Kifungo cha Miaka 15 gerezani kinaweza kumkabili "Mtoto wa Siri" wa Rais wa zamani wa Algeria kwa tuhuma za rushwa na ubadhirifu wa mali

Sam Gidori

Senior Member
Sep 7, 2020
165
414
Mwaka mpya unaonekana kuanza vibaya kwa 'mtoto wa siri' rais wa zamani wa Algeria aliyeondolewa madarakani, Abdelaziz Bouteflika, anayejulikana zaidi kwa jina la Madame Maya baada ya upande wa mashtaka kuomba kifungo cha miaka 15 kutokana na tuhuma za rushwa na ubadhirifu wa mali zinazomkabili.

Madame Maya


Mwanamke huyo, ambaye jina lake halisi ni Zoulikha-Chafika Nachinane mwenye umri wa miaka 65, alihukumiwa kwa mara ya kwanza kifungo cha miaka 12 gerezani na kulipa faini ya dinari za Algeria milioni 6 (Sawa na TSh. milioni 105) hapo Oktoba 14. Lakini kesi yake iliendelea kusikilizwa katika mji wa Tipaza mwishoni mwa wiki iliyopita, ikimhusisha yeye na wenzake 13. Upande wa mashtaka umeomba kifungo cha miaka 15 dhidi yake na miaka 10 dhidi ya binti zake wawili, Imene na Farah. Anakabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha, matumizi mabaya ya madaraka, matumizi mabaya ya mali ya umma na kusafirisha kwa njia haramu fedha za kigeni.

Ugunduzi wa Pango la Ali Baba
Madame Maya, ambaye hakuwa akifahamika kabla ya sakata hili, alijilimbikizia mali kwa kutumia ushawishi wa fununu kuwa alikuwa mtoto wa siri wa kiongozi wa zamani wa nchi. Fununu hizi zilisambazwa hasa na watu waliokuwa watiifu kwa Rais Bouteflika, ikimwezesha Madame Maya kufaidi mema ya Algeria, ikiwamo ulinzi kutoka kwa Mkuu wa zamani wa polisi, Abdelghani Hamel.

Lakini katika upekuzi uliofanyika mwezi Julai mwaka 2019, miezi mitatu baada ya Rais Bouteflika kujiuzulu, katika moja ya nyumba zake za kifahari iliyopo katika eneo la Moretti, ufukweni katika viunga vya mji wa Algiers, wapekuzi walikumbana na 'pango la Ali Baba.'

Katika moja ya kuta, mmiliki wa nyumba hiyo alikuwa ameficha dinari milioni 9.5 (sawa na TSh milioni 167.6), Dola 30,000 za Kimarekani (sawa na TSh milioni 69.9), Euro 270,000 (sawa na TSh milioni 762.2) pamoja na kilo 25 za dhahabu zenye thamani ya Euro milioni 1.3 (sawa na TSh bilioni 36.7). Zaidi, Madame Maya na binti zake walisafirisha ughaibuni kwa njia haramu zaidi ya Euro milioni 1.5 (sawa na TSh bilioni 4.2).

Ugunduzi huo ulizua mchanganyiko wa hisia za mshangao na hasira kutoka kwa umma wa Algeria.

Kuhusika kwa vigogo wa serikali ya Algeria
Tangu uchunguzi wa sakata hilo ulipoanza, viongozi wawili wa ngazi ya juu, wakiwamo mawaziri wawili wa zamani, Mohammed Ghazi na Abdelghani Zaalane pamoja na Mkuu wa zamani wa Polisi wamehukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani. Lakini upande wa mashtaka umeomba kifungo cha miaka 15 gerezani, katika rufaa ya kesi hiyo, kwa mawaziri hao wawili pamoja na kifungo cha miaka 12 kwa Abdelghani Hamel, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Algeria (ASP).

Tangu kuanguka kwa utawala wa Rais Abdelaziz Bouteflika, mamlaka nchini Algeria zimeanzisha msururu wa uchunguzi dhidi ya vitendo vya rushwa; vifungo vikali dhidi ya vigogo wa zamani wa utawala wa Bouteflika unaonesha ni kwa jinsi gani ufujaji wa mali ya umma ulivyokuwa ukifanyika kwa kiwango kikubwa.
 
Kwa hivi Tz tunavyokwenda huko siku za mbeleni kuna watu wengi watakuja kupata kesi za aina hii..Hasa ile kandarasi ya ununuzi wa ndege na chato airport
 
Back
Top Bottom