Kigoma: Zaidi ya wananchi 100 wa Jamii ya Wanyantuzu, wadaiwa kupigwa risasi na Polisi

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,492
54,895
INADAIWA zaidi ya wananchi 100 wa kabila la Wanyantuzu, wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Madai hayo yalitolewa jana Dar es Salaam na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya usalama nchini.

Alisema mauaji hayo yalitokea katika tukio la mapigano kati ya polisi na wananchi wa jamii ya Wanyantuzu wilayani Uvinza mkoani Kigoma lililotokea takribani siku 10 zilizopita.

Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, alidai katika tukio hilo, askari wawili wanadaiwa kufariki dunia.

Alidai mapigano hayo, yalitokea baada ya kabila hilo la Wanyantuzu kupeleka mifugo yao katika eneo hilo.

Alipotafutwa Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani ili kuzungumzia suala hilo alisema atafutwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma kwa kuwa tukio limetokea katika eneo lake.

Hata hivyo, MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Ottieno simu yake iliita bila kupokelewa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali mstaafu, Emanuel Maganga naye alimtaka mwandishi wa habari hizi kumtafuta RPC wa Kigoma.

Kutokana na hilo, gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ambapo alisema taarifa hizo za wananchi 100 kupoteza maisha si za kweli.

“Mimi ni Waziri wa Mambo ya Ndani, sina taarifa za aina hiyo… haina ukweli wowote, nakiri kulikuwa na operesheni ya mifugo kule na askari wetu wawili walipoteza maisha…natambua IGP yuko kule tunasubiri atuletee taarifa.

“Lakini madai wananchi wameuawa hakuna ukweli wowote…hata kuhusu suala la askari kuuawa sio rahisi kulizungumzia kwa sasa, ninamsubiri IGP aniletee taarifa kamili,”alisema Lugola.

ALICHOSEMA ZITTO

“Wiki iliyopita yalitokea mauaji ya askari wa Jeshi la Polisi katika eneo la Mto Malagarasi, Kijiji cha Mpeta wilayani Uvinza, mkoani Kigoma, ambapo Mkuu wa Kituo cha Polisi Nguruka aliuwawa na wanaodaiwa kuwa ni wananchi.

“Chama chetu kilitoa salamu za rambirambi kwa IGP (Simon Sirro) kutokana na mauaji hayo, kikilaani na kikitaka uchunguzi ufanyike na wahalifu wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

“Tumekuwa tukifuatilia kwa kina yote yanayojiri huko Uvinza tangu kuuawa kwa askari polisi wetu. Tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno.

“Kwani tunaambiwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi, wengine wakisemwa kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na jeshi la polisi.

“Jeshi la Polisi limekalia kimya suala hili, pamoja na IGP kutembelea eneo hilo la maafa. Haiwezekani kamwe tukio kubwa namna hii kutokea halafu Serikali ibaki kimya bila kutoa maelezo yeyote kwa wananchi. Uchunguzi wa kina unapaswa kufanywa ili kutambua nini kimetokea pale Mgeta,”alisema Zitto.

Kutokana na hilo, alisema chama chao kinaendelea kukusanya majina na taarifa za wote wanaodaiwa kuuawa na kitaweka wazi taarifa husika.

“Kwa sasa tunaitaka Serikali ieleze nini hasa kimetokea Mgeta, maelezo hayo yawe ya kina na yawe ya ukweli. Chama chetu kinaendelea kukusanya majina na taarifa za wote wanaodaiwa kuuawa, na kitaweza wazi taarifa husika,”alisema Zitto.

Katika hatua nyingine, Zitto pia alizungumzia matukio ya watu kutekwa, kushambuliwa kwa risasi huku akishangazwa kwa wahalifu kutokamatwa mpaka sasa.

“Tanzania katika miaka mitatu, imekuwa ni nchi ya watu kutekwa, kushambuliwa kwa risasi na ‘watu wasiojulikana’, kuokotwa miili yao ikiwa imeuawa, kuwekwa kwenye viroba na kutupwa kwenye fukwe za bahari na mito yetu. Ni jambo la kawaida sasa mtu kutekwa au askari kufyatulia risasi makumi na mamia ya wananchi.

“Tunayo mifano iliyo wazi, msaidizi wa Kiongozi wa Upinzani, Ben Saanane, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Kibondo na Diwani wa Kata ya Kagezi, Simon Kanguye na mwandishi wa habari za uchunguzi wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda wamepotezwa, huku watuhumiwa namba moja wakiwa ni vyombo vya dola.

“Mpaka sasa hakuna yeyote aliyekamatwa kutokana na tukio la kumpiga risasi nyingi kwa lengo la kumuua Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, pamoja na shambulizi kutokea ndani ya eneo la Bunge. Serikali inadhani kwa kuchagua kukaa kimya, damu ya watu hawa itapotea kimyakimya? Haiwezekani!

“Miaka hii mitatu tumeshuhudia mamia ya wananchi wenzetu wakiuawa na kupotezwa katika eneo la MKIRU (Mkuranga, Kibiti na Rufiji). Hivi karibuni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Siro, akizungumzia sakata la kutekwa kwa Mohammed Dewji alitoa dondoo kidogo kwamba walilazimika kutumia nguvu kule MKIRU kuwaondosha watu aliodai sasa wamekimbilia Msumbiji. Kwa mara ya kwanza IGP Sirro alikiri kuna watu wengi waliuawa,”alisema Zitto.

Alisema chama chake cha ACT-Wazalendo kimepaza sauti juu ya masuala hayo ndani ya miaka mitatu, pamoja na Serikali kuamua kutokueleza ukweli au kuchukua hatua kuyazuia, hawatakaa kimya.

Alisema wataendelea kusisitiza kuundwa kwa tume ya kutafuta ukweli wa mauaji ya MKIRU na kupigania watu wote waliochukuliwa misikitini katika Wilaya za Kilwa na Lindi warejeshwe wakiwa hai ama ndugu na jamaa zao waelezwe kama wameuawa.

Pia alisema wataendelea kuhamasisha Watanzania kuendelea kushikamana kuwapigania Azory Gwanda, Simon Kanguye na Ben Saanane mpaka pale watakapopatikana au ukweli juu yao kujulikana.

Alisema ukweli wa mambo ni kuwa mfanyabiashara Mohammed Dewji (MO) asingepatikana bila nguvu ya umma,Watanzania wasingepaza sauti naye angepotezwa tu kama Saanane, Kanguye na Azory.

Aliwataka Watanzania waendeleza mshikamano huo kwa watu wengine ili kukomesha kabisa vitendo hivyo vya utekaji na watu kupotea.

“Tutaendelea kuitaka Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) ijitathimini. Kwa muda mrefu tumepigania mageuzi ya kimfumo na ya kiuendeshaji ndani ya TISS. TISS si usalama wa CCM wala serikali. TISS ni usalama wa taifa.

“Yanapotea matukio makubwa yanayotishia usalama wa taifa letu, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa anapaswa kuwajibika. TISS ikikaa kimya huku matukio yanayotishia usalama wa wananchi yakikita mizizi, hisia kwamba ‘watu wasiojulikana ni TISS’ zitapata uhalali. Wakati umefika kwa wazalendo ndani ya TISS kuamka na kurejesha hadhi ya chombo hicho.

“Tutaendelea kuyasema bungeni na katika kila mahali tutakapopata nafasi ya kupaza sauti yetu. Tutafanya hilo la kupaza sauti pamoja na kutambua unyeti wa usalama wa nchi yetu, lakini tukipinga njia ya kuua, kuteka, kupoteza na kutesa wananchi wenzetu kwa kigezo cha kulinda usalama wa nchi, ni njia inayowajaza hofu tu wananchi.

“Hofu ni ishara ya kukosa uhuru na bila uhuru watu hawawezi kusemwa kuwa wapo salama. Pia, bila uhuru hakuna maendeleo,”alisema Zitto

Chanzo: Mtanzania

MY TAKE:

Mimi kilichonisikitisha sana, ni kwamba kuna watu wanne jamii ya Wanyantuzi[Wasukuma] waliojeruhiwa wakati wa mapigano, baada ya siku kama tano wakaenda hospitali(Kituo cha afya cha Nguruka) kupata matibabu ya majeraha yao, Polisi walipopata taarifa wakaenda kuwachukua na kuwaua wote. Kwanini wasingepelekwa mahakamani? Mtu kaenda Hospital, kwanini asipewe huduma huku kafungwa pingu?

