Kikwete asita kuikubalia Somalia

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Mwandishi Wetu

Toleo la 242
6 Jun 2012

242_somalia.jpg



TANZANIA iko katika mtihani mgumu wa kukubali maombi yaliyowasilishwa na serikali ya mpito ya Somalia ya kujenga na kuboresha taasisi za ulinzi na usalama za nchi hiyo inayokabiliwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu.


Rais wa muda wa Somalia, Sheikh Sheriff Ahmed mwishoni mwa wiki hii, aliwasilisha maombi hayo katika mazungumzo ya faragha kati yake na Rais Jakaya Kikwete, mjini Arusha.

Rais Ahmed aliwasili katika wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kupokewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, akitokea nchini Uturuki alikokuwa kwenye vikao vya kutafuta amani ya nchini yake.


Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho zimesema ya kuwa Rais Kikwete akitumia uzoefu wake katika masuala ya kidiplomasia hakuweza kukubali moja kwa moja maombi hayo ya Somali.


Na sababu kubwa inaelezwa kuwa Rais Kikwete hakufanya uamuzi wa moja kwa moja wa kukubali kutokana na ukweli kuwa, uamuzi wa kukubali maombi hayo, kwa namna fulani ni sawa na "kukialika" kikundi cha kigaidi cha Al-Shabab kuanza kuishambulia Tanzania kwa kuwa mshirika wa serikali ya mpito ya Somalia.


Kikundi hicho kimekuwa kikifanya mashambulizi ya kigaidi katika nchi ambazo ama kwa namna moja au nyingine zimekuwa zikiisadia Somalia kijeshi au kiuchumi.


Tayari kundi la Al-Shabb limekwishakufanya mashambulizi katika baadhi ya nchi zilizoonekana kuiunga mkono Serikali ya Somalia. Nchi hizo ni pamoja na Uganda, Kenya na Ethiopia ambazo kwa muda sasa zimekuwa zikiendesha operesheni maalumu za kijeshi nchini Somalia kukabiliana na Al-shabab.


"Rais wetu ametumia hekima ya kutokubaliana moja kwa moja na maombi hayo wala kukataa akijipa muda zaidi wa kushauriana na wajuzi wa masuala ya usalama na viongozi wenzake. Lengo hasa ni kutoingiza nchi katika matatizo yasiyo na lazima," alieleza mtoa habari wetu aliyekuwa akifuatilia mkutano huo wa wakuu hao wa nchi.


Sababu nyingine zinazoifanya Tanzania kujihadhari ni suala la muda wa kuwapo madarakani kwa Serikali ya mpito ya Rais Ahmed ambayo kwa mujibu wa makubaliano, inatakiwa kumaliza muda wake Agosti, mwaka huu. Hitimisho la kuwapo kwa Serikali hiyo madarakani ni pamoja na kufanyika kwa uchaguzi huru nchini humo.


"Kuna kila dalili kuwa maazimio hayo si rahisi kufikiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo vita inayoendelea na pia udhaifu wa serikali ya mpito ambayo imeshindwa kurudisha hali ya amani nchini humo," alieleza mtoa habari wetu.


Baada ya mazungumzo hayo, Rais Kikwete alitoa kauli fupi kwa waandishi wa habari akisema: "Tumefanya mazungumzo ya kushauriana na kuangalia hali ikoje nchini Somalia, nchi ambayo imekumbwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu."


Kwa upande wake, Rais Ahmed alisema: "Tuna kila sababu pia ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi zetu mbili na kwamba Somalia itahitaji kupata uzoefu wa masuala mbalimbali kutoka Tanzania katika nyanja za ulinzi na usalama."


Rais Ahmed alimshukuru Rais Kikwete na Watanzania kwa ujumla kwa kusaidia kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa amani ya Somalia katika masuala mbalimbali kama vile ya kisiasa, maendeleo, ulinzi na usalama.


"Bado tunahitaji maendeleo, kujenga taasisi imara za ulinzi na usalama na sekta bora za kijamii na kwa hiyo tunaomba msaada wa Tanzania," alisema kwa kifupi.


Rais huyo aliwasili Arusha akitokea Uturuki ambako kulikuwa na mkutano ulioandaliwa na Serikali ya Uturuki kujadili mustakabali wa nchi hiyo isiyotawalika tangu mwaka 1991, baada ya kuangushwa kwa utawala wa Rais Siad Barre.


Miaka zaidi ya 20 ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe imesababisha nchi hiyo kupoteza watu zaidi ya milioni kutokana na maradhi, njaa na vita huku maelfu wakikimbia makazi yao na kuishi katika kambi za wakimbizi katika nchi jirani ya Kenya.


Katika hatua nyingine, hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, alieleza msimamo wa Tanzania kuhusu kuanzishwa kwa tawi la Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), katika nchi za Afrika Mashariki.


Akishiriki katika kipindi cha televisheni kinachoendeshwa na mwandishi mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu, kinachorushwa kila Jumatatu saa mbili na nusu usiku katika Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Membe alisema kuanzishwa kwa Tawi la Mahakama hiyo mkoani Arusha-Tanzania hakuna uhusiano na kushinikiza watuhumiwa wa makosa ya kijinai wa nchini Kenya kesi zao zisikilizwe katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.


"Hii haina maana tunalenga kushinikiza kesi za Wakenya katika Mahakama ya Makosa ya Jinai ziletwe nchini, ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kinachoanzishwa hapa ni tawi la Mahakama hiyo," alisema Membe.













 
Bravo President Kikwete... Hapo kwa kweli nakupa kudos...

Hataki Al Shabab watuingilie kuwatafuta hao Wabunge wa Kisomali na kumwaga Damu ya Watanzania...
 
Back
Top Bottom