Kiongozi wetu awe na sifa na si jinsia | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Kiongozi wetu awe na sifa na si jinsia

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by chuhila, Sep 6, 2010.

 1. c

  chuhila Member

  #1
  Sep 6, 2010
  Joined: Aug 18, 2009
  Messages: 11
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 3
  KIONGOZI WETU AWE NA SIFA NA SI JINSIA

  Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuna utaratibu wa kubadilisha viongozi wa ngazi mbalimbali za kisiasa kila baada ya miaka mitano. Viongozi ninaowalenga kwa siku ya leo ni rais, wabunge na madiwani. Hawa ndio wawakilishi wa matakwa yetu wananchi. Rais huunda serikali ili aweze kuyafanya yale ambayo wanachi wanamtarajia ayafanye au awaongoze katika mchakato mzima wa kuyafanya yeye akiwa kama kiongozi mkuu wa serikali. Bila kujadili sana kazi zao, wabunge ndio wawakilishi wa karibu zaidi wa wananchi kwa serikali yao, hawa ndio wanaotakiwa kupeleleka matatizo mbalimbali katika serikali ili kuweza kupatiwa ufumbuzi. Hawa huweza kupeleka matakwa ya wananchi wakiwa bungeni au popote serikali ipatikanapo.

  Kama tulivyoona muungozo wa katiba; mwaka huu 2010, ni mwaka wa kuwabadilisha viongozi wetu. Nieleweke kwamba kuwabadilisha haina maana kuwaondoa wale wote waliokuwepo katika nafasi za uongozi, hapana. Tunawabadilisha kwa kuwachagua wale tuwadhaaniao wana uwezo mzuri katika kutuongoza, kwa hiyo basi kama waliokuwepo madarakani wana uwezo bado tunaweza kuwachagua tena katika nafasi zao hizo, lakini kama uwezo wao umeshuka basi tuwaweke wengine wenye uwezo zaidi. Tena hawa waliokuwa madarakani ni vyepesi sana kuwapima kwani waliyotufanyia yanaweza kupimika kwa mizania yeyote ile.

  Si nia yangu leo kuelezea majukumu au matarajio ya wananchi kutoka kwa viongozi wao. Nia yangu ni kujaribu kujadili na kujiuliza ni sifa zipi kiongozi wetu anapaswa kuwa nazo. Kwa mujibu wa katiba yetu kifungu cha 33(1) kinasema wazi wazi kwamba kutakuwa na rais, kwa hiyo kulingana na kifungu hiki nchi yetu ni lazima iwe na rais kwa misingi ya katiba.

  Kifungu cha 39(a-d) kinatoa sifa ambazo rais wetu atakayetokana na katiba anatakiwa awe nazo, chache nikizitaja kwa tafsiri yangu ni kwamba ni lazima awe raia wa Tanzania, awe na umri wa miaka si chini ya arobaini, ni lazima awe mwanachama wa chama cha siasa na ateuliwe na chama chake kugombea nafasi hiyo, na ni lazima awe na sifa za kumwezesha kuwa mbunge au kuwa katika baraza la wawakilishi.

  Hizi ndiyo sifa za jumla atakiwazo kuwa nazo rais wetu mtarajiwa. Katika vifungu hivi vyote hatujaona katiba ikitaja kuwa mtu huyu awe mzee sana, awe kijana sana, awe mwanaume, awe mwanamke, awe kabila gani au dini gani, katiba haijui vitu hivyo, si vya msingi katika kumpata rais na wala havitakiwi kabisa katika siasa na uongozi wa nchi hii.

  Katika nafasi ya ubunge katiba inataja sifa za mwenzetu huyu atakaye kutuongoza katika kifungu cha 67(1-2), kwamba ni lazima awe raia wa Tanzania, ajue kusoma na kuandika kwa Kiswahili au kiingereza, awe na akili timamu, na sifa nyingine nyingi. Katiba hiyo hiyo kifungu cha 66(1) inaainisha aina za wabunge katika kifufungu kidogo (b) inaelekeza aina moja wapo ya wabunge kuwa ni kundi la wanawake ambao idadi yao haitakiwi kuwa chini ya asili mia 15 ya wabunge wa majimbo na wale kutoka katika baraza la wawakilishi, wawakilishi hawa wanawake huteuliwa kwa uwiano wa vyama vyenye uwakilishi bungeni. Kifungu cha 78 kinatoa maagizo ya namna ya kuwapata wabunge wa aina hii.

