King Mirambo na Askari wake waliojulikana kama Rugaruga

King Mirambo na Askari wake waliojulikana kama Rugaruga

100 others

JF-Expert Member
Joined
Aug 5, 2017
Posts
8,791
Reaction score
30,991
King Mirambo alikuwa mtawala mashuhuri wa kabila la Wanyamwezi katika karne ya 19 huko eneo la Unyamwezi (magharibi mwa Tanzania ya leo).

Katika Afrika Mashariki na kati yote hakuna Chief ambaye aliongeza maeneo yake ya utawala kwa nguvu za kijeshi na silaha kama King Mirambo.

Jeshi lake la rugaruga walikuwa wakiogopeka kila mahali, hata wanawake ambao walitaka kunyamazisha watoto wao waliokuwa wanalia waliwaambia 'Hulikaga Limilambo likwiza' ikiwa na maana 'Nyamaza/kaa kimya Mirambo anakuja'.

Inasemekana Mirambo alizaliwa kati ya miaka ya 1830-1840, waliobahatika kumuona King Mirambo ambao walikuwa ni wazee sana miaka ya 1950s wanasema Mirambo alikuwa mrefu sana na pua ndefu ya Kitutsi, alikuwa na rangi ya brown.

Wengine walidai hawakuamini kama Mirambo alikuwa mnyamwezi halisi kitu ambacho ndugu zake waliokuwa wana taarifa za uhakika kumhusu walithibitisha Mirambo alikuwa Nyamwezi.

Father Simeon Lourdel, moja ya wazungu waliobahatika kufika katika mji alipokuwa akiishi Mirambo March 1883, alishangazwa sana na muonekano wa Mirambo, katika report yake aliandika kwamba 'Mirambo ambaye jina lake linaogopeka kuanzia Nyanza hadi Tanganyika ametupokea kwa adabu na heshima, ni moja ya Waafrika wazuri zaidi ambapo sijapata kuona' aliandika nanukuu 'He is one of the most handsome africans that i have never seen, you might think that you were in the presense of one of the giants of Djurd-jura in Kabylia in North Africa'.

Father Simeon anaendelea kuandika katika report yake kwamba mwili wa Mirambo ulikuwa umejengeka kwa misuli, rangi yake ni brownish na urefu wake si wa kawaida, anatumia muda wake mwingi kuwinda simba na chui na nyumba yake ya wageni ameipamba kwa ngozi hizo za wanyama.

Askari wa Mirambo walikuwa ni wapiganaji wenye hasira kali na wakali kweli kweli, ambapo King Mirambo aliwapa jina la rugaruga , rugaruga walivaa nguo nyekundu kama damu wakiziita pembamoto ikiwa na maana nguo za moto.

Kulikuwa na askari wengine wakiitwa B' ishima ambao hao kazi yao ilikuwa kumlinda King Mirambo katika nyakati za vita, walivaa nguo nyeusi na vilemba kichwani.

Rugaruga wao walikuwa na nywele ndefu, walikuwa wakitisha katika muonekano, wakionekana kama wanyama, walikuwa wakivuta bangi, macho yao yalikuwa mekundu.

Rugaruga walikuwa wakivaa nguo fupi kiunoni, wanabeba pochi zenye pistols kiunoni, na kila mmoja akiwa na pistols mbili, kila moja upande mmoja yaani kulia na kushoto, pia walibeba kama pembe ya mnyama kwa kubebea unga wa risasi.

Begani walibeba bunduki iliyokuwa inashikiliwa na mkanda.

Nywele zao zilikuwa hawazipunguzi.

Hao ndio rugaruga ambao nataka nieleze matukio yao ya ajabu.



Rugaruga walipokuwa wakienda vitani walijipaka rangi ya udongo mwekundu kichwani(ochre), walipokuwa wakipita kwenye mapori walisugua vichwa vyao kwenye miti, watu walipokuja kupita hilo eneo walisema 'Malambo gabitaga henaha' wakiwa na maana 'Warambo walipta hapa'


Rugaruga walipovuta bangi walibadilika na kuwa kama wanyama wa mwituni na walikuwa na nyimbo yao ya vita..

Uhuu! Chuma , tukahumilwa
nanali ku ng'wa Kapela? (
twice)
Ga machimu machimu,
Uhuu! Kiya kwape,
Li Kube Linyabangwe,
Li Sida Linyabangwe.


Mirambo yeye alikuwa havuti bangi kama askari wake, yeye alipendelea kutumia ugoro.

Hawa jamaa walikuwa wakiingia vitani walikuwa hawarudi nyuma, walikuwa wakipigana vita si mchezo.
Kuna kisa kimoja walikwenda kupambana na Wanyaturu, hii ndio vita iliwasumbua sana, hii kwa sababu walisafiri umbali mrefu kwenda walipo Wanyaturu.


Hawa Wanyaturu uaambiwa walikuwa wanapiga fimbo haijapata kuonekana, maana askari wa Kinyaturu walikuwa kila mmoja ana fimbo mbili zile ngumu kabisa, rugaruga walikuwa wakijiandaa kupiga risasi basi fimbo imeshafika kichwani na kuvunja kichwa, walikufa askari wengi sana wa Mirambo.

Ukijiandaa kupiga risasi tayari fimbo imefika kichwani, ukikosea pia kulenga fimbo inakuhusu 'paah'... hapo ikabidi Mirambo awaambie askari wake 'Watatumaliza hawa muiteni Cheyo' , huyo Cheyo alikuwa ni rugaruga pia alikuwa na utaalamu sana wa nguvu za kimiujiza, sijui tuseme ni uchawi.

Cheyo alipokuja ndipo akawapa upako kuanzia King Mirambo na askari wote, baada ya hapo Mirambo na askari wake walifanikiwa kupita hadi nyuma ya maadui pasipo maadui(Nyaturu) kuwagundua ukisikia wazungu wanasema behind the enemy lines, mnatuma makomando kuingia ndani kabisa ya himaya ya adui pasipo wao kujua lolote, ndivyo ilivyokua.

Vita iliendelea na ikafika kipindi Mirambo na askari wake wanaishiwa risasi na silaha.

King Mirambo baada ya kuona vita imekuwa ngumu sana akawaambia askari wake inabidi watumie strategy ya kivita, maana hata baada ya kurudi nyuma Wanyaturu walikuwa wakiwafuata na kuwashambulia.

Hio strategy ya kivita ilikuwa ni kuwapika(Mubadeka) , hivyo kama Mnyaturu alikuwa akipigwa risasi na kufa , mwili wake ulikatwa vipande vipande , halafu wanawasha moto mkubwa , wanaweka chungu kikubwa na kumpika askari wa Kinyaturu, baada ya hapo wanaondoka huku nyama za askari wa Kinyaturu zikiendelea kuchemka kwenye chungu, halafu wanaacha mguu au mkono ukining'inia nje ya chungu.

Askari wa Kinyaturu wakifika hilo eneo na kukuta mwenzao anachemkia jikoni waliogopa sana na kushangaa na walisema 'Wasukuna ni wala watu' na morali ya vita iliwaishia kabisa kupambana na rugaruga ambao waligundua ni wala watu.

Hio ndio strategy Mirambo alitumia kukimbia vita ya Turu War, kuna vita nyingi alipambana za kushangaza na hadithi za kusisimua sana nitakuja kuelezea.


Niruke kwanza hapo.


Twende kwenye jinsi walikuwa wakisheherekea baada ya kushinda vita.
Kwanza kule vitani walikuwa wanaua wanaume, wanawake walichukuliwa kama mateka na kupelekwa Urambo kwa ajili ya kuolewa tena.

Vijana wadogo walichukuliwa ili waje kuwa bakoboko ili wajifunze sanaa ya vita.

Walipofika makao makuu Isela-Magazi baada ya kutoka vitani. Mirambo aliwaruhusu askari wake kuchukua mali walizokuwa wamechukua huko vitani.

Mirambo aligawana ng'ombe na askari wake, na alioa mwanamke mrembo zaidi katika wale ambao wameteka kutoka vitani.

Hivyo kila siku jeshi lake lilikuwa linakua.

Hivyo hata majeshi kutoka makabila mengine walikuwa wanakuja kujiunga na Mirambo sababu ya sifa zake, hivyo jeshi la Mirambo lilikuwa na askari wenye makabila tofauti lakini kabila kubwa likiwa Nyamwezi.

Baada ya mapumziko kidogo King Mirambo aliamrisha ng'ombe nne ama tano zichinjwe ili kufanya sherehe ya ushindi walioupata.

Ng'ombe wanono zaidi kuliko wengine ndio walichaguliwa na kuchinjwa, nyama ilichukuliwa na kuwekwa kwenye vyungu vikubwa , hio nyama ilichanganywa na magome ya aina fulani ya miti, waliweka na masega ya nyigu yaliokuwa na larvae wa nyigu, walifanya hivyo ili askari wanapokula ile nyama wawe wakali kama nyigu.

Inasemekana hata wawindaji wa kipindi hiko waliwafanyia hivyo mbwa wao ili wawe wakali, na mbwa walikuwa wakali kweli kweli kama nyigu.

