Kinana ataka ubunifu kurahisisha shughuli za Wananchi

SautiYaMnyonge

JF-Expert Member
May 13, 2018
439
742
~Amtaka waziri wa TAMISEMI kufika Moshi kumaliza migogoro

~Ataka ubunifu urahisishaji shughuli za wananchi

~Ampongeza Rais Samia kuimarisha uhusiano na Kenya


Mapema mwezi Mei, 2021 Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alifanya ziara ya siku mbili ya kikazi nchini Kenya kutokana na uhusiano wa mataifa hayo kuonekana kudorora na kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi pamoja na kuwa kikwazo kwa biashara.

Ziara hiyo aliyokutana na kuzungumza na Rais wa Jamuhuri ya Kenya Mheshimiwa Uhuru Kenyatta ilifungua milango ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili na kuimarisha uhusiano wao kwa kubaliana kushirikiana bila kuwepo kauli au vitendo vya kukwazana .


Hali hii ilipelekea wananchi kuweza kuendelea na shughuli za biashara baina ya nchi hizi mbili bila usumbufu. Akizungumza mkoani Kilimanjaro Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Ndg Abdulrahman Omar Kinana amesema ziara hiyo ya Rais Samia Suluhu Hassan haikuwa ya bahati mbaya bali alikuwa akitekeleza maelekezo ya chama hicho kupitia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025.

"Kazi kubwa tuliyonayo CCM ni kurahisisha shughuli za wananchi katika kujiletea maendeleo. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kurahisisha shughuli za wananchi baina ya mpaka wetu na Kenya kupitia ziara aliyofanya mwaka jana. Hii ndio kazi ya CCM na niwahakikishie watanzania tutaendelea kuifanya bila kuchoka."

Kupitia mkutano huo wa ndani uliofanyika katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Ndg Kinana alisema viongozi na watendaji wa serikali wajenge utamaduni wa kufanya maamuzi shirikishi kwa kuwashirikisha na kuwasikiliza wananchi ili kuja na maamuzi mazuri yatakayotekelezwa kwa ushirikiano wa pande zote.

"Kukosekana kwa ushirikishwaji wa wananchi kumefanya baadhi ya viongozi na watendaji serikalini kuwa mahiri kwa kusimamia sheria kuliko kuwa wabunifu wa kurahisisha shughuli za wananchi. Sasa niwatake tubadilike tuanze kuwasikiliza wananchi, wananchi wanajua matatizo yao na majibu yanayotakiwa tusiwapuuze." Amesisitiza Kinana

Akiendelea kuwahutubia Wana-CCM Kinana amesema chama hicho kimekuwa madarakani muda mrefu kwa sababu ya uhuru na haki ya wanachama kuchagua na kuchaguliwa pamoja na utoaji wa maoni kwenye vikao. Aidha, alisisitiza misingi imara iliyoachwa na waasisi wa chama hicho hayati Mwl Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume ya haki, utu, usawa, uadilifu na utumishi wa watu nayo imekuwa chachu hivyo ienziwe kwa vitendo.

"Tusikubali mambo haya yakatutoka maana nguvu ya ushawishi na uimara wa CCM utapungua au kuyumba. Tusikubali wanachama wakaona siku hizi haki na uhuru hakuna au wananchi wakaona chama walichokiheshimu na kukiamini hakiwasikilizi tutajiweka kwenye hatari."

Kinana amesema atazungumza na waziri wa ofisi ya Rais Tamisemi Mheshimiwa Innocent Bashungwa ili afike mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kukutana na kuwasikiliza madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Moshi na Moshi Manispaa kwa lengo la kutatua migogoro iliyojitokeza ili kuleta utulivu na kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Kinana amehitimisha kwa kuwataka viongozi na watendaji wa chama na serikali mkoani humo kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na mshikamano ili kuwatumikia wananchi kwa ufanisi.
IMG-20220426-WA0049.jpg
IMG-20220426-WA0059.jpg
IMG-20220426-WA0039.jpg
IMG-20220426-WA0059.jpg
IMG-20220426-WA0064.jpg
IMG-20220426-WA0054.jpg
IMG-20220426-WA0045.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom