HILI NI BUNGE LA POSHO MPYA AU BUNGE LA KATIBA MPYA ?
Kwa vyovyote na kwa hali yeyote ile sikubaliani kabisa kuwa eti posho katika bunge la katiba ziongezwe.Ni aibu kwa mbunge yeyote aliyeteuliwa au aliyepo bungeni kusimama na kutoa hoja isiyo ya msingi kama hii. Hoja hii imelenga nini hasa? Ikiwa mjumbe mmoja analipwa laki tatu [ Tshz 300,000/=] kama posho kwa siku moja, unataka nini zaidi hapo? Mtanzania wa chini ambaye anajaribu kuweka imani katika bunge hili kwamba katiba aminifu itapatikana hapa, je aliamini vipi tena bunge hili ikiwa limegeuza malengo toka katiba aminifu au mpya kwenda posho mpya? Kila mwanadamu ana mahitaji lakini kuyapata mahitaji hayo inategemea na kipato chake kwa siku. Ikiwa ewe mjumbe unaingiza sh. 300,000 kwa siku na unaishi TANZANIA, je haitoshi wewe kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hilo? Kama wewe wataka zaidi ya hapo na upo bungeni mpaka sasa, hakika hiyo ni DHAMBI na unapaswa kutubu kwa hilo.
Najua na natambua wapo wajumbe wa bunge la katiba ambao kimsingi na kiuwazi wameenda kwa nia moja tu ya kutetea yale maoni ya wananchi na si kitu kingine katika kuhakikisha katiba aminifu inapatikana niseme tu mchango wao na kazi yao inatambulika na itakumbukwa katika taifa hili. Lakini BAADHI ambao wamekosa utu, ambao wamekosa heshima na adabu hakika jamii itawaadabisha katika hili. Ni maisha gani magumu zaidi yaliyopo DODOMA hata posho hiyo isimtoshe mbunge? Ukiachilia mbali malipo mengine? Ni mbunge yupi au nani aliyeteuliwa na raisi ambaye hali yakeni kama za watanzania wengi masikini hapa nchini? Ni kwa sababu gani mtu kama huyo ambaye ameenda kuchuma pesa anastahiki kuwepo bungeni hadi sasa? Hakika ni hoja dhulumishi, hafifu na iliyokosa utu iliyoweza kutolewa katika kipindi hiki ambacho tegemeo kubwa la wengi ni katiba mpya na katiba aminifu kupatikana.
Siku zote nimekuwa nikiamini katika UTU, HAKI NA USAWA. Lakin utakubaliana name kuwa nchi hii imefika wakati ipate kiongozi ambaye ni zaidi ya hata alivyokuwa GADAFFI[DICTATOR]. Kwa kuwa wapo baadhi ya viongozi mfano wabunge wanaodai posho kama hizi, wananchi tungenufaika na viongozi wa mabavu kama huyu. Ifike mahali tupate mtu atakayekemea, na kuchukua hatua stahiki mara moja pindi masuala ya ajabu na aibu yanapotokea katika taifa letu. Wapo watakaosema ni ukiukaji wa haki za binadamu kutumia nguvu katika hili lakini niseme tu kila kitu kina faida na hasara na pindi faida inapoonekana basin a kitumiwe kwa manufaa ya taifa. Zimekuwepo shutuma nyingi za UCHOCHEZI kwa baadhi ya viongozi , Lakini niseme tu huu ndio uchochezi wa wazi kabisa kuwahi kufanyika. Kwa nini nasema hivyo ni kwa sababu kwa hoja kama hii, kwanza wananchi watagawanyika, wajumbe watagawanyika, katiba itagawanyika, na hatimaye taifa litagawanyika kwani wapo watu wanaosimama katika haki na kweli na wapo wale wanyonyaji na wakandamizaji wa haki ambao mfano mzuri ni hao watakaokubali POSHO ZIONGEZWE.
Mwisho niseme tu HAKUNA HAKI PASIPO NA HAKI RAISI litazame hili kwa makini na ufanye maamuzi kwa manufaa ya wengi kwani wapo wengi waliokwisha tenda MAOVU NA MABAYA mengi sana kwa kuwakandamiza wananchi lakini kwa kutenda HAKI kwa siku za mwisho wao walilinda heshima yao na kukumbukwa japo kwa HAKI ya siku moja katika muda wa MADARAKA YAO.
BUNGE LA KATIBA LISIWE SEHEMU YA KUCHUMIA MALI NA UMAARUFU