Baada ya nyama kupikwa ilisambwazwa juu ya ngozi iliyokuwa chini, askari walisimama pembeni kwenye mstari akija mmoja mmoja kuchukua nyama kwa midomo pasipo kutumia mikono, katika aina hii ya ulaji walikuwa wakifundishwa kuwa kama simba hata katika kula.

Baada ya kula walianza kucheza ngoma za kivita, huku wanalipua bunduki zao hewani huku wakiimba, hapo alitokea senior officer katika hao askari anagusia nyimbo nyingine huku wakiendelea kucheza na askari wakiitikia, hapo Mirambo na yeye alikuwa anaingia kati na yeye na kuanza kucheza.

Mirambo aliingia akicheza akiwa na pistol mkononi akiongea kwa sauti akisema maneno na skari wake wanaitikia , hapo King Mirambo alipiga risasi hewani akiimba nyimbo za majigambo na kujisifu...

King Mirambo alipandisha sauti na kusema 'Nene Chota-Manumba' akiwa na maana anaota moto kwa nyumba zinazoungua moto, anasema 'Nene Mino-ga-Mbwa' akimaanisha nina meno ya mbwa , anaendelea na kusema 'Nene Nzwala-Mino' akiwa na maana navaa meno.

Alisema hivyo anavaa meno kwa sababu King Mirambo alikuwa akishawapiga adui zake , anamng'oa jino na kutengenezea mkufu, mjukuu mmoja wa Mirambo alikuwa na mkufu una meno 85 ya waarabu ambao aliwaua katika vita ya Tabora.


Kwa leo nimendika kwa kifupi sana , nitakuja tena kuandika kwa urefu zaidi.
 
Noma sana.
Sehemu kubwa ya vtabu vya historia wameficha mengi, hii ndio hadithi ya kweli , mwandishi alisafiri hadi Tabora akaonana na wajukuu wa Mirambo ambao nao walikuwa wazee miaka ya 1960s, hiki kitabu kimeandikwa miaka hio 1960s.

Ni moja ya vitabu adimu sana. Mwenyewe nilikuta kwenye moja ya vitabu vya babu yangu.
 
Sehemu kubwa ya vtabu vya historia wameficha mengi, hii ndio hadithi ya kweli , mwandishi alisafiri hadi Tabora akaonana na wajukuu wa Mirambo ambao nao walikuwa wazee miaka ya 1960s, hiki kitabu kimeandikwa miaka hio 1960s.

Ni moja ya vitabu adimu sana. Mwenyewe nilikuta kwenye moja ya vitabu vya babu yangu.
Kwa kweli kizazi cha sasa tunakosa mambo mengi adimu historia kama hizi hazipatikani.
 
Bunduki alikuwa anatoa wapi enzi hizo wamissionari bado hawajaingia?
Alikuwa anawatumia wafanya biashara ambao walikuwa wanaenda Pwani, hawa watu waliitwa Bundeba , Hizo silaha zote zilitoka maeneo ya Pwani ya Afrika Mashariki, hivyo Mirambo aliwapa hao Bundeba(wafanya biashara matajiri) pembe za ndovu ili kubadilishana na bunduki na unga wa risasi, huko Pwani kulikua na waarabu ambao walikuwa wanafanya hio kazi ya kubadilishana bunduki na unga wa risasi kwa pembe za ndovu.

Hivyo ndicyo ilivyokuwa.
 
Kwa kweli kizazi cha sasa tunakosa mambo mengi adimu historia kama hizi hazipatikani.
Exactly, hakuna uhalisia wa hadithi nyingi, hivi sasa hakuna mtu atakuambia askari wa Mirambo rugaruga walikuwa wakivuta bangi kabla ya kuingia vitani. Hakuna mtu atasema Mirambo aliwapika kwenye masufuria askari Wanyaturu ili kuwaogopesha wengine.
 
Exactly, hakuna uhalisia wa hadithi nyingi, hivi sasa hakuna mtu atakuambia askari wa Mirambo rugaruga walikuwa wakivuta bangi kabla ya kuingia vitani. Hakuna mtu atasema Mirambo aliwapika kwenye masufuria askari Wanyaturu ili kuwaogopesha wengine.
Hakika mkuu historia inamengi ya kutueleza.
 
Sehemu kubwa ya vtabu vya historia wameficha mengi, hii ndio hadithi ya kweli , mwandishi alisafiri hadi Tabora akaonana na wajukuu wa Mirambo ambao nao walikuwa wazee miaka ya 1960s, hiki kitabu kimeandikwa miaka hio 1960s.

Ni moja ya vitabu adimu sana. Mwenyewe nilikuta kwenye moja ya vitabu vya babu yangu.
Pengine ungeki-scan mkuu ili wengi zaidi tupate kukisoma.
 
Back
Top Bottom