  Hizi ndizo baadhi ya sifa ambazo tunaongozwa kuzifuata ili kupata watu wa kutuongoza. Tunaweza kumpata kiongozi mtarajiwa mwenye sifa nzuri zaidi ya zilizoainishwa na katiba , hilo ni jambo zuri, lakini haiwezekani hata kidogo kumpata kiongozi asiyekidhi hata sifa za msingi zilizoainishwa na katiba yetu.
  Katika michakato inayoendelea hivi sasa kuelekea uchaguzi mkuu kumetokea kampeni za aina mbalimbali zikiwemo za wagombea wenyewe ndani ya vyama vyao vya siasa, wapambe wao na hata asasi za kiraia zimekuwa zikitoa miongozo ya ni namna gani tuchague viongozi wetu.

  Vyombo vya habari ndivyo vimekuwa nguzo pekee ya kufikisha ujumbe wa wana-kampeni hawa kwa watanzania wa kawaida. Kinachonishangaza na kilichonifanya nikamate karamu yangu na kutumia muda wangu kuandika ni jinsi wana-kampeni hawa walivyosahau kabisa sifa za msingi za atakiwaye kuwa kiongozi katika Jamhuri yetu. Zinaendelea kampeni za kimatabaka. Nasema bila wasiwasi kwamba zipo kampeni za kimatabaka. Mwalimu Nyerere katika mkutano wake na waandishi wa habari Machi,13,1995 alishauri kuwa ni vizuri kwanza kuangalia masuala mbalimbali yanayotukumba kwa muda tuliopo ndipo sasa tuangalie ni nani mwenzetu atakayefaa kutuongoza ili kuyafanya masuala yetu hayo. Na alisisitiza kuwa Matanzania yeyote mwenye sifa aweza kuwa kiongozi.

  Kampeni za matabaka ninazo zisema ni zile zinazonadi watu (viongozi watarajiwa) wachaguliwe kwa kuzingatia ujinsia wao, umri wao na elimu yao. Haya yote kwa bahati mbaya ilioje hayapo katika sifa za msingi za atakaye kuwa kiongozi wetu kwa mujibu wa katiba.

  Ninashindwa kushangaa na ninajiuliza ujasiri huu wa wagombea kuomba kura kwa wananchi kwa kutumia jinsia zao au umri wao wanautoa wapi? Jibu jepesi kwa wanawake litakuwa ili kutimiza au kufikia adhma ya asilmia 50/50 ya uwakilishi katika vyombo mbalimbali vya maamuzi.

  Tujiulize asilimia 50/50 kati ya wanawake na wanaume katika nafasi za maamuzi kwa maslahi ya nani? Kwani tunaenda kuoana huko kwamba tuwe sawa ili mtu asikose mwenza wake? Tanzania leo tunahitaji kutaka uwiano huo ndipo tuweza kuyakabili masuala ya kimaendeleo anayoyasema mwalimu Nyerere? Nchi zilizoendelea zimeshafikia hatua nzuri zaidi ya maendeleo katika karibu kila idara, nadharia hii ya kutaka uwiano sawa hapa kwetu inaasilia huko kwao kama sharti mojawapo la sisi kuendelea kupewa usaidizi katika mambo tofauti tofauti ya kifedha, kitaalamu au kiteknolojia.

  Na kwa sababu hii, nchi zetu hizi za Afrika ambazo bado ni changa kimaendeleo kuliko umri wao ambao zimekwishafikia, ni lazima tu zikubaliane na mataifa (Bosi) yanayowasaidia na ndiyo maana sera hii imechukuliwa na karibia nchi zote za ulimwengu wa tatu. Chukulia mfano Marekani, nchi iliyoendelea-inayojitegemea, wana kampeni kali za ujinsia katika nafasi za uongozi kama hizi za kwetu? Kwani wao hawapendi uwiano sawa? Jibu ni kwamba watu huchaguliwa kwa sifa zao.

  Mashirika (asasi za kiraia/wanaharakati) mengi yamejitokeza awali kupigia debe wanawake wagombee, na kwa sasa wameteka vyombo vya habari kwa matangazo ya kutaka tumchague mwanamke kwani akiwezeshwa anaweza. Sijui hapa wanamaanisha awezeshwe na nani. Na akishawezeshwa sijui atakuwa huru kiasi gani kwa huyo aliyemuwezesha katika kutenda kazi zake za kila siku.

  Cha ajabu kabisa kabisa, kampeni zimekuwa nyingi katika siasa kuliko katika shida nyingine za kijamii ambazo mama zetu na dada zetu wanazipata hasa huko vijijini, huko katika kliniki za uzazi nk. Ni kwa nini nguvu zaidi katika siasa tu? Wanavyopenda kutoa majibu mepesi watasema nguvu zaidi katika siasa ili wakawawakilishe wanawake hao wenzao wenye shida huko bungeni. Sijui kama nitakubaliana na jibu kama hili.

  Nitamke upesi hapa kwamba mimi nimezaliwa na Mwanamke, tumeoana na Mwanamke na nina mtoto wa kike na ninapenda sana miongoni mwao au wote wapate nafasi katika vyombo mbalimbali vya maamuzi; nitafurahi sana. Maana hawachelewi hawa wanaojiita wanaharakati kuniuliza kama si kuniambia moja kwa moja kwamba naongea kama sikuzaliwa na mwanamke.

