokana na uelewa wetu mbovu. Tukitenda yasiyo sahihi tusahau kuhusu amani yetu na furaha yetu. Baraka hutokana na fikra na matendo sahihi. Njia zetu zitabarikiwa ikiwa tu tunatenda na kufikiri sahihi. Mneno hujenga na maneno hubomoa. Hakuna ufalme, utawala wala kitu chochote kilichojengwa pasipo fikra. Ubora wa taifa lolote hutokana na ubora wa fikra. Vitu vyote vimeundwa kutokana na fikra kazini. Miili yetu ni chombo tu ambacho fikra hukitumia kujenga miji na mataifa. Fikra mbovu hujenga mataifa mabovu. Kwahiyo miili ni chombo tu ambacho fikra hukitumia. Mikono na miguu hutumiwa na fikra kukamilisha matendo yetu. Unapotaka kwenda mjini huwaza kwanza kabla ya kwenda. Unapouunda chungu fikra hazionekani lakini mikono huonekana na ndio inayofanya kazi kukamilisha fikra na kutoa chungu kilichokamili. Kama fikra ni bora hutoa chungu bora inategemea na wazo akilini mwa mtu. Ubora wa fikra ndio ubora wa chungu.



Fikra hazionekani lakini vitu vinavyoumbwa na fikra huonekana. Kwahiyo ni muhimu sana kuangalia jinsi tunavyofikiri ndio msingi. Tukiwa na fikra bora tutajenga vizuri familia zetu, miji yetu na taifa letu katika ubora. Tuepuke kuwa wepesi wa kuongea bila kufikiri. Hili jambo ni muhimu sana kwetu. Kwahiyo mataifa bora hutokana na fikra bora.

Mpumbavu yeyote husema na kuongea pasipo kufikiri kwanza. Mwenye busara hufikiri kwanza na hutenda kutokana na maarifa. Hili ni jambo la msingi ambalo wote tunapaswa kulifahamu. Kama tunataka kujifunza tunaweza kujifunza. Kwasababu maarifa ni kitu cha msingi sana katika maisha ya binadamu. Maarifa ndio yanayotufanya tuendelee. Pasipo maarifa hakuna mtu au taifa litakaloendelea. Kuwa na maarifa ni kujua. Kujua jambo katika ufanisi wake. Kujua kiini cha jambo. Ukiwa na maarifa unatawala jambo unalolijua. Usipotawala jambo unalolijua huna maarifa. Kuwa na maarifa ni kutawala. Huu ni ukweli kwasababu Mungu ana maarifa zaidi yetu ndio maana anatutawala. Uelewa wake ni mkubwa kuliko wetu. Mtu mwenye uelewa mkubwa atamtawala mwenye uelewa mdogo wakati wote. Wote tunapaswa kulijua hili. Na kama tunataka kuendelea lazima tutafute maarifa. Ni lazima tufikiri. Tukiamua kuacha fikra na kufuata ujinga ndio tunajichimbia kaburi wenyewe.


Mataifa ya ulaya maarifa yao yamewasaidia sana kuwafikisha hapo walipo. Ni wakati wetu sasa kuzinduka na kutafuta maarifa ambayo yatatusaidia sisi na kizazi chetu. Hili ni jambo la muhimu kwasababu bila maarifa hatutafika popote. Bila watu wetu kutenda katika busara taifa hili halitoendelea. Ni muhimu tukajitambua kama taifa. Hatuwezi kufika tunapotaka kufika pasipo maarifa. Safari yetu hatuwezi kufika tukiwa wajinga ila tukiwa werevu. Taifa linapaswa kujua hili na kupata uelewa nalo. Ni muhimu kujenga taifa la watu wanaojitambua. Tutajenga msingi imara wa taifa hili ikiwa watu wetu wakiwa wanajitambua.



Watu wenye uelewa mdogo hawawezi kuendelea lazima tujue hili. Taifa letu ni la watu wenye uelewa mdogo. Ni wajibu wetu kufanya jitihada kukuza uelewa wa watu wetu. Ndipo tutakapoendelea. Wazungu wanalijua hili. Wana hazina kubwa ya maarifa kuliko sisi. Na maarifa ndio msingi wa nguvu zao. Kila mtu ana nguvu za mwili hata sisi, walichotuzidi ni maarifa. Maarifa yao ndio siri ya kututawala. Ninachoomba kutoka kwenu ni kubadilika kwetu ili kufanya mapinduzi katika taifa letu. Kwa hiki kitabu kidogo cha busara natumaini kitaamsha hisia kwenu za kutaka mabadiliko katika taifa letu. Mabadiliko ya fikra na ya kimtazamo. Tukae tukijua mtu mwenye akili na maarifa atamtawala asiye na akili na maarifa. Mjinga siku zote hutawaliwa ukombozi wake ni kupata maarifa. Kama Ng’ombe asivyoweza kumtawala binadamu ndivyo mtu mjinga asivyoweza kumtawala mtu mwenye akili na maarifa. Mtu mwenye akili humtawala mtu mjinga. Nawaombeni tutafute maarifa kwaajili ya ukombozi wa taifa letu. Ujinga utaendelea kutufanya watumwa na kuuza uhuru wetu. Tusiwe taifa la wapumbavu bali la wenye akili.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom