Leila Sheikh na utafiti wa historia Bibi Titi

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,921
30,266
LEILA SHEIKH NA UTAFITI WA HISTORIA YA BIBI TITI

Ilikuwa ni katika miaka ya 1980 ndipo nilipofahamiana na Leila Sheikh mwanadada kutoka Tanga.

Siku hizo ndiyo kwanza alikuwa katoka masomoni Uingereza na kaajiriwa na Daily News.

Leila alikuwa mke wa rafiki yangu Sharif Ahmed Sagaf.

Tukazoeana sana na akawa mzungumzaji wangu mkubwa kila tulipokutana Salamander Restaurant ilipokuwa ofisi ya mumewe au nyumbani kwake nilipowatembelea.

Leila alikuwa ana akili kubwa unaweza kuzungumzanae kuanzia muziki wa Tchaikovsky hadi Mao Tse Tung.

Kikubwa Leila hakuwa mjinga wa dini yake.

Wakati huo nilikuwa nimemaliza kuandika mswada wa kitabu cha Abdul Sykes natafuta mchapaji, yaani "publisher.''

Kila mchapaji niliyempa mswada ule alikuwa anakisifia kitabu lakini anaogopa kukichapa.

Leila akaniomba nimpe asome kile nilichoandika ili ajue hicho kinachotisha wachapaji ni nini hasa.

Nilimpa nakala na sikuichukua nilimwachia ibakie kwake.

Nilifanya hivi kwa kusudi na lengo maalum.

Endapo mimi nitakufa kabla kitabu hakijachapwa na Leila ana mswada ule nilikuwa na uhakika atamtafuta mchapaji amwonyeshe.

Nilikuwa nikiomba dua nikimwambia Allah usinichukue hadi kitabu kimechapwa.

Kulikuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa watu waliokuwa wanafahamu kuwa nimeandika kitabu hicho hoja yao ikiwa kitabu kitoke wakati wengi niliowataja katika kitabu wako hai ili kama kuna wanachoona kimekosewa waweze kusema ukweli ukweli wake.

Niliwapa nakala ya mswada ule watu wachache nilioamini kuwa wanajua thamani ya kile nilichoandika.

Naamini kuwa kama Leila alisoma historia ya Bibi Titi kwa mara ya kwanza basi alimsoma katika mswada huu wa kitabu cha Abdul Sykes.

Historia ya Bibi Titi imeungana na historia ya Julius Nyerere.

Historia ya Abdul Sykes imeungana na historia ya Julius Nyerere..

Historia ya Bibi Titi imeungana na historia ya Abdul Sykes.

Historia hizi zilikuwa historia ambazo hazikuwa zinafahamika kabisa.

Historia yote ya TANU na uhuru wa Tanganyika ilikuwa ni ya Julius Nyerere peke yake.

Naamini kabisa Leila alivutiwa na mswada uliokuwa mikononi mwake.

Nyakati zile zilikuwa nyakati za siasa za haki za wanawake kupewa usawa na wanaume.

Bila shaka alivutiwa na historia ya Bibi Titi kuona mwanamama Muislam na ikamshangaza aliwezaje katika jamii Ile iliyomzunguka akaweza kufanya yale yote aliyofanya?

Akapanda jukwaani kuwahutubia wanaume?

Mimi na Leila hatukupata kukaa kitako tukajadili mswada wangu wala kumjadili Bibi Titi.

Haya yalikuja baadae sana kiasi cha miaka 30 na zaidi mbele.

Leila alinieleza mara ya kwanza walipokwenda nyumbani kwa Bibi Titi kumuomba awe mlezi wa TAMWA ( Chama Cha Waandishi Wanawake wa Tanzania).

Leila anasema bila kusita Bibi Titi aliwakubalia.

Bibi Titi kama alivyoinyanyua TANU kwa kuipamba kwa wanawake, nyimbo na misemo ya kuhamasisha na kutia ari katika miaka ya 1950 wakati wa ukoloni, ilikuwa kazi nyepesi sana kuwafunza wanawake hawa vijana na wasomi mbinu za kujenga chama kwa staili hiyo katika Tanzania huru.

Leila anasema Bibi Titi aliingiza katika chama chao utamaduni mpya kabisa.

Bibi Titi aliwafungulia Leila na wenzake makabati yake ya khanga za zamani zinarudi nyuma miaka na miaka.

Khanga zilikuwa zinatoka zimeandikwa maneno kutokana na matukio na wakati mwngine maneno ya mafumbo hata vijembe.

"Mwanlela khanga hizi mvae katika shughuli zenu muwe wanawake khasa na muonekane nyie ni watoto wa kike na mcheze ngoma katika mavazi haya mmepiga vibwewe huo ndiyo ujanajike mmekalia masuruali na viatu vua mchuchumio."

Viatu vya mchuchumio vikawekwa pembeni.

Ikafika mahali Bi. Titi haimbishi tena nyimbo za lelemama katika mikutano na shughuli za TANWA ikawa wao ndiyo wanamchokoza kwa nyimbo zilezile alizowafunza, ''Mkataa Umoja Kala Hasara Huyo,'' na nyinginezo.

Chama kikawa hakika kimepata Mlezi wa kweli na wa uhakika, mjuzi wa uhamasihaji.

Leila anasema Bibi Titi alipokifikisha chama katika kiwango kile ndipo yeye akazidi kuwa karibu zaidi na yeye.

Hapa ndipo Leila alipoanza kumdodosa Bibi Titi kuhusu maisha yake.

"Mwanlela mimi nikidhani mwali wangu umekuja nyumbani kwangu kunikagua ujue hali yangu nimeamkaje kumbe umekuja na kadha wa kadha?"

Leila atacheka sana kwa majibu yale.

"Ehe Mwanlela nikishakueleza nilivyokuwa mwanamari naanza shule nakwenda madrasa kusoma sasa ndiwe iweje kwako?

"Unataka kunijua?

Mwanlela mimi nimekushinda wewe huna hata talaka moja."

Mazungumzo, maskhara ya bibi na mjukuu wake mwanamke ampendae.

Leila anasema hivi ndivyo ulivyoanza usuhuba mkubwa baina yao na Bibi Titi akamwondolea Leila Sheikh pazia.

Bibi Titi akawa anampigia Leila hadithi ya maisha yake kila wanapokutana faragha nyumbani kwake.

''Paukwa pakawa mwanangu Mwanasiti kijino kama chikichi...'

Leila anafungua mkoba wake anatoa zana zake za kazi.

Naam sufuria ilikuwa imepata mfuniko.
Kazi hii ilikuwa miaka mingi.

Hakikuwa kazi ya leo kumalizika kesho.
Leila akakusanya mzigo mkubwa wa notes, sauti ya Bibi Titi na video.

1701703232300.jpeg

Leila Sheikh
 
Back
Top Bottom