  Hoja yangu hapa ieleweke kwamba mtu asipewe na hapaswi kupewa au kupiganiwa nafasi ya uongozi au nafasi yoyote ya maamuzi kwa kuangalia kwamba huyu ni mwanamke au mwanaume. Mtu apewe kitu kile anachostahiri kwa mujibu wa sifa zake na uwezo wake wa kuzifanya. Na mtu huyu azipate hizo sifa kwa nguvu zake alizozitoa katika mazingira sawa na ya yule wa jinsia nyingine siyo tena apendelewe kupata sifa hizo kama mkakati wa kumuandalia nafasi hiyo.

  Hawa wanaharakati wanafanya kazi zao kulingana na katiba za taasisi zao na miongozo ya wakubwa wao wanaowapatia pesa kwa ajili ya kufanyia shughuli hizo, watafanya nini basi tofauti na kile walichoambiwa wakifanye. Wakifanya tofauti si watakosa ulaji.

  Rai yangu kwa kila mpenda maendeleo ya nchi hii yetu tunayoipenda ni kwamba, tusiende kumchagua mtu kwa vigezo vya kuwa yeye ni mwanamke akiwezeshwa anaweza, au yeye ni mwanaume bali twendeni sote tukawachague viongozi tunaodhani kuwa watatuongoza vyema katika miaka mitano mingine ya kikatiba. Kwa nchi changa kimaendeleo kama yetu hakuna maana ya kuanza kuangalia uwiano wa kijinsia, hii ni mbinu tu ya kuendelea kutuchelewesha katika maendeleo.

  Kwa sababu, hii kwa sasa imeletwa kama ajenda, kokote uendako utakuta linaongelewa 50/50, hili halina maana cha msingi ni kiongozi anayefaa awe mwanamke au mwanaume haipunguzi chochote katika maendeleo yetu, labda misaada ya wanaotuambia tuufuate mfumo huo. Kwangu mimi hata wanawake wakiwa zaidi ya asilimia 90 wana sifa za kuingia katika ngazi za maamuzi tuwape nafasi hizo bila kujali kwamba na wanaume ni lazima wawepo asilimia 50, vile vile kwa upande wa pili. Uwanauke na uwanaume hauna lolote la kufanya katika kuongoza kinachomata hapa ni uwezo na si jinsia.

  Kigezo hiki cha asilimia 50/50 kina lengo la kutufanya watanzania tujikite katika suala hilo la kuangalia ni namna gani wanawake na wanaume watapewa madaraka sawa katika nafasi za uongozi badala ya kujikita katika kujadili masuala nyeti ya maendeleo na hivyo kwa kufanya hivi tunaendelea kuwa wategemezi hata katika umri wetu wa karibu nusu karne sasa.

  Tutazidi kuwa nyuma kimaendeleo kwa sababu hili suala la 50/50 limetugawa na tunakuwa kama tunaoneana wivu hivi kwamba, wanaume wanafanya kazi katika nafasi nyingi zaidi au wanawake wanapewa nafasi za bila jasho, haya makundi yanayotengenezwa yanaondoa ule umoja unaotakiwa tuwe nao kama taifa lenye lengo moja la kujiletea maendeleo na hivyo si rahisi kupata maendeleo katika hali kama hii. Tuwanadi watu au viongozi watarajiwa kwa sifa zao na si jinsia zao.

  Hongera ni kwa wanawake wote majasiri ambayo hawasubri haki yao ya kikatiba ya kupendelewa katika nafasi za bunge kama kifungu cha 78 cha katiba kinavyoelekeza bali wamejipima na kuona wanaweza na hawahitaji kuwezeshwa na mtu yoyote zaidi ya wao kwenda kunadi sera zao na za vyama vyao kwa wananchi ili wapate ridhaa ya kuwatumikia. Na kwa wale wanaosubiri kifungu tajwa kiwape ubunge watafute sifa (kama zinatafutwa) za kuwafanya viongozi awamu zijazo, msibweteke kusubiri kifungu hiki, kama hamjui kifungu hiki kinawakandamiza, kwa nini mwanamke tu ndio apewe nafasi ya kuteuliwa au viti maalumu? Mimi nilidhani wanawake ndio watakuwa wa kwanza kutaka kifungu hiki cha katiba kifutwe ili kuwe na usawa wa kijinsia katika uwanja sawa wa siasa na maendeleo.

