NA MWANDISHI WETU
7th June 2010
Rais Jakaya Kikwete amesema matukio ya mimba kwa wanafunzi wa kike nchini yanasababishwa na viherehere vya wanafunzi wenyewe.
Utoro, mimba wanafunzi wa kike vyamshtua JK
23rd July 2014
Rais Jakaya Kikwete ameshtushwa na kiwango kikubwa cha wanafunzi katika mkoa wa Ruvuma kushindwa kumaliza shule kwa sababu mbalimbali, ukiwamo utoro na mimba kwa wanafunzi wa kike.
Utoro na mimba za wanafunzi ni mambo, ambayo yamezungumzwa kama changamoto za Wilaya ya Namtumbo, mkoa wa Ruvuma na Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa, alipozungumza katika mkutano wa hadhara, uliohutubiwa na Rais Kikwete, kwenye uwanja wa michezo wa Namtumbo jioni juzi.
Kwa mujibu wa takwimu za tatizo la mimba katika mkoa wa Ruvuma, watoto wa kike 155 wameshindwa kumaliza masomo yao ya shule za msingi na sekondari katika miezi 18 iliyopita kwa sababu ya kupata mimba.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa mwaka 2013, watoto 16 wa shule za msingi na wanafunzi 78 wa shule za sekondari walikatisha masomo kutokana na mimba wakati mpaka mwezi uliopita, wasichana watano wa shule za msingi na 56 wa shule za sekondari waliacha shule kwa sababu ya kupewa mimba.
Changamoto ya utoro nayo ni kubwa katika mkoa wa Ruvuma. Takwimu za utoro zinaonyesha kuwa kati ya watoto 41,801 walioanza shule ya msingi mwaka 2007 ni watoto 30,698 waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2013.
"Suala hilo nalirudisha kwenu nyie madiwani. Kuweni makini, hawa ni watoto wenu. Nataka kila miezi sita mpatiwe ripoti ya mahudhurio ya wanafunzi katika shule zote za mkoa huu," alisema Rais Kikwete.
Aliongeza: "Na kila mwezi, wakuu wa shule zote nchini watoe taarifa za mahudhurio ya wanafunzi kwa maofisa elimu. Pia Kamati za Maendeleo ya Jamii za Halmashauri nazo lazima zidai ripoti za mahudhurio kutoka kwa wakuu wa shule."
Aliwaagiza viongozi kushirikiana na vyombo vya sheria mkoani na wilayani kukabiliana na tatizo hilo kubwa.
Home