Kinachotokea Zimbabwe kiwe fundisho

Kinachotokea Zimbabwe kiwe fundisho

Noel Shao

Member
Joined
Jan 19, 2017
Posts
89
Reaction score
185
Kalamu yangu kuhusu yaliyo tokea Zimbabwe, au Soma katika gazeti la [HASHTAG]#Mwananchi[/HASHTAG] la jana !
[emoji116][emoji116]

========

Awali niweke wazi msimamo wa kutokubaliana na mapinduzi yoyote ya kijeshi katika kuiondoa Serikali iliyowekwa madarakani kwa mchakato wa kidemokrasia.

Pamoja na msimamo huo, sihalalishi kiongozi au chama chochote kujimilikisha na kujirasimishia madaraka. Siungi mkono kiongozi kukaa madarakani huku wananchi wakiwa hawanufaiki na matunda ya uongozi wake.

Tabia ya viongozi na vyama vya siasa kujimilikisha nchi mithili ya kuwa na hatimiliki imeshaota mizizi Afrika. Kwa mtazamo wangu si afya kwa kiongozi katika nchi zilizo katika mfumo wa kidemokrasia, kukaa madarakani kwa miongo kadhaa kana kwamba ndiye pekee mwenye uwezo wa kuongoza.

Kinachoumiza na kurudisha nyuma maendeleo katika uongozi wa namna hii ni kile kitendo cha kugawana madaraka kwa upendeleo. Mara nyingi ndugu wa kiongozi husika, kabila lake, watu wa ukanda wake au marafiki zake wa karibu ndio hunufaika.

Haiwezekani viongozi wakawa wanagawana madaraka mithili ya keki ya sherehe.

Madhara yake ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na utawala wa sheria. Wale walio karibu na watawala huwa wananufaika kuliko wengine.

Mwisho wake husababisha maendeleo duni ya kiuchumi, maendeleo ya upande mmoja na kuacha umaskini, ukabila, chuki, uovu na ukiukwaji wa haki za kibinadamu ukitamalaki.

Katika hatua hii ndipo dhana ya wananchi kutoridhika huanza kumea na kuanza kudai mabadiliko kwa nguvu kubwa huku kikundi kilicho madarakani nacho kikionyesha kutokuwa tayari kuachia madaraka.

Au ikifika hatua hiyo ndipo jeshi linapoamua kuingilia kati kwa manufaa ya nchi. Kama ilivyotokea nchini Zimbambwe.

Historia ya Rais Robert Mugabe ilikuwa ni ya kudumishwa kuanzia harakati zake za ukombozi wa bara la Afrika, ila kama ilivyo kwa viongozi wengine wa Afrika, Mugabe amekuwa wa kushindwa kusoma nyakati na kudhani kwamba wao ndio wenye uhalali wa kuhodhi kila kitu katika nchi.

Na mbaya zaidi akataka kugawa madaraka kwa wengine kama zawadi, mwisho wao huwa ni wa aibu na fedheha

Mugabe amekaa madarakani kwa miaka 37. Kuna viongozi nao wapo madarakani kwa miaka mingi kama rais wa Cameroon, Paul Biya ambaye amekaa kwa miaka 37, Yoweri Musseveni (34), Theodore Nguema wa Equtorial Guinea yupo madarakani kwa miaka 37.

Sijajua ni maradhi gani yanawakumba viongozi wengi hawa hadi kuwa na usugu wa kung’ang’ania madaraka?

Aidha, Afrika inahitaji maendeleo. Ingekuwa vizuri viongozi kujikita katika kutatua changamoto lukuki zinazolikabili bara la Afrika, kufuata katiba na msingi ya utawala bora.

Jambo hata liwe bora kiasi gani lazima liwe na kiasi; iwe madaraka, heshima, uhuru, nguvu au matendo. Mambo yaliyo na kiasi huleta ustawi katika jamii, mapatano, haki na amani katika taifa. Fikiria kama usiku usingekuwa na kikomo, au baridi au jua vingefuliliza bila ukomo?

Rai yangu kwa viongozi na vyama vilivyo madakani kutazama ni wakati gani na sahihi wa kuongoza na kuachia madaraka.

Katika hili, Mwalimu Julius Nyerere atakuwa rejea sahihi. Alijua wanamhitaji lakini akaona ni wakati sahihi kwake kung’atuka na kuwaachia wengine baada ya kuongoza kwa miaka 24. Hata uwe mwanamuziki bora kiasi gani, kuna wakati lazima ushuke kutoka jukwaani.

Viongozi watambue kuwa siasa safi zenye ushindani wa haki huchochea maendeleo. Siasa chafu, na uchu wa madaraka ni shimo la maangamizi.

Noel Shao ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii. 0769735826 calvin.noelshao@gmail.com
 
Nilimsikia Bashite akipiga chapuo la 2025 nikashangaa. Lengo lake ni kula mema ya nchi as much as possible.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom