Kichwa kimehifadhi mengi lakini nini sababu iondoe ajabu?

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,268
KICHWA KIMEHIFADHI MENGI LAKINI NINI SABABU IONDOE AJABU?

Kuna wakati naogopa kusema nikihofia watu watasema huyu Mohamed Said ni muongo inawezekanaje yeye amjue kila mtu tena anaweza akasema huyo mtu akimjua baba yake au babu yake nk. nk.

Au nimefanya hiki na kile na nikaeleza kisa ambacho kikamshangaza anaenisikiliza au kunisoma.

Jana kuna rafiki yangu mmoja mtoto wa Kariakoo kama mimi lakini miaka mingi yuko Ulaya kafanya kazi huko na sasa amestaafu huko huko Ulaya.

Kaniandikia kuniuliza vijana wachezaji mpira waliowika Dar es Salaam wakati sisi ni wadogo na wengine ni umri wetu lakini walikuwa na vipaji vya ajabu kuwa walikuja kucheza mpira na ‘’senior players’’ katika Timu ya Taifa, Yanga Simba na Cosmopolitan.

Wengi wa hawa wametangulia mbele ya haki na wengine wapo.

Basi huyu ndugu yangu akaniomba niandike chochote kuhusu Kesi Kibuda, Ahmed ‘’Mnubi” Johari, Jamil ‘’Denis Law’’ Hizam, Abdul Masikio na wengine lakini nimewataja hawa kwa kuwa nilisuhubiananao kwa karibu wengine kwa sana na wengine kiasi cha kutoleana salaam kila mtu akashika hamsini zake.

Lakini ukimfuata ukamuuliza kama ananijua atakujibu kuwa ananifahamu.
Kaniomba niandike kitu kuhusu Kesi Kibuda.

‘’Brilliant fooballer’’ utapenda kumtazama akicheza mpira kavaa jezi No. 10.
No. ya Pele.

Msomaji naingia Maktaba kuangalia nimeandika nini kuhusu Kesi.
Huwa naona tabu kuandika kitu ambacho kila mtu anakijua.

Hii ndiyo fikra iliyonijia kuwa siwezi kumweleza huyu ndugu yangu kuwa Kesi Kibuda aliwaahidi Yanga kuwa anahamia kwao asubuhi jioni Yanga wanacheza na Cosmo, Yanga wamepigwa na butwaa kumuona Kesi kavaa jezi ya Cosmo anaingia Ilala Stadium.

Kesi kawachezea Yanga akili.
Yanga walifungwa.

Kisa maarufu wakati ule kwa miaka mingi kilikuwa kikihadithiwa.
Nikaamini huyu ndugu yangu na yeye pia anakijua.

Nimerejea udogoni kabisa mwaka wa 1963 au 1964 mimi na Kesi Kibuda tuko Uwanja wa Shule ya Mnazi Mmoja tunacheza mpira.

Naingia Maktaba:
‘’Kesi Kibuda ni makamo yangu.

Siku moja tuna umri wastani kiasi miaka 10 hivi tunacheza mpira uwanja wa Shule ya Mnazi Mmoja.

Mimi niko nyuma ya Kesi namkaba lakini kwa dhati yangu namjua hawezekani ila ninachokusudia ni "harassment," tu.

Ikapigwa "high ball," mimi na yeye sote tunaiangalia na ndiyo wenzetu wanatutazama kwa mbali tucheze mpira ule.

Akili yangu mimi imeniambia nisubiri utue nigombanie na Kesi.

Kesi hakusubiri aliufuata mpira juu kiasi mgongo wake ulikuwa sawa na kichwa changu na uko "perpendicular" na ardhi akapiga tik tak kuelekea golini.

Siku zote nikimuusudu uchezaji wake lakini siku ile niliiambia nafsi yangu kuwa Kesi hakuwa wa kawaida.

Hakika alifika kucheza Timu ya Taifa."

Mara ya mwisho baada ya kupoteana miaka mingi nimemuona Kesi kwenye Khitma Kariakoo tukaa pamoja wakati wa chakula.

Nikimwangalia namuona ni mgonjwa masikini ndugu yangu.
Chakula kizuri lakini hawezi kula.

Huyu si Kesi niliyekuwa namjua udogoni nikimtazama akicheza mpira.
Alikuwa amedhoofu.

Haukupita muda taaarifa zikanifikia kuwa Kesi Kibuda amefariki sehemu za bara.

Jana nasoma kuhusu kifo cha John Lennon wa Beatles.
John Lennon.

Katika utoto wangu miaka hiyo ya 1960 mwanzoni na kuendelea hadi 1970 nikisikiliza muziki wa Beatles na kuzipiga baadhi ya nyimbo zake katika guitar langu.

Katika makala hiyo imetajwa Dakota Building.

Hii ni nyumba mashuhuri Manhattan yenye ‘apartments’’ za kifahari inatazamana na Central Park, New York.

