Kikwete aambiwa abebe mizigo yake!


• WABUNGE WADAI MSEKWA NI GAMBA JINGINE CCM

na Salehe Mohamed, Dodoma

MAKADA na wabunge kadhaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanatilia shaka uwezo na dhamira za baadhi ya mawaziri katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, na sasa wamemtaka awaondoe kama anataka kunusuru chama na serikali yake.


Wanasema Rais Kikwete asipofanya mabadiliko sasa, hataungwa mkono na wananchi, wakiwamo baadhi ya wana CCM wenye nguvu na ushawishi wanaoitakia mema nchi hii.
Makada hao wanakiri kwamba serikali imepoteza heshima mbele ya jamii kutokana na kukithiri kwa vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na kukosa uamuzi mgumu kwenye ufumbuzi wa matatizo ya wananchi, likiwamo tatizo la mgawo wa umeme.


Wanadai sasa hivi Bunge ndilo limebaki kuwa mkombozi wao maana linajadili yale yaliyoishinda serikali, na hata kuiagiza ifanye na kurekebisha makosa ya wazi.
Na baada ya wabunge wa CCM kuona serikali imelala usingizi, na chama kinachoongozwa na mwenyekiti ambaye ndiye rais, kinashabikia udhaifu a serikali, wameshtuka na kuanza kuishambulia serikali, hasa baada ya kuona wabunge wa upinzani wanatoa hoja zinazogusa maisha ya wananchi wa kawaida.


Miongoni mwa wabunge ambao wameamua kuungana na wapinzani katika kutetea masilahi ya wananchi ni Deo Filikunjombe (Ludewa), Beatrice Shelukindo (Kilindi), Christopher ole Sendeka (Simanjiro), Dk. Khamis Kigwangalah (Nzega) na Kaika Telele (Ngorongoro).


Wabunge hawa, kwa nyakati tofauti, wamewashambulia viongozi wao kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo na hivyo kusababisha matatizo kwa wananchi.


Hata hivyo, duru za siasa zinadai kwamba inawezekana mashambulizi ya wabunge hawa wa CCM ni kiinimacho cha kudhoofisha nguvu ya wapinzani, kama ilivyokuwa kwa waliojiita wapambanaji wa ufisadi, ambao miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu uliopita walitumika kupoka ajenda ya ufisadi kutoka kwa wapinzani, hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ili CCM iweze kuaminiwa tena na umma.


Telele na Sendeka walimshambulia Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, kwa kutoa vibali vya ujenzi wa hoteli yenye hadhi ya nyota tano katika hifadhi ya Bonde la Ngorongoro ambalo haliruhusiwi kwa shughuli za kibinadamu.


Shelukindo naye alimshambulia Waziri wa Maliasili na Utalii kwa kumteua Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Benno Malisa, katika kamati ya kusimamia ugawaji wa vitalu vya uwindaji wakati hana sifa zinazostahili.


Mbunge huyo pia katika vikao vya wabunge wa chama hicho, alimshambulia Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kwa kufanya ukabila kwenye Idara ya Wanyamapori.


Mashambulizi ya wabunge hawa yameonekana kuwashtua baadhi ya viongozi wa chama hicho ambao mara kadhaa wamekuwa wakilinda udhaifu wa watendaji wa chama na serikali kwa lengo la kuogopa kuharibu taswira ya chama.


Kutajwa kwa Msekwa katika uuzaji wa maeneo akitumia jina la Rais Jakaya Kikwete kumezua maswali miongoni mwa makada wa chama hicho juu ya uhalali wa dhana ya kujivua gamba inayopigiwa chapuo hivi sasa.


Hoja inayojengwa na makada hao ni kuwa kama Msekwa anashiriki katika vitendo vya ufisadi atakuwa na mamlaka gani ya kuwahoji makada wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo hivyo?


Hata hivyo, baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili wameweka wazi kuwa kulinda maovu hayo ni kukiua chama chao na wabunge wake ambao hivi sasa wameamua kutetea masilahi ya majimbo yao bila woga.


Baadhi yao wamebainisha kuwa kama serikali itashindwa kuwasikiliza, wao wataachana nayo, na wataendelea kutetea majimbo yao.


“Hivi sasa kilichopo ni kutetea wananchi wetu kwenye majimbo tuliyotokea, tukifanya mchezo wananchi watapoteza imani kwetu kama walivyofanya kwenye chama,” alisema mbunge mmoja kwa sharti la kutotajwa jina.


Wachambuzi wa masuala ya siasa wanabainisha kuwa miongoni mwa mambo yanayoifanya CCM kupoteza mvuto kwa jamii ni kupanda kwa mafuta, tuhuma za ufisadi, maisha magumu na mgawo wa umeme.


Mmoja wa viongozi serikalini amelidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa baadhi ya mawaziri wanashindwa kuwajibika kikamilifu kiasi cha kushindwa kuwawajibisha watendaji wasiotekeleza majukumu yao.


“Tunaisubiri NEC (Halmashauri Kuu ya CCM) itakayokutana mwezi ujao kama itafanya maamuzi ya kukinusuru chama chetu. Isiporekebisha mambo hali itakuwa mbaya zaidi. Si umeona bungeni mambo yanavyotuwia magumu?” alisema.


Kada mmoja wa siku nyingi kutoka Kanda ya Ziwa alisema, “Kama rais hataki kutuondolea hii mizigo yake, tunaweza kumlazimisha na yeye akafunga virago akaondoka nayo.”


Alidai kwamba ingawa JK katika siku za hivi karibuni ameleta dhana ya kujivua gamba kama njia ya kukihalalisha chama mbele ya umma, kitendo cha rais kushindwa kuchukua hatua mapema dhidi ya wale anaowadhania kuwa ni magamba kimemfanya aonekane kiongozi dhaifu.


Alisema hata utekelezaji wa dhana hiyo ukifanyika vibaya unaweza kumdhuru rais mwenyewe kwa sababu amewapa watu wengi muda wa kufanya tafakuri ya kutosha, na wamegundua kwamba magamba ndani ya CCM ni zaidi ya hao ambao wamekuwa wakitajwa.


Alienda mbali hata kudai kwamba uchambuzi wa kina ukifanywa, hata mwenyekiti mwenyewe anaweza kujikuta ni gamba ndani ya chama, jambo ambalo litakiletea chama madhara makubwa kuliko ilivyodhaniwa.


Alisema wabunge wameshtuka kwa sababu wamegundua rais anawatumia kujiimarisha kisiasa wakati akijua yeye anastaafu miaka minne ijayo, na baadhi yao watakuwa bado wanahitaji kujijenga kisiasa kwa malengo ya siku zijazo.


“Kwa sababu hiyo, tutafika mahali tutampuuza kwa masilahi ya watu wetu, chama chetu na nchi yetu. Haaminiki tena, maana kama ameweza kuchonganishwa na watu waliomtafutia urais, itakuwaje sisi tusio karibu naye?”


 
hamna kitu hapa
  • kama hawana imani naye si wapige kura ya kutokuwa na imani naye
  • wanatumia kauli za wapinzani ili waonekane nao wapo wanao wajali wananchi
  • ni ngumu sana ku control baraza la watu 52 (wakimo PM na AG) cha msingi wizara na mawaziri wapunguzwe hadi 26
  • kitengo cha DPP kiondolewe PCCB wafanye kazi ya kushitaki pia kwani wanakuwa na ushahidi wa UFISADI/RUSHWA
 
Back
Top Bottom