Serikali ifanye uchunguzi na itupe ukweli ili tujue mbivu na mbichi. Nasubiri kauli ya Mamlaka husika juu ya hivi vifo. Kamanda Sirro alienda kule bado hajatoa maelezo ya alichokiona. Ukute alifichwa.
 
Khaaa watu 100? na vyombo vyetu vya habari vimekaa kimya mpaka Zitto ajilipue? Yani wamevitisha vyombo vya habari mpaka hatujui hata nini kinaendelea tena.. Cha Kushangaza Musiba na Tanzanite wanaandika upuuzi kila siku na wapo mtaani wanadunda.
 
Najua apa wachangiaji watapungua lakini nchi hii inawindwa na ubaguzi wa hali ya juu, kwa MO kila dakika iliandikwa lakini kwa ndugu zetu 100 wa Kigoma watu wanapuuza Nawaambia endeleeni na tabia ya kupuuza siku yakiwafika msilalamike.
Kila mtu achukue furushi lake.
Namkumbuka marehemu J.Kalikawe aliiba wimbo akisema "Omukyemba ky Omugaiga embaga yona eliomwo chonka omw'omworo nalira na boruganda bonka"
Tafsiri isiyorasmi ("Kwenye msiba wa tajiri umati mkubwa wako pale lakini kwa maskini analia na wanaukoo tu)
Acha wanakigoma walie na wanaukoo lakini hakuna aliye salama.
 
Aache kiki...kufa watu 100 sio kitu kidogo, hiyo ni mass murder isingewezekana kukosekana wa ushahidi wa hayo anayosema kwa dunia ya sasa ambayo simu zimekuwa ndo kla ktu. Watu mia wafe na wasijulikane walipo!!? Kwenye hiyo press yake anatuaminisha kusema kwamba hajapata jina hata moja adi aseme chama chake knafanya jitihada za kujua majina ya wote waliokufa!!
 
Mkutano wake ungekuwa wa maana km angekuwa na orodha ya watu waliouawa huko uvinza...zaid ya hao polisi wawili hajataja raia ata mmoja alafu anataka tumwamini kiivo
 
Ukiona vyombo vya dola na serekali vinatupiana mpira nani ajibu basi ujue hilo tukio ni la kweli. Hapo ndio alipotufikisha rais mzalendo, kavisitisha vyombo vya habari hadi vinaogopa kuripoti hizo habari mbaya, na polisi wanatumia mwanya huo kujikalia kimya au kutenda uovu. Hili tukio ni zaidi ya wiki lakini polisi na serekali wako kimya maana wanataka kufumbia mmacho, iwapo sio Zitto tungejuaje haya?
 
Aache kiki...kufa watu 100 sio kitu kidogo, hiyo ni mass murder isingewezekana kukosekana wa ushahidi wa hayo anayosema kwa dunia ya sasa ambayo simu zimekuwa ndo kla ktu. Watu mia wafe na wasijulikane walipo!!? Kwenye hiyo press yake anatuaminisha kusema kwamba hajapata jina hata moja adi aseme chama chake knafanya jitihada za kujua majina ya wote waliokufa!!
Nyie endelea kushabikia ujinga
 
Aiseeeh huko tunapokwenda, sijui kama tutafika kwa hali hii....

Hongera sana Mh Zitto Kabwe, kwa kutufumbua macho watanzania....ni wazi kwamba vyombo vya habari vilifumbwa midomo juu ya huo uchafu ulifanywa huko kigoma.

Poleni sana wanakigoma,, poleni sana watanzania wote.....

Nadhani ni wakati sahihi sasa, wa watanzania wote, kusimama kidete na kuunga mkono jitiada za kulikomboa taifa letu mama, zidi ya haya yanayoendelea hivi sasa.
 
Back
Top Bottom