  Maana kifungu hiki kinawafanya kama vile wanawake hawajiwezi na wanahitaji usaidizi, hili si la kweli mbona wapo wenye uwezo, tuwaache watende. Kwa kutambua hatari ya viti vya upendeleo katika bunge Rais wa Jamhuri alitoa angalizo kwamba, nafasi hizi zinaua nafasi ya demokrasia, alishindwa tu kutamka moja kwa moja kwamba hapendi aina hii ya uwakilishi. Hii ilikuwa ni salamu tosha kwamba kazaneni nendeni majimboni na katani kugombea. Hizi nafasi za katiba na nyinginezo nyingi za kupewa zikataeni, kataeni kupendelewa kwani huyo atakayekupendelea atakuamulia pia nini ukifanye ukiwa katika nafasi hiyo uliyonayo. Ninatambua kwamba wapo wanawake makini sana wasiotaka hata kusemewa na mtu, wengine pia igeni mifano hii myema.

  Mnapigania kwenda Bungeni kuwawakilisha wanawake wenzenu wakati leo mkiwa mnapanda daladala wote mnashindwa hata kumpisha mwenzenu mmoja akae kwa sababu ana mtoto mdogo, au katika foleni za benki kuwapisha wajawazito wapate huduma kwanza kabla ya wazima, huku na lugha mbaya mkizitoa sasa mkiwezeshwa mtaweza nini? Kama haya madogo tu mnashindwa kuyafanya mkiwezeshwa kwenda Bungeni ndio mtawakumbuka. Nawashukuru akina baba ambao katika matukio hayo niliyoyataja ndiyo huwa wanawabika ipasavyo na kwa lugha za ukarimu. Kumbe mwakilishi wa kweli wa mwanamke anawezakuwa mwanaume.

  Nimalizie kwa kuongelea suala moja la wale wanaonadi sera zao kwa kigezo cha umri. Hili nalo linachekesha kama si kushangaza, tukuchague wewe kwa kuwa ni kijana, hapa pia kuna yale yale kijana akiwezeshwa anaweza. Kijana ana nini cha pekee cha kufanya Bungeni kwa kutumia ujana wake? Ana nini pia cha pekee cha kukifanya pale Ikulu kwa kutumia ujana wake? Tofauti gani tutakayoipata au kuiona tukiongozwa na kijana au mzee. Ujana au uzee pia havina nafasi hata kidogo katika uongozi kwa sababu kule bungeni haihitajiki mtu mwenye misuli sana, kwa kuwa hatupeleki wabunge wakashindane kunyanyua vyuma vizito au mizigo mizito, hatupeleki mtu ikulu akawe bondia kwa kutumia nguvu za ujana wake. Kwa wewe kuwa kijana ni jambo la kwanza lakini la pili na muhimu zaidi ni sifa ulizonazo.

  Lakini pia mambo mengine ni ya kutumia busara za kawaida tu kwa wazee wetu waliotumikia taifa letu kwa uaminifu mkubwa na kwa muda mrefu. Sawa, mwaweza kuwa bado mna sifa nzuri za kuendelea kuwa viongozi au wabunge, lakini tumieni busara kung’atuka muda ukiwadia kabla ya wananchi kuwakataa hadharani kwa sababu hii ni aibu zaidi.

  Utakuta mtu amekuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 20 na ametumikia wizara karibia zote lakini mzee huyu bado tu ananga’ang’ania majukwaa, chukueni mifano ya Mh. Waziri mkuu Pinda aliyetangaza kuwa hiki ni kipindi chhake cha mwisho akipata ridhaa ya wananchi kurudi tena bungeni au Mh Mzindakaya ambaye kastaafu kwa heshima kubwa na wengine wa aina yao. Nitoe pole kwa wazee waliostaafishwa kwa manufaa ya wapiga kura wao, hawa walichokwa na wakakang’anga’nia na ndipo wakabwagwa.

  Wazee wasome alama za nyakati na waachie madaraka muda ukifika, vijana wenye sifa wagombee na wanadi sifa zao na si ujana wao. Kama tutafanya hivi, kuheshimiana kati ya wanasiasa chipukizi au vijana na wazee kutakuwepo kwa kiasi cha hali ya juu kabisa.

  Mwisho kabisa, jamani katiba inamtaka mtu kuwa mbunge ajue kusoma na kuandika kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza, kuna haja gani basi ya kuwatukana au kuwadharau wagombea kwa kigezo cha wao kuwa na elimu ndogo? Ndiyo natambua ukweli kwamba watashindwa katika baadhi ya mambo kule bungeni, cha kufanya hapa tuwachuje na sera zao kama wanafaa tuwape, hawafai tuwaache ila tusiwadharau na kuwakejeli tuwaache wapate haki yao ya kikatiba.
  Mungu tupe ujasiri watanzania.

  Mwandishi ni mfuatiliaji wa masuala ya kisiasa, anapatikana kama;
  Maxmillian J. Chuhila
  E-mail- chuhilamj@yahoo.com
  Cell phone- +255 784 687 530
   
Loading...