John Lennona na mkewe wa Kijapani Yono Ono wakikaa hapo na mimi nikipita nje ya jumba hili kwa miguu kuingia Central Park kisha kutokea upande wa pili kufika Madison Avenue.

John Lennon alipigwa risasi nje ya jumba hili alipokuwa akiishi.

Mkewe ameweka kumbukumbu ya mumewe, "John Lennon Memorial," ndani ya Central Park.

Central Park nikipapenda kwa kuwa ni uwanja mkubwa wenye bustani Wamarekani wenyewe wanasema wameitengeneza kuiwezesha New York kupumua.

Madison Avenue nikiipenda kwa kitu kimoja.
Mtaa huu una maduka na maofisi yanayoakisi utajiri wa Wamarekani.

Utafurahi ukipita nyakati za jioni watu wanatoka makazini vijana wadogo, wake kwa waume na suti zao na lap top mabegani wakitoka maofisini.

Sikuambii hayo maduka yalivyo.

Niko ndani ya gari kuna mtu kaja kunichukua tunakwenda New Jersey tukapita Dakota Building na siku hiyo ndiyo akanifahamisha jina la hilo jengo na akaniambia kuwa yeye alifika kumuona John Lennon jana yake kabla hajapigwa risasi nje ya jumba hilo na kufa.

Akaniambia John Lennon alikuwa rafiki yake kipenzi.
Nilipata mshtuko.

Nikamwimbia, ‘’Things We Said Today.’’
Ilikuwa zamu yake yeye kushtuka.

Kisha nikaiimba nyimbo hiyo kwa ‘’lyrics za Kiswahili, ‘’Umenitoroka Nyumbani Kwangu.’’

Nikamfahamisha kuwa nikiipiga nyimbo hiyo kwenye guitar langu nikiwa kijana mdogo.

Sasa tunaelekea New Jersey akaniambia kuwa atanipitisha Audubon Hall alipouliwa Malcolm X mwaka wa 1965.

Hakika kabisa tukapita mahali hapo nikapaona na kupiga picha.

Nilipofika New York nimekuta kitabu kipya cha Malcolm X kimetoka, "A Life of Reinvention Malcolm X," kimeandikwa na Manning.

Mwandishi huyu akafa juma ambalo alikuwa azindue kitabu hiki.

Nilimfahamisha mwenyeji wangu kuwa nimenunua kitabu kipya cha Malcolm X.

Kidogo kushangaa kwa kujifaragua kwangu.

Lakini niliyekuja kupata mshangao mkubwa zaidi ni mimi tulipofika nyumbani kwake akanionyesha wanae na kuniambia kuwa wakati walipokuwa watoto wote walikuwa cast katika play ‘’Sound of Music,’’ katika Theatre hadi walipokuwa wakubwa hawawezi tena kuigiza.

Hukaa nikaangalia nyuma nikamshukuru Allah.
Hii ni nini?

Ndiyo nikaanza kwa kusema wakati mwingine naogopa nitakuja kuitwa muongo kuwa kila kitu nakijua mimi.

Tunaelekea Bibi Titi Festival Ikwiriri, Rufiji.
Kuna picha ninayo Maktaba ya Bibi Titi na Dossa Aziz wamepiga pamoja.

Aliyenipatia picha hiyo ananiambia kuwa ilipigwa Mlandizi nyumbani kwa Dossa Aziz.

Picha hii inanikumbusha watu wawili ambao nimepata kufanyanao mazungumzo kwa nyakati tofauti miaka mingi baada ya wao kuwa wametupwa na historia hawana thamani tena juu ya yote waliyofanya katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Katika miaka ya 1980 nilikwenda Temeke nyumbani kwa Bibi Titi.
Wakati ule alikuwa akiishi maisha ya chini sana.

Nyumba zake zimetaifishwa.
Hakutukuzungumza.

Kilichonifikisha kwake ni kuwa nilikuwa namsindikiza rafiki yangu ambae alikuwa anaoa katika ukoo wa Bibi Titi na harusi ilikuwa kwake.

Lakini nilikuja kufika nyumbani kwa Bibi Titi miaka mingi baadae nyumbani kwake Upanga kwenye nyumba yake ambayo alirudishiwa na Rais Mwinyi.

Bibi Titi wa Temeke hakuwa huyu Bibi Titi wa Upanga.

Kulikuwa na mabadiliko makubwa sana.
Safari hii tulizungumza.

Bibi Titi akaniambia kuwa anawajua baba zangu vizuri sana.

Dossa Aziz na yeye aliniambia maneno hayo hayo pia nilipokwenda nyumbani kwake Mlandizi nikiwa na Ally Sykes.

Kasema msemaji, ‘’Kuzaliwa mjini dawa.’’

Picha Bibi Titi na Dossa Aziz, Mwandishi John Lennon Memorial, Central Park, New York na Kitabu cha Malcolm X.

1700508589590.jpeg

1700508632779.jpeg

1700508661224.jpeg
 
Back
Top Bottom